Thursday, November 23, 2017

UHASAMA KATI YA KOREA KASKAZINI NA KOREA KUSINI

Na Masudi Rugombana.

Mgogoro wa Peninsular ya Korea ni zao la vita baridi (cold war) kati ya Mataifa ya Kibepari ya Ulaya Magharibi na Mataifa ya Kijamaa ya Ulaya Mashariki. Ikumbukwe kuwa Korea ilikuwa moja chini ya Ukoloni wa Japan hadi mwaka 1945 baada ya Japan kushindwa vita kuu ya pili ya Dunia.

CHANZO CHA KUGAWANYIKA KWA
PENINSULA YA KOREA.
Chanzo cha mgawanyiko ni vita ya kumuondoa Mjapan katika peninsula ya Korea iliyoongozwa na Marekani na Urusi. Urusi ilianzisha mapambano ya kumuondoa Mjapani ikitokea Upande wa Kaskazini mnamo Mwezi August 1945. Kwa kuwa tangazo la Urusi la vita dhidi ya Japan liliungwa mkono na Mataifa ya Marekani na Uingereza kwenye mkutano wa Marais watatu wa nchi hizo uliofanyika Yalta, Crimea (Yalta Conference) mnamo August 4 hadi 11 Mwaka 1945, kwa kuhofia Peninsular yote ya Korea kuangukia mikononi mwa Urusi, Marekani iliiomba Urusi katika vita yake dhidi Japan huko Korea iishie kwenye mstari wa latitudo unaofahamika kama 38th Paralleh north unaogawa peninsula ya Korea pande mbili sawa za Kusini na Kaskazini. Upande wa kusini wa 38th Paralleh north kilikuwa kituo cha mwisho kwa majeshi ya Japan kujisalimisha kwa vikosi vya Marekani, na upande wa kaskazini ilikuwa kituo cha mwisho kwa majeshi ya Japan kujisalimisha kwa vikosi vya Urusi.


September 8, 1945 Majeshi ya Marekani yaliingia upande wa Kusini na kuanzisha Serikali ya kijeshi chini ya jeshi la Marekani baada ya vikosi vya Japan kusalimu amri na kuondoka.   Kwa hivyo 38th Paralleh north ukawa ndio mpaka unatenganisha majeshi ya Marekani upande wa kusini na Majeshi ya Urusi kwa upande wa Kaskazini.

38th Paralleh

Marekani na Urusi zilijaribu kutaka kuunganisha tena Korea lakini juhudi hizo zilikumbana na vikwazo kutokana na migawanyiko ya itikadi za kisiasa baina ya Wafuasi wa sera za kijamaa walioungwa mkono na  Urusi na Wale wa vuguvugu la utaifa (Nationalist) ambao waliegemea kwenye siasa za kibepari waliokuwa wakiungwa mkono na Marekani.

Kitendo cha Marekani na Urusi kuweka mbele itikadi zao za kibebari na Kijamaa ndicho kilikuwa chanzo cha kushindwa kuunganisha tena Korea kuwa nchi moja. Marekani ilipendekeza ufanyike uchaguzi wa kidemokrasia ili kuwapa fursa wananchi wa Korea kuchagua uongozi wao ambapo upande wa Kaskazini chini ya Urusi ulikataa mapendekezo hayo. Hali hii ilipelekea Marekani kuitisha uchaguzi upande wa Kusini na kumkabidhi nchi Mwanaharakati wa vita dhidi ya Ukoloni wa Japani Syngman Rhee August 15, 1948 ambaye alishinda kwa asilimia 92.


Urusi nayo mnamo 9 September 1948  ilimsimika Kiongozi wa Chama cha kikomunist Kim Il-Sung kuwa Rais wa Korea Kaskazini ya Kijamaa na Mwezi October Mwaka 1948 Urusi ilitangaza kumtambua Kim kuwa ndiye kiongozi halali wa Korea yote ikiwemo Korea Kusini.

NINI CHANZO CHA MGOGORO UNAOENDELA HADI SASA
Tawala zote mbili zilikataa kutambuana ambapo kila upande ulijitangaza kuwa ndiye mtawala wa peninsula yote ya Korea. Na msimamo huu umeendelea mpaka sasa. Baada ya Marekani na Urusi kujiondoa kijeshi kutoka Korea, hali ya wasiwasi na kutokuaminiana iliendelea katika eneo la mpaka wa nchi hizi mbili, ambapo kulikuwa na kushambuliana mara kwa mara baina ya pande mbili.

