Na Masudi Rugombana
Augusto Pinochet alikuwa afisa wa Jeshi na kiongozi kwa kiimla wa Chile aliyechukua madaraka kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoungwa mkono na Marekani kwa kumpindua Rais mjamaa Salvador Guillermo Allende mnamo Septemba 11, 1973 na kuitawala Chile kwa mkono wa chuma hadi Machi 11, 1990.
Utawala wake uligubikwa na mfumuko wa bei, umasikini na vitendo wa kikatili dhidi ya viongozi wa upinzani.
General Pinochet alizaliwa Novemba 25, 1915 katika jiji la Valparaiso, mji wa bandari unaopatikana kilomita 120 Kaskazini Magharibi ya mji mkuu wa Chile, Santiago. Baba yake mzee Augusto Pinochet Vera ni mtoto kutoka kwenye familia ya Wahamiaji wa Kifaransa waliofika Chile karne ya 18. Mama yake anaitwa Avelina Ugarte Martinez. Pinochet alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika shule ya Seminari ya San Rafael mjini Valparaiso kabla ya kujiunga na shule ya jeshi jijini Santiago mnamo mwaka 1931.
General Augusto Pinochet |
Alihitimu mafunzo na kujiunga rasmi na Jeshi mnamo mwaka 1935 akiwa na umri wa miaka ishirini akianzia na cheo cha luteni-usu (second Lieutenant) na kupanda ngazi hatua kwa hatua hadi kufikia Cheo cha General na hatimaye kuteuliwa na Rais Salvador Allende kuwa mkuu wa majeshi ya Chile mnamo tarehe 23 August 1973 baada ya kufanya kazi nzuri ya kusambaratisha maandamano ya wananchi waliokuwa wakipinga sera za uchumi za kijamaa za serikali ya Rais Allende.
Tarehe 11 Septemba 1973, siku kumi na nane baada ya kuteuliwa kuwa mkuu wa majeshi, General Pinochet aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Rais Salvador Allende na chama chake za mrengo wa kushoto cha Unidad Popular aliyeitawala Chile kwa muda wa miaka minne tu (1970-1973) na punde baada ya kufanikisha hayo mapinduzi, General Pinochet alijitangaza kuwa kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Chile hadi tarehe 17 Disemba 1974 alipojitangaza rasmi kama Rais wa Chile.
Ikumbukwe kuwa Rais Salvador Allende hakuwa na mahusiano Mazuri na serikali ya Marekani kutokana na msimao wake wa kufuata sera za uchumi za kijamaa, miaka minne ya utawala wake ilitawaliwa na maandamano na migomo iliyochochewa na makundi ya wananchi waliokuwa wakipinga sera zake za kimarxist.
Allende alitoa hotuba yake ya mwisho wakati vikosi vilivyoongozwa na General Pinochet vikiwa vimeizingira Ikulu, katika hotuba yake Rais Allende aligoma kujiuzulu huku akisistiza kuwa yeye ndiye rais halali wa Chile. Inaelezwa kuwa mara baada ya kumaliza kuhutubia Rais Allende alijiua kwa kujipiga risasi, akitumia bunduki aina ya AK-47 aliyozawadiwa na rais Fidel Castro wa Cuba, madai ambayo yanapingwa na wananchi wengi wa Chile, wakiamini kuwa aliuliwa.
Katika miaka mitatu ya mwanzo ya utawala wake, General Pinochet aliwakamata, kuwatesa na kuwasweka ndani wananchi laki moja na elfu thelasini (130,000) wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani waliokuwa wakipinga utawala wake. Kupitia operation mbaya na ya kikatili iliyoitwa Condor (Operation condor), Pinochet na viongozi wenzake watano wa mataifa ya Amerika kusini waliwauwa viongozi na wafuasi elfu themanini (80,000) wa vyama vya mrengo wa kushoto.
Je ni nini hiyo Operation Condor?
Hiyo ilikuwa ni operation maalum iliyoratibiwa na kufadhiliwa na Marekani kwa lengo la kupambana na sera na fikra za kijamaa katika mataifa ya Kusini mwa bara la Amerika. Tawala zilizoshiriki kwenye operation hiyo ya kikatili ni za mataifa ya Argentina, Bolivia, Brazil, Chile, Paraguay na Uruguay.
Ni hivi👉 Katikati ya miaka ya 1970, serikali za nchi sita za Amerika kusini ambazo ni Brazil, Chile, Argentina, Paraguay, Bolivia, na Uruguay zilikuwa zikikabiliwa na matukio yanayofanana. Serikali hizo zilikuwa zikitawaliwa na ama viongozi wa kihafidhina ( Conservative regimes), tawala za kiimla (Dictatorship regimes) au tawala za kijeshi ( Military Juntas) zilizokuwa zikiungwa mkono na Marekani.
