SERIKALI YAWAGEUKIA WAVAMIZI WA VIWANJA.
Dar es Salaam. Serikali imeapa kukomesha tabia ya uvamizi wa viwanja vya michezo na maeneo ya wazi kama moja ya harakati zake katika kuhamasisha na kuinua sekta ya michezo nchini.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwa sekta ya michezo haiwezi kupiga hatua kama maeneo ambayo yalitakiwa kuzalisha vipaji yanatumika kwa shughuli zisizo za kimichezo.Nape alisema Serikali ya awamu ya tano imechoka kuwavumilia wavamizi wa maeneo ya wazi kwa sababu ni miongoni mwa maadui wakuu wanaorudisha nyuma michezo nchini.
“Tulishasema baada ya bunge tutafanya operesheni kubwa ya kurudisha viwanja vilivyovamiwa. Haijalishi ni nani kajenga, turudishe. Nadhani kwa kuwa Bunge limeisha, tutaanza operesheni.
“Dar es Salaam inaongoza kwa maeneo mengi yaliyovamiwa. Nitoe wito kwa madiwani waache uhuni wa kuvamia maeneo ya wazi na kuyagawa kwa ajili ya matumizi mengineyo.
“Hatutaacha badala ya kwenda mbele, tukiruhusu maeneo kuendelea kuvamiwa na kuchukuliwa maana yake tutakuwa tunarudi nyuma,” alisema Waziri Nape.
Waziri huyo alitoa agizo kuwa kuanzia sasa mamlaka zinazo husika na mipango miji, zianze kutenga maeneo ya wazi kwenye eneo lenye makazi ya watu kwa ajili ya kuibua vipaji mbalimbali za michezo.
“Tuache sasa kupanga mipango ya matumizi ya ardhi bila kuweka maeneo kwa ajili ya michezo. Kuna maeneo mengi yanapangwa matumizi kwa ajili ya makazi halafu wanasahau kuwa katika makazi ni vizuri kukawa na maeneo kwa ajili ya michezo,” alisema Nape.
No comments:
Post a Comment