Saturday, December 22, 2018

MISRI ILISHINDA VITA YA YOM KIPPUR DHIDI YA ISRAEL NAYO ISRAEL ILISHINDA DHIDI YA SYRIA.

Na Masudi Rugombana.

Vita ya Yom Kippur (Yom Kippur war) kama inavyojulikana huko Israel au Operation Badri kama inavyojulikana huko nchini Misri au Ramadan War kama inavyojulikana katika Ulimwengu wa Kiarabu na ukipenda unaweza kuiita Vita baina ya Waarab na Waisrael ya mwaka 1973 (Arab-Israel war of 1973) ilipiganwa baina ya Misri na Syria kwa upande mmoja dhidi ya Israel.

Kulikuwa na mambo makuu mawili yaliyopelekea kuzuka kwa vita hii. Jambo la kwanza ni kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro uliotokana na matokeo ya vita ya siku sita. Mgogoro huo si mwingine bali ni kurejeshwa kwa ardhi iliyotekwa na Israel ambayo ni eneo la Sinai kwa upande wa Misri na Milima ya Golan kwa upande wa Syria. Juhudi za kuleta amani zilizofanywa na umoja wa mataifa kupitia azimio namba 242 na zile za Rais Anwar Sadat wa Misri hazikuzaa matunda.

Anwar Sadat

Mara baada ya kuingia Madarakani tarehe 15 October 1970, Rais Mohamed Anwar el-Sadat alikusudia kufikia makubaliano ya kudumu ya amani na Israel ambapo Misri ingeitambua rasmi Israel kama taifa huru iwapo Israel ingejiondoa katika eneo la Sinai. Hata hivyo Israel chini ya Waziri mkuu Bi Golda Meir ilikataa mazungumzo na Misri na pia ilikataa kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Sinai.

Sababu ya pili iliyopelekea kuzuka kwa vita ya Yom Kippur inafanana na ile ya kwanza, nayo ni kwamba Israel haikuwa na nia ya kufikia makubaliano ya amani na Waarab kwa kujiondoa kwenye ardhi ya Waarab iliyoiteka katika vita ya siku sita badala yake Israel iligeuza maeneo ya Waarabu iliyoyateka kuwa kama ukanda mkubwa uliokatazwa kufanyika harakati za kijeshi  (Huge buffer zone) kwa ajili ya kujihakikishia usalama wake. Jeuri hii ya Israel ilitokana na kuamini kuwa Jeshi lake (IDF) lilikuwa na nguvu kubwa ya kutoweza kushindwa na majeshi ya nchi za kiarabu.

Kwa kuzingatia kwamba hapakuwa na maendeleo yeyote kuelekea kupatikana kwa amani itakayorejesha eneo la Sinai kwa Misri, Rais Anwar Sadat aliamua kuingia vitani kwa malengo yenye mipaka maalum.
Anwar el-Sadat, mwanasiasa mwenye kipaji na mwanajeshi aliyerithi madaraka kutoka kwa rais wa muda mrefu Gamal Abdel Nasser aliamini kuwa hakuwa na chaguo lingine isipokuwa kuingia vitani dhidi ya Israel. Aliamini kuwa Israel chini ya Waziri mkuu shupavu Mwanamama Goda Meir kamwe isingeweza kuingia kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu bila kutishiwa kijeshi.

Sadat hakuwa amepanga kuiangamiza Israel kwa sababu aliamini kuwa hilo lisingewezekana kutokana na Uimara wa Jeshi la Israel, pia alitambua kuwa Marekani kamwe isingekubali kumuona Mshirika wake Israel akiangamia.

Hivyo kusudio lake ilikuwa ni kushusha kipigo cha kushtukiza ili kulitikisa jeshi la Israel ambalo lilikuwa limejengwa kisaikolojia kama jeshi lisiloshindwa kirahisi kufuatia ushindi mkubwa wa kihistoria lililopata katika vita ya siku sita dhidi ya Mataifa Manne ya kiarabu (The Six day war or 1967 Israel-Arab war).
Sadat aliwahi kunukuliwa akisema "Kama tukifanikiwa kuteka angalau hata inchi nne za ardhi ya Sinai basi hali itabadilika kuanzia Mashariki, Magharabi na Sehemu zote"

Sadat aliamini kuwa alipaswa kushambulia kwa nguvu na kwa haraka na kwamba kitisho cha mashambulizi kingelazimisha Marekani na Soviet Union kujiingiza katika vita kwa Marekani kuilinda Israel na Soviet  kuisaidia Syria ili kuimarisha ushawishi wao katika eneo la Mashariki ya kati.

Hali hii ingeulazimu umoja wa Mataifa kuingilia kati ili kusimamisha mapigano katika wakati ambao Misri ingekuwa tayari imesharudisha baadhi ya sehemu yake ya  ardhi iliyotekwa na Israel katika vita ya siku sita  hivyo kurahisisha uwezekano wa kufikia Makubaliano ya kudumu ya amani na Israel.

Misri ilianza kuimarisha majeshi yake mwishoni mwa mwaka 1972 kwa kununua zana za kisasa za kijeshi kutoka
Soviet Union kama vifaru aina ya  T-62 ndege za kivita (Jet fighters) aina ya Mig 23, Mig 21, Mig 17, Su 7 nk. Pia makombora ya kutungua ndege (Ant-Aircraft missiles), makombora ya kulipua vifaru (ant-tank missiles) na Makombora yenye kuongozwa na mitambo maalum (Guided Missiles)

Hata hivyo maandalizi yote ya Misri kuhusiana na kuvuka mfereji wa Suez yalivuja hivyo kumpa Rais Anwar Sadat sababu ya kuwafukuza wakufunzi wa kijeshi elfu ishirini kutoka Urusi (Soviet Union) mnamo tarehe 01 Julai mwaka 1972 ikiwa ni mojawapo katika mkakati wa kujenga taswira ya kuaminika na Marekani na hivyo kuitumia Marekani
kuishawishi Israel ikubali pendekezo la Misri la kufanya mazungumzo ili kufikia amani ya kudumu.

Katika jitihada za kufanikisha mpango huo,  Rais Anwar Sadat alianzisha Cheo kipya cha Mshauri wa Masuala ya Usalama na kumteua Mwanadiplomasia Mohammed Hafez Ismail ambaye alikuwa balozi wa Misri kwa nyakati tofauti katika nchi za Uingereza, Ufaransa na Italia kuwa mshauri wake wa Masuala ya Usalama. Lengo la uteuzi huo lilikuwa ni kufungua mlango wa majadiliano na Israel kwa lengo la kufikia makubaliano ya kudumu ya amani.

Mei 20 Mwaka 1973 Rais Sadat alimtuma mshauri wake wa masuala ya Usalama Mwanadiplomasia  Mohammed Hafez Ismail kwenda Marekani kufanya Mazungumzo na Mshauri wa Masuala ya usalama wa Marekani Dr. Henry Kissinger kwa lengo la kuishawishi Marekani ikubaliane na mpango wa amani wa Misri ambapo Misri ingeitambua haki ya Israel kama taifa huru kwa makubaliano kuwa Israel irejeshe ardhi ya Sinai kwa Misri.

Marekani ilikubaliana na pendekezo hilo na kuliwasilisha rasmi kwa Waziri mkuu wa Israel Golda Meir na Waziri wake wa Ulinzi Moshe Dayan. Israel ilikataa pendekezo la Misri na hivyo kuendelea kukalia eneo la Sinai.

Hatua ya Israel kukataa kufanya mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu ndiyo iliyopelekea Rais Anwar Sadat kuingia rasmi vitani.

Syria nayo ilikuwa katika maandalizi mazito ya vita kama ilivyokuwa kwa upande wa Israel kwa lengo la kukomboa ardhi yake ya Milima  ya Golan. Rais Hafez al Assad aliamini kuwa njia pekee ya kuweza kurudisha ardhi ya Milima ya Golan sio nyingine zaidi ya ushindi kwenye medani ya vita. Chini ya Marais Anwar Sadat na Hafez al Assad, Misri na Syria zilikubaliana kuunganisha majeshi yao chini ya kamandi moja.

Ilipofika Octoba 03 mwaka 1973 maandalizi yote ya vita yalikuwa yamekamilika  na vita ilipangwa kuanza tarehe 6 October 1973 Mwezi wa Ramadhan ambapo tarehe kama hiyo nchini Israel ilikuwa ni sikukuu ya kidini kubwa kuliko zote ijulikanyo kama Yom Kippur. Siku ambayo shughuli zote za kiserikali husimama ikiwa ni pamoja na matangazo katika vituo vya radio na runinga. Pia wanajeshi wengi nchini Israel huwa wanakuwa mapumziko wakisherehekea sikukuu hii tukufu kwa imani ya Kiyahudi.

Misri ilipeleka wanajeshi laki moja iliyowagawa katika Makundi (divisions) tano sambamba na vifaru 1350 na mizinga 2000 ikiwa ni maandalizi ya shambulio la kuvuka mfereji wa Suez (Suez Canal).

Ilipofika October 6 majira ya saa nane kamili mchana Misri ilifanya shambulizi zito la kustukiza la anga likihusisha ndege za kivita 200 dhidi ya Vikosi vya Israel vilivyokuwa vimejiimarisha kwenye mstari wa kujihami wa Bar lev (Bar-Lev Defensive line). Mstari huu wa kujihami wa Bar-lev ni tuta kubwa la udongo lililokuwa na kimo cha futi 66 na umbali wa kilomita 150 (Maili 93) kutoka Kaskazini hadi kusini ya mfereji wa Suez.

Tuta hilo ilitengenezwa na Israel upande wa Mashariki wa Mfereji wa Suez wakati wa vita iliyojulikana kama Vita ya Msuguano ( The War of attrition) iliyopiganwa kati ya July 1, 1967 hadi August 7, 1970 baina ya Israel dhidi ya Syria, Jordan, Chama cha ukombozi wa Palestina (P.L.O) na Misri ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyotokana na ushindi mnono wa Israel katika vita ya siku sita. Israel ilitengeneza tuta hili kama ngao kwa ajili ya kujihami na mashambulizi kutoka majeshi ya Misri yaliyokuwa upande wa Magharibi ya mfereji wa Suez.

Askari 32,000 wa Misri walifanikiwa kuvuka mfereji wa Suez na kuwatimua askari wa Israel waliokuwa wakiimarisha ulinzi kwenye mstari wa kujihami wa Bar lev na hivyo kufanikiwa kuzishambulia ngome za majeshi ya Israel. Kwa mujibu wa Kamanda Saad Mohamed el-Shazly ambae alikuwa mnadhimu mkuu wa jeshi la Misri wakati wa vita ya Yom Kippur ni kwamba ndani ya masaa sita tokea kuanza kwa vita majeshi ya Misri yalikuwa tayari yameshasambaratisha ngome kumi na tano za kijeshi za Israel na hivyo kusonga mbele kilomita kadhaa ndani ya ardhi ya Sinai.

Wanajeshi wa Misri
Wakisimika bendera ya Taifa
lao Mara baada ya kuingia
Katika ardhi ya Sinai 
Baada ya siku tatu tokea kuanza kwa Mashambulizi ya Misri, Israel ilikuwa tayari imeshahamasisha askari wake tayari kwa vita ambapo ilipeleka vikosi zaidi kwa ajili ya kuongeza nguvu huko Sinai na hatimaye kufanikiwa kuyazuia majeshi ya Misri kusonga mbele zaidi.

Kwa upande wa milima ya Golan askari elfu arobaoni wa Syria wakiongozwa na Luteni Jenerali Ali Aslan wakiwa na Vifaru 1300 vingi kati ya hivyo ni aina ya T-55s vya Kisoviet, mizinga 600, ndege za kivita 100 na Makombora 400 ya kutungulia ndege walivuka mstari wa kusitisha vita wa mwaka 1967 unaojulikana kama Purple ( Purple Cease fire line ) na kuyashambulia majeshi ya Israel yaliyokuwa na vifaru 170 tu na mizinga 60 hivyo  kuyarudisha nyuma hadi kwenye mpaka wa nchi hiyo na Israel wa kabla ya mwaka 1967.
Majeshi ya Syria hayakuishia hapo bali yaliendelea kufanya mashambulizi mazito ndani ya ardhi ya Israel.

Hali ilikuwa mbaya kwa upande wa Israel kwa sababu ndani ya siku nne tu ndege zake 49 za kivita ziliangushwa pamoja na vifaru 500 vilikuwa tayari vimeshaharibiwa. Hali ya hofu ilitawala ndani ya Serikali. Kwenye kikao chake na Waziri mkuu Golda Meir, waziri wa Ulinzi Moshe Dayan alijadili kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za Nyuklia, kwani kwa wakati huo Israel ilikuwa na Mabomu 13 ya Nyuklia kwenye ghala lake la makombora mjini Jericho.
Waziri Mkuu Golda Meir hakukubaliana na pendekezo la kutumia silaha za nyuklia, badala yake aliomba msaada wa silaha kutoka Marekani.

