Dmitry Anatolyevich Medvedev ni Waziri mkuu wa Urusi na Mwenyekiti wa chama cha United Russia, chama tawala cha kihafidhina cha mrengo wa kulia kikubwa kuliko vyama vyote vya siasa nchini Urusi. Mwanasiasa huyu shupavu mwenye umri wa miaka 52 anatajwa kuwa mtu wa karibu zaidi na mwenye ushawishi mkubwa kwa Rais Vladmir Putin akifuatiwa na bwana Vladislav Surkov mwenye asili ya Chechnya, msaidizi wa Rais Vladmir Putin ambaye nyuma ya pazia ana nguvu kubwa katika maamuzi yanayotolewa kwenye Ikulu ya Urusi (Kremlin). Vladislav Surkov pia alishawahi kuwa naibu Waziri Mkuu wa Urusi kati ya December 2011 hadi May 2012.
Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev |
Wengine wanaounda timu ya watu wa karibu zaidi na Rais Putin (Putin's inner cycle) ni mfanyabiashara Igor Sechin, huyu ni Afisa mtendaji mkuu (CEO) wa kampuni ya Rosneft, kampuni kubwa ya Mafuta ambayo nusu ya hisa zake zinamilikiwa na serikali ya Urusi, Sechin pia alishawahi kuwa naibu Waziri mkuu wa Urusi kuanzia mwaka 2008 hadi 2012. Pia kuna Mfanyabiasha bilionea Gennady Timchenko, mshirika wa karibu zaidi na Putin ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya Volga Group inayojishughulisha na uwekezaji katika nishati, usafirishaji na miundombinu. Bilionea huyu mwenye Uraia wa nchi tatu za Urusi, Armenia na Finland anashikilia nafasi ya 85 Duniani kwa utajiri kwa mujibu wa Jarida la Forbes la Marekani.
Wengine ni Spika wa Bunge la Urusi (DUMA) Vyacheslav Volodin. Sergey Chemezov jasusi wa zamani wa KGB aliyefanya kazi pamoja na Vladmir Putin huko Ujerumani Mashariki. Arkady Rotenberg na Boris Rotenberg, ndugu wawili ambao ni wafanyabiashara mabilionea. Wamiliki hawa wa kampuni ya ujenzi ya SGM Group wanatajwa kuwa na urafiki mkubwa na Putin ulioanzia tangu enzi za utotoni. Pia kuna Yury Kovalchuk mfanyabiashara bilionea, mwenyekiti na mmiliki mkubwa zaidi wa hisa wa beki ya Rossiya, mojawapo ya benki kubwa kabisa nchini Urusi, pia anatajwa kama mtu anayeshughulikia masuala ya kifedha katika account binafsi za Rais Vladmir Putin zilizopo kwenye benki mbali mbali (Putin's personal banker).
Medvedev, Rais wa Urusi kuanzia mwaka 2008-2012 ndiye kijana zaidi kuliko Marais wote waliowahi kuiongoza Urusi tangu mwaka 1918, anatajwa kuwa ni kiongozi aliyepata mafanikio makubwa katika uongozi wake wa miaka minne nchini Urusi. Chini ya uongozi wake Urusi imepata mafanikio makubwa Kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.
UCHUMI
Anasifika kwa kuanzisha, kuhamasisha na kusimamia kikamilifu mkakati wa kuugeuza uchumi wa Urusi kuwa wa kisasa (modernization of the Russia economy) kwa kuifanya nchi ipunguze utegemezi katika sekta za mafuta na gesi na kuanzisha mfumo wa uchumi mseto (diversified economy) unaotegemea zaidi teknolojia ya hali ya juu pamoja na ubunifu. Hatua hizi za Medvedev ambazo kwa sasa anaendelea kuzisimamia kwenye wadhifa wake wa Waziri mkuu wa Urusi zimeifanya Urusi kupiga hatua kubwa kwenye teknolojia za mawasiliano, matibabu, madawa, uhandisi wa nguvu za kinyuklia (nuclear power engineering) mawasiliano ya simu na anga.
