Sunday, November 19, 2017

MKATABA WA NYUKLIA WA IRAN (IRAN NUCLEAR DEAL-JCPOA) NI KITISHO KWA ISRAEL NA SAUDI ARABIA

Na Masudi Rugombana

Iran ilianza harakati za kumiliki technolojia ya Nyuklia miaka ya 1970 kwa kusaidiwa na Marekan wakati ikiwa chini ya utawala wa Mohammad Reza Pahlav (Shah) ambapo kinu cha kwanza cha Nyuklia cha Bushehr (Bushehr Nuclear Plant) kilijengwa na makampuni ya Kijerumani. Mpango huo ulisimama baada ya mapinduzi ya kiislamu yaliyoongozwa na Sayyid Ruhollah Khomein mwaka 1979 ambapo ilishuhudiwa baadhi ya wataalam wa Nyuklia wa Iran wakiikimbia nchi baada ya mapinduzi hayo.


Iran Ilianzisha tena mpango wa nyuklia miaka ya 1980 kwa kusaidiwa na Pakistan. Mwaka 2003 ilibainika kuwa kwa takribani miaka 18 Iran ilikuwa ikificha shughuli zake za nyuklia kinyume na mkataba wa kimataifa iliosaini mwaka 1968 unaozuia kuenea kwa silaha za nyuklia ( Treaty on the Non-Proliferation of Nuclear Weapons-NPT).
Katika kipindi hicho Iran ilijenga kwa Siri vinu viwili vya Nyuklia, kile cha maji Mazito cha Arak (Arak heavy water facility) na cha urutubishaji uranium cha Natanz (Natanz Uranium enrichment reactor).

Kituo cha uzalishaji maji mazito cha Arak
(Arak heavy water facility)


Mwezi February mwaka 2003 Rais Muhammad Khatami ilithibitisha uwepo wa vinu hivyo viwili na kusisitiza kuwa Iran ilikuwa inarutubisha kiwango kidogo cha Uranium kwa ajili ya kuzalisha umeme hatua iliyopelekea Wakaguzi kutoka Wakala wa Kimataifa wa nguvu za atomic (IAEA) kutembelea kinu cha Nyuklia cha Natanz. Mwezi May mwaka 2003 serikali ya Iran iliwaruhusu wakaguzi kutoka IAEA kutembelea Kampuni ya umeme ya Kalaye kwa masharti ya kutochukua sampuli zilizokuwa zikitumika kuzalisha umeme.

Hali hii ilipelekea Wakala wa Kimataifa wa nguvu za atomic katika ripoti yake ya June 2003 kulijulisha baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwa Iran imeshindwa kufikia viwango vilivyoainishwa katika mkataba wa NPT hivyo kupelekea kuanzishwa kwa mazungumzo ya kidiplomasia baina ya Iran na nchi tatu za umoja wa Ulaya (The EU3) ambazo ni Ufaransa, Ujerumani na Uingereza na kufikia azimio kuwa Iran imekubali kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa nguvu za Atomic (IAEA).

Mwezi November Mwaka 2004 Iran na Jumuiya ya Ulaya zilifikia makubaliano jijini Paris (Paris accord) kuwa Iran Ifunge vinu vyake vya Natanz na Arak, isimamishe kurutubisha Uranium ikiwa ni pamoja na kutengeneza, kufunga, kufanya majaribio na kuendesha cenfrifuges wakati mazungumzo yakiendelea ili kufikia makubaliano ya muda mrefu.

Mwezi August 2005 Kiongozi mwenye msimamo mkali ambaye aliwahi kuwa meya wa Jiji la Tehran Mahmoud Ahmednejad alichaguliwa kuwa Rais wa Iran. Ahmednejad Aliwatuhumu kwa makosa ya Uhaini wajumbe wa Iran walioshiriki kwenye majadiliano ya mkataba wa Paris. Miezi miwili baadae Rais Mahmoud Ahmednejad aliiondoa Iran kwenye Mkataba wa Paris na kuvunja mazungumzo yaliyokuwa na lengo la kufikia makubaliano ya muda mrefu. Iran iliujulisha wakala wa kimataifa ya nguvu za atomic kuwa inaanzisha upya urutubishaji wa Uranium kwenye kituo chake cha Esfahan. Mnamo mwezi February mwaka 2006 Iran ilifungua kinu chake cha Natanz na mwezi June 2006 ilifungua kinu chake kingine cha Arak na hivyo kuendelea kurutubisha uranium kwa spidi ya kiwango cha juu.