Golda Meir
Rais Richard Nixon na Mshauri wake wa Masuala ya Usalama Dr. Henry Kissinger waliamini kuwa Israel kushindwa vita na nchi zinazotumia silaha za Kisoviet ungekuwa ni mkasa wenye athari mbaya sana kwa maslahi ya Marekani. Hivyo basi rais Richard Nixon aliidhinisha msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 2.2 kwenda Israel.

Jeshi la anga la Marekani lilizindua operation iliyopewa jina la Nickel Grass (Operation Nickel Grass) kati ya October 14  na November 14, 1973 kwa kusafirisha tani elfu 22 za silaha kuelekea Israel. Miongoni mwa silaha zilizosafirishwa ni  Vifaru aina ya M60,  Mizinga na Mabomu. Tani nyingine elfu 33 za silaha zilisafirishwa kwa njia ya bahari. Inaelezwa kuwa huo ilikuwa ni zaidi ya  msaada wa kijeshi, ulikuwa ni msaada wa kuokoa maisha.

Baada ya kuongezewa nguvu na Marekani, Majeshi ya Israel yakiongozwa na Makanda Rafael Eitan, Dan Laner, na  Moshe Peled yalijibu mashambulizi kwa ustadi wa hali ya juu na hivyo kufanikiwa kuyaondoa majeshi ya Syria kutoka milima ya Golan ndani ya siku tatu. Baada ya kuikamata  milima ya Golan, Israel ilifanya mashambulizi makali ndani ya Syria kwa muda wa siku nne mfululizo na ndani ya wiki moja vifaru vya Israel vilikuwa vikishambulia viunga vya mji mkuu wa Syria Damascus kutoka umbali wa takriban kilometa 30 tu. Ikumbukwe kuwa Mji mkuu wa Syria Damascus unapatikana Kilomita 71.93 sawa na Maili 44.70 tu kutoka eneo la Milima ya Golan.

Kwa upande wa Sinai Vikosi vya Israel ambayo vilipangwa katika divisions tatu vikisaidiwa na ndege za kivita aina ya A-4E Skyhawk na  F-4E Phantoms havikufanikiwa kuyarudisha majeshi ya Misri nyuma ila viliweza kuyazuia kusonga mbele kwa upande wa Kaskazini mashariki na katikati ya mfereji wa Suez.

Kwa upande wa kusini ya mfereji wa Suez, kati ya October 16 hadi October 27 vikosi vya Israel vikiongozwa na makamanda Ariel Sharon, Danny Matt, Amnon Reshef, Haim Erez na Avraham Adon vilifanikiwa kuwazingira kila upande wanajeshi 35,000 wa Misri kutoka kikosi cha tatu chini ya Makamanda Abd Rab el-Nabi Hafez Na Ibrahim El-Orabi hivyo kuzuia shehena ya silaha na chakula iliyotakiwa kwenda kwa vikosi hivyo, lengo likiwa ni kuvilazimisha vikosi hivyo kusalimu amri jambo ambalo halikufanikiwa

Baada ya kufanikiwa kuwazingira askari hao wa Misri vikosi vya Israel vilifanikiwa kuvuka mfereji wa Suez kwa upande wa kusini bila upinzani mkubwa na kufanikiwa kuteka eneo la ardhi lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 1600 (1600 square Km) karibu na Miji ya Suez na Ismailia hivyo kuviwezesha kuwa umbali wa Kilomita 100 kuelekea mji mkuu Cairo katika operation iliyopewa jina la Abirey-Halev. Operation iliyosababisha vifo vya askari wengi na uhalibifu mkubwa wa dhana za kivita kwa pande zote mbili.

Hata hivyo vikosi vya Israel havikuweza kusonga mbele zaidi kuelekea Cairo kutokana na uhaba wa Silaha na uchache wa askari kuweza kukabiliana na mashambulizi   ya anga yaliyokuwa yakifanywa na Misri katika eneo hilo lililotekwa na Israel ikiwa ni pamoja na kuvunja daraja ili kuzuia vikosi vya Israel kuingia au kutoka kwa sababu askari wa Israel walikuwa wanategemea njia moja tu ya kuwawezesha kuingia na kutoka katika eneo hilo la mashariki ya Suez. Hali hii ilipelekea mkwamo wa kijeshi (Militarily stalemate) kwa kila upande kushindwa kusonga mbele.

Mkwamo huo ulisababisha hali ya Wasiwasi wa kushambuliana kijeshi  baina ya Marekani na Soviet baada ya kiongozi wa Soviet Leonid Brezhenev kutishia kuchukua hatua za kijeshi iwapo Israel ingeendelea na msimamo wake wa kuzuia mahitaji ya kibinadamu kuwafikia askari wa Misri iliyokuwa imewazingira katika eneo la kusini Mashariki ya mfereji wa Suez. Kitisho hiki kutoka Soviet kiliifanya Marekani nayo kuviweka vikosi vyake katika hali ya tahadhari.

Ni wakati huo ndipo rais Anwar Sadat alipotoa mwito wa kusitishwa kwa vita akisema kwamba aliingia vitani huku akijua uwezo halisi wa nchi yake na kwamba halikuwa kusudio lake kupigana vita na Marekani akilaumu msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Marekani kwenda Israel.

Bahati nzuri wasiwasi ulitanzuliwa baada ya Israel kwa kushinikizwa na Marekani kukubali kuruhusu mahitaji ya kibinadamu kuwafikia askari hao.

Katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo, kati ya tarehe 21 October 1973 hadi tarehe 7 November 1973 rais Richard Nixon alimtuma Mshauri wake wa Masuala ya Usalama Dr. Henry Kissinger kwenda Moscow, Tel Aviv  na Cairo kujadiliana na kiongozi wa Soviet  Leonid Brezhenev, Waziri Mkuu Golda Meir na rais Anwar Sadat  namna ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita.

Hatimaye tarehe 11 November 1973 Israel na Misri zilisaini makubaliano ya kusitisha vita yaliyoandaliwa na Dr. Henry Kissinger na Rais Anwar Sadat yaliyopelekea vikosi vya Israel kuondoa mzingiro dhidi ya kikosi cha tatu cha jeshi la Misri na wakati huo huo Misri ilisitisha mashambulizi ya anga dhidi ya wanajeshi wa Israel waliokwama umbali wa km 100 kutoka Cairo hivyo kuwapa nafasi ya kuvuka mfereji wa Suez na kurejea Sinai.

Syria ilikataa kusaini makubaliano hayo ingawa pande hasimu yaani Israel na Syria zilikubali kusitisha mapigano. Mnamo tarehe 31 May 1974 nchi hizo zilifikia makubaliano ambapo Israel ilirudisha majeshi yake nyuma hadi kwenye mstari wa kusitisha vita wa mwaka 1967 (Purple cease fire line) huko kwenye milima ya Golan.

MATOKEO YA VITA KWA UPANDE WA SYRIA:
Malengo ya Syria kuikomboa Milima ya Golan yalishindwa na badala yake Israel ilifanikiwa kuendelea kuikalia milima hiyo huku ikihamishia uwanja wa vita ndani ya ardhi ya Syria hadi kufikia hatua ya kutishia kuuteka mji mkuu wa Syria Damascus.

MATOKEO YA VITA KWA UPANDE WA MISRI:
 1. Misri ilirejesha kipande kidogo cha sehemu ya ardhi iliyotekwa na Israel kwenye eneo la Sinai. Kipande hicho ni pwani ya Mashariki ya Mfereji wa Suez.

 2. Misri alifanikiwa katika mkakati wake wa kuileta Israel katika meza ya Mazungumzo ya amani ili kufikia makubaliano ya kudumu

 3. Mazungumzo ya amani ya Camp David (1978 Camp David Accords)
yaliyotokana na matokeo ya vita ya Yom Kippur yalipelekea kusainiwa kwa mkataba wa kudumu wa Amani baina ya Misri na Israel hivyo Israel kujiondoa moja kwa moja kwenye ardhi ya Sinai.

Mkataba wa amani wa Camp David  ulipelekea Israel na Misri kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Hivyo kuifanya Misri kuwa taifa la kwanza la Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Hatua iliyosababisha Rais Anwar Sadat kuchukiwa na Ulimwengu wa Kiarabu.

Rais Anwar Sadat, (Kushoto) na
   Waziri mkuu wa Israeli Menahem
Begin wakishikana mkono baada
ya  kusaini mkataba wa amani
mbele ya Rais Jimmy Carter
(katikati) kwenye Ikulu ya
Marekani (White house)
 March 26, 1979. 
Hii ndiyo sababu inayofanya Misri kila mwaka kufanya sherehe za kuadhimisha kumbukumbu ya Ushindi dhidi ya Israel katika vita ya Yom Kippur licha la kwamba katika vita hiyo idadi ya wanajeshi wake waliopoteza Maisha ilikuwa kubwa zaidi kuliko Israel sambamba na zana nyingi za kivita kuharibiwa vibaya, lakini malengo yote yaliyopelekea Misri kuingia vitani yalifanikiwa.

NINI KILITOKEA NCHINI ISRAEL BAADA YA MATOKEO MABAYA YA VITA YA YOM KIPPUR?
Waziri mkuu wa Israel Mwanamama Golda Meir alitangaza kujiuzulu mnamo April 10, 1974 na kukabidhi rasmi madaraka mnamo June 3, 1974 kwa Waziri mkuu mpya Yitzak Rabin kufuatia shutuma nzito alizotupiwa kutokana na kupuuza baadhi ya taarifa muhimu za kiintelijensia hivyo kupelekea matokeo mabaya ya vita ya Yom Kippur yaliyopelekea hasara kubwa ya mali na vifo vya askari wengi wa Israel kuwahi kutokea katika historia ya Israel tangu kuasisiwa kwa taifa hilo mwaka 1948.

Israel ilipata funzo kupitia Vita ya Yom Kippur kuwa licha ya ushindi iliyowahi kupata katika vita vilivyotangulia vya mwaka 1948, mgogoro wa Suez na vita ya siku sita isingeweza tena kuwa na uhakika wa kuzitawala kijeshi nchi za kiarabu. Hofu hii ndiyo iliyopelekea Israel kulainika na kulazimika kuingia kwenye mazungumzo kutafuta suluhu ya mgogoro wake na mataifa ya kiarabu.

Ukinakili makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.

© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

•Napatikana kwa mawasiliano yafuatayo:-
Simu namba  +255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com
            rugombanamasudi@live.com

Friday, November 9, 2018

ZHOU ENLAI: MWANADIPLOMASIA MASHUHURI ALIYEMALIZA UHASAMA KATI YA CHINA NA MATAIFA YA ULAYA MAGHARIBI NA KUJENGA MSINGI WA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA MATAIFA YA AFRIKA.

Na Masudi Rugombana.

“Kwa hakika huyu ni mtu mwenye ubongo bora kuliko watu wote niliowahi kukutana nao katika nyanja ya siasa za kimataifa” Maneno haya aliyatamka Dag Hammarskjöld wakati huo akihudumu katika nafasi ya ukatibu mkuu wa umoja wa mataifa alipokuwa akimzungumzia Zhou Enlai, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Utawala wa Mao Zedong (Mao Tse Tung)

Zhou Enlai

Zhou Enlai (tamka Chou En-lai) anatajwa kuwa miongoni mwa wanadiplomasia mashuhuri kabisa kuwahi kutokea nchini China na barani Asia. Alihudumu katika cheo cha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya watu wa china kuanzia Octoba 1949 hadi Januari 1976 na wakati huo huo akitumikia cheo cha Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China kati ya mwaka 1949 hadi mwaka 1958. Anaheshimika zaidi nchini mwake kuwa ndiye Muasisi wa diplomasia ya China na Mhamasishaji mkubwa wa amani Duniani. Yeye pamoja na Mao ndio waliosisi na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa sera huru ya mambo ya nchi za nje ya China. Ndiye mwanadiplomasia aliyefanya juhudi kubwa za kuondoa uhasama uliokuwepo baina ya Jamhuri ya watu wa China na Mataifa ya Ulaya Magharibi, uhasama uliotokana na vita ya Korea.

Mwaka 1971 Zhou Enlai alikutana kwa siri na Henry Kissinger, mshauri wa masuala ya usalama wa rais Richard Nixon wa Marekani alipokwenda China kwa ajili ya kuandaa mkutano kati ya marais Richard Nixon na Mao Tse Tung. Ni matokeo ya mkutano huo ndio yaliyoanzisha uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China ambapo Marekani iliruhusu meli zake kufanya biashara na China huku zikipeperusha bendera za nchi nyingine (under foreign flags) na kuruhusu China kuuza bidhaa zake nchini Marekani kwa mara ya kwanza tokea kumalizika wa vita vya Korea.

