Thursday, July 28, 2022

XINJIANG: KICHAKA CHA MATAIFA YA MAGHARIBI KATIKA HARAKATI ZA KUIDHOOFISHA CHINA.

 Na Masudi Rugombana   


Xinjiang ni mkoa mkubwa kuliko yote nchini China. Mkoa huu unaopatikana kaskazini magharibi ya China una jumla ya kilometa za mraba milioni moja, laki sita na elfu sitini na tano (1.665 million km²). Kwa ukubwa wa eneo mkoa huu umeizidi kidogo nchi ya Iran. Mkoa huu unajulikana rasmi kama XUAR yaani Mkoa unaojiendesha wa Wauighur wa Xinjiang ( Xinjiang Uighur Autonomous Region ) ni eneo lenye utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo Mafuta, gesi asilia, makaa ya mawe na dhahabu unapakana na nchi za Mongolia, Russia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Afghanistan, India na Pakistan. 



Mbali na utajiri wa maliasili, mkoa huu wenye utajiri mkubwa wa kitamaduni wenye  idadi ya makabila yenye asili, lugha, imani za kidini, mila na tabia ya tofauti umekuwa na mawasiliano ya karibu ya kiuchumi na kiutamaduni na nchi jirani inazopakana nazo. Mkoa una jumla ya watu milioni 25, ambapo watu milioni 12 sawa na asilimia 44.96 ni wa jamii ya Uighur. Wauighur, ni jamii ya Kituruki yenye uhusiano wa kitamaduni na eneo la Mashariki na Asia ya Kati. Watu wa jamii ya Han huko Xinjiang ni asilimia 42.24 na asilimia 12.80 ni watu wa jamii za Kazakh, Kyrygz, Hui, Mongol , Tibet, Xibe, Tajik, Ozbek, Manchu, Daur, Tatar na Russians (Warusi).  Lugha rasmi  zinazozungumzwa mkoani Xinjiang ni Uighur na Mandarin. Waislam ni zaidi ya nusu ya wakazi wote wa Xinjiang.  Mji mkuu wa mkoa ni Ürümqi.


China imekuwa ikishutumiwa na mataifa ya Ulaya Magharibi  kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo kufanya   mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa Uyghur sambamba na  makabila mengine yenye idadi kubwa ya watu wanaofuata imani ya dini ya Kiislam hasa katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Xinjiang.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanailaumu China kwa kuwazuilia zaidi ya Wauyghur milioni moja kinyume na matakwa yao katika makambi ya mateso ( Concentration Camp), hata hivyo serikali ya China inasema kuwa hayo sio makambi ya mateso bali  ni vituo vya mafunzo (Education training centers) vyenye lengo la kukomesha itikadi kali za kidini na kuwapa watu ujuzi mpya. 


Mapema katika karne ya 20, Marekani na nchi nyingine za Ulaya Magharibi zilianzisha juhudi za kuunga mkono harakati za kujitenga kwa mkoa wa Xinjiang ili kuunda Taifa litakalojulikana kama Turkestan Mashariki ( East Turkestan), juhudi hizo zilizokwenda sambamba na kufadhili matendo ya kigaidi huko Xinjiang kwa lengo la kuiyumbisha China na kudhibiti kasi yake ya Maendeleo.


Mnamo Mwezi August 2018 akizungumza katika taasisi ya Ron Paul (Ron Paul Institute) kanali mstaafu Lawrence Wilkerson, mkuu wa zamani wa wafanyakazi (Former Chief of staff) katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wakati huo ikiongozwa na General Mstaafu Collin Powell, alisema kwamba mojawapo ya sababu za Marekani kuwepo nchini Afghanistan ni kwa sababu kuna watu wa jamii ya Uighur huko Xinjiang wapatao milioni 20, kwa hivyo CIA ingetaka kuivuruga China kupitia harakati za WaUighur na kwamba hiyo ndiyo ingekuwa njia bora ya kufanya ili kuzusha machafuko baina ya jamii za WaUighur na Han na kwamba Marekani ingewasaidia WaUighur kuwatimua watu wa jamii ya Han na kuwaondoa katoka mkoa wa Xinjiang. 


Kwa miaka mingi, kumeibuka idadi ya taasisi zinazoipinga China ikiwa ni pamoja na kuanzishwa makundi yenye itikadi kali yanayopigania kuanzishwa kwa taifa la  Turkistan Mashariki kupitia kile kinahoitwa "uhuru" wa Xinjiang. Miongoni mwa harakati hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa bunge la Uighur na Serikali ya Turkistan Mashariki, vyote vikifanya kazi uhamishoni kwa kufadhiliwa na Marekani na Uturuki. Kwa mujibu wa vyanzo vya kiintelijensia vya China,  mwaka 2004,  Marekani ilitoa dola  milioni 8.76 kwa makundi ya watu wanaoishi nje ya Uighur wanaofanya kampeni dhidi ya China huko Xinjiang.


Ufadhili huo kutoka Marekani umesababisha kuenea haraka kwa fikra za itikadi kali za Kiislam huko Xinjiang na hivyo kupelekea Magaidi kutoka katika medani za vita nchini Afghanistan, Pakistan na Syria kumiminika kwa wingi mkoani Xinjiang. Baadhi ya makundi ya kigaidi yenye nguvu yaliendesha kampeni kali kushambulia raia wa China kupitia vuguvugu la Kiislamu la Turkestan Mashariki (East Turkestan Islamic Movement (ETIM) kati ya mwaka 1997 na 2014  yaliyogharimu maisha ya zaidi ya raia 1,000. Ikumbukwe kwamba kundi la Kiislam la ETIM lina uhusiano wa karibu na Mtandao wa Alqaeda unaoongozwa na Dr. Ayman al Zawahir. 


Katika kukabiliana na tishio la mashambulizi, serikali ya China imechukuwa hatua muhimu kuhakikisha utulivu na amani vinapatikana ili kuwezesha watu wa imani tofauti kuishi kwa pamoja katika mkoa wa Xinjiang. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kupambana kutokomeza makundi ya itikadi kali za kidini na kuweka sheria zinazolinda haki na uhuru wa kufanya ibada kwa watu wa imani zote. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha vyuo vya mafunzo ambapo makundi ya vijana wanaokamatwa kutokana na kuhusika na vurugu za kidini na kikabila hupelekwa kupewa ujuzi pamoja na kufundishwa uzalendo wa Kichina. 


Kufuatia hatua kali za kukabiliana na makundi ya itikadi kali za kidini zilizochukuliwa na serikali ya China, sasa ni miaka minne mfululizo hapajawahi kutokea shambulizi lolote la kigaidi huko Xinjiang. China inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha huduma za kijamii katika Uighur ikiwemo ukarabati wa misikiti. 


Xinjiang kuna misikiti elfu ishirini na nne, Mingi katika hiyo imejengwa miaka ya 1980 na 1990, na haikujengwa kwa Ubora unaotakiwa. Kutokana na ukuaji wa miji na vijiji kuna baadhi ya misikiti inawawia vigumu Waislamu kufanya Ibada kutokana na uchavu na kuna baadhi ya misikiti haifikiki kirahisi. Kwa hivyo Serikali ya China inafanya mambo matatu kwa ruhusa ya Waislamu wenyewe kupitia Serikali zao za mitaa. 


1. Kubomoa misikiti inayohatarisha Usalama na kujenga misikiti mipya, imara na ya kisasa.

2.Kukarabati Misikiti ya zamani 

3. Kuhamisha misikiti iliyojengwa mahala ambapo ni vigumu kufikika kwa kujenga sehemu ambayo ni kubwa zaidi na rahisi kufikika sambamba na upanuzi wa misikiti yenye maeneo madogo ya kufanyia ibada. 


Kinachofanywa na vyombo vya habari vya Ulaya Magharibi ni kupiga picha misikiti mibovu inapovunjwa kwa ajili ya ukarabati na kisha kuitangazia Dunia kuwa China inavunja misikiti huko Xinjiang. Lengo la propaganda hizo ni kuichafua China katika Ulimwengu wa Kiislamu. Propaganda ambazo zimeshindwa kuyashawishi Mataifa mengi ya Kiislam ikiwemo Umoja wa Ushirikiano wa nchi za Kiislamu (OIC) kuilaani China. 


Suala la Waislamu kuzuiwa kusali, kuzuiwa kutumia majina ya Kiarabu, kuzuiwa kufunga saumu ya Ramadhani na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe ni mojawapo ya propaganda chafu zinazoenezwa na vyombo vya habari vya magharibi dhidi ya China. Ukweli ni kwamba Uhuru wa kuabudu mkoani Xinjiang ulikuwa mashakani kipindi ambacho makundi ya Itikadi kali za kidini yalipoimarisha harakati zao, ilikuwa ni vigumu kwa Waislamu kufanya ibada hadharani kutokana na tishio la kushambuliwa, pia viongozi wengi wa Kiislamu waliopingana na makundi ya itikadi kali walilengwa na kuuawa. 


Mara baada ya Serikali ya China kukomesha harakati za makundi ya Kiislam yenye itikadi kali, katika kipindi cha miaka minne mfululizo Waislamu wamekuwa wakifanya ibada misikitini bila hofu sambamba na kushiriki ibada nyingine kama hija na funga ya Ramadhan. Kati ya mwaka 1996 hadi 2019, Jumuiya ya Kiislamu ya China  kwa kushirikiana na Serikali imeweza kugharamia hija kwa Waislamu elfu hamsini wa Xinjiang kwa safari za ndege za kukodi kwenda Makka, na pia kutoa huduma za tafsiri na matibabu. 


China ni Taifa linaloongozwa na serikali isiyofuata imani yeyote ya kidini (Secular State) ikiwa na Jumla ya watu Bilioni moja na milioni mia nne kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020. Waislamu wanakadiriwa kufikia milioni 28 sawa na asilimia 1.73 wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya Hui wakifuatiwa na watu kutoka jamii ya Uighur. Hata hivyo kwa takwimu zisizo rasmi China inakadiriwa kuwa na idadi ya Waislamu milioni 150. Asilimia 74.5 ya Wachina ni Wapagani, Mabudha ni asilimia 18.3 na Wakristo ni asilimia 5.1.


