Monday, May 29, 2017

KAMPENI ZA UCHAGUZI KENYA ZAANZA RASMI

Kampeni zimeanza rasmi nchini Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 8 mwezi wa nane mwaka huu.

Wakati uo huo Tume ya Uchaguzi imeanza zoezi la siku mbili kuwaidhinisha wagombea urais.

Rais Uhuru Kenyata ambaye pia ni mgombea wa
chama cha Jubelee akisalimiana na
Rais Donard Trump wa Marekani kwenye mkutano wa nchi za G7.
Mgombea wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga tayari ameidhinishwa pamoja na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka na kuzindua kampeni zake rasmi jijini Nairobi.


Akiwahutubia wafuasi wake, Odinga amesema ikiwa atashinda urais, atapambana na ufisiadi na wale wenye doa hawataruhisiwa kufanya kazi katika serikali yake.

Aidha amesema kuwa serikali yake itahakikisha kuwa inashusha gharama ya maisha kwa muda wa siku 90 watakazokuwa madarakani lakini pia kupunguza kodi ya nyumba.

Rais Uhuru Kenyatta anayewania kwa muhula wa pili, anatarajiwa kuidhinishwa leo na Tume ya Uchaguzi na baadae kuzindua kampeni zake katika uwanja wa michezo wa Nyayo jijini Nairobi.

Mbali na wagombea hao wawili wakuu wanaopewa nafasi kubwa kupambana katika kinyanganyiro hicho, wagombea wengine nane wamejitosa uwanjani wengi wakiwa wagombea binafsi.

Maswala muhimu yatakayojiri katika kampeni:-
Rais Uhuru Kenyatta anasema anataka kuendeleza rekodi anayosema ni ya maendeleo nchini humo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli ya kisasa na mradi wa umeme kuwafikia idadi kubwa ya wakenya hadi kijijini.

Kenyatta anajivunia ujenzi wa reli ya kisasa atakayoizindua wiki ijayo kutoka Mombasa hadi jiji kuu Nairobi. Mradi huu unatarajiwa kurahihisha usafiri wa abiria na mizigo kati ya miji hiyo miwili.
Rais Kenyatta na mgombea mwenza wake ambaye ni Naibu rais William Ruto, wanatarajiwa kutumia mafanikio haya kujitafutia uungwaji mkono.

Hata hivyo, upinzani umeendelea kuishutumu serikali ya rais Uhuru Kenyatta kwa kujihusisha na ufisadi na kukopa fedha kupita kisiasi kutoka nje ya nchi. Utovu wa usalama pia ni suala ambalo upinzani unasema serikali ya sasa imeshindwa kushughulikia.

Kundi la Al Shabab limekuwa likiwashambulia raia wa kawaida na maafisa wa usalama kama polisi na wanajeshi, tangu kuingia madarakani mwaka 2013.
Kupanda kwa gharama za maisha hasa siku za hivi karibuni uhaba wa unga wa mahindi na sukari.
Serikali imelazimika kuingilia kati na kuamua kununua mahindi kutoka nchini Mexico ili kuwawezesha wananchi kupata unga kwa bei nafuu.

Wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema ushindani mkubwa wa kisiasa unatarajiwa kati ya rais Kenyatta na Odinga. Siasa za Kenya bado hazijaegemea sera lakini zinaendelea kuegemea ukabila na ukanda.

Thursday, May 25, 2017

UJUE UGONJWA WA KIDOLE TUMBO (APPENDIX), DALILI ZAKE NA MATIBABU.

Kidole tumbo au Appendix hupatikana katika utumbo mkubwa, urefu wake ni kama kidole cha mwisho cha mkono. Sehemu hii hupitisha myeyuko wa chakula na endapo katika chakula hicho kuna michanga au vitu vidogovidogo vigumu, hujikita humo na kushindwa kutoka.


Kidole tumbo pia kinapatikana upande wa kulia wa tumbo kutoka usawa wa kitovu na nyonga ya kulia.
Taka ngumu hizo zikishajikita kwenye kidole  tumbo na kushindwa kutoka ndipo kinapoanza kuvimba, hali hii kitaalam huitwa ‘Inflammation’. Hapa kidole tumbo kinavimba na kuwa na maumivu na pia hupata maambukizi ya bakteria.



Dalili za ugonjwa
Mgonjwa huanza kuhisi maumivu ya tumbo  kuanzia usawa wa kitovu ambayo huwa makali na kuacha kisha kusambaa taratibu kuelekea upande wa kulia.