Hali hii ilipelekea Korea Kaskazini ikishauriwa na China na Soviety Union kuamua kuivamia kijeshi Korea Kusini June 25, 1950 na kufanikiwa kuuteka mji mkuu Seoul June 28, 1950. Kufuatia uvamizi huo June 27, 1950 baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura na kuidhinisha kupeleka Vikosi vya umoja huo ili kuiondoa kwa nguvu Korea Kaskazini kutoka kwenye ardhi ya Korea Kusini.

Urusi haikuhudhuria kikao hicho kwa sababu ilikuwa imesusia vikao vya baraza la usalama kuanzia mwezi January 1950 kupinga kiti cha China kwenye baraza hilo kukaliwa na Jamhuri ya China (Taiwan) badala ya Jamhuri ya Watu wa China (China Bara) hivyo haikuweza kupinga maamuzi hayo kwa kupiga kura ya turufu (Veto). Jeshi la Umoja wa Mataifa liliongozwa na Marekani ambayo ilitoa karibu asilimia 88 ya wapiganaji wote, huku ikiungwa mkono zaidi na wanachama wa NATO kama vile Uingereza, Canada, Uturuki na Ufaransa.

Vikosi vya umoja wa Mataifa chini ya Marekani vilianza rasmi vita ya kuiondoa Korea Kaskazini kutoka kwenye ardhi ya Korea Kusini July 2, 1950 ambapo vilifanikiwa kuukomboa mji mkuu Seoul mwezi September 1950 na kusonga mbele zaidi ndani ya Korea Kaskazini na kufanikiwa kuuteka mji mku Pyongyang October 19, 1950. Vikosi vya Marekani chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa vilisonga mbele zaidi kuelekea kwenye mpaka kati ya Korea Kaskazini na China. Hatua hii ilipelekea China kuingilia kati kijeshi kuisadia Korea Kaskazini kwa kudeploy askari Milion Moja. Urusi nayo iliiunga mkono China kwa kutuma ndege za kivita na wakufunzi wa kijeshi.

Vikosi vya China na Korea Kaskazini vilifanikiwa kuiondoa Marekani Kutoka Korea Kaskazini, na kuuteka tena mji mkuu Pyongayanga mnamo December 5, 1950. Vikosi vya China vilisonga mbele zaidi na kufanikiwa kuuteka  tena mji mkuu wa Korea Kusini (Seoul) January 1951. Marekani na washirika wake chini ya Mwamvuli wa UN walifanikwa kuuteka tena mji mkuu Seoul mwezi March 1951 na kuyarudisha Nyuma majeshi ya China hadi kwenye mpaka wa Korea mbili kabla ya vita. (The 38th parallel north). Marekani haikusonga mbele zaidi badala yake iliitaka China wakae kwenye meza ya Mazungumzo ili kuangalia namna ya kufikia makubaliano.

MAKUBALIANO YA KISITISHA VITA (ARMISTICE AGREEMENTS)
July 27, 1953 Korea ya Kaskazini ikiungwa mkono na china walifikia makubaliano ya kusimamisha Vita na Korea Kusini (armistice agreements) kwa kuchora mpaka mpya wa kijeshi (Military Demarcation Line-MDL)  ambao kwa jina lingine unajulikana kama armistice line unaozungukwa na eneo la kilometa nne kaskazini na kusini mwa mpaka lisiloruhusiwa kufanyika harakati za kijeshi (Demilitarized Zone-DMZ).

Mpaka wa Korea mbili baada ya Makubaliano
ya kusitisha vita July 27, 1953.

Tokea hapo hapajawahi kuwa na mkataba wa Kumaliza mgogoro baina ya Korea mbili huku kila upande ukiendelea kudai kuwa na mamlaka ya utawala wa Korea yote, wakati huo huo pande zote zikiendelea kujiimarisha kijeshi nje ya eneo la mpaka wa mataifa hayo mawili. Hali hii ya kutokuwa na mkataba wa kumaliza mgogoro ndio unaozifanya Korea zote mbili kuendeleza uhasama hadi sasa.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com



No comments:

Post a Comment