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.


© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇


Email: masudirugombana@gmail.comSimu: 


0743 184 044

Monday, June 27, 2022

HATIMA YA UKRAINE IPO MIKONONI MWA URUSI.

Na Masudi Rugombana  

Tarehe 21 February 2022 Rais Vladmir Putin wa Urusi alitangaza kutambua uhuru wa eneo la Donbass, Jimbo la Mashariki ya Ukraine linaloundwa na mikoa miwili ya Luhansky na Donetsky, mikoa inayokaliwa na idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi. Mikoa hii ilijitangazia uhuru kutoka Ukraine mwaka 2014 kutokana na kura ya maoni iliyoongozwa na makundi ya wapiganaji kufuatia mgogoro wa kisiasa uliozusha maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Rais Viktor Yanukovych kiongozi aliyeegemea zaidi upande wa Urusi hatua ambayo Rais Vladmir Putin aliifananisha na mapinduzi ya kijeshi. Kuondolewa madarakani kwa Victor Yanukovych kulifuatiwa na maandamano makubwa ya makundi ya watu wanaounga mkono Urusi huko Mashariki na kusini mwa Ukraine ambapo mkoa wa Crimea wenye idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi uliitisha kura ya maoni iliyopelekea wakazi wake kuchagua kujiunga na Urusi hivyo kuipa uhalali Urusi kuitwaa Crimea na kuifanya eneo lake. 

Tangazo la Putin kutambua uhuru wa Donbass lilifuatiwa na uingiliaji kati kijeshi tarehe 24 February 2022  katika Operesheni inayokusudia kuvunja nguvu za kijeshi za Ukraine na kuondoa matendo ya kikatili yanayofanywa na wapiganaji wa jeshi la Ukraine wenye siasa kali za kizalendo zilizogubikwa na fikra za kinazi ( Operation demilitalize and denazify). Kiuhalisia, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine una malengo mapana zaidi ya hicho kinachoitwa ukombozi wa Donbass. Ni uvamizi unachagizwa na mambo mengi ya kiusalama na kimaslahi yanayohusu Urusi zaidi ya kusudio la kuikomboa Donbass.  

Baada ya umoja wa kisoviet kuanguka mwaka 1990, Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) ulijitanua kuelekea upande wa Mashariki na hatimaye kuyachukua mataifa ya eneo la Baltic, Jamhuri za Lithuania, Latvia na Estonia ambazo zilikuwa sehemu ya umoja wa Kisovieti (Soviet Union ) na kupeleka umoja huo wa kijeshi kujisogeza karibu na  Moscow kwa kupakana moja kwa moja Urusi. Mwaka 2008 NATO iliweka wazi mipango yake ya kutaka kuisajili Ukraine. Ikumbukwe kuwa  Rais Vladmir Putin aliwahi kusema kwamba kusambaratika kwa umoja wa Kisovieti lilikuwa ni janga kubwa katika karne ya ishirini lilipelekea Urusi kuporwa haki yake kama mojawapo ya Mataifa yenye nguvu kubwa Duniani. Putin ametumia miaka 22 madarakani kujenga upya jeshi la Urusi kwa lengo la kurejesha nguvu yake ya kiushawishi kwenye siasa, ulinzi pamoja na mahusiano ya kimataifa  (Geopolitical clout)

Putin alishaweka wazi kuwa kujitanua kwa NATO kuelekea Mashariki sambamba na mkakati wake wa kuisajili Ukraine kwamba ni kitisho kisichovumilika dhidi ya Urusi, akilaumu uwepo wa vikosi vya Marekani na makombora yao kibalistic  ya masafa Marefu nchini Ukraine, huku akisisitiza kuwa Ukraine ni sehemu muhimu ya Urusi kisiasa na kiutamaduni.Hivyo basi kutokana na tishio la NATO, Urusi iliamua kuongeza nguvu za kijeshi kuelekea upande wa Magharibi kwenye mpaka wake na Ukraine kwa lengo moja tu ambalo ni kufanya shambulizi (Pre-emptive strike) dhidi ya Ukraine kwa lengo la kujihami dhidi ya kitisho cha NATO. Katika jithada za kuepusha vita, NATO na Ukraine walitaka Urusi kuacha kujijenga kijeshi kwenye mpaka wake na Ukraine hivyo kufungua meza ya majadiliano baina ya pande mbili. Urusi ilitoa masharti makuu matatu ili ombi hilo la NATO liweze kutekelezwa. 

1. Ipewe hakikisho kwamba Ukraine haitajiunga na NATO.

2. NATO iondoe vikosi vyake katika nchi za Ulaya Mashariki.

3. Jeshi la Ukraine Kusitisha mapigano kwenye eneo la  Donbass kwa mujibu wa makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015  ambayo yaliweka masharti ya kuondolewa kwa silaha nzito kutoka kwenye uwanja wa vita, kuachiliwa kwa wafungwa wa pande zote mbili, na marekebisho ya katiba nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na utoaji wa uhuru kwa mikoa ya Donetsk na Luhansk.

NATO na Ukraine waliyakataa madai yote ya Urusi, hivyo kupelekea Urusi kutokuwa na namna nyingine zaidi ya kulinda  usalama wake kwa kuivamia Ukraine katika kile kinachoitwa oparesheni maalum ya kijeshi ( Special military operation) ili kuzuia isijiunge na NATO. Ni uvamizi mkubwa wa kijeshi barani  Ulaya tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia. Lengo kubwa la Rais Vladmir Putin katika operesheni hii ni kurudisha Usawa baina ya Urusi na Marekani kwa kupunguza kitisho cha NATO. 

Urusi chini ya Putin ikisimama peke yake dhidi ya Ukraine inayoungwa mkono na NATO kifedha na kijeshi inapigana kwa tahadhari kubwa, akili nyingi na kwa mipango na mikakati ya kueleweka. Jeshi lake linasonga mbele taratibu lakini kwa uhakika, likipiga hatua tatu mbele na kurudi hatua moja nyuma pale uwanja wa mapambano unapokuwa mgumu. Urusi inashinda kwenye uwanja wa vita, inapambana kwenye uwanja wa Diplomasia na inashinda kwenye kampeni kali ya vikwazo dhidi ya uchumi wake na hivyo kumkatisha tamaa Rais Volodymyr Zelenskyy na washirika zake kutoka NATO na Umoja wa nchi za Ulaya ambazo kwa kiasi kikubwa uchumi wao umeathirika vibaya kutokana na vikwazo vyao wenyewe wanavyoweka dhidi ya Urusi. 

Kutekwa kwa miji muhimu kama Kherson na Mariupol lilikuwa pigo kubwa kwa Zelenskyy na NATO, lakini kudondoka kwa jiji la Severodonetsky, mji mkuu wa wakazi wa mkoa wa Luhansky wanaopinga kujitenga na Ukraine kunatuma ujumbe kwa Zelenskyy na mabwana zake wa Magharibi kuhusu uimara wa jeshi la Urusi na hatari ya Ukraine kugawanywa vipande viwili katika siku za usoni. 


Kuna kila dalili kuwa Ukombozi wa Donbass hautakuwa mwisho wa uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine, kwani lengo hasa la Putin ni kuhakikisha sehemu yote ya Mashariki na kusini mwa Ukraine inakuwa chini ya Urusi, hivyo basi kutekwa kwa mikoa mitano ya Kharkiv, Dnipropetrovsk, Zaporizhia, Mykolaiv na Odesa kuelekea Tranistria ni mojawapo ya malengo yajayo  ya operation maalum ya kijeshi ya Urusi inayoendelea nchini Ukraine. Hivyo basi kuna uwezekano mkubwa mapigano kuendelea kwa muda mrefu. 

Hatima ya Ukraine itaamuliwa na Urusi baada ya kuteka eneo la Mashariki na kusini mwa Ukraine, hapo ndipo itajulikana kama Ukraine itamegwa na kuanzishwa taifa jipya ama eneo hilo kuwa sehemu rasmi ya Urusi. Katika sakata hili la Ukraine ni dhahiri kuwa aliyeanzisha mapigano ndiye huyo huyo atakayeyamaliza mapigano naye siye mwingine isipokuwa ni Vladmir Putin. 


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.

© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇

Email: masudirugombana@gmail.com

Simu: 0743 184 044

Saturday, August 22, 2020

DENG XIAOPING: MBUNIFU WA CHINA YA KISASA ALIYEIFUNGUA CHINA NA CHINA IKAFUNGUKA

Na Masudi Rugombana

Huyu ndiye Baba wa uchumi wa China, ndiye aliyeasisi, aliyejenga na kusimamia ipasavyo misingi ya mfumo wa uchumi wa soko huria, na kufanya mageuzi mengi yanayoifanya leo hii China kuwa dola kuu la pili kiuchumi baada ya Marekani na hata kutishia kuipiku Marekani. Waswahili husema ukiona vyaelea ujue vimeundwa, kwa hivyo ukiona China ya kisasa namna inavyomeremeta basi tambua kuwa ni kazi nzuri iliyofanywa na Deng Xiaoping. 

Deng Xiaoping

Yaani huyu mzee kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake, imefikia hatua Dunia nzima inamtambua kama Mbunifu wa China ya kisasa (the architect of Modern China). Naam, ni huyu ndiye aliyeifungua China na China ikafunguka.

CHINA ILIKUWAJE HAPO KABLA?
Tarehe 1 Octoba 1949 Mao Tse Tung alitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu China, nchi ya Chama kimoja, ikiongozwa na Chama cha Kijamaa cha CPC. Katika kipindi chote cha utawala wake, Mwenyekiti Mao aliiongoza China katika misingi ya kijamaa akifanya maamuzi mengi magumu kupitia kampeni mbali mbali zilizokwenda sambamba na mipango ya muda mrefu na muda mfupi. Lengo likiwa ni kuibadilisha China kutoka taifa lenye kutegemea Kilimo pekee na kuwa taifa la viwanda. 