MAENDELEO YA JAMII
Ilikuwa ni serikali yake iliyoanzisha na kuelekeza moja kwa moja fedha katika mfuko maalumu wa kampeni ya kukuza kiwango cha kuzaliana baada ya Urusi kukumbwa na tatizo la upungufu wa watu hivyo alifanikiwa katika kupunguza tatizo la upungufu wa idadi ya watu nchini Urusi.Pia ni katika kipindi cha utawala wake alileta mageuzi katika jeshi la polisi na kuzifanya mahakama kuwa huru zaidi. Miongoni mwa alama za uongozi wake ni pamoja na kufanya mabadiliko ya katiba kwa kuongeza muda wa kikomo cha Urais kutoka miaka minne hadi sita. Pia aliongeza muda wa ukomo wa bunge kutoka miaka minne hadi mitano.
DIPLOMASIA
Katika ngazi ya kidiplomasia, anasifika kwa kuimarisha uhusiano kati ya Urusi na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU). Ni katika utawala wake ndipo uhusiano wa Marekani na Urusi uliimarika zaidi hasa baada ya msuguano mkali uliosababishwa na hatua yake ya kuingia vitani dhidi ya Georgia mnamo August 8, 2008 (miezi mitatu baada ya kuingia madarakani) katika mgogoro wa Abkhazia na South Ossetia katika oparesheni iliyojulikana kama "Operation Clear Field" ambapo Urusi ilishinda vita ndani ya siku nne na kuyaondoa majeshi ya Georgia kwenye majimbo hayo ambayo baadae Urusi ilitangaza kuyatambua kama ni nchi huru mnamo August 26, 2008.
Dmitry Medvedev na Barack Obama |
Medvedev alifanikiwa kupunguza kasi ya NATO kujitanua kuelekea Mashariki ya Ulaya na kuzuia nchi za CIS (Nchi kumi na moja ambazo ni Jamhuri za zamani za Sovieti union) kujiunga na NATO. Diplomasia yake ilisadia kwa kiasi kikubwa kujenga picha nzuri ya Urusi katika jumuiya ya kimataifa.
VITA DHIDI YA RUSHWA
Vita yake dhidi ya rushwa aliyoitangaza rasmi mwaka 2008 mara baada ya kuingia madarakani haikuleta mafanikio makubwa. Mwaka 2011 alitangaza rasmi kuwa mkakati wake wa kupambana na rushwa ulikuwa umeshindwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo aliendeleza vita dhidi ya rushwa kuanzisha mkakati wa taifa wa kupambana na rushwa, sera ya serikali ya muda mfupi inayofanyiwa marekebisho kila baada ya miaka miwili.
Medvedev alikumbana na changamoto kubwa Mwezi March 2017 baada ya kiongozi wa Upinzani Alexei Navalny kumtuhumu kwa kujihusisha na rushwa, tuhuma ambazo zilishindwa kuthibitishwa. Akizungumzia tuhuma hizo, Msemaji wa Rais Medvedev Natalya Timakova aliziita ni "propaganda zilizopenyezwa kwa hila", naye Msemaji wa Rais Vladmir Putin bwana Dmitry Peskov akizungumzia tuhuma hizo alimwita bwana Alexei Navalny kuwa ni "raia hatari aliyetiwa hatiani kwa sifa mbaya" Ikumbukwe kuwa Alexei ambaye alitangaza nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018, February 2017 alitiwa hatiani kwa makosa ya ubadhirifu (embezzlement) na kuhukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitano.Hukumu ambayo imemfanya akose sifa za kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.
Uchunguzi unaonyesha kwamba Alexei alilishwa taarifa hizo na wanasiasa wa ngazi ya juu wenye lengo la kuwachafua wenzao katika harakati zao za kutaka kuwa na nguvu ya ushawishi katika Ikulu ya Kremlin. Urusi inashika nafasi ya 131 Duniani kwa viwango vya rushwa kwa mujibu wa ripoti ya Transparency international ya kwaka 2016.