Juhudi za Mwanadiplomasia Zhou Enlai zilipelekea uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Marekani kuimarika zaidi baada ya kufanikisha ziara ya kihistoria ya rais Richard Nixon mnamo mwaka 1972.  Na hatimaye  Marekani kutangaza rasmi kuitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kuvunja uhusiano wa moja kwa moja wa kidiplomasia na Kisiwa cha Taiwan mwaka 1979. Pia umahiri wake katika masuala ya diplomasia ndio uliofanikisha kurejesha kiti cha Jamhuri ya Watu wa China katika umoja wa Mataifa mnamo October 25 mwaka 1971,  awali ya hapo,  Taiwan ndiyo ilikuwa ikitambuliwa rasmi kama Mwakilishi halali wa wananchi wa China katika umoja wa Mataifa.

USHIRIKIANO BAINA YA CHINA NA MATAIFA YA AFRIKA
Ni Zhou Enlai ndiye aliyeasisi  Ushirikiano baina ya China na Afrika. Ni baada ya kuhudhuria mkutano wa Bandung ( Bandung Conference), mkutano wa Kwanza mkubwa baina ya Nchi za Afrika na bara la Asia ulifanyika huko nchini Indonesia mwaka 1955 uliohudhuriwa na mataifa 29, sita kutoka Afrika ambayo ni Ethiopia, Misri, Libya, Sudan, Liberia na Guinea. Mkutano huo ulikusudiwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi za Asia na Afrika, pia kupinga ukoloni na ukoloni mamboleo. Mkutano  wa Bandung ulikuwa ni mojawapo katika hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote ( The Non-Aligned Movement ).

Ni katika mkutano huo ndipo Zhou Enlai alipofanya majadiliano ya kwanza na nchi za Kiafrika yaliyopelekea kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia  baina ya China na nchi za kiafrika. Na mwaka ulifuata (Mwezi May, 1956) Misri ikawa taifa la kwanza barani Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China. Hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1960 nchi kumi za Afrika ikiwa ni pamoja na Morocco, Algeria na Sudan zilikuwa tayari zimeshaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China.

Uhusiano baina ya China na Afrika uliimarika zaidi baada ya Ziara ndefu ya siku 51 ya Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai kwenye mataifa kumi ya Afrika kati ya December 14, 1963 hadi February 04, 1964, akiweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu katika Serikali ya China kuzuru bara la Afrika akitembelea mataifa ya Misri, Somalia, Tunisia,  Ethiopia, Algeria, Morocco, Ghana, Mali, Guinea na Sudan. Ziara hiyo inaelezwa kuwa ndio ziara ndefu kuliko zote kuwahi kufanywa na kiongozi wa China barani Afrika.

ZHOU ENLAI  AITEMBELEA TANZANIA
Tanganyika ilikuwa ni miongoni mwa nchi alizopanga kutembelea, lakini ziara yake iliahirishwa kutokana na kuingiliana na tukio la kihistoria la mapinduzi ya Zanzibar. Hata hivyo Zhou Enlai alifanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania mnamo June 4, 1965 kwa Mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Julius Nyerere. Ziara ambayo ilifungua ushirikiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi baina ya China na Tanzania.

Zhou Enlai na Julius Nyerere

Ni wakati huo ndio vita baridi ikishika kasi na Mataifa mengi ya Afrika yakijipatia uhuru kutoka kwa Wakoloni. Mengi yakiogopa kufuata sera za kijamaa na kushirikiana na Mataifa Makubwa ya kijamaa kama China na Urusi kwa hofu ya kutengwa,  kuwekewa vikwazo na kunyimwa misaada na Wakoloni wao wa zamani ambayo ni Mataifa ya kibepari ya Ulaya Magharibi. Ndipo china ilipotoa hakikisho kwa mataifa hayo kuwa:

"Kama watawaletea maneno matupu bila vitendo,  China itawafanyia kwa vitendo,  na kama Watajenga nusu, kisha wakaacha bila kumalizia,  China itakuja kumalizia sehemu iliyobaki" hiyo ilikuwa ni ahadi nzito kwa Mataifa ya Afrika  kutoka Jamhuri ya watu wa China iliyotolewa na Waziri Mkuu Zhou Enlai alipokuwa akizungumza na Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ziara yake hapa Tanzania.

Julius Nyerere hakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka Afrika Mashariki  kufanya mazungumzo na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka China. Kwani wakati wa harakati za kupinga ukoloni barani Afrika,  mwanaharaka kutoka visiwani Zanzibar na mfuasi kindakindaki wa sera za kijamaa Abdulrahaman Mohammed Babu wakati huo akiwa katibu wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party ndiye alikuwa Mwafrika wa kwanza kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati  kutembelea Jamhuri ya watu wa China mwaka 1959 akiwa katika kampeni ya kushawishi taifa hilo la kijamaa kuunga mkono harakati za kupinga ukoloni barani Afrika. Ni wakati huo ndipo Abdulrahman Babu alipokutana na kufanya Mazungumzo na viongozi wa chama cha kijamaa cha China (Chinese Communist Party-CCP) akiwemo Waziri mkuu na Waziri wa Mambo ya nchi za nje Zhou Enlai.

Ni ukaribu huo wa Abdulrahman Babu na Wachina ndio uliopelekea watawala wa kikoloni wa Uingereza visiwani Zanzibar kumwita "The best known Sinophile in Tanzania”  ikimaanisha mtu anayevutiwa sana na aina ya maisha na utamaduni wa Kichina.

Abdulrahaman Mohammed Babu  akihudumu katika cheo cha Waziri wa biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa kiungo muhimu kati ya China na Tanzania na anaelezwa kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mkataba wa mradi wa ujenzi wa reli ya TAZARA inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia. Reli iliyotoa mchango mkubwa sana katika  harakati za ukombozi kwa Mataifa ya Kusini mwa Afrika.

HUYU NDIYE ZHOU ENLAI
Alizaliwa tarehe 05 March 1898 katika Mji wa Huaian, Jimbo la Jiangsu Mashariki ya China katika familia ya watu wasomi yenye kipato cha hali ya juu. Bahati mbaya wazazi wake walifariki akiwa bado mtoto hivyo alichukuliwa na mjomba wake mwaka 1910 na kwenda kuishi katika mji wa Shenyang kaskazini ya China, Ilipata elimu yake ya msingi katika shule ya Dongguan Model Academy, Mwaka 1913 mjomba wake alihamishiwa katika mji wa Tianjin ambapo Zhou Enlai alihama pamoja na mjomba wake na kuendelea na masomo katika shule maarufu ya Nankai Middle School shule iliyokuwa ikifundisha kwa kufuata mitaala ya elimu ya Kimarekani.

Baada ya kumaliza masomo na kupata ufaulu mzuri katika shule ya Nankai, mwaka 1917 Zhou Enlai alikwenda Tokyo Japan kuendelea na elimu ya juu. Mwaka 1919 Zhou Enlai alirejea China na kushiriki katika Maandamano  yaliyojulikana kama May Fourth Movement ( Maandamano makubwa yaliyoshirikisha vijana wasomi wakipinga hatua dhaifu zilizochukuliwa na serikali ya China dhidi ya mkataba wa  Versailles (Treaty of Versailles) uliomaliza vita kuu ya kwanza ya Dunia na kupelekea peninsula ya Shadong ambayo ni ardhi ya China iliyokuwa ikikaliwa na Ujerumani kuangukia Mikononi mwa Japan. Zhou Enlai alikuwa ni miongoni mwa Waandamanaji waliokamatwa na kutupwa jela.

Baada ya kuachiwa huru mnamo mwaka 1920 Zhou alisafiri kuelekea Marseilles nchini Ufaransa kwa ajili ya kazi na masomo. Alijiunga na Chama Cha Kijamaa cha China (CCP) akiwa nchini Ufaransa mara tu baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1921 ikiwa ni matokeo ya  harakati za May Fourth Movement.

Baada ya kumaliza masomo nchini ufaransa, Mwaka 1924 Zhou Enlai alirejea nchini China na kuendeleza harakati za kisiasa katika chama cha CCP katika mji wa Guangzhou. Mwaka uliofuata (1925) alimuoa Deng Yingchao, mwanafunzi mwanaharakati ambaye baadaye alikuwa mwanachama maarufu wa chama cha CCP. Umaarufu wa Zhou katika chama cha CCP uliongezeka zaidi na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama sambamba na kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa idara ya jeshi katika kamati kuu ya chama cha CCP mwaka 1927.

Kutokana na kushika kasi kwa vita vya kiraia vya China kati ya Wafuasi wa Chama tawala cha Kuomintang chenye kufuata sera za kibepari na wafuasi wa chama cha kijamaa cha CCP,  Zhou aliukimbia mji wa Guangzhou na kwenda katika mji wa Jiangxi kushirikiana na Mao Zedong ambaye alikuwa akiendeleza kambi za kijamaa katika maeneo ya vijijini tangu mwaka 1928. Baada ya wafuasi wa sera za kijamaa kushinda vita na kukiondoa madarakani chama Tawala cha Kuomintang mwaka 1949 , Chama cha CCP kilitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Uongozi wa Mao Tse Tung ambaye alimteua Zhou Enlai kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa mambo ya nje. Zhou Enlai aliaga Dunia mjini Beijing tarehe 8 January 1976  akiwa na umri wa miaka 77,  alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kibofu cha mkojo akiacha mke na watoto wawili wa kupanga (Adopted Children)

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

Thursday, July 19, 2018

AHMED MOHAMED KATHRADA: ALAMA YA MAPAMBANO DHIDI YA UBAGUZI WA RANGI NCHINI AFRIKA KUSINI


Na Masudi Rugombana

Alikuwa Mwanasiasa, mtetezi wa haki za binadamu na Mwanaharakati mkubwa wa kupinga sera za kibaguzi za utawala wa Makaburu wa Afrika ya Kusini. "Uncle Kathy" kama anavyojulikana kwenye mitaa ya miji mbalimbali huko Afrika kusini jina lake halisi ni Ahmed Mohamed Kathrada.

Ahmed Mohamed Kathrada

Mwanaharakati huyu anayeheshimika kama alama ya mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi (Anti Apartheid Icon) alihukumia kifungo cha maisha jela mwaka 1964 sambamba na Nelson Mandela, Walter Sisulu, Govan Mbeki, Andrew Mlangeni, Billy Nair, Elias Motsoaledi, Raymond Mhlaba and Denis Goldberg katika kesi maarufu iliyojulikana kama Rivonia akishtakiwa kwa makosa ya hujuma, kutaka kuiangusha serikali na kuanzisha vita vya msituni (guerrilla war)

MAISHA YAKE YA UTOTONI NA HARAKATI ZAKE DHIDI YA UBAGUZI WA RANGI
Ahmed Mohamed "Kathy" Kathrada alizaliwa tarehe 21 August 1929 katika mji mdogo wa Schweizer Reneke katika jimbo la Western Transvaal  ( North West Province). Ni mtoto wa nne kati ya watoto sita waliozaliwa na Wazazi wahamiaji Waislamu wa madhehebu ya Bohra kutoka jimbo la Gujarat nchini India.

Kutokana na asili yake ya kihindi, hakuweza kuandikishwa shule katika jimbo la Transvaal kwa sababu sera ya elimu ya wakati huo ilikuwa inapiga Marufuku Watu wasiokuwa wazungu kusoma katika shule za wazungu na wasiokuwa Waafrika kusoma katika shule za Waafrika. Hivyo alilazimika kwenda katika jiji la Johanesburg umbali wa mile 200 kujiunga na shule ya Wahindi (Indian School).

Akiendelea na masomo, Kathrada ilivutiwa na harakati za kupinga ubaguzi wa rangi dhidi ya watu wa jamii ya kihindi katika jimbo la Transvaal zilizokuwa zikifanywa na Dr. Yusuph Dadoo kiongozi wa harakati za kudai uhuru katika jimbo la Transvaal. Harakati zake kisiasa zilianza mwaka 1941 akiwa na umri wa miaka 12 wakati alipojiunga na jumuiya ya vijana wanaofuata itikadi ya ujamaa (Young Communist League of South Africa) akisambaza vipeperushi mitaani vilivyokuwa vikipinga sera za kibaguzi. Kathrada alikuwa mjumbe mwanzilishi wa jumuiya ya vijana wa kihindi wanaofanya kazi za kujitolea katika jimbo la Transvaal (Transvaal Indian Volunteer Corps) ambayo baadae ilibadili jina na kuitwa Transvaal Indian Youth Congress na kumchagua Kathrada kuwa mwenyekiti wake.