Miongoni mwa kampeni hizo ni Kampeni dhidi ya wapinzani wa mfumo wa kijamaa katika kile kilichoitwa Mapinduzi ya utamaduni ikilenga kuwamaliza kabisa wafuasi wa Chama cha Kuomintang, Wafanyabiashara matajiri na wanasiasa ambapo watu milioni mbili na laki sita walikamatwa, watu milioni moja na laki tatu walitupwa magerezani. Katika kampeni hii watu laki saba waliuawa na wengine kwa maelfu kulazimika kukimbilia Taiwan.  

Baada ya kukamilika kwa kampeni dhidi ya wapinzani wa sera ya kijamaa, Mwenyekiti Mao alianzisha kampeni kubwa ya mageuzi ya umiliki wa ardhi iliyoitwa Tugai ( Chinese Land Reform Movement) iliyohusika na utaifishaji wa ardhi ukihusisha mashamba na majengo yaliyokuwa yakimilikiwa na watu binafsi, lengo la kampeni hii likiwa ni kupambana na tatizo la ukosefu wa usawa wa kiuchumi kwani wakulima matajiri ambao walikuwa ni asilimia kumi (10%) tu ya Wachina wote walimiliki asilimia 80 ya ardhi yote yenye rutuba huku Wakulima wadogo ambao ni asilimia tisini (90%)wakimiliki asilimia 20.

Mao aliwapokonya umiliki wa mashamba wakulima Matajiri na kuyagawa kwa wakulima masikini ambapo jumla ya wakulima masikini milioni mia tatu walipewa asilimia 45 ya ardhi yote iliyokuwa ikimilikiwa na wakulima matajiri. Ni kampeni iliyofanywa katika hali ya kutisha kwani wamiliki wa ardhi na nyumba waliuawa kwa kushambuliwa na wakulima wadogo pamoja na wapangaji wao,  huku wengine wakilazimika kuimbia China bara na kuhamia Taiwan. 

Miaka tisa baadae (1958) Mao alianzisha kampeni nyingine ngumu iliyojulikana kama hatua kubwa kuelekea mbele (The great leap forward) ambapo watu waliondolewa kwenye mashamba yao binafsi na kuhamishiwa kwenye mashamba ya ujamaa. Kilimo katika mashamba binafsi kilipigwa Marufuku huku Mamilioni ya wakulima wengine wakilazimishwa kuachana na kilimo na kufanya kazi kwenye viwanda vya uzalishaji chuma kwani uzalishaji chuma ulipewa kipaumbele kama hitaji muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Viwanda. 

Kutokana na mageuzi hayo hali ya uzalishaji chakula ilipungua kati ya mwaka 1958 hadi 1962 kutokana na sekta ya kilimo kuyumba hivyo kupelekea China kuingia kwenye janga kubwa la njaa. Licha ya matokeo chanya hapo baadae, madhara makubwaa yaliyosababishwa na kampeni hii katika miaka mitatu ya mwanzo ni kuibuka kwa janga kubwa la njaa kati ya mwaka 1958 hadi 1962 lililopekea vifo vya watu milioni 15 kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya China.

Ni maamuzi hayo magumu yaliyomuwezesha Mwenyekiti Mao kuujenga uchumi wa China kwa mpangilio, kuibadilisha China kuwa nchi ya viwanda huku akiwezesha wananchi kushiriki kimamilifu katika ujenzi wa nchi na kufanikiwa kuondoa tofauti kubwa ya kipato baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. Ni mafanikio yaliyoacha majeraha makubwa miongoni mwa Wachina huku utawala wake ukipelekea China kutengwa na jamii ya kimataifa, hasa mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani.

CHINA CHINI YA UONGOZI WA DENG.
Muda mfupi baada ya kushika hatamu ya kuongoza China mnamo tarehe 22 December 1978, Deng alianzisha mkakati uliopewa jina "kuondoa machafuko na kurudi katika hali ya kawaida"akikusudia kurekebisha matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na sera ya Mapinduzi ya utamaduni iliyotekelezwa kipindi cha utawala wa Mao Tse Tung.

Aliifanyia marekebisho sera ya uchumi wa kijamaa iliyotekelezwa na Mao kwa kuanzisha Ujamaa mpya unaoendana na mazingira ya China katika kile kilichoitwa sera ya uchumi mchanganyiko (Mixed Economy) ambapo baadaye mnamo mwaka 1992 mrithi wake Jiang Zemin aliibadilisha jina na kuiita sera ya kijamaa ya uchumi wa soko (socialist market economy). Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kiuchumi waliitambua kama sera ya ubepari wa kidola (State Capitalism)

Ni hapo ndipo alipoifungua China kwa uwekezaji wa kigeni na kuondoa vizuizi vingine vya biashara huku serikali ikiendelea kushikilia njia kuu za uchumi wakati huo huo ikishirikiana kwa karibu na makampuni binafsi makubwa yanayomilikiwa na matajiri wazawa kama Huawei, ZTE, Lenovo na Alibaba. Uwekezaji mkubwa wa makampuni kutoka nje hasa Barani Ulaya na Marekani umeshika kasi kutokana na uhakika wa Malighafi, soko na nguvu kazi. Leo hii China ni taifa la kwanza kwa kuwa na uchumi mkubwa (PPP ranking) Duniani ikifuatiwa na Marekani.


Licha ya sera yake  kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wahafidhina ndani ya chama lakini imefanikisha sana kuifanya China kuwa mojawapo ya mataifa yenye uchumi imara (GDP ranking) ikishika nafasi ya pili baada ya Marekani huku idadi ya Wachina waliokuwa wakiishi kwenye umasikini uliokithiri ikipungua kutoka asilimia tisini (90%) mwaka 1981 mpaka asilimia mbili (2%) mwaka 2013. 

Pamoja na mafanikio makubwa aliyopata, utawala wake unakumbukwa zaidi kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza. 
Nguvu kubwa iliyotumika kusambaratisha Waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa Tiananmen (Tiananmen square) jijini Beijing June 04 mwaka 1989 wakidai Demokrasia na uhuru wa kujieleza ilipelekea vifo vya mamia kwa maelfu ya waandamanaji na hivyo kuutia doa utawala wake mbele ya jumuiya ya kimataifa. Walichosahau waandamanaji waliokuwa wakiungwa mkono na mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani ni kwamba Deng Xiaoping aliruhusu Demokrasia ya Uchumi na hakutaka Demokrasia ya siasa.

HUYU NDIYE DENG XIAOPING
Alizaliwa tarehe 27 August 1904 katika kijiji cha Paifang, kwenye mji wa Xiexing, jimbo la Sichuan. Ni mtoto kutoka familia ya wasomi, iliyokuwa na hali nzuri kimaisha, akitumia jina la Xixian enzi za utotoni. Baba yake Mzee Deng Wenming alikuwa msomi wa Sheria na Sayansi ya siasa, Mama yake alijulikana kwa jina la Dan na alifariki akimwacha mwanae wa mwisho Deng akiwa bado kijana mdogo. 

Mwaka 1920 baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya Chongqing, akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 16, Deng Xiaoping na vijana wenzake 80 waliosoma shule moja walipanda meli kuelekea Ufaransa kwa lengo la kujiendeleza kimasomo. Ikumbukwe kuwa Ufaransa ni taifa la kwanza barani Ulaya kupokea wahamiaji kutoka China. 

Nchini Ufaransa mambo hayakuwa sawa kama alivyotarajia kwani alijikuta akitumia muda wake mwingi kufanya kazi, zaidi kazi zisizokuwa na ujuzi kama vibarua kwenye viwanda vya magari na chuma hadi kazi za usaidizi wa wapishi kwenye migahawa. Kwani hali ya uchumi barani Ulaya na Dunia kwa ujumla haikuwa nzuri kwa wakati huo kutokana na athari zilizotokana na vita kuu ya kwanza ya Dunia. Hata familia yake huko China haikuwa na uwezo wa kumtumia ada. Hivyo alitumia mshahara mdogo aliopata kujilipia ada ya shule (middle school) huko Chatillon, jijini Paris.

Kipindi cha miaka mitano alichotumia kwenye masomo yake huko Ufaransa, kutoka umri wa miaka 16 hadi 21, kilibadilisha fikra zake kutoka kwenye kundi la vijana wazalendo na kuwa mfuasi wa itikadi ya Karl Max (Marxism ideology). Ni hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa kufuata nadharia za kijamaa na  kimapinduzi akizisambaza kwa vijana raia wa China waliokuwa masomoni barani Ulaya kupitia makala alizokuwa akiandika kwenye Jarida la Nuru Nyekundu (Red Light), jarida lililoanzishwa mahususi kuwawezesha Wachina waliokuwa wakiishi kwenye mataifa ya Ubelgiji, Ujerumani na Ufaransa kujifunza nadharia za kizalendo kwa taifa lao. 

Kiwango cha fikra pevu kilianza kuongezeka miongoni mwa wanafunzi wa Kichina barani Ulaya kwani wengi walianza kuamini katika nadharia ya kijamaa. Chini ya ushawishi wa wakubwa zake kama Zhou Enlai na Zhao Shiyan, Deng Xiaoping alianza kujifunza itikadi za kijamaa na kufanya propaganda za kisiasa. Mwaka 1922 alijiunga na jumuia ya vijana ya Chama cha kijamaa cha China barani Ulaya na mwaka 1924 alijiunga rasmi na chama cha kijamaa cha China (Chinese Communist Part-CCP) na kuwa mmojawapo wa viongozi wa tawi kuu la vijana la chama barani Ulaya.

Mwaka 1926 Deng Xiaoping na kundi la vijana wenzake wa Chama cha kijamaa waliondoka Ufaransa kuelekea Moscow nchini Urusi (Soviet Union) na kujiunga na chuo kikuu cha kijamaa cha Toilers of the East (KUTV) kabla ya kuhamishiwa kwenye chuo kikuu cha Sun yat-sen, chuo kilichopewa jina kwa heshima ya Muasisi wa mapinduzi ya China. Huyu alikuwa mwanafalsafa, mwanafizikia na mwanasiasa  aliyeongoza mapinduzi dhidi ya Utawala wa kinasaba wa Qing (Qing dynasty). Sun yat-sen Ndiye Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China na kiongozi wa kwanza wa Chama tawala cha Kuomintang (Nationalist Part of China). Huko nchini Taiwani anatambulika kama Baba wa taifa.

