Saturday, February 8, 2020

IRAN: TAIFA LINALOLIPIGA HATUA KUBWA MBELE LICHA YA VIKWAZO VIKALI VYA KIUCHUMI.


Na Masudi Rugombana.

Iran, taifa linalopatikana katika eneo la kimkakati la Magharibi ya bara la Asia kati ya bahari mbili Muhimu za Arabian na Caspian linapakana na mataifa saba ambayo ni Iraq na Uturuki kwa upande wa magharibi na kaskazini Magharibi, Armenia na Azerbaijan kwa Upande wa Kaskazini, Turkmenstan kwa upande wa Kaskazini Mashariki, Afghanistan kwa upande wa Mashariki na Pakistan kwa upande wa kusini Mashariki.



Taifa hilo la kiajemi linaloshika nafasi ya 19 Duniani kwa  ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 1,648,195 limebarikiwa utajiri mkubwa wa maliasili ambazo ni mafuta (petroleum), gesi asilia( natural gas), Makaa ya mawe (coal) pamoja na madini ya chromium, copper, iron ore, lead, manganese, zinc na sulfur.

Iran ni Jamhuri ya Kiislam yenye kuongozwa kwa kufuata misingi ya sharia za kiislam chini ya kiongozi wa Kidini Ayatollah Sayyid Ali Khamenei aliyechukua madaraka mnamo tarehe 4 June, 1989 mara tu baada ya kufariki kwa kiongozi na muasisi wa mapinduzi matukufu ya Kiislam ya mwaka 1979  Sayyid Ruhollah Musavi Khomeini aliyefariki tarehe 3 June, 1989. Ayatollah Sayyid Ali Khamenei ndiye kiongozi mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu ( commander-in-chief )
 wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama vya Iran. Kiongozi wa Shughuli za Serikali ni Rais ambaye huchaguliwa na wananchi kwa njia ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura mara moja kila baada ya miaka minne. Rais wa sasa wa Iran anaitwa Hassan Rouhani.

Iran ni taifa la pili lenye nguvu kubwa za kijeshi katika eneo la mashariki ya kati baada ya Uturuki, linashika nafasi ya kumi na nne Duniani likiwaacha nyuma mahasimu wake wakuu Israel inayoshika nafasi ya kumi na saba na Saudi arabia inayoshika nafasi ya ishirini na tano (hii ni kwa mujibu wa rank za global fire power kwa mwaka huu wa 2019).

Tofauti na mataifa mengine ya mashariki ya kati, Iran ni taifa lenye uzoefu mkubwa wa kupigana vita vya muda mrefu bila kusaidiwa na mataifa mengine sambamba na kupigana vita mbadala (proxy war) za muda mrefu tena kwa mafanikio makubwa dhidi ya mahasimu wake Marekani, Israel na Saudi Arabia katika eneo lote la mashariki ya kati kuanzia Syria, Lebanon, Israel/Palestina, Iraq na Yemen ikifadhili na kutoa mafunzo ya kijeshi kwa makundi ukombozi ya wapiganaji ya Hamas, Hizbullah, Hauth na Makundi makubwa ya wapiganaji wa Kishia ya Mahd na Badr nchini Iraq ambayo yalipigana kwa mafanikio makubwa sambamba na jeshi la Iraq dhidi ya kundi la Kigaidi la Islamic State lililokuwa likifadhiliwa na kupewa mafunzo kijeshi na mataifa ya Qatar, Saudi Arabia, Israel na Uturuki.

Ni ufadhili na mafunzo ya kijeshi ya Iran ndiyo yaliyoliwezesha kundi la Hizbullah kuyashinda na kuyatimua majeshi ya Israel katika eneo la kusini mwa Lebanon katika vita iliyojulikana kama South Lebanon conflict au Security zone conflict iliyopiganwa kwa muda wa miaka kumi na tano (1985-2000). Pia ni ufadhili na mafunzo hayo hayo ya kijeshi kutoka Iran yaliyoliwezesha kundi la Hizbullah kuipeleka puta Israel katika vita baina yao iliyopiganwa mwaka 2006 kati ya July 12 hadi August 14. Vita hii inajulikana huko nchini Israel kwa lugha kiebrania kama Milhemet Levanon HaShniya ikimaanisha vita ya pili ya Lebanon (Second Lebanon War) iliyopelekea vifo vya makomandoo 121 wa Israel na wanamgambo wa Hizbullah 250. Ni katika vita hii ndipo baraza la usalama wa umoja wa mataifa lilipoingilia kati kwa kusimamia makubaliano ya kusitisha vita ikiwa ni pamoja na kupeleka askari wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa na jeshi la Lebanon kushika udhibiti katika maeneo yaliyokuwa yakishiliwa na  Hizbullah baada ya vikosi vya Hizbullah kutakiwa kujiondoa katika maeneo hayo.

