Friday, May 12, 2017

Rais Sudani Kusini amfuta kazi mkuu wa majeshi

Juba.

Habari zinasema kuwa, Rais Salva Kiir, amechukua hatua ya kumfuta kazi Paul Malong Awan, kufuatia majenerali wengi wa ngazi ya juu jeshini kujiuzulu kutokana na kuwepo ubaguzi na jinai nyingi za kivita zinazofanywa na jeshi la Sudan Kusini.

Rais Salva Kiir akimpandisha cheo mkuu mpya wa Majeshi
James Ajongo

 Habari zinasema kuwa, Rais Kiir amemteua James Ajongo kuchukua nafasi ya Malong Awan kwa ajili ya kusimamia shughuli za jeshi la taifa hilo changa zaidi barani Afrika. Inafaa kuashiria kuwa, mbali na serikali ya Juba kupambana na wanamgambo wa upinzani, lakini pia jeshi la serikali nalo linakabiliwa na mgogoro wa ndani, ambapo makamanda kadhaa jeshini wamekuwa wakitangaza kujiuzulu nyadhifa zao.

Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko mwezi Disemba mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwamba alikula njama za kutaka kumpindua. Katika machafuko hayo, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Licha ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita mwezi Agosti mwaka 2015, lakini bado machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea nchini Sudan Kusini.

No comments:

Post a Comment