Baadaa ya miaka sita nje nchi, hatimaye Deng alirejea China mwaka 1927 akitokea Urusi (Soviet union). Alirejea kipindi ambacho hapakuwa tena na ushirikiano baina ya chama cha Kijamaa (CCP) na Chama tawala cha Kuomintang ambapo hali ya kisiasa ilikuwa tete, huku taifa likiekea kugawanyika baina ya wafuasi wa sera za kijamaa na kibepari kutokana na vita vya kiraia. Alipata mafunzo ya kijeshi na kuwa miongoni wa wapiganaji wa jeshi la chama cha kijamaa ambalo baadae lilibadishwa jina na kuitwa Jeshi la ukombozi la watu wa China. 

Baada ya chama cha kijamaa kupata ushindi dhidi ya chama cha Kuomintang na Mao Zedong kutangaza kuanzisha Jamhuri ya watu wa China mnamo mwaka 1949, Deng Xiaoping alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Chama, Serikali na Jeshini kuanzia Katibu mkuu wa Chama cha kijamaa(CCP)  kwa nyakati tofauti mpaka mwaka 1956, Waziri wa fedha kuanzia mwaka 1953-1954, mkuu wa Jeshi la China kati ya mwaka 1975 mpaka 1980, Naibu Waziri mkuu 1977-1978 na hatimaye Kiongozi mkuu wa China kuanzia mwaka 1978 mpaka 1989.

Alifariki tarehe 19 February mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 92 kwa ugonjwa wa mapafu na ugonjwa wa kutetemeka mwili pasina hiari unaojulikana kama Parkinson. Alikuwa Baba wa watoto watano aliozaa na mkewe Zhuo Lin. Msiba wake uliombolezwa kitaifa kwa muda wa wiki moja huku bendera zikipepea nusu mlingoti. Viungo vyake (Organs) vilitumika katika utafiti wa kimatibabu, mwili wake ulichomwa moto na majivu yake yalitawanywa baharini kama alivyoelekeza kabla kifo chake.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia👇👇👇
Email: masudirugombana@gmail.com
Simu: 0743 184 044

TARECK EL AISSAMI: MSHIRIKA WA RAIS MADURO ANAYETAFUTWA SANA NA MAREKANI.

Na  Masudi Rugombana.

Venezuela, taifa la Amerika ya kusini lenye hifadhi kubwa ya mafuta ghafi sasa limejikuta likikumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta na gesi. Vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani kwa lengo la kutaka kuiangusha Serikali ya  Chama cha kijamaa ya Rais Nwicolas Maduro vimesababisha wawekezaji wa kigeni kuondoka na wananchi takriban milioni tatu wa taifa hilo kuikimbia nchi yao na kwenda kutafuta unafuu wa maisha ughaibuni. 

Vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 28,644,603 vimeilenga zaidi sekta ya mafuta ambayo ndicho chanzo kikuu cha mapato cha Venezuela. Kwa miaka kadhaa uhaba wa mafuta na gesi umekuwa ukiathiri zaidi maeneo ya vijijini, lakini katika miezi ya hivi karibuni tatizo hilo limehamia mijini hasa kwenye miji yenye msongamano wa watu wengi ukiwemo mji mkuu Caracas. Uhaba wa mafuta unazidi kushika kasi wakati taifa hilo likikabiliana na ugonjwa wa Covid19.

Venezuela inavichukulia vikwazo vya Marekani kama ni vita rasmi ya kiuchumi na mapambano ya kuokoa uhai na ustawi wa Wananchi wake. Vita hii ya kiuchumi ni kongwe na ilianza toka enzi za utawala wa Hugo Chavez, ni vita iliyotangazwa rasmi mwaka 1998, kwa hakika ni muendelezo ule ule wa mpango wa Marekani katika kuhakikisha chembe chembe za kijamaa zinatokomezwa kabisa kwenye eneo lote la Amerika ya kusini. 

Kama ilivyo kawaida kwenye uwanja wa vita huwa kuna wapiganaji shupavu, wazalendo wa kweli na watu wenye uchungu na taifa lao. Kamanda mkuu wa mapambano haya ya vita vya kiuchumi ni Raia Nicolas Maduro akisaidiwa na makamanda wengine shupavu wenye uzalendo wa hali juu. 

Miongoni wa makamanda wanaofanya kazi kubwa zaidi kwenye vita hii ya kiuchumi na wenye kuaminika na pia wenye ushawishi mkubwa katika Serikali ya Rais Nicolas Maduro ni waziri wa viwanda na uzalishaji ambaye pia ni waziri wa mafuta Bwana Tareck Zaidan El Aissami Maddah. 

Tarreck al Aissami

Tareck El Aissam, gavana wa zamani wa jimbo la Aragua alizaliwa mwaka 1974 kwenye mji wa El Vigia, Merida, magharibi ya nchi ya Venezuela. Mama yake May Maddah ni muhamiaji kutoka Lebanon na Baba yake Zaidan El Aissami ni muhamiaji kutoka Syria. Kama ilivyo kawaida kwa maji kufuata mkondo basi ndivyo ilivyo kwa Tareck El Aissami, huyu anatoka kwenye familia yenye historia ya uongozi kwani baba yake mkubwa Shibli El Aissami alikuwa katibu mkuu msaidizi wa Chama cha Baath (Chama tawala cha Syria) na Makamu wa Rais wa Syria kati ya 28 December 1965 – 23 February 1966 wakati huo Syria ikiongozwa na Rais Amin el Hafez.

Tareck amesomea Sheria na Elimu ya jinai (law and criminology) katika Chuo kikuu cha Andes jijini Merida. Ni katika chuo hicho ndipo alipomezeshwa itikadi za kijamaa na mwalimu wake Adan Chavez ambaye ni kaka yake na Rais wa zamani wa Venezuela Marehemu Hugo Chavez. Baba yake Zaidan El Aisami maarufu kama Carlos Zaidan alikuwa rafiki wa Hugo Chavez na miongoni mwa watu waliokamatwa kwa kuhusika na Jaribio na mapinduzi dhidi ya serikali lilioongozwa na Hugo Chavez mnamo Mwezi February mwaka 1992.

Baada ya kutunukiwa shahada ya sheria, El Aissami aliingia katika utumishi wa umma mwaka 2003 ambapo serikali ya Rais Hugo Chavez ilimteua kuwa mkuu wa kwanza wa Misheni iliyojulikana kwa jina la  Identidad (mpango wa kusimamia kadi za utambulisho wa taifa). Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya ndani.  Ni katika wadhifa huo ndipo alipoanza kutazamwa na Marekani kwa jicho la pili, kwani ilimtuhumu kuwapatia vitambulisho vya uraia na hati za kusafiria za Venezuela maelfu ya wanaharakati wa makundi ya Hizbullah na Hamas hivyo kuwawezesha kuingia na kuishi Venezuela wakiendesha harakati zao dhidi ya Marekani na Israel. Ni hapo ndipo Marekani ilipoanza kumuwekea vikwazo. 

Akiwa kama kiongozi mwandamizi wa serikali kwa miaka mingi, El-Aissami mwenye umri wa miaka 45, amehudumu kwenye nafasi mbalimbali. Amekuwa Waziri wa mambo ya ndani, Waziri wa viwanda na uzalishaji wa taifa, na Makamu wa Rais wa Venezuela, wadhifa uliompa jukumu la kusimamia idara ya ujasusi ya taifa hilo inayojulikana kama SEBIN. (The Bolivarian National Intelligence Service). 

Sambamba na kuongoza wizara ya viwanda, mwezi April 2020 rais Nicolas Maduro alimteua kuwa Waziri wa Mafuta. Uzoefu pekee alionao katika sekta  ya mafuta unatokana na nafasi aliyokuwa akiishikilia ya Mkurugenzi wa masuala ya nje wa shirika la taifa la mafuta na gesi asilia la Venezuela (PDVSA). Ni mshirika mkubwa wa Iran na Urusi na ndiye aliyeratibu zoezi zima la kusafirisha mamilioni ya tani za mafuta na gesi kutoka Iran kwenda Venezuela mwezi May 2020 hatua iliyosababisha msuguano na taharuki baina ya Marekani na Iran kutokana na kukiuka vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hizo mbili washirika. Anatajwa kuwa ni miongoni mwa watu wa karibu na Rais Nicolas Maduro wanaopewa nafasi ya kuiongoza Venezuela baada ya rais Nicolas Maduro kumaliza muda wake.

Mwaka 2017, ofisi ya idara ya Hazina ya Marekani yenye kuhusika na  udhibiti wa rasilimali za kigeni (OFAC) ilisema kuwa El Aissami aliwezesha kufanikisha operesheni za usafirishaji wa wadawa ya kulevya na kuwapa ulinzi  wasafirishaji wengine wa madawa ya kulevya wanaofanya shughuli zao nchini Venezuela. Kwa mujibu wa OFAC, El Aissami alipokea malipo kutoka kwa mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya kulevya, raia wa Venezuela mwenye asili ya Syria bwana Walid Makled kwa ajili ya kusaidia kuratibu usafirishaji wa madawa ya kulevya kwenda Marekani. 

Ripoti ya Marekani pia ilisema kwamba El Aissami anashirikiana kibiashara na Los Zetas, msambazaji maarufu wa dawa za kulevya (drug cartel) raia wa Mexico na Daniel Barrera Barrera raia wa Colombia anayejulikana kama kiongozi mkuu wa wauza madawa ya kulevya katika eneo la Mashariki ya Colombia. Pia Marekani inamtuhumu kwa kujihusisha na masuala ya kigaidi utakatishaji fedha na biashara ya magendo ya dhahabu. 

Gazeti la The times of Israel la January 10, 2017 linamtaja bwana Aissami kama mpatanishi baina ya Iran na Argentina kwenye mpango wa kuwaficha watuhumiwa wa shambulizi la kigaidi dhidi ya kituo cha Wayahudi jijini Buenos Aires. Inaelezwa kuwa shambulizi dhidi ya kituo hicho kinachojulikana kama AIM liliua Wayahudi 85 na kujeruhi wengine mia tatu. Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyetiwa hatiani kutokana na shambulio hilo. 