Baada ya muda mgonjwa huanza kutapika  kisha kupata homa. Dalili hizi huwa haziji pamoja, huanza moja na kufuata nyingine lakini mgonjwa akiwahi kupata tiba dalili nyingine haziendelei. Baada ya hapo mgonjwa hupata homa.

Dalili za ugonjwa zinatofautiana kufuatana na aina ya ugonjwa huu ambapo kawaida umegawanyika katika hali ya ukali ‘Acute’ na hali ya usugu ‘chronic’. Maumivu makali yanayoambatana na homa na kutapika tunaita ni ‘Acute’
Maumivu ya ugonjwa huu ukifikia hatua mbaya husambaa hadi katika uti wa mgongo usawa wa kitovu au ‘Belly button’.

Pamoja na kwamba maumivu huanzia usawa wa kitovu, lakini dalili za awali kabisa huanzia juu ya kitovu ambayo huja na kupotea na mgonjwa anaweza kujihisi ana ugonjwa wa vidonda vya tumbo, baadaye ndipo hushuka chini taratibu na kusambaa.

Dalili hizi ni tofauti na watoto ambao hulalamika tumbo linauma sehemu zote kukiwa hakuna eneo maalam na baadaye maumivu huwa makali sana kwa tumbo lote hata akiguswa linauma sana.
Hali ya tumbo kuuma huambatana na kujaa gesi kwa wote yaani wanaume, wanawake na watoto.

Chanzo cha tatizo
Kama tulivyoona hapo awali chanzo cha tatizo, maumivu makali ‘Acute’ hapa hutokana na vile vitu vigumu vilivyoingia katika kidole tumbo kushindwa kutoka hivyo huziba kwa juu na zile taka ngumu huganda humo na kidole tumbo kuzidi kuvimba.

Hali ya usugu wa maumivu hutokana na taka ngumu hizo kukaa humo kwa muda fulani na baadaye hutoka huku ukiacha hali ya kidole tumbo kuwa na uvimbe.

Hali ya uvimbe ikikaa muda mrefu husababisha mzunguko wa damu kuzuiliwa sehemu hiyo hivyo kidole tumbo huvimba zaidi na husababisha kuta za Appendix kuharibika ‘Necrtotic’ na kukusanya majimaji kama usaha.
Hali hii husababisha tatizo liitwalo ‘Peritonitis’ yaani tumbo lote huathirika na kuuma. Mgonjwa akichelewa kupata tiba, usaha huu husambaa katika mfumo wa damu na kusababisha kifo.

Uchunguzi
Huzingatia historia ya mgonjwa, dalili na ishara zitajitokeza, vipimo vya damu vitafanyika, vipimo vingine ni vya Ultrasound na CT Scan ya tumbo vitasaidia kujua tatizo kwa undani zaidi.
Zipo pia njia mbalimbali za uchunguzi ambazo daktari anaweza kuzitumia mfano ‘Rovsing’s sign’ na  sitokovkty’s sign na nyinginezo.

Matibabu
Tatizo hili katika hatua za awali mgonjwa anaweza kutibiwa kwa dawa lakini tatizo linapoendelea inabidi afanyiwe upasuaji kuondoa Appendix.


Tatizo likiwa kubwa, upasuaji wa dharura hufanyika. Ni vema uwahi hospitali kwa uchunguzi na tiba.

Saturday, May 13, 2017

FAO LA KUJITOA LAFUTWA

Dodoma. Serikali imesema fao la kujitoa halipo, badala yake imekuja na fao la bima ya afya.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Vijana), Jenista Mhagama alisema hayo bungeni jana kuwa suala la fao la kujitoa haliwezekani kwa sasa na badala yake imeanzisha mchakato wa fao la bima ya afya ambalo itakuwa
ni mbadala wa fao la kujitoa.

Waziri Jenister Mhagama


“Katiba ya Tanzania katika kifungu cha 11 kinaeleza namna ambavyo mifuko hiyo(akimaanisha ya hifadhi ya jamii) inapaswa kuwa, lakini hata juzi Mheshimiwa Rais aliagiza utengenezwe utaratibu katika bima ya mfuko na itakuwa ni mbadala wa watu wasiokuwa na ajira,” alisema Mhagama.

Mapema bungeni jana, swali kuhusu malipo ya mafao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii liliwaibua wabunge wengi waliotaka kuuliza maswali ya nyongeza licha ya mawaziri kutoa majibu.