Rais Mahmoud Ahmednejad akikagua kituo cha Nyuklia
cha Natanz.


Mwaka 2009 mwezi September, Rais Barack Obama aliishutumu Iran kwa kujenga kwa siri kinu kikubwa cha chini ya ardhi cha kurutubisha Uranium kwenye eneo la Fordow karibu na mji wa Qom. Kitendo cha Iran kujenga kinu kipya cha Nyuklia bila kuifahamisha IAEA  kilisababisha hofu kubwa katika jumuiya ya kimataifa iliyopelekea Israel kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

Mkurugenzi mkuu wa IAEA Dr. Mohammed El Baradei ilionya kuwa hatua za kijeshi dhidi  ya Iran zitasababisha janga kubwa na hivyo kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kukaa mezani na Iran kwa ajili ya kutafuta suluhisho kwa njia ya amani.

Mwezi March 2013 Marekani ilianzisha mazungumzo ya siri na maofisa wa Iran huko Oman yalioongozwa na Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani William Joseph Burns na mshauri wa masuala ya usalama wa Taifa wa Makamu wa Rais wa Marekani Jacob Jeremiah Sullivan (Jake Sullivan) ambapo kwa upande wa Iran yaliongozwa na Mwana Diplomasia nguli Ally Asghar Khaji naibu Waziri wa mambo ya nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya Ulaya na Amerika. Katika mazungumzo hayo hapakuwa na muafaka uliofikiwa.

Mwaka 2013 mwezi June Mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani Hassan Rouhan alichaguliwa kuwa rais wa Iran. Siku tatu baada ya kuchaguliwa Rais Hassan Rouhani alitoa wito wa kufufuliwa mazungumzo thabiti ya kumaliza mgogoro wa nyuklia kati ya Iran na mataifa ya Magharibi yatakayoshirikisha nchi 5 wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na Ujerumani (P5+1).

September 2013, Rais wa Marekani Barack Obama alizungumza kwa njia ya Simu na Rais Hassan Rouhan yakiwa ni mazungumzo ya kwanza kwa viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hizo tangu yalipotokea Mapinduzi matukufu ya Kiislamu mwaka 1979. Mazungumzo hayo yalifuatiwa na mkutano kati ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Mwenzake wa Iran Muhammad Javad Zarif hivyo kuashiria kuwa Madola hayo mawili yameamua kuanzisha ushirikiano wa wazi. Huo ndio ukawa mwanzo wa kuanzishwa kwa Mazungumzo ya Nyuklia ya Iran yaliyopelekea kusainiwa kwa mkataba wa JCPOA.

JCPOA:
Mkataba wa nyuklia wa Iran ambao unajulikana kama  (JCPOA-The Joint Comprehensive Plan of Action- kwa Kiswahili Mpango wa kina wa utekelezaji wa pamoja) ni makubaliano ya kimataifa kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran yaliyofikiwa huko Vienna nchini Switzeland mnamo 14 July 2015. Makubaliano hayo yalifikiwa kati ya Iran na nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa ambazo ni China, Ufaransa, Urusi, Marekani na Uingereza  jumlisha na Ujerumani au kwa kifupi P5+1.

Wajumbe wa P5+1 na Iran wakiwa Vienna Uswiz kwenye
mazungumzo ya kutanzua mzozo wa nyuklia wa Iran.Kutoka
kushoto ni Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry, Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond, Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius, Mkuu wa sera za nje wa Jumuiya ya Ulaya Bi Catherine Ashton na Waziri wa Mambo ya nje wa China Wang Yi.



