Doha.
Imebainika kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulikula njama ya kuishambulia kijeshi Qatar, kwa kutumia maelfu ya mamluki waliopata mafunzo ya kijeshi kutoka kampuni moja ya Marekani.
Abdullah bin Hamad al-Attiyah, Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar ameliambia gazeti la Uhispania la ABC kuwa, Umoja wa falme za Kiarabu (UAE) ilikodisha kampuni binafsi ya usalama ya Marekani iliyojulikana kama "Blackwater-linked" ambayo kwa sasa inafahamika kama Academi, kwa lengo la kuwapa mafunzo mamluki ambao wangetumwa katika operesheni ya kijeshi ya kuivamia Qatar.
Bin Hamad al-Attiyah amesema lengo la Umoja wa falme za Kiarabu kuwapa mamluki hao mafunzo ya kijeshi lilikuwa ni kuivamia kijeshi nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi na kumuondoa mamlakani kwa nguvu Amir wake Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani lakini ilishindwa kupata uungaji mkono wa Marekani.
Duru za habari zimeliambia gazeti la ABC kuwa, mamluki hao wa Umoja wa falme za kiarabu wamekuwa wakipokea mafunzo hayo ya kijeshi katika kambi ya Liwa Oasis mjini Abu Dhabi.
Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu (UAE), Bahrain na Misri tarehe 5 Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi nyingine za Ghuba.
Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar vikwazo vya kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima.
Qatar imekanusha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Ufalme wa Saudia.
No comments:
Post a Comment