Na Masudi Rugombana
Tarehe 21 February 2022 Rais Vladmir Putin wa Urusi alitangaza kutambua uhuru wa eneo la Donbass, Jimbo la Mashariki ya Ukraine linaloundwa na mikoa miwili ya Luhansky na Donetsky, mikoa inayokaliwa na idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi. Mikoa hii ilijitangazia uhuru kutoka Ukraine mwaka 2014 kutokana na kura ya maoni iliyoongozwa na makundi ya wapiganaji kufuatia mgogoro wa kisiasa uliozusha maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Rais Viktor Yanukovych kiongozi aliyeegemea zaidi upande wa Urusi hatua ambayo Rais Vladmir Putin aliifananisha na mapinduzi ya kijeshi. Kuondolewa madarakani kwa Victor Yanukovych kulifuatiwa na maandamano makubwa ya makundi ya watu wanaounga mkono Urusi huko Mashariki na kusini mwa Ukraine ambapo mkoa wa Crimea wenye idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi uliitisha kura ya maoni iliyopelekea wakazi wake kuchagua kujiunga na Urusi hivyo kuipa uhalali Urusi kuitwaa Crimea na kuifanya eneo lake.
Tangazo la Putin kutambua uhuru wa Donbass lilifuatiwa na uingiliaji kati kijeshi tarehe 24 February 2022 katika Operesheni inayokusudia kuvunja nguvu za kijeshi za Ukraine na kuondoa matendo ya kikatili yanayofanywa na wapiganaji wa jeshi la Ukraine wenye siasa kali za kizalendo zilizogubikwa na fikra za kinazi ( Operation demilitalize and denazify). Kiuhalisia, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine una malengo mapana zaidi ya hicho kinachoitwa ukombozi wa Donbass. Ni uvamizi unachagizwa na mambo mengi ya kiusalama na kimaslahi yanayohusu Urusi zaidi ya kusudio la kuikomboa Donbass.
Baada ya umoja wa kisoviet kuanguka mwaka 1990, Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) ulijitanua kuelekea upande wa Mashariki na hatimaye kuyachukua mataifa ya eneo la Baltic, Jamhuri za Lithuania, Latvia na Estonia ambazo zilikuwa sehemu ya umoja wa Kisovieti (Soviet Union ) na kupeleka umoja huo wa kijeshi kujisogeza karibu na Moscow kwa kupakana moja kwa moja Urusi. Mwaka 2008 NATO iliweka wazi mipango yake ya kutaka kuisajili Ukraine. Ikumbukwe kuwa Rais Vladmir Putin aliwahi kusema kwamba kusambaratika kwa umoja wa Kisovieti lilikuwa ni janga kubwa katika karne ya ishirini lilipelekea Urusi kuporwa haki yake kama mojawapo ya Mataifa yenye nguvu kubwa Duniani. Putin ametumia miaka 22 madarakani kujenga upya jeshi la Urusi kwa lengo la kurejesha nguvu yake ya kiushawishi kwenye siasa, ulinzi pamoja na mahusiano ya kimataifa (Geopolitical clout)
Putin alishaweka wazi kuwa kujitanua kwa NATO kuelekea Mashariki sambamba na mkakati wake wa kuisajili Ukraine kwamba ni kitisho kisichovumilika dhidi ya Urusi, akilaumu uwepo wa vikosi vya Marekani na makombora yao kibalistic ya masafa Marefu nchini Ukraine, huku akisisitiza kuwa Ukraine ni sehemu muhimu ya Urusi kisiasa na kiutamaduni.Hivyo basi kutokana na tishio la NATO, Urusi iliamua kuongeza nguvu za kijeshi kuelekea upande wa Magharibi kwenye mpaka wake na Ukraine kwa lengo moja tu ambalo ni kufanya shambulizi (Pre-emptive strike) dhidi ya Ukraine kwa lengo la kujihami dhidi ya kitisho cha NATO. Katika jithada za kuepusha vita, NATO na Ukraine walitaka Urusi kuacha kujijenga kijeshi kwenye mpaka wake na Ukraine hivyo kufungua meza ya majadiliano baina ya pande mbili. Urusi ilitoa masharti makuu matatu ili ombi hilo la NATO liweze kutekelezwa.