Kwa tuhuma hizo, Tareck el Aissami anatajwa kwenye orodha ya watu kumi wenye kutafutwa zaidi na Marekani kwa sasa akielezwa kuwa ni mtu hatari kwa usalama wa Marekani. Marekani imemuwekea vikwazo vya kuingia nchi humo na kuzuia mali zake zote zilizopo Marekani, pia imetangaza dau la dola za kimarekani milioni 10 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 23 kama donge nono kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwake. Sambamba na Marekani, nchi za Canada na Jumuiya ya Ulaya pia zimemuwekea vikwazo vya kusafiri ikiwa ni pamoja na kuzuia mali zake.

Hata hivyo bwana Aissami anakanusha kuhusika na tuhuma hizo za Marekani akisema kuwa ni tuhuma zisizokuwa na msingi pia amekanusha kumiliki mali za aina yeyote nchini Marekani au taifa lolote nje ya Venezuela.


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.

© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇

Email: masudirugombana@gmail.com


Saturday, February 8, 2020

IRAN: TAIFA LINALOLIPIGA HATUA KUBWA MBELE LICHA YA VIKWAZO VIKALI VYA KIUCHUMI.


Na Masudi Rugombana.

Iran, taifa linalopatikana katika eneo la kimkakati la Magharibi ya bara la Asia kati ya bahari mbili Muhimu za Arabian na Caspian linapakana na mataifa saba ambayo ni Iraq na Uturuki kwa upande wa magharibi na kaskazini Magharibi, Armenia na Azerbaijan kwa Upande wa Kaskazini, Turkmenstan kwa upande wa Kaskazini Mashariki, Afghanistan kwa upande wa Mashariki na Pakistan kwa upande wa kusini Mashariki.



Taifa hilo la kiajemi linaloshika nafasi ya 19 Duniani kwa  ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 1,648,195 limebarikiwa utajiri mkubwa wa maliasili ambazo ni mafuta (petroleum), gesi asilia( natural gas), Makaa ya mawe (coal) pamoja na madini ya chromium, copper, iron ore, lead, manganese, zinc na sulfur.

Iran ni Jamhuri ya Kiislam yenye kuongozwa kwa kufuata misingi ya sharia za kiislam chini ya kiongozi wa Kidini Ayatollah Sayyid Ali Khamenei aliyechukua madaraka mnamo tarehe 4 June, 1989 mara tu baada ya kufariki kwa kiongozi na muasisi wa mapinduzi matukufu ya Kiislam ya mwaka 1979  Sayyid Ruhollah Musavi Khomeini aliyefariki tarehe 3 June, 1989. Ayatollah Sayyid Ali Khamenei ndiye kiongozi mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu ( commander-in-chief )
 wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama vya Iran. Kiongozi wa Shughuli za Serikali ni Rais ambaye huchaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura mara moja kila baada ya miaka minne. Rais wa sasa wa Iran anaitwa Hassan Rouhani.

Iran ni taifa la pili lenye nguvu kubwa za kijeshi katika eneo la mashariki ya kati baada ya Uturuki, linashika nafasi ya kumi na nne Duniani likiwaacha nyuma mahasimu wake wakuu Israel inayoshika nafasi ya kumi na saba na Saudi arabia inayoshika nafasi ya ishirini na tano (hii ni kwa mujibu wa rank za global fire power kwa mwaka huu wa 2019).

Tofauti na mataifa mengine ya mashariki ya kati, Iran ni taifa lenye uzoefu mkubwa wa kupigana vita vya muda mrefu bila kusaidiwa na mataifa mengine sambamba na kupigana vita mbadala (proxy war) za muda mrefu tena kwa mafanikio makubwa dhidi ya mahasimu wake Marekani, Israel na Saudi Arabia katika eneo lote la mashariki ya kati kuanzia Syria, Lebanon, Israel/Palestina, Iraq na Yemen ikifadhili na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ukombozi ya wapiganaji ya Hamas, Hizbullah, Hauth na Makundi makubwa ya wapiganaji wa Kishia ya Mahd na Badr nchini Iraq ambayo yalipigana kwa mafanikio makubwa sambamba na jeshi la Iraq dhidi ya kundi la Kigaidi la Islamic State lililokuwa likifadhiliwa na kupewa mafunzo kijeshi na mataifa ya Qatar, Saudi Arabia, Israel na Uturuki.

Ni ufadhili na mafunzo ya kijeshi ya Iran ndiyo yaliyoliwezesha kundi la Hizbullah kuyashinda na kuyatimua majeshi ya Israel katika eneo la kusini mwa Lebanon katika vita iliyojulikana kama South Lebanon conflict au Security zone conflict iliyopiganwa kwa muda wa miaka kumi na tano (1985-2000). Pia ni ufadhili na mafunzo hayo hayo ya kijeshi kutoka Iran yaliyoliwezesha kundi la Hizbullah kuipeleka puta Israel katika vita baina yao iliyopiganwa mwaka 2006 kati ya July 12 hadi August 14. Vita hii inajulikana huko nchini Israel kwa lugha kiebrania kama Milhemet Levanon HaShniya ikimaanisha vita ya pili ya Lebanon (Second Lebanon War) iliyopelekea vifo vya makomandoo 121 wa Israel na wanamgambo wa Hizbullah 250. Ni katika vita hii ndipo baraza la usalama wa umoja wa mataifa lilipoingilia kati kwa kusimamia makubaliano ya kusitisha vita ikiwa ni pamoja na kupeleka askari wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa na jeshi la Lebanon kushika udhibiti katika maeneo yaliyokuwa yakishiliwa na  Hizbullah baada ya vikosi vya Hizbullah kutakiwa kujiondoa katika maeneo hayo.

Ni ufadhili wa Iran ndio ulioanzisha na kuimarisha kundi la Hamas huko ukanda wa Gaza mnamo mwaka 1985. Ni mafunzo ya kijeshi ya Iran na msaada wa silaha ndio unaolipa nguvu kubwa tawi la kijeshi la Hamas la Izzudin al Qassam na kuwaibua makamanda shupavu wa Kipalestina kama vile Mohammed Deif (Abuu Khalid) na Marwan Issa. Ni mipango iliyokwenda shule ya Iran iliyoliwezesha kundi la Hamas kutembeza kipigo cha mbwa koko kupitia mashambulizi ya kustukiza dhidi ya askari wa Israel na Walowezi wa Kiyahudi huko Gaza hadi kupelekea Waziri mkuu wa Israel Jenerali Ariel Sharon kuyaondoa majeshi ya Israel pamoja na Walowezi wa Kiyahudi huko Gaza mnamo mwaka 2005 ikiwa ni pamoja na kubomoa nyumba za Walowezi hao.

Ni ufadhili wa Iran pamoja na mafunzo ya kijeshi ndio umeifanya Saudi Arabia iliyotangaza kuwa itashinda vita vya Yemen ndani ya mwezi mmoja mwaka 2015 kushindwa kutekeleza azma yake na kujikuta ikiendelea kupigana vita bila mafanikio kwa muda wa miaka mitano sasa dhidi ya Wapiganaji wa Houthi huko Yemen licha ya kupewa misaada lukuki ya kiintelijensia na Mataifa ya Israel na  Marekani. Yaani Saudi Arabia inatia huruma kwa namna drone za wapiganaji wa Houth ambazo zinatengenezwa nchini Iran zinavyowachapa ndani ya Saudia kila kukicha.

Kinachowaumiza vichwa maadui wa Iran ni kwamba silaha inazotumia Iran katika hizo vita zote zinatengenezwa nchini Iran na wataalamu ambao ni raia wa Iran tena kwa teknolojia yao wenyewe Wairan. Mifumo ya Ulinzi wa anga ya Iran ya Khordad 3, Khordad 15 advance Air defense System na Bavar 373 ni tishio kubwa kwa ndege vita za maadui. Marekani ilionja makali ya mfumo wa Ulinzi wa anga wa Iran pale ndege yake ghali zaidi isiyokuwa na rubani (UAV) au ukipenda unaweza kuiita drone aina ya RQ-4A Global Hawk yenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 222 ilipodunguliwa mara tu ilipojaribu kuingia kwenye anga ya Iran kupitia mlango bahari wa Hormuz.  Thamani ya hiyo drone iliyodunguliwa na kombora aina ya Sayyad 3 lililovurumishwa kutoka kwenye mfumo wa ulinzi wa anga wa Khordad 3 ni sawa na ndege mbili za kizazi cha tano za F-35C stealth fighter.

Iran imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali licha ya vikwazo vikali vya kiuchumi ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za Ulaya Magharibi. Mafanikio hayo yametokana na taifa hilo kuwekeza zaidi katika Elimu hatua ambayo imewawezesha kupata wataalamu wengi katika fani mbali mbali hivyo kujitosheleza katika sekta mbalimbali kuanzia elimu, afya, kilimo, viwanda, nishati, madini n.k.

Leo hii Iran inatengeneza Magari yao wenyewe kuanzia ya kijeshi hadi ya kiraia tena ya kisasa, vifaru, Nyambizi, ndege za kivita na kiraia zikiwemo ndege zisizokuwa na rubani (UAV/Drones)makombora ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu, Rockets kwa ajili ya mambo ya utafiti wa anga za mbali, meli za kivita na meli za kiraia, simu za mikononi (Smartphones) pamoja na vifaa tiba vya aina mbalimbali. Ikiwa na asilimia ishirini (20%) ardhi yenye rutuba, Iran ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa chakula katika eneo lote la Mashariki ya kati na katikati ya bara la Asia.


Nyambizi ya Iran inayoitwa Fateh ni mojawapo ya zana za kivita
 zinazotengenezwa nchini Iran.