Mkataba huo uliosainiwa baada ya majadiliano ya kina yaliyodumu kwa miaka miwili kwa lengo la kuzuia Iran kutengeneza silaha za Nyuklia.
Chini ya makubaliano hayo ya JCPOA, Iran alikubali kuondoa akiba yake yake ya uranium iliyokuwa tayari imerutubushwa kwa kiwango cha kati (medium-enriched uranium), kuondoa hadi asilimia 98 ya akiba ya uranium iliyokuwa imerutubishwa kwa kiwango cha chini ( low-enriched uranium ) na kupunguza kwa karibu theluthi mbili ya idadi ya centrifuges kwa miaka kumi na tatu.

Mkataba unairuhusu Iran kutumia maji mazito kutoka kwenye kinu chake cha Arak kwa ajili ya shughuli za viwanda na utafiti na kuuza ziada inayobaki ya maji mazito kwenye soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kwa miaka kumi na tano ijayo Iran itakuwa ikirutubisha uranium hadi asilimia 3.67 tu. Pia Iran ilikubali kutojenga vituo vyovyote vipya vya maji mazito (heavy-water facilities ) katika kipindi  hicho cha miaka kumi na tano. Mkataba unataka katika kipindi cha miaka kumi urutubishaji wa Uranium ufanyike katika kituo kimoja kwa kutumia idadi ya first generation centrifuges 5,060 tu badala ya 19,060 ambapo Iran inatakiwa kutenganisha (disconnect) centrifuges 14000, pia vituo vingine vitabadilishwa matumizi ili kuepuka urutubishaji wa iranium.

Kufuatilia na kuhakikisha kuwa Iran inatekeleza makubaliano, Mkataba unataka wakaguzi kutoka Wakala wa kimataifa wa nguvu za atomic (IAEA) ambao idadi yao itaongezwa kutoka 50 hadi 150 waruhusiwe kufika mara kwa mara kwenye vituo vyote vya nyuklia vya Iran kwa ajili ya ukaguzi kuanzia kwenye viwanda vya Uranium hadi kwenye ununuzi wa technolojia zinazohusiana na nyuklia.

Mkataba unairuhusu IAEA kufunga vifaa vya kisasa (sophisticated monitoring technology) kama fibre-optic seal, survaillance camera, radiation-resistant Cameras na infrared satelite imagery ili kufuatilia kwa karibu zaidi nyendo za Iran katika vituo vyake vya Nyuklia. Kama wakaguzi watatilia shaka kuwa Iran inaendeleza program ya Nyuklia kwenye maeneo ambayo hayajatangazwa (non-declared sites) wataomba ruhusa ya kuingia kwenye hayo maeneo ambapo mkataba unataka wakaguzi kutoka wakala wa Kimataifa wa nguvu za atomic watakao husika kuingia katika maeneo hayo watoke kwenye nchi ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia na Iran.

VIKWAZO
Mkataba unaeleza kwamba IAEA itakapothibitisha kuwa Iran imetekeleza makubaliano , vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani, Umoja wa Mataifa (UN) na Jumuiya ya Ulaya (EU) vitaanza kuondolewa ndani ya miezi sita tokea kusainiwa kwa mkataba na ndani ya miaka nane tokea kusainiwa kwa makubaliano, vikwazo dhidi ya makampuni ya Iran, makombora ya kibalistiki, taasisi na watu binafsi vilivyowekwa na Jumuiya ya Ulaya vitasitishwa . Hata hivyo vikwazo visivyohusiana na masuala la Nyuklia vilivyowekwa na Marekani kama vile ukiukwaji wa haki za binadamu, makombora na kufadhili ugaidi havitaathiriwa na makubaliano haya ya JCPOA.

NANI AMEFAIDIKA
Marekani na mataifa ya Ulaya wamefanikiwa kuizuia Iran  kutengeneza silaha za nyuklia kwa muda wa miaka 15. Na baada ya kumalizika kwa mkataba itachukua mwaka mmoja kwa Iran kurudisha program yake ya nyuklia katika kiwango ilichofikia kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa JCPOA.