Sasa basi kama ilivyo kawaida kwenye taifa lolote linalotawaliwa na mojawapo ya aina hizo za utawala upinzani mkali huwa haukosekani. Mataifa hayo yalikabiliwa na upepo mkali wa kuongezeka kwa makundi ya upinzani na wanaharakati waliokuwa wakitaka mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi. Kitisho kikubwa kwa Marekani na tawala hizo ilikuwa ni makundi au vyama vya siasa vya mrengo wa kushoto yaliyokuwa yakiungwa mkono na Cuba pamoja na Umoja wa nchi za Kisovieti.
Ili kukabiliana na hali hiyo na kuzuia ushawishi wa Soviet union katika eneo hilo, ndipo ilipoanzishwa Operation condor, operation chafu, operation ya kikatili iliyoshuhudia viongozi wa vyama vya siasa vya mrengo wa kushoto na wafuasi wao waliokuwa mstari wa mbele katika harakati, viongozi wa dini na vyama vya wakulima, wanafunzi na walimu wakikamatwa, kuteswa na kuuawa kikatili. Katika kufanikisha mkakati huo Marekani ilishiriki kikamilifu kwa kupanga mikakati na kuratibu mafunzo juu ya utesaji ikiwa ni pamoja na misaada ya kiufundi, fedha na kijeshi.
Hali ya kiuchumi na kisiasa katika utawala wake:
Aliunda timu ya vijana wachumi waliojulikana kama Chicago boys waliosomea Marekani kwenye idara ya uchumi ya Chuo kikuu cha Chicago kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
Alipunguza kodi, kubinafsisha mashirika ya umma na kuhamasisha uwekezaji kutoka nje ya nchi. Mabadiliko ambayo yalichochea kwa kiasi kikubwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Chile.
Utawala wa Pinochet uliunda katiba mpya iliyoanza kufanya kazi Mwezi Septemba mwaka 1980 akiachana na katiba ya mwaka 1925. Katiba mpya ilimpa uhalali wa kuendelea kubaki madarakani kwa muda wa miaka nane hadi mwaka 1988 ambapo hatima yake ya kuendelea kuiongoza Chile ingeamuliwa kupitia kura ya maoni.
Kwenye kura ya maoni iliyopigwa mnamo tarehe 5 Octoba 1988 asilimia 56 ya wananchi walipinga Pinochet kuendelea kuingoza Chile na hivyo kuhitimisha utawala wake uliodumu kwa muda wa miaka 16. Kilichopelekea mpaka utawala wa kiimla wa Pinochet kukubaliana na matokeo ni shinikizo kubwa kutoka kwa Wafanyabiashara wakubwa na jumuia ya kimataifa. Pamoja na kushindwa kwenye kura za maoni, General Pinochet aliendelea kuwa mkuu wa Majeshi ya Chile hadi tarehe 11 Machi 1998.
Mwisho wa zama zake.
Mwaka 1998 mwezi October, alipokwenda nchini Uingereza kwa matibabu, alizuiliwa kuondoka nchini humo kwa ombi la mahakama ya Hispania baada ya kufunguliwa mashataka ya kuhusika na utesaji wa Raia wa Hispania huko Chile wakati wa utawala wake. Hata hivyo kwa sababu ya kuzorota kwa afya yake, Waziri wa Mambo ya ndani wa Uingereza Jack Straw aliamua kuwa aruhusiwe kurudi Chile badala ya kupelekwa Hispania kukabiliana na Mashtaka. Hivyo alirejea Chile mwaka 2000 na kupokelewa na maandamano makubwa ya Wananchi waliokuwa wakimpinga.
Kutokana na shikinikizo kubwa kutoka kwa wananchi huko Chile la kutaka Pinochet ashtakiwe kwa kuhusika na mauaji na utesaji, katiba ya nchi hiyo ilifanyiwa marekebisho na kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, hivyo mwaka 2006 alifunguliwa mashtaka ya mauaji, utekaji na utesaji lakini siku chache baada ya kufunguliwa mashtaka hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya moyo na hatimaye kufariki dunia siku ya tarehe 10 Disemba 2006 akiwa na umri wa miaka 91. Wakati wa uhai wake General Pinochet alimuoa Maria Lucia Rodriguez na kufanikiwa kupata watoto watano
Wananchi wa Chile wanatofautiana mitazamo kuhusiana na General Pinochet. Wengine wanamuona kama shujaa aliyewaokoa kutoka kwenye sera za ujamaa zilizokuwa zikifuatwa na mtangulizi wake Salvador Guillermo Allende. Mafanikio ya ukuaji wa uchumi katika utawala wake yamefanya Wananchi kumuona kama shujaa na mzalendo wa kweli kwa taifa lake.
Wengine wanamuona kama ni kiongozi katili wa kiimla aliyekandamiza wapinzani wake wa kisiasa na kuhusika na mauaji ya maelfu watu waliokuwa wakiupinga utawala wake. Mafanikio yake kiuchumi wanayachukulia si lolote si chochote kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wasiokuwa na ajira, umasikini pamoja na viwango vidogo vya mishahara kwa wafanyakazi.
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana.
Email: masudirugombana@gmail.com
No comments:
Post a Comment