Akijibu swali la wafanyakazi waliopatikana na vyeti feki kama wanaweza kulipwa mafao yao, Waziri wa Utumishi Angella Kairuki ali hatuwezi kutoa taarifa kwa sasa kwani bado wanashughulikia jambo hilo ili kuona namna bora ya kufanya na wakifikia hatua nzuri watatoa majibu ya kuaminika na kuomba wapewe muda kwa sasa

Mapema mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel alitaka kujua kwa nini wafanyakazi waliopatikana na vyeti feki wasilipwe mafao yao.
Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Anthony Mavunde alisema kuanzishwa kwa mifuko ya jamii kumefikia hatua mbalimbali ikiwamo kukamilika kwa tathimini ya mifuko ya hifadhi ya jamii (actuarial evaluation) ambayo imetoa mapendekezo kuhusu namna bora na mambo ya kuzingatia katika kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Mpaka sasa Serikali haijafanya uamuzi rasmi wa idadi ya mifuko itakayobaki baada ya kulinganisha mifuko iliyopo hivi sasa,” alisema Mavunde. Source: Gazeti la Mwananchi

Friday, May 12, 2017

Rais Sudani Kusini amfuta kazi mkuu wa majeshi

Juba.

Habari zinasema kuwa, Rais Salva Kiir, amechukua hatua ya kumfuta kazi Paul Malong Awan, kufuatia majenerali wengi wa ngazi ya juu jeshini kujiuzulu kutokana na kuwepo ubaguzi na jinai nyingi za kivita zinazofanywa na jeshi la Sudan Kusini.

Rais Salva Kiir akimpandisha cheo mkuu mpya wa Majeshi
James Ajongo

 Habari zinasema kuwa, Rais Kiir amemteua James Ajongo kuchukua nafasi ya Malong Awan kwa ajili ya kusimamia shughuli za jeshi la taifa hilo changa zaidi barani Afrika. Inafaa kuashiria kuwa, mbali na serikali ya Juba kupambana na wanamgambo wa upinzani, lakini pia jeshi la serikali nalo linakabiliwa na mgogoro wa ndani, ambapo makamanda kadhaa jeshini wamekuwa wakitangaza kujiuzulu nyadhifa zao.

Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko mwezi Disemba mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kwamba alikula njama za kutaka kumpindua. Katika machafuko hayo, maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Licha ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita mwezi Agosti mwaka 2015, lakini bado machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea nchini Sudan Kusini.

Trump alaumiwa kwa mapokezi aliyompa Lavrov

Serikali ya Marekani imekumbwa na changamoto mpya kufuatia kuenea picha za Rais Donald Trump wa nchi hiyo akimkaribisha kwa hadhi Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov katika ikulu ya White House.

Rais Trump akizungumza na Waziri wa Mambo ya nje wa
Urusi Sergey Lavrov(kushoto) Ikulu mjini Washington.

Rais Trump amekutana na Lavrov pamoja na balozi wa Russia mjini Washington, Sergueï Kisliak katika ikulu ya nchi hiyo. Hata hivyo, picha zilizomuonyesha Trump akionyesha tabasamu kwa kukutana na viongozi hao wa Russia, zimeibua malalamiko kwa Wamarekani ambao wanaiona Moscow kuwa hasimu wa taifa hilo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani, mkutano huo wa Trump na viongozi hao wa Russia, haukuwafurahisha wanadiplomasia wa Marekani na kwamba mapokezi ya Trump kwa Lavrov hufanyiwa viongozi wenye hadhi ya urais. Habari zaidi zinasema kuwa, kitendo cha kutandikwa zulia jekundu kwa wanadiplomasia hao wa Russia, ni harakati ya kuzisifia siasa za Moscow, katika hali ambayo hadi sasa nchi hiyo inatuhumiwa kuingilia uchaguzi wa rais wa mwaka jana nchini Marekani.

Wamarekani anaoandamana kumpinga Rais Trump
Katika mkutano huo baina ya Rais Donald Trump na Sergey Lavrov viongozi hao wamezungumzia juu ya namna ya kutekelezwa makubaliano kwa ajili ya kutengwa maeneo yenye kiwango cha chini cha mivutano chini Syria hususan karibu na mipaka ya Syria na Jordan. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, katika mazungumzo hayo hakukujadiliwa vikwazo vya Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya nchi yake.