Mwaka 1951, alijiunga na Chuo Kikuu cha Witwatersrand,  baadaye aliachana na masomo ya chuo ili apate muda wa kutosha wa kujishughulisha na harakati za ukombozi. Ni mwaka huo huo ndipo alipochaguliwa kuongoza ujumbe wa vijana kutoka makundi ya watu wenye rangi mchanganyiko (multi-racial South African delegation)  kuhudhuria mkutano wa vijana Duniani uliofanyika huko Berlin nchini Ujeruman na mkutano wa kimataifa wa Wanafunzi uliofanyika Warsaw nchini Poland.
Alipokuwa Poland, alipata fursa ya kutembelea kambi ya mateso na mauaji ya Auschwitz (Auschwitz concentration camp) ziara inayoelezwa kuwa iliongeza chachu katika harakati zake za kupinga ubaguzi rangi. Baadae alikwenda Budapest nchini Hungary ambapo alifanya kazi kwa muda wa miezi tisa katika makao makuu ya Shirikisho la kimataifa la demokrasia kwa vijana (World Federation of Democratic Youth) kabla ya kurejea Afrika Kusini kuendeleza harakati za ukombozi.

Kutokana na kuimarika kwa ushirikiano baina ya vyama vya Kihindi na Kiafrika katika mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi kwenye miaka ya 1950, ni wakati huo ndipo Ahmed Kathrada alipokuwa na mawasiliano ya Karibu na viongozi wa chama cha African National Congress (ANC) kama Nelson Mandela na Walter Sisulu na alikuwa ni miongoni mwa wanaharakati 156 walioshitakiwa kwa makosa ya uhaini katika kesi iliyodumu kuanzia mwaka 1956 hadi 1960 na hatimaye kuachiwa huru baada ya kukutwa hawana hatia.
Baada ya chama cha ANC na taasisi kadhaa zilizokuwa zikiendesha kampeni ya kupinga ubaguzi wa rangi kupigwa marufuku nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 1960, Ahmed Kathrada aliendeleza harakati zake za kisiasa licha ya kukamatwa mara kwa mara. Mara baada ya kuzidi sana kuwekewa vizuizi vya nyumbani, mwaka 1962 Ahmed Kathrada aliamua kuendesha harakati zake za ukombozi akiwa mafichoni.

Tarehe 11 July 1963, mwaka mmoja baada ya kukimbilia mafichoni, Ahmed Kathrada alikamatwa akiwa ndani ya makao makuu ya kikundi ya kijeshi cha Umkhonto we Sizwe (Vuguvugu la kupigania haki na tawi la kijeshi la chama cha ANC) huko katika kitongoji cha Rivonia, nje kidogo ya jiji la Johannesburg. Alishitakiwa pamoja na Nelson Mandela na wanaharakati wengine nane na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1964 katika kesi maarufu iliyojulikana kama kesi ya Rivonia.

Alitumikia kifungo kwenye magereza yenye ulinzi wa hali ya juu katika kisiwa maarufu cha Robben (Robben Island) na Pollsmoor la jijini Capetown hadi mwaka 1989 alipopata msamaha na kuachiwa huru. Akiwa kifungoni huku akilipiwa ada ya tuition na familia yake Kathrada alikamilisha shahada za historia, kuhusu masuala ya uhalifu na siasa za Afrika katika Chuo kikuu cha Afrika kusini.

HARAKATI ZAKE ZA SIASA BAADA YA KUTOKA GEREZANI
Baada ya marufuku dhidi ya chama cha A.N.C kuondolewa mwaka 1990 Ahmed Kathrada alichaguliwa kuwa Mbunge katika bunge la Afrika Kusini, mjumbe wa kamati kuu na mkuu wa idara ya mahusiano ya umma katika chama cha ANC. Mara tu baada Nelson Mandela kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini, alimteuwa Ahmed Kathrada kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya siasa.

Nelson Mandela alipostaafu, Ahmed Kathrada naye aliamua kustaafu na kuanzisha taasisi yake iliyojulikana kama Kathrada foundation. Alimuoa mwanamama mpinga ubaguzi Barbara Anne Hogan ambaye ni waziri wa zamani wa Afya na Makampuni ya umma katika serikali ya Afrika Kusini chini ya chama cha A.N.C.
Ahmed Kathrada alipata fursa ya kwenda kuhiji Maka mwaka 1992.

KIFO CHAKE
Alifariki mwezi Machi mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka 87 baada ya kuugua kwa muda mfupi na kufanyiwa Mazishi ya kitaifa kwenye makaburi ya Westpark jijini Johanesburg tarehe 29 Machi 2017.
Huyo ndiye Alhaji Ahmed Mohamed Kathrada (Uncle Kathy), mpigania uhuru, mtetezi wa haki za binadamu na mpinga ubaguzi wa rangi ambaye wakati wa uhai wake, aliandika kitabu kuhusu maisha yake na kile alichopitia wakati akiwa Gerezani katika harakati za kulikomboa taifa la Afrika Kusini. Kitabu chake kinafahamika kama No Bread for Mandela: Memoirs of Ahmed Kathrada, Prisoner No. 468/64.


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com


Wednesday, July 18, 2018

HUYU NDIE DR. ABIY AHMED ALI WAZIRI MKUU WA ETHIOPIA, NYOTA YA KIZALENDO INAYOCHOMOKA NA INAYONG'ARA BARANI AFRIKA.

Na Masudi Rugombana

Anaitwa Abiy Ahmed Ali au Abiyyi Ahimad Alii kama inavyoandikwa na kutamkwa kwa lugha ya kabila lake la Oromo. Jina lake la utotoni ni Abiyot likimaanisha Mapinduzi, jina maarufu walilokuwa wakipewa watoto waliozaliwa baada ya Mapinduzi ya Ethiopia ya mwaka 1974 yaliyoundoa madarakani utawala wa mfalme Haile Selasie.

Kijana huyu ambaye tarehe 15 August 2018 atatimiza umri wa miaka 42, ndiye Waziri mkuu wa sasa wa Ethiopia. Pia ndiye kiongozi wa serikali kijana zaidi barani Afrika. Anajulikana kama Waziri mkuu mwenye uwezo wa kuzungumza lugha mbalimbali ( Multilingual Prime Minister) akiwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza kwa ufasaha Lugha nne ambazo ni Afaan Oromo, Amharic, Tigrinya and Kiingereza.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Waziri mkuu huyu mwanamageuzi ( Reformist ) Alizaliwa tarehe 15 August 1976 katika mji wa Beshasha katikati ya Ethiopia, mji huu unapatikana kwenye jimbo la Oromia, jimbo kubwa zaidi kwa eneo na lenye idadi kubwa zaidi ya watu kuliko mikoa yote nchini Ethiopia. Anazaliwa kwenye familia ya Wakulima wa kahawa wa kabila la Oromo yenye dini mchanganyiko ambapo baba yake Ahmed Alli ni Muislamu na Mama yake Tizita Wolde ni Mkristo. Abiy Ahmed ni baba wa mabinti watatu aliowapata kwa mke wake Zinash Tayachew.

Kwa hiyo Waziri Mkuu Abiy Ahmed ni Muislamu kutoka kabila la Oromo ambalo ndilo kabila kubwa kuliko yote nchini Ethiopia linalounda asilimia 34.4 ya idadi ya raia wote wa Ethiopia wanaofikia milioni 102. Idadi ya watu wa kabila la Oromo inakadiriwa kuwa ni zaidi ya milioni 35. Pia Waoromo wanapatikana katika baadhi ya maeneo ya Kenya na Somalia.

ELIMU YAKE NA UTUMISHI JESHINI.
Masomo na utumishi wake jeshini ni vitu vilivyokwenda sambamba. Alisoma elimu ya msingi katika shule ya Msingi Beshasha na elimu ya Secondary katika shule ya Agaro (Agaro Secondary School) katika mji wa Agaro. Mwaka 1990 akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na Muungano wa jeshi la Waasi la EPRDF (Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front ) liliokuwa likipigana kuindoa Madarakani Serikali ya Mengitsu Haile Mariam na mara tu baada ya kuanguka serikali ya Mengitsu mwaka 1991 Abiy Ahmed alichukua rasmi mafunzo ya kijeshi na kujiunga rasmi na Jeshi la Ethiopia ( Ethiopian National Defense Force ) akiwa na umri wa miaka 15.

Akiendelea na utumishi jeshini, Abiy aliendelea na elimu ya juu na kufanikiwa kupata shahada ya kwanza (Bachelor's degree ) ya uhandisi wa Computer ( Computer Engineering) mwaka 2001 kutoka chuo cha Microlink Information Technology cha mjini Addis Ababa. Mwaka 2005 alihitimu na kupata cheti huko Pretoria Afrika Kusini katika masomo ya Cryptography ( Elimu ya njia ya kuhifadhi na kusambaza data katika fomu maalumu ili wale tu waliokusudiwa ndio watakaoweza kusoma na kuzichakata).

Ana Master of Art (M.A) ya Mabadiliko na Mageuzi ya uongozi (Transformational Leadership and Change ) kutoka Chuo kikuu cha Greenwich, London Uingereza. Pia ana Master degree ya Usimamizi wa biashara ( Business Administration ) kutoka chuo cha utawala na uongozi cha Leadstar cha jijini Addis ababa aliyoipata mwaka 2013.
Ana shahada ya Uzamivu (Ph.D) aliyotunukiwa na taasisi ya amani na mafunzo ya usalama katika chuo kikuu cha Addis ababa mnamo mwaka 2017. Katika utumishi wake Jeshini, alipanda ngazi hadi kufikia cheo cha Luteni Kanali ( Lieutenant Colonel ), alishiriki vita dhidi ya Erithrea kupitia kitengo cha ujasusi (military intelligence ).
Anatajwa kuwa ndiye mwanzilishi wa Shirika la kitaifa la taarifa za kiuslama ( National Information Security Agency - INSA ) ambayo ni idara muhimu inayotuma taarifa za kijasusi kwa shirika na ujasusi la Ethiopia ( National Intelligence and Security Service-NISS). Alianzisha na kuongoza shirika hilo kuanzia mwaka 2007 hadi 2010. Abiy Ahmed alikuwa ni miongoni wa askari wa kulinda amani wa umoja wa mataifa waliopelekwa nchini Rwanda mwaka 1995.

HARAKATI ZAKE ZA KISIASA.
Alianza harakati za kisiasa mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 15 pale alipochaguliwa kuwa mjumbe kwenye halmashauri kuu ya chama cha Oromo People's Democratic Organization (OPDO), chama tawala cha kikabila katika jimbo la Oromia ambacho ni miongoni mwa vyama vinne vilivyoungana kuunda Serikali nchini Ethiopia kupitia mwamvuli wa Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF). Alipata mafanikio ya haraka kisiasa hadi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama tawala cha Ethiopia (EPRDF) na baadae kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi mbalimbali za mashirika ya umma. Katika uchaguzi mkuu wa Ethiopia wa mwaka 2010 Abiy Ahmed alichaguliwa kuwa mjumbe katika bunge dogo la Ethiopia na mwaka 2015 alichaguliwa tena kwa mara ya pili kuwa mjumbe wa bunge hilo.
Umaarufu wake uliongezeka zaidi wakati wa vurugu za kupinga hatua ya Serikali kunyakua ardhi kinyume cha sheria katika jimbo la Oromia katika kile kilichodaiwa kuwa ni upanuzi wa mji mkuu Addis ababa. Abiy aliachia nyadhifa zake zote serikalini ili kuungana na wananchi katika kupigania mabadiliko katika jimbo la Oromia uamuzi uliomfanya kuwa kinara katika vurugu hizo zilizopelekea majeruhi na vifo. Hata baada ya unyakuaji huo wa ardhi kusitishwa rasmi mwaka 2016 bado vurugu hizo ziliendelea na kubadilika kutoka kwenye kupinga unyakuaji wa ardhi hadi kuwa vurugu za kisiasa zilizosambaa nchi nzima.
Ni mapambano hayo ndiyo yaliyomjengea heshima kubwa kwa watu wa mkoa wa Oromia na kumpandisha kwenye ngazi ya mafanikio ya kisiasa. Mwezi October mwaka 2015 Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn alimteua Abiy Ahmed kuwa Waziri wa Sayansi na teknolojia wa Ethiopia nafasi aliyoitumikia kwa muda wa mwaka mmoja kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Rais wa jimbo la Oromia katika kipindi cha utawala wa Rais Lemma Magersa wa jimbo hilo. Wakati akiwa naibu Rais wa Oromia, Abiy Ahmed aliendelea na nafasi ya uwakilishi katika bunge la Ethiopia na baadae kushika madaraka ya Uenyekiti wa Chama cha Oromo (OPDO) tarehe 22 Februari 2018.

MIGOGORO YA KIKABILA NCHINI ETHIOPIA YAMPANDISHA ABIY AHMED HADI KWENYE CHEO CHA UWAZIRI MKUU.
Ethiopia imekuwa ikikabiliwa na chuki za kikabila kwa miaka mingi, Jamii ya watu wa kabila la Oromo ambao ni asilimia 34.4 ya Waethiopia na jamii ya watu wa kabila la Amhara ambao ni asilimia 27 ya Waethipia wote zimekuwa zikilalamikia kutengwa katika nafasi za uongozi kwenye serikali kuu inayoongozwa na watu wa jamii ya Tigraya kupitia chama chao cha kikabila cha Tigrayan People's Liberation Front (TPLF) na Chama cha Southern Ethiopian People's Democratic Movement (SEPDM).