1. Ipewe hakikisho kwamba Ukraine haitajiunga na NATO.
2. NATO iondoe vikosi vyake katika nchi za Ulaya Mashariki.
3. Jeshi la Ukraine Kusitisha mapigano kwenye eneo la Donbass kwa mujibu wa makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015 ambayo yaliweka masharti ya kuondolewa kwa silaha nzito kutoka kwenye uwanja wa vita, kuachiliwa kwa wafungwa wa pande zote mbili, na marekebisho ya katiba nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na utoaji wa uhuru kwa mikoa ya Donetsk na Luhansk.
NATO na Ukraine waliyakataa madai yote ya Urusi, hivyo kupelekea Urusi kutokuwa na namna nyingine zaidi ya kulinda usalama wake kwa kuivamia Ukraine katika kile kinachoitwa oparesheni maalum ya kijeshi ( Special military operation) ili kuzuia isijiunge na NATO. Ni uvamizi mkubwa wa kijeshi barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia. Lengo kubwa la Rais Vladmir Putin katika operesheni hii ni kurudisha Usawa baina ya Urusi na Marekani kwa kupunguza kitisho cha NATO.
Urusi chini ya Putin ikisimama peke yake dhidi ya Ukraine inayoungwa mkono na NATO kifedha na kijeshi inapigana kwa tahadhari kubwa, akili nyingi na kwa mipango na mikakati ya kueleweka. Jeshi lake linasonga mbele taratibu lakini kwa uhakika, likipiga hatua tatu mbele na kurudi hatua moja nyuma pale uwanja wa mapambano unapokuwa mgumu. Urusi inashinda kwenye uwanja wa vita, inapambana kwenye uwanja wa Diplomasia na inashinda kwenye kampeni kali ya vikwazo dhidi ya uchumi wake na hivyo kumkatisha tamaa Rais Volodymyr Zelenskyy na washirika zake kutoka NATO na Umoja wa nchi za Ulaya ambazo kwa kiasi kikubwa uchumi wao umeathirika vibaya kutokana na vikwazo vyao wenyewe wanavyoweka dhidi ya Urusi.
Kutekwa kwa miji muhimu kama Kherson na Mariupol lilikuwa pigo kubwa kwa Zelenskyy na NATO, lakini kudondoka kwa jiji la Severodonetsky, mji mkuu wa wakazi wa mkoa wa Luhansky wanaopinga kujitenga na Ukraine kunatuma ujumbe kwa Zelenskyy na mabwana zake wa Magharibi kuhusu uimara wa jeshi la Urusi na hatari ya Ukraine kugawanywa vipande viwili katika siku za usoni.
Kuna kila dalili kuwa Ukombozi wa Donbass hautakuwa mwisho wa uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine, kwani lengo hasa la Putin ni kuhakikisha sehemu yote ya Mashariki na kusini mwa Ukraine inakuwa chini ya Urusi, hivyo basi kutekwa kwa mikoa mitano ya Kharkiv, Dnipropetrovsk, Zaporizhia, Mykolaiv na Odesa kuelekea Tranistria ni mojawapo ya malengo yajayo ya operation maalum ya kijeshi ya Urusi inayoendelea nchini Ukraine. Hivyo basi kuna uwezekano mkubwa mapigano kuendelea kwa muda mrefu.
Hatima ya Ukraine itaamuliwa na Urusi baada ya kuteka eneo la Mashariki na kusini mwa Ukraine, hapo ndipo itajulikana kama Ukraine itamegwa na kuanzishwa taifa jipya ama eneo hilo kuwa sehemu rasmi ya Urusi. Katika sakata hili la Ukraine ni dhahiri kuwa aliyeanzisha mapigano ndiye huyo huyo atakayeyamaliza mapigano naye siye mwingine isipokuwa ni Vladmir Putin.
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana
Napatikana kupitia๐๐๐
Email: masudirugombana@gmail.com
Simu: 0743 184 044
Safi mkuu
ReplyDelete