Saturday, July 16, 2016

TRUMP ATEUA MGOMBEA MWENZA

Indiana, Marekani

Mgombea wa urais mtarajiwa kwa tikiti ya chama cha Republian nchini Marekani, Donald Trump, siku ya Ijumaa alitangaza kuwa Gavana wa jimbo la Indiana Mike Pence ndiye atakuwa mgombea mwenza kuelekea kwa uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu.

Gavana wa Jimbo la Indiana, Mike Pence
Katika ujumbe alioutuma kupitia mtandao wa twitter Ijumaa asubuhi, Trump alisema alikuwa na furaha kumteua gavana Pence kama mgombea mwenza ambaye atachukua wadhifa wa makamu wa rais endapo mfanya biashara huyo tajiri atachaguliwa kama rais wa Marekani.
"Nitafanya mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na swala hilo kesho saa nne asubuhui," alisema Trump.

Pence, mwenye umri wa miaka 57, alikutana na Trump na familia yake nyumbani kwake Indianapolis siku ya Alhamisi na kupelekea uvumi kuwa angekuwa mgombea mwenza wa Trump .
Mwanasiasa huyo wa vuguvugu la siasa la mrengo wa Tea Party ametajwa na wachambuzi wa maswala ya siasa za Marekani kama ambaye huenda akamsaidia kuwavutia vigogo katika chama chake na kumsaidia Trump kupata kura nyingi.
Pence alikuwa ametajwa na Trump kama mmoja wa watu ambao huenda wangeteuliwa kwenye nafasi hiyo. Wengine walikuwa spika wa zamani Newt Gingrich na gavana wa sasa wa jimbo la New Jersey, Chris Christie.

Kabla ya kuwa Gavana wa Indiana, nafasi ambayo ameshikilia tangu mwaka wa 2013, pence aliwahi kuhudumu katika bunge la Congress la Marekani kwa miaka 12.

Trump anatarajiwa kuidhinishwa kama mgombea rasmi wa chama cha Republikan kwenye kongamano litakalofanyika mjini Cleveland, Ohio, kuanzia Jumatatu, tarehe kumi na nane Mwezi Julai. Watagombania nafasi ya urais na Bi Hillary Clinton, ambaye ndiye mgombea mteule wa chama cha Demoktarik na ambaye pia anatarajiwa kuidhinishwa kwenye mkutano mkuu wa chama utakaofanyika mjini Philadelphia kuanzia tarehe 25 Mwezi July

No comments:

Post a Comment