Saturday, August 22, 2020

DENG XIAOPING: MBUNIFU WA CHINA YA KISASA ALIYEIFUNGUA CHINA NA CHINA IKAFUNGUKA

Na Masudi Rugombana

Huyu ndiye Baba wa uchumi wa China, ndiye aliyeasisi, aliyejenga na kusimamia ipasavyo misingi ya mfumo wa uchumi wa soko huria, na kufanya mageuzi mengi yanayoifanya leo hii China kuwa dola kuu la pili kiuchumi baada ya Marekani na hata kutishia kuipiku Marekani. Waswahili husema ukiona vyaelea ujue vimeundwa, kwa hivyo ukiona China ya kisasa namna inavyomeremeta basi tambua kuwa ni kazi nzuri iliyofanywa na Deng Xiaoping. 

Deng Xiaoping

Yaani huyu mzee kwa mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake, imefikia hatua Dunia nzima inamtambua kama Mbunifu wa China ya kisasa (the architect of Modern China). Naam, ni huyu ndiye aliyeifungua China na China ikafunguka.

CHINA ILIKUWAJE HAPO KABLA?
Tarehe 1 Octoba 1949 Mao Tse Tung alitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu China, nchi ya Chama kimoja, ikiongozwa na Chama cha Kijamaa cha CPC. Katika kipindi chote cha utawala wake, Mwenyekiti Mao aliiongoza China katika misingi ya kijamaa akifanya maamuzi mengi magumu kupitia kampeni mbali mbali zilizokwenda sambamba na mipango ya muda mrefu na muda mfupi. Lengo likiwa ni kuibadilisha China kutoka taifa lenye kutegemea Kilimo pekee na kuwa taifa la viwanda. 

Miongoni mwa kampeni hizo ni Kampeni dhidi ya wapinzani wa mfumo wa kijamaa katika kile kilichoitwa Mapinduzi ya utamaduni ikilenga kuwamaliza kabisa wafuasi wa Chama cha Kuomintang, Wafanyabiashara matajiri na wanasiasa ambapo watu milioni mbili na laki sita walikamatwa, watu milioni moja na laki tatu walitupwa magerezani. Katika kampeni hii watu laki saba waliuawa na wengine kwa maelfu kulazimika kukimbilia Taiwan.  

Baada ya kukamilika kwa kampeni dhidi ya wapinzani wa sera ya kijamaa, Mwenyekiti Mao alianzisha kampeni kubwa ya mageuzi ya umiliki wa ardhi iliyoitwa Tugai ( Chinese Land Reform Movement) iliyohusika na utaifishaji wa ardhi ukihusisha mashamba na majengo yaliyokuwa yakimilikiwa na watu binafsi, lengo la kampeni hii likiwa ni kupambana na tatizo la ukosefu wa usawa wa kiuchumi kwani wakulima matajiri ambao walikuwa ni asilimia kumi (10%) tu ya Wachina wote walimiliki asilimia 80 ya ardhi yote yenye rutuba huku Wakulima wadogo ambao ni asilimia tisini (90%)wakimiliki asilimia 20.

Mao aliwapokonya umiliki wa mashamba wakulima Matajiri na kuyagawa kwa wakulima masikini ambapo jumla ya wakulima masikini milioni mia tatu walipewa asilimia 45 ya ardhi yote iliyokuwa ikimilikiwa na wakulima matajiri. Ni kampeni iliyofanywa katika hali ya kutisha kwani wamiliki wa ardhi na nyumba waliuawa kwa kushambuliwa na wakulima wadogo pamoja na wapangaji wao,  huku wengine wakilazimika kuimbia China bara na kuhamia Taiwan. 

Miaka tisa baadae (1958) Mao alianzisha kampeni nyingine ngumu iliyojulikana kama hatua kubwa kuelekea mbele (The great leap forward) ambapo watu waliondolewa kwenye mashamba yao binafsi na kuhamishiwa kwenye mashamba ya ujamaa. Kilimo katika mashamba binafsi kilipigwa Marufuku huku Mamilioni ya wakulima wengine wakilazimishwa kuachana na kilimo na kufanya kazi kwenye viwanda vya uzalishaji chuma kwani uzalishaji chuma ulipewa kipaumbele kama hitaji muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Viwanda. 

Kutokana na mageuzi hayo hali ya uzalishaji chakula ilipungua kati ya mwaka 1958 hadi 1962 kutokana na sekta ya kilimo kuyumba hivyo kupelekea China kuingia kwenye janga kubwa la njaa. Licha ya matokeo chanya hapo baadae, madhara makubwaa yaliyosababishwa na kampeni hii katika miaka mitatu ya mwanzo ni kuibuka kwa janga kubwa la njaa kati ya mwaka 1958 hadi 1962 lililopekea vifo vya watu milioni 15 kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya China.

