Mgogoro unaoendelea sasa baina ya China na Taiwan ni matokeo ya mivutano ya tofauti za mitazamo ya kisiasa ya wafuasi wa vuguvugu la utaifa (Nationalist ) wenye kupendelea mfumo wa uchumi wa Kibepari waliokuwa wakiungwa mkono na Marekani dhidi ya wafuasi wa sera za kiuchumi za kijamaa (Communist) waliokuwa wakiungwa mkono na Soviet Union. Mivutano hii iliendelea kwa muda mrefu hadi kupelekea pande mbili kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kugombania madaraka.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China (The Chinese Civil War) ilipiganwa kuanzia mwaka 1927 hadi mwaka 1949. Vita ilihusisha wafuasi wa Nationalist wa Chama chenye mrengo wa kibebari cha Kuomintang (KMT) kilichokuwa kinatawala Jamhuri ya China dhidi ya Wafuasi wa sera za kijamaa wa Chama cha upinzani cha Kikomunist cha China (CPC).
Vita ilipiganwa katika hatua mbili, hatua ya kwanza ni kuanzia Mwaka 1927 hadi mwaka 1937 ambapo vita ilisitishwa na pande mbili hasimu ziliungana ili kukabiliana na kitisho ya jeshi la Japan, lengo la kuungana lilikuwa ni kuilinda China isisambaratike. Pande hasimu zilirudi tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Mwaka 1946 baada ya kitisho cha Japan kumalizika.
Mwaka 1949 Wakomunist wakiongozwa na Mao Tse Tung walishinda vita na kuitimua madarakani Serikali ya Rais Chiang Kai-shek wa Chama cha kibebari cha Kuomintang (KMT) kisha kuunda Jamhuri ya Watu wa China (People's Republic of China-PRC).
Baada ya kushindwa vita, Mwaka 1949 serikali ya Kuomintang chini ya jenerali Chiang Kai-shek na mabaki ya jeshi lake pamoja na wafuasi wake wengi ilihamia kwenye Kisiwa cha Taiwan na visiwa vingine vidogo vinavyoizunguka Taiwan ambapo waliendelea kutawala huku wakisisitiza kuwa serikali yao ndiyo serikali halali ya Jamhuri ya China. Wakomunisti walikosa nguvu ya kuwafuata hadi kwenye visiwa kutokana na vitisho vya Marekani. Hivyo serikali katika kisiwa cha Taiwan iliendelea kujiita "serikali halali ya Jamhuri ya China" (Republic of China-ROC) na kutangaza shabaha yake ya kuikomboa China yote kutoka mikononi mwa Chama cha kikomunist cha Mao Tse Tung.
Wakati huo huo Serikali ya Kikomunist huko China Bara nayo ilijitangaza kuwa ndio serikali halali ya China yote huku ikitangaza shabaha yake ya kukikomboa kisiwa cha Taiwan kutoka mikononi wa wafuasi wa chama cha Kuomintang na kukiunganisha tena na Jamhuri ya watu wa China.
Serikali ya Chama cha Kuomintang katika kisiwa cha Taiwan iliendelea kutambuliwa na umoja wa mataifa kuwa ndiye serikali halali ya China na ilikalia kiti cha China katika umoja wa mataifa hadi tarehe 25 Oktoba 1971 ambapo mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa uliamua kwamba Jamhuri ya Watu wa China (PRC) iwe mwakilishi halisi wa China kwenye Umoja wa Mataifa (UN) , hivyo Jamhuri ya China (Taiwan) ilifukuzwa. Hali hii ilipelekea Mataifa mengi zaidi ikiwemo Marekani na Washirika zake kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Kufunga ofisi zao za ubalozi huko Taiwan
Kwa kuwa hakuna mkataba wa amani uliofikiwa baina ya pande mbili hasimu mpaka sasa, kila upande bado unaamini kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe baina yao bado havijamalizika.
KUIBUKA KWA SERA YA CHINA MOJA (ONE CHINA POLICY)
Serikali zote mbili yaani Jamhuri ya China (Taiwan) na Jamhuri ya watu wa China ( China Mainland-Beijing)ziliweka msimamo wa kuitambua China moja tu (One China Policy) hivyo basi ziliweka sharti kwa mataifa mengine kuwa hayaruhusiwi kuwa na uhusiano rasmi na serikali zote mbili kwa pamoja kwa madai kuwa kufanya hivyo kunachochea mgawanyiko wa China. Hivyo kama nchi fulani itakuwa na uhusiano rasmi na Jamhuri ya China (Taiwan) italazimika kuvunja uhusiano rasmi na Jamhuri la watu wa China (China Mainland-Beijing) au kinyume chake(vice versa).
FAIDA NA HASARA ZA SERA YA CHINA MOJA (ONE CHINA POLICY) KWA PANDE ZOTE MBILI.
Jamhuri ya watu wa China (China Mainland) imenufaika zaidi na sera hii kwa kufanikiwa kupata uungwaji mkono kidiplomasia kutoka mataifa mengi.Katika bara la Africa, Burkina faso ndiyo nchi pekee yenye uhusiano rasmi na Taiwan huku ikiwa haina uhusiano wowote na China. Afrika kusini, Libya na Nigeria zina uhusiano rasmi na China wakati huo huo zikiwa na uhusiano usio rasmi na Taiwan. Mataifa mengine yote ya bara la Afrika yana uhusiano rasmi na China bila kuwa na uhusiano usio rasmi na Taiwan. 98% ya mataifa yote Duniani (Yakiwemo mataifa yote Makubwa) yana uhusiano rasmi na China. Hali hii inaipa China nguvu ya kuendelea kuichukulia Taiwan kama jimbo lake lililojitenga. Hata hivyo Uhusiano wa kijeshi unaoendelea kunawiri kati ya Taiwan na Marekani umekuwa ni kitisho kwa Jamhuri ya Watu wa China.
Kwa upande wa Taiwan, sera hii imewawezesha kuendelea kujitawala bila kusumbuliwa. Pia imekuwa na uhusiano usio rasmi na mataifa yote ya Ulaya Magharibi, Amerika na baadhi ya mataifa ya Asia. Ingawa kuna harakati nyingi za kijeshi kwenye eneo la mlango bahari wa Taiwan (Taiwan strait) unaotenganisha nchi hizi mbili bado raia wa nchi hizi mbili wanatembeleana na ikiwa ni pamoja na kufanya biashara. Inakadiriwa kuwa raia milioni mbili wa Taiwan wanaishi na kufanya kazi China. Pia uungwaji mkono kiuchumi kutoka kwa Marekani na Washirika zake umeifanya Taiwan kuwa miongoni mwa Mataifa yaliopiga hatua kubwa Kimaendeleo huku ikishika nafasi ya 21 kwa kuwa na uchumi mzuri duniani. Hasara iliyopata Taiwan ni kutengwa kidiplomasia na mataifa mengi Duniani.
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana
Napatikana kupitia simu namba
+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com
No comments:
Post a Comment