Hali hii ilipelekea makabila haya makubwa kuunganisha nguvu ndani ya Muungano wa EPRDF (chama tawala) kupitia vyama vyao vya Amhara National Democratic Movement (ANDM) chini ya Demeke Mekonnen na Oromo Peoples' Democratic Organization (OPDO) chini ya Abiy Ahmed. Pia Makabila haya yaliunganisha nguvu nje ya chama tawala kupitia kambi ya upinzani chini ya muungano wa chama cha United Ethiopian Democratic Forces (UEDF)

Licha ya vyama vyote vitatu pamoja na chama kingine cha nne cha Southern Ethiopian People's Democratic Movement (SEPDM) kinachoongozwa na Hailemariam Desalegn (Waziri mkuu aliyejiuzulu) kuunda mwamvuli wa chama tawala cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front ( EPRDF ) bado jamii ya watu wa Tigraya ilikuwa na nguvu kubwa ya maamuzi ndani ya Muungano huo.

Hatua ya serikali inayoongozwa kwa wingi na watu wa kabila la Tigraya kunyakua ardhi kwa nguvu katika jimbo la Oromo kwa kisingizio cha upanuzi wa jiji la Addis ababa ndio ilikuwa kichocheo kikubwa wa vurugu kubwa za kisiasa na kikabila zilizopelekea mauaji ya waandamanji mia saba. Kusambaa kwa vurugu hizo kulipelekea Waziri mkuu Hailemariam Desalegn kutangaza hali ya hatari nchi nzima na hatimaye kujiuzulu mnamo tarehe 15 February 2018 baada ya kushindwa kudhibiti hali ya mambo.

Ili kuhakikisha kuwa nchi inarudi katika hali ya utengamano, tarehe 27 March 2018 vyama vinavyounda muungano wa EPRDF ambao ndio unaoitawala Ethiopia viliamua kumchagua Abiy Ahmed kuwa kiongozi wao na hivyo moja kwa moja kuwa Waziri mkuu wa Ethiopia akichukua nafasi ya Hailemariam Desalegn aliyejiuzulu. Abiy Ahmed aliapishwa rasmi kuiongoza Ethiopia tarehe 02 April 2018 siku tano baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama tawala cha EPRDF.

ABIY AHMED NA SERA ZA MAGEUZI
Mara tu baada ya kuapishwa Waziri mkuu Abiy Ahmed Alli alitoa hotuba ya kihistoria iliyoonyesha uelekeo wa kurejesha umoja wa kitaifa. Aliwaomba msamaha wananchi wa Ethiopia kwa mauaji yaliyofanywa na vikosi vya Serikali dhidi ya Waandamanaji zaidi ya mia saba wakati wa vurugu za kisiasa zilizotokana na kampeni ya kupinga unyakuaji wa ardhi, alikwenda mbali zaidi katika hotuba yake baada ya kuwataka Wapinzani wa Serikali waliokimbilia nje ya nchi kurejea Ethiopia ili kufikia Maridhiano na serikali yake katika kuijenga Ethiopia. Jambo hili halijawahi kufanywa na Serikali zilizopita za Ethiopia chini ya Hailemariam Desalegn, Melez Zenawi, Mengitsu Haile Mariam na hata mfalme Haile Selasie.
Mara baada ya kuingia ofisini kuanza kazi ya Uwaziri mkuu, Abiy Ahmed aliondoa amri ya hali ya hatari (a state of emergence), Serikali yake imeshafunga moja ya gereza lililokuwa tishio na hatua ya kwanza ya kuwaachia wafungwa wa kisiasa imekwishaanza. Pia alitangaza mpango mkubwa wa mageuzi ya uchumi yatakayojumuisha ubinafsishaji wa Mashirika ya umma (state-run firms) na kuuza sehemu ya hisa za makampuni yanayomilikiwa na serikali kwa wawekezaji wa kigeni. Kiongozi huyu anaendelea kuzunguka nchi nzima akihimiza mshikamano na kuahidi mageuzi makubwa zaidi Serikalini ikiwa ni pamoja na kuondoa vizuizi vyote vya kibiashara baina ya Ethiopia na Somalia.

Hatua yake ya kutangaza kuheshimu masharti yote ya makubaliano ya amani yaliohitimisha vita vya kugombea mpaka vya mwaka 1998 hadi 2000 kati ya nchi yake na hasimu wake Erithrea imefungua njia ya kupatikana kwa amani ya kudumu baina ya majirani hao wa pembe ya Afrika. Hatua hii imeivutia Erithrea hadi kufikia hatua ya kutuma ujembe maalum kwenda Ethiopia kwa lengo la kujadiliana namna ya kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili ambayo ni ndugu.

Mgogoro wa mpaka kati ya nchi hizo mbili uliopelekea kuzuka kwa vita umekuwa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi ya mataifa hayo kwani yamekuwa yakielekeza bajeti kubwa kwenye ulinzi na kusababisha sekta nyingine kudorora.

MLIPUKO WA BOMU KWENYE MKUTANO WA HADHARA JIJINI ADDIS ABABA TAREHE 23/6/2018.
Mlipuko huo ulisababisha kifo cha mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati maelfu ya Wananchi walipohitimisha matembezi ya kuunga mkono sera za mageuzi za Waziri mkuu Abiy Ahmed kwa kufanya mkutano mkubwa wa hadhara jijini Addis ababa siku ya Jumamosi tarehe 23 June 2018.

Watu nane wanachunguzwa kwa kuhisiwa kuhusika na shambulizi hilo akiwemo naibu kamishna wa polisi wa Addis ababa ambaye anachunguzwa kutokana na mapungufu ya kiuslama yaliyojitokeza kwenye mkutano huo.
Waziri mkuu Abiy Ahmed amelielezea shambulio hilo kuwa ni jaribio lisilofanikiwa lililotekelezwa na askari wasiotaka kuona raia wa nchi hiyo wakiwa na umoja.

Huyu ndie Dr Abiy Ahmed Ali waziri mkuu wa kwanza kijana na wa kwanza kutoka kabila la oromo pia ni wa kwanza Muislam kutawala taifa hilo lenye historia kubwa AFRIKA na lenye kasi kubwa ya ukuwaji wa Uchumi

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

Saturday, March 3, 2018

KUSAMBARATIKA KWA YUGOSLAVIA NA MACHAFUKO KATIKA ENEO LA  KUSINI MASHARIKI YA ULAYA

Na Masudi Rugombana
Shirikisho la kijamaa la Jamhuri ya watu wa Yugoslavia ilikuwa ni nchi katika eneo la kusini mashariki ya bara la Ulaya. Taifa hilo liliundwa baada ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia tarehe 29 Novemba 1945. Taifa hili la kijamaa lilikuwa ni mojawapo katika mataifa yaliyoendelea zaidi kuliko mataifa mengine katika eneo la kusini mashariki ya bara la Ulaya ( eneo hili linajulikana kama Balkan).

Shirikisho hilo la kijamaa liliundwa na muungano wa Jamhuri sita ambazo ni Bosnia-Herzegovina, Croatia, Macedonia, Montenegro, Serbia, na Slovenia. Jamhuri hizi zilikuwa na mchanganyiko wa makundi ya makabila na dini mbali mbali. Kosovo na Vojvodina yalikuwa ni majimbo yenye utawala wa ndani (autonomous provinces) ndani ya Jamhuri ya Serbia.

Yugoslavia ya Zamani

Yugoslavia, ikiwa na maana ya nchi ya Waslav wa Kusini ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 255,804 (sawa na maili za mraba 98,766). Ilipakana na mataifa ya Italy kwa upande wa magharibi, Austria na Hungary kwa upande wa kaskazini, Bulgaria na Romania kwa upande wa Mashariki, Albania na Ugiriki kwa upande wa Kusini. Mji mkuu wa taifa hilo la kijamaa ulikuwa Belgrade ambao kwa sasa ni mji mkuu wa Jamhuri ya Serbia. Kiongozi wa kwanza wa Shirikisho hilo la kijamaa alikuwa Josip Broz Tito.

Josip Broz Tito
Serikali ya kijamaa chini ya Josip Tito iliegemea zaidi upande wa Ulaya Mashariki (Eastern bloc) hadi mwaka 1948 ilipoamua kuwa nchi isiyofungamana na upande wowote baada ya kutokea sintofahamu kati ya Rais Josip Tito na mshirika wake Rais Joseph Stalin wa USSR (Union of Soviet Socialist Republics) baada ya Josip Tito kukataa kuifanya Yugoslavia kuwa nchi inayoendeshwa kwa ushawishi wa Urusi kiuchumi, kisiasa na kijeshi (Satelite state) kama zilivyokuwa nchi nyingine za umoja wa Soviet.

Ikumbukwe kuwa Rais Josip Tito alikuwa ni miongoni mwa viongozi waasisi wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (The Non-Aligned Movement (NAM), viongozi wengine ni Jawaharlal Nehru wa India, Sukarno wa Indonesia, Gamal Abdul Nasser wa Misri na Kwame Nkrumah wa Ghana.

KUFARIKI KWA JOSIP TITO NA KUANZISHWA KWA MTINDO WA UONGOZI WA URAIS WA PAMOJA.
Josip Tito alifariki tarehe 4 May 1980. Kufuatia kifo cha Josip Tito ambaye alikuwa ni rais wa maisha, Yugoslavia iliongozwa kwa mtindo wa Urais wa pamoja (collective presidency) kwa kuanzisha Ofisi ya Rais wa Urais wa Yugoslavia (The office of the President of the Presidency of Yugoslavia) ambapo nafasi ya Urais ilikuwa ni ya kupokezana kwa zamu kila mwaka baina ya Jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho la Yugoslavia. Kuanzia kwa Rais Lazar Koliševski aliyechukua madaraka baada ya kufariki Josip Tito tarehe 4 May 1980 hadi kwa Rais Branko Kostić tarehe 27 April 1992 ambapo ndio ulikuwa mwisho wa uhai wa Shirikisho la kijamaa la Yugoslavia.

KUIBUKA KWA HARAKATI ZA UTAIFA KWA MISINGI YA UKABILA NA UDINI
Kufuatia kifo cha Josip Tito, ambaye aliiunganisha Yugoslavia kwa mkono wa chuma, kuliibuka harakati kubwa za utaifa kwa misingi ya ukabila na udini zilizoleta migawanyiko baina ya raia katika jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho hilo.

Kuanguka kwa ujamaa katika eneo la Ulaya Mashariki, kuporomoka kwa uchumi na kushindwa kwa mazungumzo ya kulifanyia mageuzi shirikisho baina ya Jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho hilo kulipelekea baadhi ya Jamhuri hizo kujitangazia uhuru na uhuru wao kutambuliwa na baadhi ya mataifa ya Ulaya. Hali hiyo ilipelekea kuanguka kwa Shirikisho la Yugoslavia kwa jamhuri hizo kutangaza kujitenga rasmi kulingana na mipaka ya shirikisho hivyo kupelekea kuibuka kwa vita iliyojulikana kama vita vya Yugoslavia ( Yugoslav Wars)

NANI NI CHANZO CHA KUSAMBARATIKA KWA YUGOSLAVIA?
Ni Slobadan Milosevic, mwanasiasa wa Serbia mwenye msimamo mkali aliyeingia madarakani kupitia harakati kali za utaifa wa Serbia, baada ya kushika hatamu ya madaraka  ya rais wa urais wa Jamhuri ya kijamaa ya Serbia mnamo tarehe 8 May 1989 hadi tarehe 11 January 1991 na Urais wa Jamhuri ya Serbia kuanzia tarehe 11 January 1991– 23 July 1997.
Slobadan Milosevic
Kitendo chake cha kutaka kuwapa nguvu kubwa raia wachache wenye asili ya Serbia ambao ni Wakristo katika jimbo la Kosovo dhidi ya raia wenye asili ya Albania walio wengi ambao ni Waislamu kwa madai kuwa raia wenye asili ya Serbia ambao ni Wakristo walikuwa wanabaguliwa katika jimbo hilo. Pia hatua yake ya kupingana na jamhuri nyingine zilizokuwa zinaunda shirikisho la kijamaa la Yugoslavia katika mpango wa kulifanyia mageuzi shirikisho hilo kulipelekea kuibuka kwa chuki kali dhidi ya raia wenye asili ya Serbia waliokuwa wakiishi katika Jamhuri nyingine za shirikisho.

Akiungwa mkono na wanaharakati wa utaifa wa Serbia walio wachache kutoka Kosovo na Bosnia-Herzegovina pia kwa kupewa msaada na  washirika wake katika television ya Taifa ya Serbia, aliendelea kueneza chuki miongoni wa raia wenye asili ya Serbia walio wachache katika jamhuri za Croatia na Bosnia. Television ya Serbia ilikuwa ikionyesha matukio ya mauaji ya kutisha yaliyofanywa na mafashisti wa Croatia dhidi ya Waserb wakati wa vita kuu ya pili ya Dunia. Hofu ilitawala miongoni mwa jamii ya Waserb huko Croatia na Bosnia kwamba hatima kama hiyo iliyowakuta wenzao na wao inawasubiri.