Ni maamuzi hayo magumu yaliyomuwezesha Mwenyekiti Mao kuujenga uchumi wa China kwa mpangilio, kuibadilisha China kuwa nchi ya viwanda huku akiwezesha wananchi kushiriki kimamilifu katika ujenzi wa nchi na kufanikiwa kuondoa tofauti kubwa ya kipato baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho. Ni mafanikio yaliyoacha majeraha makubwa miongoni mwa Wachina huku utawala wake ukipelekea China kutengwa na jamii ya kimataifa, hasa mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani.

CHINA CHINI YA UONGOZI WA DENG.
Muda mfupi baada ya kushika hatamu ya kuongoza China mnamo tarehe 22 December 1978, Deng alianzisha mkakati uliopewa jina "kuondoa machafuko na kurudi katika hali ya kawaida"akikusudia kurekebisha matatizo ya kiuchumi na kijamii yaliyotokana na sera ya Mapinduzi ya utamaduni iliyotekelezwa kipindi cha utawala wa Mao Tse Tung.

Aliifanyia marekebisho sera ya uchumi wa kijamaa iliyotekelezwa na Mao kwa kuanzisha Ujamaa mpya unaoendana na mazingira ya China katika kile kilichoitwa sera ya uchumi mchanganyiko (Mixed Economy) ambapo baadaye mnamo mwaka 1992 mrithi wake Jiang Zemin aliibadilisha jina na kuiita sera ya kijamaa ya uchumi wa soko (socialist market economy). Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya kiuchumi waliitambua kama sera ya ubepari wa kidola (State Capitalism)

Ni hapo ndipo alipoifungua China kwa uwekezaji wa kigeni na kuondoa vizuizi vingine vya biashara huku serikali ikiendelea kushikilia njia kuu za uchumi wakati huo huo ikishirikiana kwa karibu na makampuni binafsi makubwa yanayomilikiwa na matajiri wazawa kama Huawei, ZTE, Lenovo na Alibaba. Uwekezaji mkubwa wa makampuni kutoka nje hasa Barani Ulaya na Marekani umeshika kasi kutokana na uhakika wa Malighafi, soko na nguvu kazi. Leo hii China ni taifa la kwanza kwa kuwa na uchumi mkubwa (PPP ranking) Duniani ikifuatiwa na Marekani.


Licha ya sera yake  kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wahafidhina ndani ya chama lakini imefanikisha sana kuifanya China kuwa mojawapo ya mataifa yenye uchumi imara (GDP ranking) ikishika nafasi ya pili baada ya Marekani huku idadi ya Wachina waliokuwa wakiishi kwenye umasikini uliokithiri ikipungua kutoka asilimia tisini (90%) mwaka 1981 mpaka asilimia mbili (2%) mwaka 2013. 

Pamoja na mafanikio makubwa aliyopata, utawala wake unakumbukwa zaidi kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza. 
Nguvu kubwa iliyotumika kusambaratisha Waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa Tiananmen (Tiananmen square) jijini Beijing June 04 mwaka 1989 wakidai Demokrasia na uhuru wa kujieleza ilipelekea vifo vya mamia kwa maelfu ya waandamanaji na hivyo kuutia doa utawala wake mbele ya jumuiya ya kimataifa. Walichosahau waandamanaji waliokuwa wakiungwa mkono na mataifa ya Ulaya Magharibi na Marekani ni kwamba Deng Xiaoping aliruhusu Demokrasia ya Uchumi na hakutaka Demokrasia ya siasa.

HUYU NDIYE DENG XIAOPING
Alizaliwa tarehe 27 August 1904 katika kijiji cha Paifang, kwenye mji wa Xiexing, jimbo la Sichuan. Ni mtoto kutoka familia ya wasomi, iliyokuwa na hali nzuri kimaisha, akitumia jina la Xixian enzi za utotoni. Baba yake Mzee Deng Wenming alikuwa msomi wa Sheria na Sayansi ya siasa, Mama yake alijulikana kwa jina la Dan na alifariki akimwacha mwanae wa mwisho Deng akiwa bado kijana mdogo. 

Mwaka 1920 baada ya kumaliza elimu ya msingi katika shule ya Chongqing, akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 16, Deng Xiaoping na vijana wenzake 80 waliosoma shule moja walipanda meli kuelekea Ufaransa kwa lengo la kujiendeleza kimasomo. Ikumbukwe kuwa Ufaransa ni taifa la kwanza barani Ulaya kupokea wahamiaji kutoka China. 

Nchini Ufaransa mambo hayakuwa sawa kama alivyotarajia kwani alijikuta akitumia muda wake mwingi kufanya kazi, zaidi kazi zisizokuwa na ujuzi kama vibarua kwenye viwanda vya magari na chuma hadi kazi za usaidizi wa wapishi kwenye migahawa. Kwani hali ya uchumi barani Ulaya na Dunia kwa ujumla haikuwa nzuri kwa wakati huo kutokana na athari zilizotokana na vita kuu ya kwanza ya Dunia. Hata familia yake huko China haikuwa na uwezo wa kumtumia ada. Hivyo alitumia mshahara mdogo aliopata kujilipia ada ya shule (middle school) huko Chatillon, jijini Paris.