Mafanikio inayopata Iran katika nyanja mbalimbali licha ya vikwazo vikali inavyowekewa kila kukicha yanatufundisha kuwa kila palipo na changamoto ndipo inapopatikana njia ya mafanikio.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

AUGUSTO PINOCHET: KIBARAKA WA MAREKANI ALIYEITAWALA CHILE KWA MKONO WA CHUMA


Na Masudi Rugombana

Augusto Pinochet alikuwa afisa wa Jeshi na kiongozi kwa kiimla wa Chile aliyechukua madaraka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoungwa mkono na Marekani kwa kumpindua Rais mjamaa Salvador Guillermo Allende mnamo Septemba 11, 1973 na kuitawala Chile kwa mkono wa chuma hadi Machi 11, 1990.
Utawala wake uligubikwa na mfumuko wa bei, umasikini na vitendo wa kikatili dhidi ya viongozi wa upinzani.

General Pinochet alizaliwa Novemba 25, 1915 katika jiji la Valparaiso, mji wa bandari unaopatikana kilomita 120 Kaskazini Magharibi ya mji mkuu wa Chile, Santiago. Baba yake mzee Augusto Pinochet Vera ni mtoto kutoka kwenye familia ya Wahamiaji wa Kifaransa waliofika Chile karne ya 18. Mama yake anaitwa  Avelina Ugarte Martinez.  Pinochet alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika shule ya Seminari ya San Rafael mjini Valparaiso kabla ya kujiunga na shule ya jeshi jijini Santiago mnamo mwaka 1931.

General Augusto Pinochet

Alihitimu mafunzo na kujiunga rasmi na Jeshi mnamo mwaka 1935 akiwa na umri wa miaka ishirini akianzia na cheo cha luteni-usu  (second Lieutenant) na kupanda ngazi hatua kwa hatua hadi kufikia Cheo cha General na hatimaye kuteuliwa na Rais Salvador Allende kuwa mkuu wa majeshi ya Chile mnamo tarehe 23 August 1973 baada ya kufanya kazi nzuri ya kusambaratisha maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga  sera za uchumi za kijamaa za serikali ya Rais Allende.

Tarehe 11 Septemba 1973, siku kumi na nane baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa majeshi,  General Pinochet aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Rais Salvador Allende na chama chake za mrengo wa kushoto cha Unidad Popular aliyeitawala Chile kwa muda wa miaka minne tu (1970-1973) na punde baada ya kufanikisha hayo mapinduzi, General Pinochet alijitangaza kuwa kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Chile hadi tarehe 17 Disemba 1974 alipojitangaza rasmi kama Rais wa Chile.

Ikumbukwe kuwa Rais Salvador Allende hakuwa na mahusiano Mazuri na serikali ya Marekani kutokana na msimao wake wa kufuata sera za uchumi za kijamaa, miaka minne ya utawala wake ilitawaliwa na maandamano na migomo iliyochochewa na makundi ya wananchi waliokuwa wakipinga sera zake za kimarxist.

Allende alitoa hotuba yake ya mwisho wakati vikosi vilivyoongozwa na General Pinochet vikiwa vimeizingira Ikulu, katika hotuba yake Rais Allende aligoma kujiuzulu huku akisistiza kuwa yeye ndiye rais halali wa Chile. Inaelezwa kuwa mara baada ya kumaliza kuhutubia Rais Allende alijiua kwa kujipiga risasi, akitumia bunduki aina ya AK-47 aliyozawadiwa na rais Fidel Castro wa Cuba, madai ambayo yanapingwa na wananchi wengi wa Chile, wakiamini kuwa aliuliwa.

Katika miaka mitatu ya mwanzo ya utawala wake, General Pinochet aliwakamata, kuwatesa  na kuwasweka ndani wananchi laki moja na elfu thelasini (130,000) wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani waliokuwa wakipinga utawala wake. Kupitia operation mbaya na ya kikatili iliyoitwa Condor (Operation condor), Pinochet na viongozi wenzake watano wa mataifa ya Amerika kusini waliwauwa viongozi na wafuasi elfu themanini (80,000) wa vyama vya mrengo wa kushoto.

Je ni nini hiyo Operation Condor?
Hiyo ilikuwa ni operation maalum iliyoratibiwa na kufadhiliwa na Marekani kwa lengo la kupambana na sera na fikra za kijamaa katika mataifa ya Kusini mwa bara la Amerika. Tawala zilizoshiriki kwenye operation hiyo ya kikatili ni za mataifa ya Argentina, Bolivia, Brazil, Chile, Paraguay na Uruguay.

Ni hivi👉 Katikati  ya miaka ya 1970, serikali za nchi sita za Amerika kusini ambazo ni Brazil, Chile, Argentina, Paraguay, Bolivia, na Uruguay zilikuwa zikikabiliwa na matukio yanayofanana. Serikali hizo zilikuwa  zikitawaliwa na ama viongozi wa kihafidhina ( Conservative regimes), tawala za kiimla (Dictatorship regimes) au tawala za kijeshi ( Military Juntas) zilizokuwa zikiungwa mkono na Marekani.

Sasa basi kama ilivyo kawaida kwenye taifa lolote linalotawaliwa na mojawapo ya aina hizo za utawala upinzani mkali huwa haukosekani. Mataifa hayo yalikabiliwa na upepo mkali wa kuongezeka kwa makundi ya upinzani na wanaharakati waliokuwa wakitaka mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi. Kitisho kikubwa kwa Marekani na tawala hizo ilikuwa ni makundi au vyama vya siasa vya mrengo wa kushoto yaliyokuwa yakiungwa mkono na Cuba pamoja na Umoja wa nchi za Kisovieti.

Ili kukabiliana na hali hiyo na kuzuia ushawishi wa Soviet union katika eneo hilo, ndipo ilipoanzishwa Operation condor, operation chafu, operation ya kikatili iliyoshuhudia viongozi wa vyama vya siasa vya mrengo wa kushoto na wafuasi wao waliokuwa mstari wa mbele katika harakati, viongozi wa dini na vyama vya wakulima, wanafunzi na walimu wakikamatwa, kuteswa na kuuawa kikatili. Katika kufanikisha mkakati huo Marekani ilishiriki kikamilifu kwa kupanga mikakati na kuratibu mafunzo juu ya utesaji ikiwa ni pamoja na misaada ya kiufundi, fedha na kijeshi.

Hali ya kiuchumi na kisiasa katika utawala wake:
Aliunda timu ya vijana wachumi waliojulikana kama Chicago boys waliosomea Marekani kwenye idara ya uchumi ya Chuo kikuu cha Chicago kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Alipunguza kodi, kubinafsisha mashirika ya umma na kuhamasisha uwekezaji kutoka nje ya nchi. Mabadiliko ambayo yalichochea kwa kiasi kikubwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Chile.

Utawala wa Pinochet uliunda katiba mpya iliyoanza kufanya kazi Mwezi Septemba mwaka 1980 akiachana na katiba ya mwaka 1925. Katiba mpya ilimpa uhalali wa kuendelea kubaki madarakani kwa muda wa miaka nane hadi mwaka 1988 ambapo hatima yake ya kuendelea kuiongoza Chile ingeamuliwa kupitia kura ya maoni.

Kwenye kura ya maoni iliyopigwa mnamo tarehe 5 Octoba 1988 asilimia 56 ya wananchi walipinga Pinochet kuendelea kuingoza Chile na hivyo kuhitimisha utawala wake uliodumu kwa muda wa miaka 16. Kilichopelekea mpaka utawala wa kiimla wa Pinochet kukubaliana na matokeo ni shinikizo kubwa kutoka kwa Wafanyabiashara wakubwa na jumuia ya kimataifa. Pamoja na kushindwa kwenye kura za maoni, General Pinochet aliendelea kuwa mkuu wa Majeshi ya Chile hadi tarehe 11 Machi 1998.

Mwisho wa zama zake.
Mwaka 1998 mwezi October, alipokwenda nchini Uingereza kwa matibabu, alizuiliwa kuondoka nchini humo kwa ombi la mahakama ya Hispania baada ya kufunguliwa mashataka ya kuhusika na utesaji wa Raia wa Hispania huko Chile wakati wa utawala wake. Hata hivyo kwa sababu ya kuzorota kwa afya yake, Waziri wa Mambo ya ndani wa Uingereza Jack Straw aliamua kuwa aruhusiwe kurudi Chile badala ya kupelekwa Hispania kukabiliana na Mashtaka. Hivyo alirejea Chile mwaka 2000 na kupokelewa na maandamano makubwa ya Wananchi waliokuwa wakimpinga.

Kutokana na shikinikizo kubwa kutoka kwa wananchi huko Chile la kutaka Pinochet ashtakiwe kwa kuhusika na mauaji na utesaji, katiba ya nchi hiyo ilifanyiwa marekebisho na kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, hivyo mwaka 2006 alifunguliwa mashtaka ya mauaji, utekaji na utesaji lakini siku chache baada ya kufunguliwa mashtaka hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya moyo na hatimaye kufariki dunia siku ya  tarehe 10 Disemba 2006 akiwa na umri wa miaka 91.  Wakati wa uhai wake General Pinochet alimuoa Maria Lucia Rodriguez na kufanikiwa kupata watoto watano

Wananchi wa Chile wanatofautiana mitazamo kuhusiana na General Pinochet. Wengine wanamuona kama shujaa aliyewaokoa kutoka kwenye sera za ujamaa zilizokuwa zikifuatwa na mtangulizi wake Salvador Guillermo Allende. Mafanikio ya ukuaji wa uchumi katika utawala wake yamefanya Wananchi kumuona kama shujaa na mzalendo wa kweli kwa taifa lake.

Wengine wanamuona kama ni kiongozi katili wa kiimla aliyekandamiza wapinzani wake wa kisiasa na kuhusika na mauaji ya maelfu watu waliokuwa wakiupinga utawala wake. Mafanikio yake kiuchumi wanayachukulia si lolote si chochote kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira, umasikini pamoja na viwango vidogo vya mishahara kwa wafanyakazi.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana.
Email: masudirugombana@gmail.com

MAUAJI YA QASSEM SOLEIMAN NA HATMA YA USALAMA KATIKA ENEO LA MASHARIKI YA KATI.