Hali hii ilipelekea kuibuka kwa itikadi za kuweka msingi wa uanzishwaji wa Serbia kubwa "Greater Serbia" taifa ambalo halitakuwa Serbia tu, bali litakalojumuisha na maeneo ya Bosnia na Croatia yenye idadi kubwa ya wakazi wenye asili ya Serbia. Na ili kufanikisha mpango huo, mkakati uliokuwa umewekwa ilikuwa ni kuwaondoa raia wote wasiokuwa Waserb ( Ethnic Cleansing) katika Serbia na miji inayokaliwa na Waserb wengi katika jamhuri za Croatia na Bosnia.

Tarehe 26 March 1990 uongozi wa Serbia chini ya Rais Slobadan Milosevic ulikutana kujadili hali ya uhasama ulivyokuwa  ikiendelea ndani ya shirikisho la Yugoslavia na kufikia makubaliano rasmi kuwa vita katika Jamhuri za Croatia na Bosnia-Herzegovina ni suala lisiloepukika.
Tarehe 2 July 1990 bunge la Kosovo nalo lilitangaza kuwa Kosovo ni Jamhuri yenye hadhi kama zilivyo jamhuri nyingine sita zilizokuwa zikiunda shirikisho la Yugoslavia. Kufuatia tangazo hilo, Bunge la Serbia lilipiga kura kuweka marufuku kwa jimbo la Kosovo lenye Waislamu wengi ambao ni wakazi wenye asili ya Albania kuwa na Bunge lake.

KUJITENGA KWA JAMHURI ZA SLOVENIA NA CROATIA
Slovenia chini ya Milan Kučan na Croatia chini ya mwanasiasa Franjo Tudman zilijitangazia uhuru wao Juni 25 mwaka 1991 na kujiondoa rasmi kwenye shirikisho la kijamaa la Yugoslavia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoridhika na mgawanyo usio sawia wa madaraka kutokana na Waserbia kujitwalia madaraka makubwa zaidi katika Shirikisho. Hii ni kwa sababu muundo wa Urais wa Yugoslavia ulikuwa unawapa Waserbia kura nne za maamuzi kati ya nane. Kura nyingine nne zilikuwa ni za jamhuri za Bosnia-Herzegovina, Croatia, Macedonia na Slovenia.

Jeshi la Yugoslavia lililokuwa na Waserbia wengi lilijaribu kuzuia kujitenga kwa jamhuri ya Slovenia katika vita iliyodumu kwa muda wa siku kumi kuanzia tarehe 27 June 1991 hadi 7 July 1991,  ambapo vikosi vya Yugoslavia vilirudishwa nyuma na vikosi vya ulinzi wa mipaka vya Jamhuri ya Slovenia. Pande mbili zilisaini makubaliano ya kumaliza vita katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika kwenye kisiwa cha Brion nchini Croatia. Makubaliano hayo  yaliyosimamiwa na Jumuiya ya Ulaya yanajulikana kama Brioni Agreement. Tarehe 15 January 1992 Jumuiya ya Ulaya ilitangaza kutambua uhuru wa Jamhuri za Croatia na Slovenia.

Kwa upande wa Croatia, vita iliendelea hadi November mwaka 1995 dhidi ya vikosi vya Yugoslavia na wanamgambo wa Kiserbia wakiongozwa na Milan Babic waliokuwa wanapigania jimbo linalokaliwa  na Waserbia wengi la Krajina kuwa Jamhuri yenye utawala wake wa ndani (autonomous republic) katika ardhi ya Croatia. Jimbo hilo lilikuwa na jumla wa Wakazi 469, 700 ambapo idadi ya wakazi wenye asili ya Serbia walikuwa 245,800 sawa na  52.3%, Wacroatia walikuwa 168,000 (35.8%) na jamii nyingine walikuwa 55,900 (11.9%). Croatia ikiungwa mkono na Marekani ilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waserb mnamo tarehe 4 August 1995 katika vita iliyopewa jina la Operation Storm. Waserbia 2,650 waliuwa kikatili na wengine zaidi ya laki mbili (200,000) walilazimishwa kuhama katika jimbo hilo na kukimbilia katika jimbo la Vojvojina nchini Serbia, tukio hilo linaelezwa kuwa ndio tukio baya zaidi la safisha ya kikabila (Ethnic Cleansing ) barani Ulaya tokea kumalizika vita kuu ya pili ya Dunia.

KUJITENGA KWA JAMHURI YA MACEDONIA
Jamhuri ya Macedonia iliitisha kura ya maoni chini ya uongozi wa rais Kiro Gligorov kuamua kujiondoa katika Shirikisho ya Kijamaa la Yugoslavia tarehe 8 Septemba 1991 ambapo asilimia 75 ya wananchi walijitokeza na kupiga kura ya ndio kwa asilimia 95. Tangazo la uhuru likidhinishwa rasmi na bunge mnamo tarehe 25 Septemba 1991. Tofauti na Jamhuri nyingine za shirikisho hilo, kujitenga kwa Macedonia kulitawaliwa na amani. Hata migogoro michache ya mpaka iliyokuwepo baina yake na shirikisho la Yugoslavia ilijadiliwa na kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo. Taifa la Macedonia lilitambuliwa rasmi na umoja wa mataifa tarehe 8 April, 1993.

KUJITENGA KWA JAMHURI YA BOSNIA-HERZEGOVINA
Wakati Croatia ikiwa vitani dhidi ya majeshi ya Yugoslavia na wapiganaji wa kiserbia, Jamhuri ya Bosnia-Herzegovina iliitisha kura ya maoni kuhusu kujiondoa kwenye Shirikisho tarehe 29 February na tarehe 01 March 1992 ambapo asilimia 64 ya wananchi walijitokeza  kupiga kura ambapo asilimia 97 ya wapiga kura wote walipiga kura ya kukubali kujitenga. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na wakazi wenye asili ya Bosnia na wale wa jimbo la Herzeg ambao asili yao ni Croatia  huku ikisusiwa na raia wenye asili ya Serbia ambao wanaishi kwa wingi katika jimbo la Srpska (Republica Srpska).

Mnamo tarehe 3 March 1992 Mwenyekiti wa Urais wa Bosnia Alija Izetbegović ambaye ni Muislamu alitangaza rasmi uhuru wa Bosnia-Herzegovina na bunge likaidhinisha tangazo la uhuru. Mnamo tarehe 6 April 1992 Marekani na Jumuia ya kiuchumi ya Ulaya zilitangaza rasmi kuutambua uhuru wa Bosnia-Herzegovina na tarehe 22 May 1992 Bosnia ilikubaliwa kuwa mwanachama wa umoja wa mataifa(UN).

VITA VYA KUPIGANIA UHURU WA BOSNIA- HERZEGOVINA
Tangazo hilo la uhuru lilipingwa na wananchi wenye asili ya Serbia ambao wengi wao ni Wakristo. Wakiongozwa na Radovan Karadzic na General Ratko Mladic mnamo tarehe 6 April, 1992 waliamua kutangaza uasi dhidi ya raia Waislamu wa Bosnia na Wale wenye asili ya Croatia, hivyo kupelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ilikuwa ni vita ndani ya vita. Majeshi ya Croatia ambayo kwa wakati huo yalikuwa vitani dhidi ya Yugoslavia na Waasi wa kiserbia nayo yaliingia vitani pia huko Bosnia kuwaunga mkono Wabosnia na Wakroatia waliokuwa wanapigana chini ya makamanda shupavu Alija Izetbegović, Haris Silajdžić, Jenerali Sefer Halilović, Luteni kanali Rasim Delić, Meja Jenerali Enver Hadžihasanovic na Mate Boban katika vita dhidi ya raia wenye asili ya Serbia. Majeshi ya Jamhuri ya Serbia chini ya Rais Slobadan Milosevic nayo yaliingia vitani kusaidi upande wa raia wenye asili ya Serbia ambao wengi wao ni Wakristo. Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) uliunga mkono upande wa Waislamu wa Wabosnia na Wacroatia ambao waliungana kupigana na adui yao mkuu ambaye ni Mserbia.

Vita iliingia katika hatua mbaya zaidi kati ya mwaka 1993-1994 baada ya Waislamu wa Bosnia na raia wenye asili ya Croatia kushindwa kuelewana na kujikuta wakiingia katika mapigano baina yao ambapo Majeshi ya Jamhuri ya Croatia yaliwasaidia Wacroatia wenzao wa Bosnia. Hivyo kulikuwa na vita tatu ndani ya Bosnia ambapo Waislamu wa Wabosnia walikuwa wanapigana na Waserb waliokuwa wakisaidiwa na majeshi ya Jamhuri ya Serbia na Yugoslavia. Wacroatia nao walikuwa wanapigana dhidi ya Waserbia na Waislamu wa Wabosnia walikuwa wanapigana dhidi ya Wacroatia katika jimbo lao la Herzeg-Bosnia.

Hali hiyo ilipelekea Marekani kuanza juhudi za kuwapatanisha Waislamu wa Bosnia na Wananchi wenye asili ya Croatia ili wamalize tofauti zao na kuelekeza nguvu zote dhidi ya adui yao mkuu ambaye ni Serbia. Mazungumzo ya amani yalifanyika Washington Marekani na Pande mbili zifikia muafaka na kusaini makubaliano ya amani yaliyojulikana kama Makubaliano ya Washington mnamo tarehe 18 March 1994. Makubaliano hayo yalisainiwa na Waziri mkuu wa Bosnia Haris Silajdžić, Waziri wa Mambo ya nje wa Croatia Mate Granić na Rais wa Wacroatia wa Herzeg-Bosnia Krešimir Zubak.Baada ya kuondoa tofauti zao Wabosnia na Wacroatia waliunganisha nguvu katika vita dhidi ya adui yao mkuu Mserbia.

Umoja wa mataifa (UN) ulipeleka rasmi wanajeshi wa kulinda amani Mwezi February 1992 kwa lengo la kuhakikisha misaada kibinadamu inawafikia raia na pia kulinda usalama wa raia wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea kwa kuanzisha ukanda salama (safe zone) kwa ajili ya raia waliokuwa wanakimbia mapigano.

Vita ya Bosnia Ilikuwa ni vita iliyohusisha mauaji ya halaiki na safisha ya watu wa jamii na dini tofauti katika baadhi ya miji (Ethnic cleansing). Safisha hiyo ilishuhudia mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu katika Miji ya Zepa, Foča, Zvornik, Cerska, Snagovo, Banjaluka na Srebrenica inayopatika katika jimbo la Srpska lenye Waserbia wengi. Mauaji hayo yaliongozwa na kamanda wa vita Jenerali Ratko Mladic akisaidiwa na Makamanda Zdravko Tolimir na Radomir Miletic.

Katika mji wa Zepa uliokuwa na idadi ya watu 2441 ambapo Waislamu Wabosnia walikuwa 2330 sawa na asilimia 95 ya wakazi wote. Kamanda Zdravko Tolimir aliongoza mauaji ya  Waislamu 116  siku ya tarehe 25 July 1995 muda mfupi baada ya kuuteka mji huo kutoka mikononi wa askari wa kulinda amani wa umoja wa mataifa hatua iliyopelekea Waislamu wengine kulazimika kuuhama mji wa Zepa.

Katika mji wa Foca uliokuwa na idadi ya watu 48,741 ambapo Waislamu walikuwa zaidi ya nusu ya Wakazi wote sawa na asilimia 52, Waislamu 2704 waliuawa na vikosi vya Waserbia kati ya 7 April 1992 hadi January 1994. Waislamu zaidi ya  22,000 walilazimishwa kuondoka, misikiti yote 13 katika mji wa Foca ililipuliwa na kuteketezwa. Matukio hayo yalikwenda sambamba na vitendo vya ubakaji dhidi ya Wanawake na watoto wa kike wa Kiislamu. Mpaka mwisho wa vita vya Bosnia, ni Waislamu 10 tu ndio waliokuwa wamebaki katika mji wa Foca.

Katika mji wa Cerska uliokuwa na idadi ya Waislamu 1409 na kijiji cha jirani cha Velici, vikosi vya Waserb viliwauwa Waislamu 250 mwanzoni mwa mwezi March 1993 na kuwalazimisha wengine kuhamia katika mji wa Tuzla na Mashariki mwa mji wa Srebrenica.

