Thursday, July 28, 2022

XINJIANG: KICHAKA CHA MATAIFA YA MAGHARIBI KATIKA HARAKATI ZA KUIDHOOFISHA CHINA.

 Na Masudi Rugombana   


Xinjiang ni mkoa mkubwa kuliko yote nchini China. Mkoa huu unaopatikana kaskazini magharibi ya China una jumla ya kilometa za mraba milioni moja, laki sita na elfu sitini na tano (1.665 million km²). Kwa ukubwa wa eneo mkoa huu umeizidi kidogo nchi ya Iran. Mkoa huu unajulikana rasmi kama XUAR yaani Mkoa unaojiendesha wa Wauighur wa Xinjiang ( Xinjiang Uighur Autonomous Region ) ni eneo lenye utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo Mafuta, gesi asilia, makaa ya mawe na dhahabu unapakana na nchi za Mongolia, Russia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Afghanistan, India na Pakistan. 



Mbali na utajiri wa maliasili, mkoa huu wenye utajiri mkubwa wa kitamaduni wenye  idadi ya makabila yenye asili, lugha, imani za kidini, mila na tabia ya tofauti umekuwa na mawasiliano ya karibu ya kiuchumi na kiutamaduni na nchi jirani inazopakana nazo. Mkoa una jumla ya watu milioni 25, ambapo watu milioni 12 sawa na asilimia 44.96 ni wa jamii ya Uighur. Wauighur, ni jamii ya Kituruki yenye uhusiano wa kitamaduni na eneo la Mashariki na Asia ya Kati. Watu wa jamii ya Han huko Xinjiang ni asilimia 42.24 na asilimia 12.80 ni watu wa jamii za Kazakh, Kyrygz, Hui, Mongol , Tibet, Xibe, Tajik, Ozbek, Manchu, Daur, Tatar na Russians (Warusi).  Lugha rasmi  zinazozungumzwa mkoani Xinjiang ni Uighur na Mandarin. Waislam ni zaidi ya nusu ya wakazi wote wa Xinjiang.  Mji mkuu wa mkoa ni Ürümqi.


China imekuwa ikishutumiwa na mataifa ya Ulaya Magharibi  kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo kufanya   mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa Uyghur sambamba na  makabila mengine yenye idadi kubwa ya watu wanaofuata imani ya dini ya Kiislam hasa katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Xinjiang.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanailaumu China kwa kuwazuilia zaidi ya Wauyghur milioni moja kinyume na matakwa yao katika makambi ya mateso ( Concentration Camp), hata hivyo serikali ya China inasema kuwa hayo sio makambi ya mateso bali  ni vituo vya mafunzo (Education training centers) vyenye lengo la kukomesha itikadi kali za kidini na kuwapa watu ujuzi mpya. 


Mapema katika karne ya 20, Marekani na nchi nyingine za Ulaya Magharibi zilianzisha juhudi za kuunga mkono harakati za kujitenga kwa mkoa wa Xinjiang ili kuunda Taifa litakalojulikana kama Turkestan Mashariki ( East Turkestan), juhudi hizo zilizokwenda sambamba na kufadhili matendo ya kigaidi huko Xinjiang kwa lengo la kuiyumbisha China na kudhibiti kasi yake ya Maendeleo.


Mnamo Mwezi August 2018 akizungumza katika taasisi ya Ron Paul (Ron Paul Institute) kanali mstaafu Lawrence Wilkerson, mkuu wa zamani wa wafanyakazi (Former Chief of staff) katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wakati huo ikiongozwa na General Mstaafu Collin Powell, alisema kwamba mojawapo ya sababu za Marekani kuwepo nchini Afghanistan ni kwa sababu kuna watu wa jamii ya Uighur huko Xinjiang wapatao milioni 20, kwa hivyo CIA ingetaka kuivuruga China kupitia harakati za WaUighur na kwamba hiyo ndiyo ingekuwa njia bora ya kufanya ili kuzusha machafuko baina ya jamii za WaUighur na Han na kwamba Marekani ingewasaidia WaUighur kuwatimua watu wa jamii ya Han na kuwaondoa katoka mkoa wa Xinjiang. 


Kwa miaka mingi, kumeibuka idadi ya taasisi zinazoipinga China ikiwa ni pamoja na kuanzishwa makundi yenye itikadi kali yanayopigania kuanzishwa kwa taifa la  Turkistan Mashariki kupitia kile kinahoitwa "uhuru" wa Xinjiang. Miongoni mwa harakati hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa bunge la Uighur na Serikali ya Turkistan Mashariki, vyote vikifanya kazi uhamishoni kwa kufadhiliwa na Marekani na Uturuki. Kwa mujibu wa vyanzo vya kiintelijensia vya China,  mwaka 2004,  Marekani ilitoa dola  milioni 8.76 kwa makundi ya watu wanaoishi nje ya Uighur wanaofanya kampeni dhidi ya China huko Xinjiang.