UHUSIANO WAKE NA RAIS VLADMIR PUTIN
Medvedev na Putin hawakujuana barabarani, historia yao katika uongozi inaanzia mwaka 1990 wakati mwalimu wao Anatoly Sobchak alipochaguliwa kuwa Meya wa jiji la St. Petersberg. Dmitry Medvedev ndiye alikuwa meneja wa kampeni wa Sobchak . Baada ya kuapishwa Meya Sobchak aliwachukua Medvedev na Putin kuwa washauri, Putin akiwa mshauri (adviser) wa Meya na Medved akiwa mshauri (Consultant) kwenye kamati ya mambo ya nje katika halmashauri ya jiji la St. Petersberg. Baadaye Putin alipanda cheo hadi kuwa naibu Mwenyekiti wa hamshauri ya jiji la St. Petersberg.
Mwezi June 1996 baada ya Meya Sobchak kushindwa uchaguzi, Vladmir Putin alihamishiwa kwenye ofisi ya Rais jijini Moscow wakati wa utawala wa Rais Boris Yeltsin na Medvedev alirudi kufundisha Sheria katika chuo kikuu cha St. Petersberg.
Rais wa Urusi Vladmir Putin (kulia) na Waziri wake mkuu
Dmitry Medvedev
|
November 1999 kwa ushawishi wa Putin, Medvedev alihamishiwa jijini Moscow na kuteuliwa kuwa naibu mnadhimu mkuu (Deputy Chief of Staff) katika ofisi ya Rais (the Russian Presidential Administration) miezi miwili baada ya Vladmir Putin kuteuliwa na Rais Boris Yeltsin kuwa Waziri Mkuu wa Urusi.
Tarehe 31 December 1999, Rais Boris Yeltsin ambaye alikuwa anasumbuliwa na maradhi alijiuzulu ghafla na kwa mujibu wa katiba ya Urusi, Waziri Mkuu Vladmir Putin alikaimu nafasi ya Urais ( Acting President) hadi Mwezi May mwaka 2000. Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Urais, Vladmir Putin alimteua Dmitry Medvedev kuwa Meneja wake wa kampeni. Putin alishinda uchaguzi kwa kupata 53% ya kura.
Mwaka 2003 Vladmir Putin alimpandisha cheo Medvedev kutoka Naibu Mnadhimu mkuu hadi kuwa Mnadhimu mkuu wa Ikulu ya Urusi (Kremlin). November 2005, Putin alimteua Medvedev kuwa naibu wa kwanza wa Waziri mkuu wa Urusi ambaye majukumu yake yalikuwa ni kushughulikia miradi ambayo ni kipaumbele cha taifa (National Priority Projects).
Mwaka 2008 wakati Putin alipomaliza mihula miwili ya uongozi, ambapo kwa Mujibu wa katiba hakuruhusiwa kuendelea na Muhula wa tatu mfululizo, Chama cha United Russia kikiungwa mkono na vyama vingine vitatu kilimteua Dmitry Medvedev kuwa mgombea Urais na Putin alitangaza kuunga mkono uteuzi wa Medvedev. Mara tu baada ya kuapishwa kuwa Rais, Dmitry Medvedev alimteua Vladimir Putin kuwa Waziri wake mkuu nafasi aliyoitumikia kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012. Kuanzia hapo ndipo vigogo hawa walipoanza kupokezana madaraka ya chama na Serikali kwa zamu mpaka sasa hivi.
UTAWALA PACHA (TANDEM RULE)
Putin mwenye umri wa miaka 65 ana madaraka yote kama rais, lakini Medvedev mwenye umri wa miaka 52 ni waziri mkuu na kiongozi wa chama tawala cha United Russia, chama kikubwa chenye wabunge wengi bungeni kwa hivyo anaongoza chombo cha msingi cha madaraka kinachompa uwezo wa kuwa mtoaji maamuzi mkubwa.
Rais Vladmir Putin na Waziri Mkuu Dmitry Medvedev
wakifanya mazoezi ya viungo
|
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana
Napatikana kupitia simu namba
+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com
No comments:
Post a Comment