MAUAJI YA HALAIKI DHIDI YA WAISLAMU KATIKA MJI WA SREBRENICA ( SREBRENICA GENOCIDE )
Wakati vita ya kupigania Uhuru wa Bosnia ikielekea ukingoni baada ya majeshi ya Jamhuri ya Croatia yaliyokuwa  yakishirikiana na majeshi ya ulinzi wa mipaka ya Bosnia kufanikiwa kuteka maeneo mengi ya Jamhuri ya Bosnia-Herzegovina na kuelekea kuwashinda wapiganaji wa Kiserbia waliokuwa wakisaidiwa na Majeshi ya Rais Slobadan Milosevic wa Serbia pamoja na vikosi vya shirikisho la kijamaa la Yugoslavia, wapiganaji wa Kiserbia katika jimbo lao la Srpska lenye waserbia wengi walifanya mauaji makubwa ya halaiki (Genocide) na safisha ya kidini na kikabila (Ethnic Cleansing) dhidi ya Waislamu wa Bosnia katika mji wa Srebrenica.

Mji huo ambao ulikuwa ni moja wapo kati ya maeneo yaliyotengwa na Umoja wa Mataifa kama kanda salama (Safe Zone) ulikuwa chini ya ulinzi wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa kutoka Uholanzi. Vikosi hivyo vilipoteza udhibiti wa mji huo baada ya kuzidiwa nguvu na Wapiganaji wa Kiserbia wa jimbo la Srpska (Republika Srpska) waliokuwa wakiongozwa Radovan Karadžić na Jenerali Ratko Mladic siku ya tarehe 1 Julai 1995.

Kamanda Jenerali Ratko Mladic na wasaidizi wake
wakiingia katika mji wa Srebrenica mara baada
ya Wapiganaji wake kuuteka mji huo kutoka
mikononi mwa walinda amani wa umoja wa mataifa.

Wakitumia kisingizio cha kuwahamisha Waislamu wa Bosnia kwenye makazi salama, Waserb waliwasafirisha wanawake, wazee na watoto pekee wanaokadiriwa kufikia elfu thelasini (30,000) na kuwahifadhi katika makambi huku wakidai kuwa wanaume watu wazima na wavulana watasafirishwa baadae. Baada ya kufanikiwa kuwatenganisha kwenye makambi tofauti, Jenerali Ratko Mladic aliongoza Mauaji ya halaiki yaliyofanyika kati ya Julai 11–22, 1995 ambapo Waislamu Wanaume watu wazima na wavulana wanaofikia 8,373 Waliuawa kikatili na kuzikwa katika makaburi makubwa huku wanawake, wazee na watoto 30,000 waliotenganishwa wakilazimishwa kuondoka katika mji wa Srebranica.

Maiti za Waislamu wa Bosnia zikiwa zimesambaa katika
barabara za mji wa Srebrenica

Mauaji hayo yalikwenda sambamba na vitendo vya utesaji na ubakaji dhidi ya wanawake na watoto wa Kiislamu pamoja na ubomoaji wa nyumba za Waislamu na misikiti. Inaelezwa kuwa mauaji ya Srebrenica ndio makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya tokea kumalizika kwa vita kuu ya Pili ya Dunia.

Lawama kubwa zilielekezwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa kutoka Uholanzi vilivyokuwa vikiongozwa na Kanali Thomas Jakob Peter Karremans ambavyo vilipewa dhamana ya usalama wa mji Srebrenica kwa kushindwa kuzuia mji huo usiangukie mikononi mwa Waserb na pia kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mauaji ya halaiki.
Na katika hali ya kushtua ni kitendo cha walinda amani hao kuamua kujiondoa kutoka kwenye mji huo siku ya Ijumaa tarehe 21 July 1995 na hivyo kuwaacha raia bila ulinzi  wowote. Kabla ya vikosi vya UN kutoka Uholanzi kuondoka Srebrenika, Kamanda wa vikosi hivyo Kanali Thomas Karremans huku akiwa na furaha alionekana akigongeana glasi ya mvinyo na kinara wa mauaji ya Waislamu wa Bosnia huko Srebrenica Jenerali Ratko Mladic.

Kiongozi wa vikosi wa kulinda amani vya umoja wa mataifa
Kanali Thomas Karremans (aliyejishika kiuno katikati)
pamoja na kinara wa Mauaji ya Waislamu wa Bosnia mjini
Srebrenica Jenerali Ratko Mladic wakinywa mvinyo.


MAPIGANO MAKALI JIJINI SARAJEVO  SAMBAMBA NA MASHAMBULIZI YA ANGA KUTOKA VIKOSI VYA NATO
Jiji la Sarajevo lililokuwa na idadi ya wakazi 526,000 ni miongoni mwa miji iliyokumbwa na mapigano makali zaidi baada ya kuzingirwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia tarehe 5 April 1992 hadi tarehe 29 February 1996 na wapiganaji wa Kiserbia wanakadiriwa kufikia 13,000 kutoka jimbo ya Srpska (Republica Srpska) wakisaidiwa na majeshi ya Yugoslavia. Wapiganaji hao chini ya makamanda Milutin Kukanjac, Ratko Mladić,  Stanislav Galić na Dragomir Milošević walikuwa wamekusanyika kwenye milima inayozunguka jiji hilo huku wakiwa na silaha nzito. Wapiganaji hao walikuwa  wakipigania kijitangazia Jamhuri yao itakayojumuisha na maeneo yanayokaliwa  kwa wingi na Waislamu wa Bosnia.

Askari zaidi ya 70,000 wa vikosi vya ulinzi vya Bosnia chini ya makamanda Alija Izetbegović, Mustafa Hajrulahović, Vahid Karavelić, Nedžad Ajnadžić, Mušan Topalović na  Mcroatia Vladimir Šaf waliozingirwa katika jiji la Sarajevo hawakuweza kuuvunja mzingiro wa Waserb kutokana na kuwa na silaha dhaifu.

Miongoni mwa matukio mabaya ya kukumbukwa ni mauaji ya Wakristo wa Serbia waliokuwa wanaishi katika maeneo yanayokaliwa na Waislamu wengi wa Bosnia jijini Sarajevo. Mauaji hayo yalifanywa chini ya Kamanda ambaye pia ni jambazi na msafirishaji bidhaa na wahamiaji haramu kwa njia ya magendo (smuggler) Musan Topalovic ambaye aliwakusanya katika shimo la Kazan karibu na mji wa Sarajevo na kuwaua kikatili kisha kuwazika katika kaburi moja kubwa.
Tukio lingine ni kuuawa kwa Naibu Waziri mkuu wa Bosnia  Hakija Turajlic tarehe 8 January 1993 ambaye Msafara wake uliokuwa ukitokea uwanja wa ndege wa Sarajevo huku ukilindwa na askari wa umoja wa mataifa ulisimamishwa na wapiganaji wa Kiserb ambapo baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa na Hakija, walitoa amri kwa vikosi vya umoja wa Mataifa kumkabidhi mikononi mwao. Mara tu mlango wa gari alimokuwa ulipofunguliwa, askari mmoja wa Kiserb alimuua kwa kumfyatulia risasi sita za kifuani.  

Tukio baya kabisa kuliko yote ni shambulizi la mota katika soko la Markale jijini Sarajevo mnamo tarehe 5 Februari 1994 lililofanywa na wapiganaji wa Kiserb ambapo raia 68 waliuawa na wengine 200 kujeruhiwa. Waserb pia walifanya shambulio lingine kama hilo tarehe 28 August 1995 ambapo raia 43 waliuawa na wengine 75 kujeruhiwa. Ni tukio hili ndilo lililopelekea vikosi vya NATO kuingilia kati kwa kufanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya wapiganaji wa kiserbia baada ya kupata idhini kutoka baraza la usalama la umoja wa mataifa. Ni mashambuli hayo ndiyo yaliyowalazimisha Waserb kukubali kuingia kwenye mazungumzo ya amani kwa ajili ya kumaliza vita. Mazungumzo hayo yalifanyika huko Dayton, Marekani.
Jumla ya watu 14,000 waliuawa wakiwemo raia 5400 katika mapigano ya jijini Sarajevo pekee. Idadi yote ya vifo katika vita ya Bosnia inafikia watu 95,940 ikihusisha askari na raia.

MKATABA WA AMANI WA DAYTON (DAYTON-PARIS ACCORD)
Mazungumzo ya kutatua mgogoro wa vita ya Bosnia yalianza tarehe 1 had tarehe 21 November 1995. Mazungumzo hayo yalifanyika katika kambi ya ndege za kivita ya Wright-Patterson karibu na Dayton, huko Ohio nchini Marekani. Makubaliano ya amani yalifikiwa ambapo mkataba wa makubaliano hayo ulisainiwa rasmi jijini Paris nchini Ufaransa tarehe 14 December 1995 hivyo kumaliza rasmi vita nchini Bosnia. Utiaji saini wa mkataba huo ulishuhudiwa na Rais Jaques Chirac wa Ufaransa, Rais Bill Clinton wa Marekani, Waziri mkuu wa Uingereza John Major, Kansela Helmut Kohl wa Ujerumani na Waziri mkuu wa Urusi Victor Chernomyrdin.

Mkataba huo wa amani uliigawa Bosnia katika Jamhuri tatu zenye utawala wa ndani kila moja ikiwa na serikali yake, bunge na polisi. Jamhuri hizo ni ya Waislamu wa Bosnia, Wacroatia wa Bosnia katika jimbo la Herzeg na Waserb wa Bosnia katika jimbo la Sprska. Pia mkataba ulianzisha serikali kuu yenye mawaziri tisa, watatu kutoka kila jamhuri, inayoongozwa kwa mtindo wa kubadilishana madaraka kutoka Jamhuri moja kwenda nyingine.

Slobadan Milosevic (kushoto), Franjo Tudman (katikati) na
Elija Izetbegovich (kulia) wakisaini mkataba wa amani wa
Dayton kumaliza vita vya Bosnia
Washiriki katika Mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Mwanadiplomasia mashuhuri Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani bwana Warren Christopher  walikuwa rais Slobadan Milosevic wa Serbia akimwakilisha kiongozi wa Waserb wa Bosnia Radovan Karadzic, Rais Franjo Tudman wa Croatia, Rais wa Bosnia-Herzegovina Alija Izetbegovic  na waziri wa Mambo ya nje wa Bosnia-Herzegovina Mohamed Sacirbeg.

VITA YA KOSOVO NA MASHAMBULIZI YA NATO 1998-1999
Baada ya awamu ya pili ya uongozi wa Slobadan Milosevic nchini Serbia kumalizika kwa mujibu wa katiba, kiongozi huyo alichaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Yugoslavia mwaka 1997. Madaraka hayo mapya yalimpa nguvu kubwa zaidi katika Jeshi na vikosi vya Usalama ambapo alivielekeza vikosi hivyo kuanzisha mashambulizi dhidi ya wananchi wa jimbo Kosovo ambalo lilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Serbia waliokuwa wanataka kujitenga na kuanzisha taifa lao. Hatua hiyo ilipelekea machafuko makubwa ambayo baadae yaligeuka na kuwa vita kamili kati ya Mwaka 1998-1999 baina ya Majeshi ya Yugoslavia na Jeshi la Ukombozi wa Kosovo ( Kosovo Liberation Army (KLA) likiongozwa na viongozi na makamanda shupavu kama Adem Jashari, Hashim Thaçi, Bilall Syla, Hamëz Jashari, Sylejman Selimi, Agim Çeku na Ramush Haradinaj ambaye kwa sasa ndiye Waziri mkuu wa Kosovo.

Majeshi ya Yugoslavia yakishirikiana na polisi pamoja na wanamgambo wa Kiserb yalifanya mauaji na vitendo vya kikatili dhidi ya Wakazi wa jimbo la Kosovo ambao zaidi ya asilimia 90 ni Waislamu wenye asili ya Albania. Miongoni mwa mauaji ya kutisha ni yale yaliyotokea katika kijiji cha Cuska karibu na mji wa Pec ambapo Waislamu wanaume 41 waliuawa na kila nyumba ilichomwa moto. Ili kuzuia safisha ya kikabila na kidini ( ethnic cleansing) dhidi ya Waislamu wa Kosovo, Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) chini ya viongozi na makamanda Wesley Clark, Rupert Smith na Javier Solana ulifanya mashambulizi mazito ya anga yaliyopewa jina la Operation Allied Force dhidi ya majeshi ya Yugoslavia na wanajeshi wa Kiserb huko Kosovo. NATO iliweka sharti la kusitisha mashambulizi ikiwa tu rais Slobadan Milosevic atayaondoa majeshi yake na vikosi vya usalama vya Serbia huko Kosovo.

Mashambulizi ya NATO pia yalilenga miundombinu ya barabara na madaraja nchini Serbia na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa Yugoslavia. Rais Milosevic alisalimu amri na kuondoa majeshi hivyo kuruhusu walinda amani wa NATO kuingia Kosovo baada kusaini makubaliano ya kumaliza vita na NATO yaliyofanyika katika mji wa Kumanovo nchini Macedonia.Makubaliano hayo yalipewa jina la Kumanovo Agreement.