Makubaliano haya yamesaidia kwa kiasi kikubwa kulifanya eneo la Mashariki ya kati na Dunia kwa ujumla kuwa salama zaidi kutokana na kitisho cha kusambaa kwa silaha za nyuklia kwani Marekani na Washirika wake walikuwa na wasiwasi kuwa ikiwa Iran ingefanikiwa kumiliki zana za kinyuklia kungekuwa na uwezekano mkubwa kwa zana hizo kuingia mikononi mwa makundi ya Hizbullah na Ansarullah Movement (Houthis) ambayo Marekani na Washirika zake inayachukulia kama makundi ya kigaidi.

Kwa upande wa Iran, mkataba huu umeiwezesha kujiondoa kwenye kitanzi cha kutengwa na jumuiya ya kimataifa, kuiwezesha kufanya biashara na mataifa makubwa hivyo kuongeza mauzo ya mafuta nje ya nchi. Iran pia imeweza kupata mapato ya dola bilion 30 za Kimarekani kati ya dola bilioni 100 ambazo ni sehemu ya fedha zake zilizokuwa zimezuiwa kwenye mabenki mbalimbali duniani. Kwa muda mfupi toka kusainiwa kwa mkataba Iran imeweza kusaini mikataba ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 60. Pia mkataba umefungua njia kwa Iran kuweza kununua vifaa na technolojia za kisasa kama ndege za abiria, mitambo na vipuri  kutoka kwenye makampuni ya kigeni kama vile Boeng, Airbus n.k.

Pia mkataba umeiwezesha Iran kuongeza mapato zaidi kupitia mpango wake wa kuzalisha maji mazito kwenye kituo chake cha Nyuklia cha Arak. Mwaka 2016 Marekani ilitiliana saini mkataba na Iran ambapo Iran iliiuzia Marekani tani 32 za maji mazito yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 8.6 yatakayotumika kwa ajili ya viwanda na utafiti. Urusi pia mwezi April 2016 ilisaini makubaliano na Iran ambapo Iran iliiuzia Urusi tani 38 za maji mazito (heavy water) yatakayotumika katika viwanda vyake vya zana za kinyuklia pamoja na shughuli za utafiti.

HOFU YA ISRAEL NA SAUDI ARABIA.
Saudi Arabia na Israel ni mataifa ambayo hayajaridhishwa kabisa na kufikiwa kwa makubaliano haya ya JCPOA. Mataifa haya yanauona mkataba huu kama ni kitisho kikubwa kwa usalama wao na eneo zima la mashariki ya kati. Waziri mkuu wa Israel Binyamini Netanyahu aliwahi kuyaita makubaliano hayo kuwa ni mabaya (bad deal)

Israel na Saudi Arabia zinalalamika kwamba Mkataba umeshindwa kuibana Iran kuachana na mpango wa nyuklia badala yake unaibana Iran kusimamisha tu mpango wake wa  nyuklia na mara tu mkataba utakapofikia kikomo ndani ya muda mfupi Iran itakuwa na uwezo wa kurudisha program yake kama awali na kuweza kuunda bomu la nyuklia.

Programu ya Makombora ya Kibalistiki ya Iran inayotishia usalama wa Israel na Saudi Arabia.

Israel na Saudi Arabia zinalalamikia hatua ya Iran kuruhusiwa kuchukua pesa zake ambazo ni mabilioni ya dola yaliyokuwa yamezuiliwa kutaiongezea uwezo mkubwa zaidi wa kuendeleza programu yake ya kutengeneza makombora ya kibalistiki ya masafa marefu ambayo ni kitisho kikubwa kwa usalama wao, kufadhili makundi ya Hizbullah, Hamas na Houthis makundi ambayo nchi hizo zinayachukulia kama makundi ya kigaidi na kitisho kikuwa kwa usalama wao.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com



No comments:

Post a Comment