Kipindi cha miaka mitano alichotumia kwenye masomo yake huko Ufaransa, kutoka umri wa miaka 16 hadi 21, kilibadilisha fikra zake kutoka kwenye kundi la vijana wazalendo na kuwa mfuasi wa itikadi ya Karl Max (Marxism ideology). Ni hapo ndipo ulipokuwa mwanzo wa kufuata nadharia za kijamaa na  kimapinduzi akizisambaza kwa vijana raia wa China waliokuwa masomoni barani Ulaya kupitia makala alizokuwa akiandika kwenye Jarida la Nuru Nyekundu (Red Light), jarida lililoanzishwa mahususi kuwawezesha Wachina waliokuwa wakiishi kwenye mataifa ya Ubelgiji, Ujerumani na Ufaransa kujifunza nadharia za kizalendo kwa taifa lao. 

Kiwango cha fikra pevu kilianza kuongezeka miongoni mwa wanafunzi wa Kichina barani Ulaya kwani wengi walianza kuamini katika nadharia ya kijamaa. Chini ya ushawishi wa wakubwa zake kama Zhou Enlai na Zhao Shiyan, Deng Xiaoping alianza kujifunza itikadi za kijamaa na kufanya propaganda za kisiasa. Mwaka 1922 alijiunga na jumuia ya vijana ya Chama cha kijamaa cha China barani Ulaya na mwaka 1924 alijiunga rasmi na chama cha kijamaa cha China (Chinese Communist Part-CCP) na kuwa mmojawapo wa viongozi wa tawi kuu la vijana la chama barani Ulaya.

Mwaka 1926 Deng Xiaoping na kundi la vijana wenzake wa Chama cha kijamaa waliondoka Ufaransa kuelekea Moscow nchini Urusi (Soviet Union) na kujiunga na chuo kikuu cha kijamaa cha Toilers of the East (KUTV) kabla ya kuhamishiwa kwenye chuo kikuu cha Sun yat-sen, chuo kilichopewa jina kwa heshima ya Muasisi wa mapinduzi ya China. Huyu alikuwa mwanafalsafa, mwanafizikia na mwanasiasa  aliyeongoza mapinduzi dhidi ya Utawala wa kinasaba wa Qing (Qing dynasty). Sun yat-sen Ndiye Rais wa kwanza wa Jamhuri ya China na kiongozi wa kwanza wa Chama tawala cha Kuomintang (Nationalist Part of China). Huko nchini Taiwani anatambulika kama Baba wa taifa.

Baadaa ya miaka sita nje nchi, hatimaye Deng alirejea China mwaka 1927 akitokea Urusi (Soviet union). Alirejea kipindi ambacho hapakuwa tena na ushirikiano baina ya chama cha Kijamaa (CCP) na Chama tawala cha Kuomintang ambapo hali ya kisiasa ilikuwa tete, huku taifa likiekea kugawanyika baina ya wafuasi wa sera za kijamaa na kibepari kutokana na vita vya kiraia. Alipata mafunzo ya kijeshi na kuwa miongoni wa wapiganaji wa jeshi la chama cha kijamaa ambalo baadae lilibadishwa jina na kuitwa Jeshi la ukombozi la watu wa China. 

Baada ya chama cha kijamaa kupata ushindi dhidi ya chama cha Kuomintang na Mao Zedong kutangaza kuanzisha Jamhuri ya watu wa China mnamo mwaka 1949, Deng Xiaoping alipanda ngazi mbali mbali ndani ya Chama, Serikali na Jeshini kuanzia Katibu mkuu wa Chama cha kijamaa(CCP)  kwa nyakati tofauti mpaka mwaka 1956, Waziri wa fedha kuanzia mwaka 1953-1954, mkuu wa Jeshi la China kati ya mwaka 1975 mpaka 1980, Naibu Waziri mkuu 1977-1978 na hatimaye Kiongozi mkuu wa China kuanzia mwaka 1978 mpaka 1989.

Alifariki tarehe 19 February mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 92 kwa ugonjwa wa mapafu na ugonjwa wa kutetemeka mwili pasina hiari unaojulikana kama Parkinson. Alikuwa Baba wa watoto watano aliozaa na mkewe Zhuo Lin. Msiba wake uliombolezwa kitaifa kwa muda wa wiki moja huku bendera zikipepea nusu mlingoti. Viungo vyake (Organs) vilitumika katika utafiti wa kimatibabu, mwili wake ulichomwa moto na majivu yake yalitawanywa baharini kama alivyoelekeza kabla kifo chake.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia๐Ÿ‘‡๐Ÿ‘‡๐Ÿ‘‡
Email: masudirugombana@gmail.com
Simu: 0743 184 044

No comments:

Post a Comment