Ni ufadhili wa Iran ndio ulioanzisha na kuimarisha kundi la Hamas huko ukanda wa Gaza mnamo mwaka 1985. Ni mafunzo ya kijeshi ya Iran na msaada wa silaha ndio unaolipa nguvu kubwa tawi la kijeshi la Hamas la Izzudin al Qassam na kuwaibua makamanda shupavu wa Kipalestina kama vile Mohammed Deif (Abuu Khalid) na Marwan Issa. Ni mipango iliyokwenda shule ya Iran iliyoliwezesha kundi la Hamas kutembeza kipigo cha mbwa koko kupitia mashambulizi ya kustukiza dhidi ya askari wa Israel na Walowezi wa Kiyahudi huko Gaza hadi kupelekea Waziri mkuu wa Israel Jenerali Ariel Sharon kuyaondoa majeshi ya Israel pamoja na Walowezi wa Kiyahudi huko Gaza mnamo mwaka 2005 ikiwa ni pamoja na kubomoa nyumba za Walowezi hao.

Ni ufadhili wa Iran pamoja na mafunzo ya kijeshi ndio umeifanya Saudi Arabia iliyotangaza kuwa itashinda vita vya Yemen ndani ya mwezi mmoja mwaka 2015 kushindwa kutekeleza azma yake na kujikuta ikiendelea kupigana vita bila mafanikio kwa muda wa miaka mitano sasa dhidi ya Wapiganaji wa Houthi huko Yemen licha ya kupewa misaada lukuki ya kiintelijensia na Mataifa ya Israel na  Marekani. Yaani Saudi Arabia inatia huruma kwa namna drone za wapiganaji wa Houth ambazo zinatengenezwa nchini Iran zinavyowachapa ndani ya Saudia kila kukicha.

Kinachowaumiza vichwa maadui wa Iran ni kwamba silaha inazotumia Iran katika hizo vita zote zinatengenezwa nchini Iran na wataalamu ambao ni raia wa Iran tena kwa teknolojia yao wenyewe Wairan. Mifumo ya Ulinzi wa anga ya Iran ya Khordad 3, Khordad 15 advance Air defense System na Bavar 373 ni tishio kubwa kwa ndege vita za maadui. Marekani ilionja makali ya mfumo wa Ulinzi wa anga wa Iran pale ndege yake ghali zaidi isiyokuwa na rubani (UAV) au ukipenda unaweza kuiita drone aina ya RQ-4A Global Hawk yenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 222 ilipodunguliwa mara tu ilipojaribu kuingia kwenye anga ya Iran kupitia mlango bahari wa Hormuz.  Thamani ya hiyo drone iliyodunguliwa na kombora aina ya Sayyad 3 lililovurumishwa kutoka kwenye mfumo wa ulinzi wa anga wa Khordad 3 ni sawa na ndege mbili za kizazi cha tano za F-35C stealth fighter.

Iran imepata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali licha ya vikwazo vikali vya kiuchumi ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za Ulaya Magharibi. Mafanikio hayo yametokana na taifa hilo kuwekeza zaidi katika Elimu hatua ambayo imewawezesha kupata wataalamu wengi katika fani mbali mbali hivyo kujitosheleza katika sekta mbalimbali kuanzia elimu, afya, kilimo, viwanda, nishati, madini n.k.

Leo hii Iran inatengeneza Magari yao wenyewe kuanzia ya kijeshi hadi ya kiraia tena ya kisasa, vifaru, Nyambizi, ndege za kivita na kiraia zikiwemo ndege zisizokuwa na rubani (UAV/Drones)makombora ya masafa mafupi, masafa ya kati na masafa marefu, Rockets kwa ajili ya mambo ya utafiti wa anga za mbali, meli za kivita na meli za kiraia, simu za mikononi (Smartphones) pamoja na vifaa tiba vya aina mbalimbali. Ikiwa na asilimia ishirini (20%) ardhi yenye rutuba, Iran ni mzalishaji na msambazaji mkubwa wa chakula katika eneo lote la Mashariki ya kati na katikati ya bara la Asia.


Nyambizi ya Iran inayoitwa Fateh ni mojawapo ya zana za kivita
 zinazotengenezwa nchini Iran.


Mafanikio inayopata Iran katika nyanja mbalimbali licha ya vikwazo vikali inavyowekewa kila kukicha yanatufundisha kuwa kila palipo na changamoto ndipo inapopatikana njia ya mafanikio.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

No comments:

Post a Comment