Monday, May 29, 2017

KAMPENI ZA UCHAGUZI KENYA ZAANZA RASMI

Kampeni zimeanza rasmi nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 8 mwezi wa nane mwaka huu.

Wakati uo huo Tume ya Uchaguzi imeanza zoezi la siku mbili kuwaidhinisha wagombea urais.

Rais Uhuru Kenyata ambaye pia ni mgombea wa
chama cha Jubelee akisalimiana na
Rais Donard Trump wa Marekani kwenye mkutano wa nchi za G7.
Mgombea wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga tayari ameidhinishwa pamoja na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka na kuzindua kampeni zake rasmi jijini Nairobi.


Akiwahutubia wafuasi wake, Odinga amesema ikiwa atashinda urais, atapambana na ufisiadi na wale wenye doa hawataruhisiwa kufanya kazi katika serikali yake.

Aidha amesema kuwa serikali yake itahakikisha kuwa inashusha gharama ya maisha kwa muda wa siku 90 watakazokuwa madarakani lakini pia kupunguza kodi ya nyumba.

Rais Uhuru Kenyatta anayewania kwa muhula wa pili, anatarajiwa kuidhinishwa leo na Tume ya Uchaguzi na baadae kuzindua kampeni zake katika uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi.

Mbali na wagombea hao wawili wakuu wanaopewa nafasi kubwa kupambana katika kinyanganyiro hicho, wagombea wengine nane wamejitosa uwanjani wengi wakiwa wagombea binafsi.

Maswala muhimu yatakayojiri katika kampeni:-
Rais Uhuru Kenyatta anasema anataka kuendeleza rekodi anayosema ni ya maendeleo nchini humo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli ya kisasa na mradi wa umeme kuwafikia idadi kubwa ya wakenya hadi kijijini.

Kenyatta anajivunia ujenzi wa reli ya kisasa atakayoizindua wiki ijayo kutoka Mombasa hadi jiji kuu Nairobi. Mradi huu unatarajiwa kurahihisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya miji hiyo miwili.
Rais Kenyatta na mgombea mwenza wake ambaye ni Naibu rais William Ruto, wanatarajiwa kutumia mafanikio haya kujitafutia uungwaji mkono.

Hata hivyo, upinzani umeendelea kuishutumu serikali ya rais Uhuru Kenyatta kwa kujihusisha na ufisadi na kukopa fedha kupita kisiasi kutoka nje ya nchi. Utovu wa usalama pia ni suala ambalo upinzani unasema serikali ya sasa imeshindwa kushughulikia.

Kundi la Al Shabab limekuwa likiwashambulia raia wa kawaida na maafisa wa usalama kama polisi na wanajeshi, tangu kuingia madarakani mwaka 2013.
Kupanda kwa gharama za maisha hasa siku za hivi karibuni uhaba wa unga wa mahindi na sukari.
Serikali imelazimika kuingilia kati na kuamua kununua mahindi kutoka nchini Mexico ili kuwawezesha wananchi kupata unga kwa bei nafuu.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema ushindani mkubwa wa kisiasa unatarajiwa kati ya rais Kenyatta na Odinga. Siasa za Kenya bado hazijaegemea sera lakini zinaendelea kuegemea ukabila na ukanda.

No comments:

Post a Comment