Thursday, July 14, 2016

JERRY MURO ASALIMU AMRI

Msemaji wa Yanga Jerry Muro
HATIMAYE msemaji wa Yanga, Jerry Muro amekubali yaishe kwa uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Muro alikuwa akitunishiana kifua na TFF pale alipofungiwa kwa mwaka mmoja na faini ya Sh milioni 3, akidai kuwa hakubaliani na adhabu hiyo na kwamba akili kubwa haiwezi kuongozwa na akili ndogo.
Muro alienda mbali zaidi na kudai kuwa yeye sio muajiriwa wa TFF hivyo TFF haina mamlaka ya kumfungia kwa vile yeye sio mwanachama wa shirikisho hilo na kama kufungiwa basi ifungiwe klabu.
Hata hivyo habari ambazo HabariLeo ilizipata hivi karibuni zilisema kuwa uongozi wa Yanga ni kama umemtosa Muro kwa kile ulichodai kuwa haujamtuma Muro kutoa lugha za kashfa na kuzungumza maneno mengi kwenye vyombo vya habari.
Muro jana aliandika kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram: “Nikifikiria figisu za soka la bongo, aisee nachoka kabisa, acha nijiweke pembeni kwa muda, nitawamiss mashabiki wangu wa kimataifa, acha nikae mbali kwa mbali”.
Akizungumzia suala hilo, Katibu mkuu wa Yanga Baraka Deusdetit alisema: “Barua ya Jerry kashaipata, uongozi wa Yanga kupitia kwa mwenyekiti wetu umemwambia atulie, akae pembeni kidogo, mwenyekiti kwa sasa yupo nje ya nchi,”alisema Baraka.
Makosa yaliyomtia lupango Muro ni kukashifu, kuipinga na kuishambulia TFF kwenye vyombo vya habari hukumu ambayo imeridhiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa ambaye ndiye aliyewasilisha malalamiko ya TFF kwenye kamati ya maadili akiwa kama mtendaji mkuu wa shirikisho hilo.
Hii inakuwa ni adhabu ya pili kwa Muro baada ya Mei 5 mwaka jana, Kamati ya Nidhamu ya TFF kumpiga faini ya Sh milioni 5 kwa kutoa kauli za chuki, kisirani na uchochezi dhidi ya uongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) nchini na TFF.

No comments:

Post a Comment