Na Masudi Rugombana

Mnamo tarehe 03 January 2020, jeshi la anga la Marekani (USAF) likitumia ndege yake hatari isiyokuwa na rubani (Unmanned Aerial Vehicle-UAV) aina ya MQ-9 Reaper, kwa amri ya Rais Donald Trump lilimuua Major General Qassem Suleiman, kamanda wa ngazi ya juu katika jeshi la Ulinzi wa mapinduzi ya Kiislam ( The Islamic Revolutionary Guard Corps- IRGC) aliyekuwa akiongoza tawi la kijeshi  la Quds (Jerusalem) linalohusika na oparesheni maalumu katika vita visivyo vya kawaida (unconventional warfare) nje ya Iran na shughuli za upelelezi wa kijeshi (military intelligence operations) nje na ndani ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran.


Major General Qassem Suleiman

Qassem Suleiman ambaye vyombo vya habari vya magharibi vimembatiza jina la " the shadow commander" kutokana na umahiri wake wa kuongoza,  kupanga na kutekeleza mashambulizi dhidi ya maslahi ya Marekani na washirika zake katika eneo lote la mashariki ya kati kupitia vita vya kiwakala ( Proxy war), aliuawa nje kidogo ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq alipokuwa kwenye ziara ya kikazi. Kamanda Suleiman aliingia Iraq akitokea nchini Syria akisafiri kwa kutumia ndege ya abiria aina ya Airbus A320 mali ya kampuni binafsi ya usafiri wa anga ya Cham Wings Airlines  yenye makao yake makuu jijini Damascus nchini Syria.

Aliingia kwenye uwanja wa ndege wa Damascus akitumia gari yenye vioo vya giza( dark-tinted glass) akifuatana na askari wanne wa kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi (IRGC). Suleiman na askari wake wanne hawakuwa wamesajiliwa kwenye fomu ya usajili wa abiria ( passenger manifest form ) na gari aliyopanda Soleiman lilisimama moja kwa moja kwenye ngazi ya kupandia ndani ya ndege ( staircase ) ambapo Soleiman na wenzake walipanda ndege tayari kuelekea jijini Baghadad. Waliwasili Kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad saa sita na nusu usiku na kupokelewa na naibu kiongozi wa kundi la Wapiganaji la al-Hashd al-Shaabi (Popular Mobilazation Forces-PMF) Abu Mahdi al Muhandis akifuatana na viongozi wenzake wanne. Msafara wao uliokuwa na magari mawili ulishambuliwa kwa kombora lililorushwa kutoka kwenye ndege isiyokuwa na rubani mara tu baada ya kutoka nje ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad na hivyo kupelekea kifo cha Soleiman na wenzake kumi akiwemo mshirika wake Abu Mahdi al Muhandis.

Kamanda Soleiman alipanga kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa ikiwa ni katika juhudi za kumuunga mkono Waziri mkuu wa Iraq bwana Adil Abdul-Mahdi al-Muntafiki anayekabiliwa na maandamano ya wananchi wanaotaka aondoke madarakani kufuatia hali ngumu ya maisha inayotokana na kuyumba kwa uchumi wa Iraq. Pia Waziri mkuu Mahdi alithibitisha kuwa alipanga kukutana na Kamanda Suleiman ili kujadili namna ya kumaliza msuguano wa muda mrefu baina ya Mataifa ya Iran na Saudi Arabia muda mfupi kabla hajauawa.

Marekani, taifa tajiri lenye nguvu kubwa kiuchumi na kijeshi  kuliko taifa lolote Duniani imetetea uamuzi wa kumuua Major General Qassem Suleiman kwa kusema kwamba mauaji ya Soleimani yalikuwa ni jaribio la kuzuia mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani, wanajeshi wake pamoja na wanadiplomasia katika eneo lote la Mashariki ya kati. Uamuzi wa Marekani kuwauwa Qassem Suleiman na Abu Mahdi Al Muhandis ni jambo la hatari linaloendelea kusababisha mtikisiko mkubwa katika mataifa ya Iran, Iraq na eneo zima la mashariki ya kati kiasi cha kukaribia kusababisha vita kamili baina ya Iran na Marekani na wakati huo huo tukishuhudia kuathirika kwa uhusiano wa kiulinzi na kidiplomasia baina ya Marekani na Iraq.

Ni nani huyu Abu Mahdi al Muhandis aliyeuawa sambamba na Major General Qassem Suleiman?

Jina lake halisi ni Jamal Jaafar Muhammad Ali Al Ibrahim. Alizaliwa kwenye mji wa Basra kusini mwa Iraq tarehe 01 Julai mwaka 1954. Baba yake ni raia wa Iraq na mama yake ni raia wa Iran, mke wake pia ni raia wa Iran. Ni msomi katika fani ya uhandisi ( Engineering) aliyohitimu mnamo mwaka 1977, pia ana Shahada ya uzamivu (PhD) ya Sayansi ya siasa. Nchini Iran anajulikana sana kwa jina la Abu Mahdi al Muhandis.

Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya uhandisi, alijiunga na Dawah party, chama cha kisiasa kilichokuwa kikipinga serikali ya rais Sadam Hussein, mwaka 1979 wakati utawala wa Sadam Hussein ulipowahukumu adhabu ya kifo wafuasi wengi wa chama cha Dawah, Abu Mahdi alikimbilia Iran ambapo baadae alipewa uraia na kupatiwa mafunzo ya kijeshi kutoka jeshi la Ulinzi wa mapinduzi ya Kiislam (IRGC).

Mara baada ya kuhitimu mafunzo alianza rasmi kufanya kazi na IRGC tawi la Kuwait ambapo mwaka 1983 Abu Mahdi al Muhandis alishiriki kikamilifu katika mashambulizi ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani na Ufaransa nchini Kuwait katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuishikisha adabu Kuwait, Marekani na Ufaransa dhidi ya hatua zao za kuiunga mkono Iraq wakati wa vita baina ya Iraq na Iran ya mwaka 1980-1988. Abu Mahdi akishirikiana na raia wanne wa Lebanon alishiriki kuiteka ndege ya abiria ya Kuwait (Kuwait Airliner)  iliyokuwa ikitokea Kuwait City kuelekea Karachi nchini Pakistan siku ya tarehe 3 December 1984 na kuilekeza Tehran nchini Iran. Lengo la utekaji wa hiyo ndege lilikuwa ni kuishinikiza serikali ya Kuwait kuwaachia wanaharakati 17 wa Kishia iliyokuwa ikiwashikilia.

Kuwait ilimuhukumu adhabu ya kifo Abu Mahdi al Muhandis bila ya kuwepo mahakamani kwani alikuwa tayari amesharejea nchini Iran kwa tumia hati ya kusafiria (passport) ya Pakistan. Baada ya kurejea Iran,  aliteuliwa kuwa mshauri wa kijeshi wa Quds force, tawi la kijeshi la IRGC. Ni hapo ndipo alipofahamiana na Kamanda Qassem Suleiman. Abu Mahdi al Muhandis alirejea nchi Iraq mwaka 2003 kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Marekani uliohitimisha utawala wa miaka 24 wa Saddam Hussein al Tikrit ambapo aliteuliwa kuwa mshauri wa Masuala ya Usalama wa Waziri mkuu wa Iraq Ibrahim al Jaafari.
Ni mwaka huo (2003) ndipo alipoanzisha na kuongoza kundi la wapiganaji wa kishia la  Kata'ib Hezbollah ambalo  kwa sasa ni mojawapo katika matawi ya kijeshi ya Popular Mobilization Forces (PMF).

Mwaka 2006 Abu Mahdi al Muhandis alipobaini kuwa tayari ameshatambuliwa na maofisa usalama wa Marekani kuwa ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa mashambulizi katika balozi za Marekani na ufaransa nchini Kuwait, haraka sana aliondoka nchini Iraq na kurejea tena nchini Iran. Alirejea tena nchini Iraq mwaka 2011 kufuatia kujiondoa kwa sehemu kubwa ya vikosi vya Marekani nchini humo.

Mwaka 2014 alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa kundi la Popular Mobilazation Forces lililoanzishwa mahususi kwa ajili ya kuyaunganisha makundi ya Wapiganaji wa kishia ili kukabiliana na kundi la kigaidi la Kiwahabi la Islamic State ambalo lilikuwa tayari likishikilia sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq. Baada ya kufanikiwa kulishinda kundi la kigaidi la Islamic state, PMF ilitambuliwa rasmi kama tawi la jeshi la Iraq linalowajibika moja kwa moja kwa Waziri mkuu na wapiganaji wake kulipwa mishahara sawa na wale wa jeshi kuu la Iraq.

Mpaka umauti unamkuta, alikuwa ni Naibu kiongozi mkuu wa kundi la PMF na pia katibu mkuu wa kundi la wapiganaji wa Kishia la Kata'ib Hezbollah. Hivyo basi katika lile shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani Marekani ilifanikiwa kuwaua watu wawili iliyokuwa ikiwawinda sana na pia watu muhimu wenye ushawishi mkubwa sana nchini Iran na Iraq.

Athari za mauaji ya Qassem Suleiman na Abu Mahdi al Muhandis.
 1. Kuibuka kwa kitisho cha vita kamili kati ya Marekani na Iran. Ni baada ya Iran kuapa kuwa ingelipiza kisasi na Marekani kupitia Rais Donald Trump kutishia kushambulia maeneo muhimu 52 ya kihistoria nchini Iran ikiwa tu Iran itathubutu kujibu Mashambulizi. Iran nayo ilijibu kwa kuionya Marekani kuwa kama itathubutu kushambulia maeneo yake ya kihistoria basi na yenyewe itashambulia maeneo muhimu 36 yenye maslahi ya Marekani katika Mashariki ya kati.

 Pamoja na kitisho hicho cha Trump, Iran haikurudi nyuma badala yake siku ya tarehe 8 January 2020 saa saba usiku sawa na muda ule ule aliouwa Kamanda Qassem Suleiman, ilitekeleza mashambulizi mazito ya makombora ya kibalistic ya masafa ya kati na kupelekea uharibifu mkubwa kwenye kambi za jeshi la Iraq zinazotumiwa na vikosi vya Marekani za Ain al Assad mkoani Anbar na kambi moja ya kijeshi iliyopo Elbil mji mkuu wa Jimbo la Kurdistan katika operation iliyopewa jina la Shujaa Soleiman (Operation Martyr Soleimani)

 Kambi zote mbili ni kubwa na muhimu sana kwa vikosi vya Marekani na zimeshawahi kutembelewa na viongozi wa Sasa wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump na Makamu wake Mike Pence. Iran ilidai kuuawa askari 80 wa Marekani na kujeruhi wengine 200 , huku Marekani na Iraq zikikanusha na kusisitiza kuwa hapakuwa na madhara yeyote kwa askari wake.