Ufadhili huo kutoka Marekani umesababisha kuenea haraka kwa fikra za itikadi kali za Kiislam huko Xinjiang na hivyo kupelekea Magaidi kutoka katika medani za vita nchini Afghanistan, Pakistan na Syria kumiminika kwa wingi mkoani Xinjiang. Baadhi ya makundi ya kigaidi yenye nguvu yaliendesha kampeni kali kushambulia raia wa China kupitia vuguvugu la Kiislamu la Turkestan Mashariki (East Turkestan Islamic Movement (ETIM) kati ya mwaka 1997 na 2014  yaliyogharimu maisha ya zaidi ya raia 1,000. Ikumbukwe kwamba kundi la Kiislam la ETIM lina uhusiano wa karibu na Mtandao wa Alqaeda unaoongozwa na Dr. Ayman al Zawahir. 


Katika kukabiliana na tishio la mashambulizi, serikali ya China imechukuwa hatua muhimu kuhakikisha utulivu na amani vinapatikana ili kuwezesha watu wa imani tofauti kuishi kwa pamoja katika mkoa wa Xinjiang. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kupambana kutokomeza makundi ya itikadi kali za kidini na kuweka sheria zinazolinda haki na uhuru wa kufanya ibada kwa watu wa imani zote. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha vyuo vya mafunzo ambapo makundi ya vijana wanaokamatwa kutokana na kuhusika na vurugu za kidini na kikabila hupelekwa kupewa ujuzi pamoja na kufundishwa uzalendo wa Kichina. 


Kufuatia hatua kali za kukabiliana na makundi ya itikadi kali za kidini zilizochukuliwa na serikali ya China, sasa ni miaka minne mfululizo hapajawahi kutokea shambulizi lolote la kigaidi huko Xinjiang. China inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha huduma za kijamii katika Uighur ikiwemo ukarabati wa misikiti. 


Xinjiang kuna misikiti elfu ishirini na nne, Mingi katika hiyo imejengwa miaka ya 1980 na 1990, na haikujengwa kwa Ubora unaotakiwa. Kutokana na ukuaji wa miji na vijiji kuna baadhi ya misikiti inawawia vigumu Waislamu kufanya Ibada kutokana na uchavu na kuna baadhi ya misikiti haifikiki kirahisi. Kwa hivyo Serikali ya China inafanya mambo matatu kwa ruhusa ya Waislamu wenyewe kupitia Serikali zao za mitaa. 


1. Kubomoa misikiti inayohatarisha Usalama na kujenga misikiti mipya, imara na ya kisasa.

2.Kukarabati Misikiti ya zamani 

3. Kuhamisha misikiti iliyojengwa mahala ambapo ni vigumu kufikika kwa kujenga sehemu ambayo ni kubwa zaidi na rahisi kufikika sambamba na upanuzi wa misikiti yenye maeneo madogo ya kufanyia ibada. 


Kinachofanywa na vyombo vya habari vya Ulaya Magharibi ni kupiga picha misikiti mibovu inapovunjwa kwa ajili ya ukarabati na kisha kuitangazia Dunia kuwa China inavunja misikiti huko Xinjiang. Lengo la propaganda hizo ni kuichafua China katika Ulimwengu wa Kiislamu. Propaganda ambazo zimeshindwa kuyashawishi Mataifa mengi ya Kiislam ikiwemo Umoja wa Ushirikiano wa nchi za Kiislamu (OIC) kuilaani China. 


Suala la Waislamu kuzuiwa kusali, kuzuiwa kutumia majina ya Kiarabu, kuzuiwa kufunga saumu ya Ramadhani na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe ni mojawapo ya propaganda chafu zinazoenezwa na vyombo vya habari vya magharibi dhidi ya China. Ukweli ni kwamba Uhuru wa kuabudu mkoani Xinjiang ulikuwa mashakani kipindi ambacho makundi ya Itikadi kali za kidini yalipoimarisha harakati zao, ilikuwa ni vigumu kwa Waislamu kufanya ibada hadharani kutokana na tishio la kushambuliwa, pia viongozi wengi wa Kiislamu waliopingana na makundi ya itikadi kali walilengwa na kuuawa. 


Mara baada ya Serikali ya China kukomesha harakati za makundi ya Kiislam yenye itikadi kali, katika kipindi cha miaka minne mfululizo Waislamu wamekuwa wakifanya ibada misikitini bila hofu sambamba na kushiriki ibada nyingine kama hija na funga ya Ramadhan. Kati ya mwaka 1996 hadi 2019, Jumuiya ya Kiislamu ya China  kwa kushirikiana na Serikali imeweza kugharamia hija kwa Waislamu elfu hamsini wa Xinjiang kwa safari za ndege za kukodi kwenda Makka, na pia kutoa huduma za tafsiri na matibabu. 


China ni Taifa linaloongozwa na serikali isiyofuata imani yeyote ya kidini (Secular State) ikiwa na Jumla ya watu Bilioni moja na milioni mia nne kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020. Waislamu wanakadiriwa kufikia milioni 28 sawa na asilimia 1.73 wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya Hui wakifuatiwa na watu kutoka jamii ya Uighur. Hata hivyo kwa takwimu zisizo rasmi China inakadiriwa kuwa na idadi ya Waislamu milioni 150. Asilimia 74.5 ya Wachina ni Wapagani, Mabudha ni asilimia 18.3 na Wakristo ni asilimia 5.1.


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.


© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇


Email: masudirugombana@gmail.comSimu: 


0743 184 044

No comments:

Post a Comment