 Siku kumi baada ya kushambuliwa hatimaye wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha kuwa askari wake 11 wanapatiwa matibabu nchini Kuwait na Ujerumani kutokana na majeraha yaliyotokana na vishindo vya makombora ya Iran (Concussion). Ikimbukwe kuwa Iran iliijulisha serikali ya Iraq masaa kadhaa kabla ya kutekeleza mashambulizi hatua ambayo ilisaidia sana kupunguza idadi ya majeruhi. Labda walikusudia zaidi kuharibu miundombinu badala ya kupoteza maisha ya watu.

 Kinyume na matarajio ya wengi, Marekani haikujibu mashambulizi ya Iran kama ilivyoahidi badala yake Rais Donald Trump aliahidi kuimarisha vikwazo. Uamuzi wa Marekani kutojibu mashambulizi umesaidia sana kuepusha vita. Inawezekana Marekani iliogopa kuingia vitani kwa sasa dhidi ya Iran kwa sababu zifuatazo

 • Wananchi wa Iran walishakuwa kitu kimoja, wakiunganishwa na Mauaji ya Kamanda wao mpendwa Qassem Soleiman. Ushahidi ni namna walivyojitokea kwa mamilioni kuomboleza kifo chake huku wakitamka (chanting) maneno yenye kuhamasisha mshikamano na uzalendo kwa Taifa lao. Hivyo basi taifa zima la Iran lilikuwa na ari ya kuingia vitani, walishajipanga na kujengwa kisaikolojia kuikabili Marekani. Hapakuwa na mgawanyiko baina ya Wananchi na serikali yao.

 • Marekani yenyewe haikuwa imejipanga kuingia vitani ghafla dhidi ya Iran. Hata  washirika wake Uingereza na Ufaransa pia hawakuwa tayari kwa sababu ni suala lilioibuka ghafla kufuatia uamuzi wa Trump kuidhinisha mauaji ya Kamanda Soleiman.

 • Marekani isingeweza kuingia vitani (Iliogopa) kwa sababu mazingira ya uwanja wa vita hayakuwa rafiki na mpaka sasa bado hayajawa Rafiki. Kwa sababu turufu ya Ushindi wa Marekani dhidi ya Iran inategemea uthabiti wa amani ya Iraq na Afghanistan nchi ambazo ndio hasa Marekani inazitegemea kama sehemu ya kuweka miguu wakati wa mapigano yake na Iran. Kwa kifupi ni kwamba Marekani haiwezi kuingia vitani hali ya kuwa nchini Iraq inashambuliwa na Wapiganaji wa Kishia na kule Afghanistan inashambuliwa na wapiganaji wa Taleban. Hapo itakuwa sio vita bali ni vurugu zitakazokuwa hazina mwisho.

 • Shinikizo kutoka kwa washirika wake wa Mashariki ya kati (Kuwait, Oman, Bahrain, Qatar na Saudi Arabia). Ni wazi kuwa nchi hizo zingekuwa katika wakati mgumu zaidi, kwani mvua za makombora kutoka Iran zisingewaacha salama. Hii ni kwa sababu licha ya mataifa hayo kuitegemea Marekani kiulinzi lakini bado hayana mifumo imara ya kuzuia mvua za makombora ya kibalistic kutoka Iran. Hivyo basi nchi hizo zingepata maafa makubwa ya kupoteza watu na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.

 2. Iran kutangaza kutozingatia makubaliano yaliyopo kwenye mkataba wa nyuklia wa JCPOA.
Ni Uamuzi hatari zaidi uliochukuliwa na Iran baada ya                                  kuchukizwa na mauaji ya Kamanda Soleiman.
Tayari Rais Hassan Rouhan ameshatangaza Kuwa nchi yake itarutubisha Uranium zaidi ya kiwango kilichokubaliwa kwenye mkataba wa JCPOA. Hii inamaanisha kuwa huenda Iran inakusudia kutengeneza mabomu ya nyuklia, hatua ambayo ni kitisho kikubwa kwa maadui zake wakuu katika eneo la Mashariki ya kati ambao ni Israel na Saudi Arabia. Hali hii inaweza kusababisha ushindani wa kumiliki silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya kati jambo ambalo linaweza kusabisha hatari ya kusambaa hovyo kwa hizo silaha na hatimaye kuingia kwenye mikono isiyo salama.

 3. Uwezekano wa kuibuka upya kwa makundi hatari ya kigaidi ya kisalafi na kiwahabi mfano wa Islamic state na vita vya Kiraia nchini Iraq.
 Hii ni kutokana na uamuzi wa Iraq kutaka Marekani na mataifa  ya kigeni kuondoa askari wake nchini humo baada ya kuchukizwa na uamuzi wa Marekani kuwaua makamada Qassem Suleiman na  Abu Mahdi al Muhandis.

 Ikumbukwe kuwa kundi la Islamic state liliibuka nchini Iraq mwaka 2014 na kusambaa hadi Syria kutokana na vurugu zilizosababishwa na tofauti za kimadhehenu baina ya Waislamu wa madhehebu ya Suni na shia mara baada ya Marekani kujiondoa Iraq mwaka 2011. Hofu nyingine inayoweza kusababishwa na kuondoka kwa vikosi vya Marekani huko Iraq ni kuibuka kwa vita vya kuwania udhibiti wa madaraka nchini Iraq baina ya Jeshi la Iraq linalopatiwa mafunzo na Marekani na Makundi ya wapiganaji wa Kishia yanayofadhiliwa na Iran.

 Hivyo basi kuondoka kwa vikosi vya Marekani nchini Iraq kunaweza kusababisha janga kubwa la kibinadamu linaloweza kuleta athari mbaya hadi kwenye mataifa jirani na Iraq. Iraq inapaswa kutazama kwa makini zaidi uamuzi wa kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini humo.

 4. Mauaji ya Qassem Soleiman yanapaswa kuwa funzo kwa Iran.
 • Kuuawa kwa Major General Qassem Suleiman na kamanda Abu Mahdi al Muhandis ni ushindi kwa intelijensia ya Marekani na pigo kubwa kwa intelijensia ya Iran. Pengo la Qassem Suleiman ndani ya kikosi cha Quds na Pengo la Abu Mahdi al Muhandis ndani ya PMF sio rahisi kuzibika.

 Pamoja na kwamba kundi la PMF lina maofisa wengi wa ngazi za juu waliopata mafunzo ya kijeshi nchini Iran, lakini Abu Mahdi al Muhandis ndiye aliyekuwa kinara na msimamizi mkuu wa maslahi na ushawishi wa Iran ndani ya Iraq, kwa kushirikiana na Qassem Soleiman walifanikisha kupeleka maelfu ya wapiganaji wa kishia nchini Syria hivyo kuchangia kwa asilimia kubwa ushindi wa Rais Bashar al Assad.

 Kwa upande wa jeshi la Quds, Ingawa kamanda wake mpya Brigedier General Ismail Qaani amefanya kazi kwa muda mrefu kama msaidizi wa Soleiman lakini itamchukua muda kidogo kuweza kumudu kiukamilifu shughuli za kiutendaji zilizokuwa zikifanywa na mtangulizi wake.

 • Iran haikuweka utaratibu mzuri katika tukio la maombolezo ya kifo cha Kamanda Suleiman hali ambayo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 40 kutokana na kukanyagana (Stampede) wakati wa maombolezo na mazishi ya shujaa wao.

 • Iran ilipatwa na taharuki kutokana na mauaji ya kamanda wake wa ngazi ya juu, hata shambulizi la kulipiza kisasi dhidi ya Marekani halikupangiliwa vizuri na hivyo kupelekea mfumo wake wa Ulinzi wa anga kuangusha ndege ya abiria mali ya shirika la ndege la Ukraine International Airline na kuua abiria wote 176 wengi wao wakiwa ni raia wa Iran na raia wa Canada wenye asili ya Iran.

 Ingawa Iran imeonyesha uwezo kwa kuwa na mfumo wa makombora wenye uwezo mkubwa wa kupiga kwa usahihi kwenye maeneo yaliyokusudiwa, lakini  kwenye hali ya hatari inayohusisha uvurumishaji wa makombora dhidi ya taifa jingine tena taifa kubwa kama Marekani, ilipaswa kuchukua hatua za dharura kulinda usalama wa Raia ikiwa ni pamoja na kufunga anga (no-fly zone).

 Kwa kifupi uamuzi wa jeshi kuitungua ndege ya Kiraia kwa kudhania kuwa ni ndege ya adui ulikuwa ni uamuzi sahihi kwani ni jukumu la jeshi  kuhakikisha nchi inakuwa salama kwa kuzuia au kupambana na kitu chochote linachohisi kuwa kinaweza kuhatarisha usalama wa nchi. Katika medani ya vita madhara yasiyotarajiwa kwa raia wasiokuwa na hatia (collateral damage) huwa hayakosekani. Jambo la kutia moyo ni kwamba jeshi la Iran limeomba radhi na kuahidi kuimarisha mfumo wake wa ulinzi wa anga.

Vita baina ya Marekani na Iran vitasababisha janga kubwa la kibinadamu katika eneo la Mashariki ya kati na Dunia nzima ikiwa ni pamoja na kuzalisha makundi ya kigaidi, wimbi kubwa la wakimbizi na kuongezeka kwa bei za mafuta na gesi na hivyo kupelekea uchumi wa Dunia kutetereka. Juhudi za kidiplomasia zinahitajika ili kumaliza uhasama baina ya mahasimu hawa.

Ukinakili makala zangu kumbuka kufanya acknowledgement.
Napatikana kupitia email address: masudirugombana@gmail.com