Hatimaye tarehe 17 February 2008 Kosovo ilijitangazia uhuru baada ya azimio la kutangaza uhuru kupita kwa idadi ya kura 109 kati ya kura 120 za wajumbe wote wa bunge la Kosovo hivyo kujitenga rasmi na jamhuri ya Serbia na kuwa taifa huru ambalo kwa sasa linatambuliwa na mataifa machache ikiwemo Marekani, Canada, Uturuki na Jumuiya ya Ulaya (EU).

SHIRIKISHO LA YUGOSLAVIA BAADA YA JAMHURI NNE KUJITOA.
Baada ya Jamhuri hizo nne kufanikiwa kujitenga na kuwa nchi huru, shirikisho la Yugoslavia lilibaki kuwa muungano wa Jamhuri mbili za Serbia na Montenegro zikitumia jina la Shirikisho la Jamhuri ya Yugoslavia (Federal Republic of Yugoslavia) chini ya uongozi wa rais Slobadan Milosevic ambaye alitawala kama Rais wa Serbia hadi Mwaka 1997. Baada ya muhula wake wa pili kumalizika kama Rais wa Serbia, Milosevic alichaguliwa kuwa rais wa shirikisho la Yugoslavia kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2000 tarehe 7 October alipokabidhi madaraka kwa rais Vojslav Kostunica aliyeongoza hadi mwezi Februari mwaka 2003.

Kuanzia mwaka 2003 nchi hizo zilibadili jina na kujiita Muungano wa taifa la Serbia na Montenegro chini ya uongozi wa rais Svetozar Marovic aliyeongoza hadi tarehe 3 June Mwaka 2006 wakati jamhuri hizo zilipotengana baada ya Montenegro kuitisha kura ya maoni ya kuamua kujitenga na kuwa jamhuri huru ambapo wananchi walipiga kura ya kukubali kujitenga kwa asilimia hamsini na tano (55%). Hivyo kuanzia mwezi Juni  mwaka 2006 Serbia ikawa Jamhuri huru chini ya uongozi wa rais Boris Tadic na Montenegro nayo ikawa Jamhuri huru chini ya uongozi wa rais Filip Vujanovic.

Na huo ndio ulikuwa mwisho rasmi wa shirikisho la kijamaa la Yugoslavia ambalo kusambaratika kwake kuliambatana na  machafuko makubwa katika eneo zima la Balkan yaliyosabisha vifo vya watu 140,000 na wakimbizi milioni mbili na laki tatu.

KUANZISHWA KWA MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU WA KIVITA KATIKA ILIYOKUWA YUGOSLAVIA.
Wakati vita nchini Yugoslavia ilipokuwa inashika kasi hadi kufikia hatua mbaya ya uhalifu wa kutisha dhidi ya binadamu, ilionekana sio vyema mbele ya macho ya jamii ya kimataifa kwa watu waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kutekeleza mauaji, mateso na ubakaji kuachwa waendelee kufurahia maisha uraiani pasina kuchukuliwa hatua za kisheria.  Kwa muktadha huo Umoja wa Mataifa (UN) uliamua kuanzisha mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita uliofanyika katika vita vya Yugoslavia kwa lengo la kuwashtaki na kuwafunga jela wale wote waliohusika na uhalifu wa kivita wa kiwango cha juu. Mahakama hiyo iliitwa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu katika Yugoslavia ya zamani. (International Criminal Tribunal for the former Yugoslavia (ICTY).

ICTY ilikuwa  ni mahakama ya kwanza ya uhalifu wa kivita kuundwa na umoja wa Mataifa ikiwa ni mahakama ya kwanza ya kimataifa ya uhalifu wa kivita tokea zilipoundwa mahakama za  Nuremberg na Tokyo ambazo zilianzishwa na mataifa yaliyoshinda vita kuu ya pili ya Dunia (Allied powers- Ufaransa, Muungano wa nchi za Soviet, Uingereza na Marekani) kwa ajili ya kuwashitaki na kuwahukumu wahalifu wakuu wa kivita kutoka mataifa yaliyoshindwa vita hivyo (Axis Powers-Italy, Ujerumani na Japan). Pia vita vya Yugoslavia ndiyo ilikuwa kichocheo kikubwa kilichopelekea kutengenezwa kwa mkataba wa Rome (Rome Statue ) ulioanzisha Mahakama ya kimataifa ya uhalifu mnamo mwaka 1998 ( International Criminal Court-ICC)

Mahakama hii (ICTY) ilianzishwa tarehe 25 May, 1993 baada ya kupitishwa kwa azimio namba 827 la baraza la usalama la umoja wa mataifa na ilimaliza kazi iliyopangiwa tarehe 31 December 2017. Mahakama hiyo ilikuwa na mamlaka juu ya makundi manne ya uhalifu uliofanyanyika katika eneo la Yugoslavia ya zamani tangu mwaka 1991 ambayo ni uvunjifu wa hali ya juu wa mikataba ya Geneva ( grave breaches of the Geneva conventions), ukiukaji wa sheria au desturi za vita ( violations of the laws or customs of war), mauaji ya kimbari (genocide) na uhalifu dhidi ya ubinadamu (crimes against humanity ). Kiwango cha juu cha hukumu ambacho mahakama hiyo ilipewa uwezo wa kuhukumu  ilikuwa ni kifungo cha maisha.Mahakama hii iliweka makao yake huko Geneva nchini Switzeland.

Jumla ya watuhumiwa 161 wa uhalifu wa kivita walishtakiwa ikiwa ni pamoja na mawaziri wakuu, wakuu wa majeshi, mawaziri wa mambo ya ndani na viongozi wengine wengi wa ngazi ya juu na kati wa kisiasa, jeshi na polisi kutoka pande mbali mbali zilizopigana vita katika mgogoro wa Yugoslavia. Watuhumiwa 90 walikutwa na hatia na kuhukumiwa. Miongoni wa watuhiwa sita waliokutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela ni Makamanda Ratko Mladic, Zdravko Tolimir na Stanislav Galic wakati Radovan Karadzic alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela  na Dragomir Milosevic alihukumiwa kifungo cha miaka 33 wakiwa ni miongoni wa viongozi walifungwa miaka mingi jela. Rais Slobadan Milosevic alifariki mnamo tarehe 11 March 2006 akiwa kizuizini huko The Hague kabla ya mashtaka
yake kukamilika.

HALI YA UHUSIANO BAINA YA JAMHURI ZA ILIYOKUWA YUGOSLAVIA
Jamhuri hizo za zamani za iliyokuwa Yugoslavia zimejitahidi kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kwa manufaa ya raia wao. Serbia, Bosnia-Herzegovina, Macedonia, Montenegro na Slovenia zimekuwa na uhusiano mzuri zaidi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Serbia ndio mwekezaji wa pili mkubwa nchini Bosnia-Herzegovina.

Serikali ya za Croatia na Serbia zina uhusiano wa kidiplomasia licha ya hali ya uhasama na chuki ambazo bado hazijafutika katika fikra za wananchi wao zinazosababishwa na matukio yaliyotokea katika vita kuu ya pili ya Dunia na vita vya Yugoslavia. Pia mataifa hayo yana mgogoro wa mpaka ambao unaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo.

Hali ya uhusiano kati ya Serbia na Jamhuri ya Kosovo sio nzuri. Serbia bado inakataa kuitambua Kosovo kama nchi huru kutokana na kutokubaliana na hatua ya jimbo lake hilo la zamani kutangaza kujitenga na kuwa nchi huru. Licha ya Serbia kutoitambua Kosovo kama nchi huru, jamhuri nyingine za iliyokuwa Yugoslavia zilishatangaza rasmi kuutambua uhuru wa Kosovo hadi kufikia hatua ya kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia ikiwemo Montenegro ambayo ina mgogoro wa mpaka na jimbo la Kosovo ambao unaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo.

Viongozi wa mataifa haya wamekuwa wakiimarisha uhusiano kwa kutembeleana mara kwa mara licha ya ziara hizo kukabiliwa na upinzani wa mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya raia wa mataifa hayo ambao bado wana kumbukumbu za matukio ya kikatili yaliyofanywa na pande hasimu wakati wa vita vya Yugoslavia. Mara nyingi upinzani mkali zaidi hutokea pale kiongozi wa Serbia anapofanya ziara ya kiserikali katika nchi za Croatia, Slovenia au Bosnia na Herzegovina. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya vitendo vya kikatili dhidi ya ubinadamu vilivyotokea katika vita vya Yugoslavia vilifanywa na Wanajeshi wa Serbia waliokuwa wakipigana kuzuia Jamhuri hizo zisijitenge.

Walinzi wakimkinga Waziri mkuu wa Serbia Aleksandar
Vucic dhidi ya mashambulizi ya mawe yaliyokuwa
yakirushwa na waombolezaji katika kumbukumbu ya
mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu huko Srebrenica
nchini Bosnia Julai 11 mwaka 2015
Tukio la kukumbukwa zaidi ni la tarehe 11 Julai, 1995 ambapo Waziri mkuu wa Serbia bwana Aleksandar Vucic alipigwa mawe hadi kuvunjiwa miwani na Waombolezaji nchini Bosnia-Herzegovina waliokuwa wakimzomea kupinga uwepo wake katika kumbukumbu ya mauaji ya kikatili dhidi ya maelfu ya Waislamu wa mji wa Srebrenica. Aleksandar Vucic kwa sasa ndiye rais wa Serbia.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com


Tuesday, January 23, 2018

UJUE MGOGORO WA ARDHI KATI YA ISRAEL NA PALESTINA NA SULUHISHO LAKE

Na Masudi Rugombana.

Israel ni taifa pekee la kiyahudi Duniani. Taifa hili linapatikana Mashariki ya bahari ya Mediterrania, ni taifa dogo kwa eneo, likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 20,770. ( Imezidiwa ukubwa wa eneo na Wilaya ya Sikonge nchini Tanzania kwa tofauti ya kilomita za Mraba 7103 ).


Israel inapakana na nchi za Syria na Lebanon kwa upande wa kaskazini, Jordan na eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi (West bank) kwa upande wa Mashariki na kusini inapakana na Misri na eneo la Palestina la Ukanda wa Gaza ( Gaza strip ).Taifa hili lina idadi ya watu Milion 8,680,000 kwa takwimu za mwaka 2017.

Idadi ya Wayahudi ni Milioni 6,484,000 sawa na 74.7% (Idadi hii inajumuisha Walowezi wa Kiyahudi wanaoishi ukingo wa Magharibi (West bank) na eneo la Milima ya Golan). Waisrael Waarabu ni Milioni  1,808,000 sawa na  20.8% ya raia wote wa Israel. Idadi ya Wakristo ambao sio Waarabu pamoja na watu wa jamii ya bahai ni 388,000 sawa na 4.5% ya raia wote wa Israel. Lugha rasmi za Taifa la Israel ni Kiebrania (Hebrew) na Kiarabu (Arabic)

Wapalestina ni jamii ya Kiarabu inayopatikana kwa wingi katika ardhi yao inayokaliwa kimabavu na Israel, kwenye ukingo wa Magharibi wa mto Jordan (West bank) na eneo la Ukanda wa Gaza lililowekewa mzingiro na Taifa la Israel. (Besieged Gaza strip).

Idadi ya watu Wanaoishi katika ardhi ya Palestina ni milioni 4,543,126 kwa takwimu za mwaka 2017 ambapo Wapalestina ni 3,950,926 na Walowezi wa kiyahudi wanaunda idadi ya watu 5,92,200. Eneo la Ukingo wa Magharibi (West bank) lina ukubwa wa kilomita za Mraba 5,860 na Idadi ya Watu milioni 2,747,943 kwa takwimu za mwaka 2017. Eneo lililozingirwa la Gaza (Besieged Gaza strip) lina ukubwa wa kilomita za Mraba 360 na idadi ya watu 1,795,183 kwa takwimu za mwaka 2017. (Ukubwa wa ukanda wa Gaza umetofautiana kidogo na ukubwa wa Wilaya ya Ilala inayopatikana mkoa wa Dar es salaam nchini Tanzania kwa kilomita tano za mraba). Lugha rasmi za Wapalestina ni Kiarabu (Arabic) na Kiebrania(Hebrew).

UZAYUNI (ZIONISM) NA KUTAWANYIKA KWA WAYAHUDI
Uzayuni (Zionism) ni Itikadi ya taifa la Israel. Mazayuni (Zionists) wanaamini kuwa Uyahudi (Judaism) ni utaifa na pia ni dini. Na kwamba Wayahudi wanastahili kuwa na nchi yao katika ardhi ya mababu zao kama ambavyo Wachina wanavyostahili kuishi China au Wahindi wanavyostahili kuishi India. Itikadi hii ndiyo iliyosababisha Wayahudi kuanza harakati za kurudi tena katika ardhi ya Palestina na kuunda taifa la Israel mnamo mwaka 1948. Na hiki ndicho chanzo cha mgogoro wa sasa kati ya Wapalestina na Waisrael.

Waisrael wanapozungumzia Historia ya utaifa wao, huanzia kwenye ufalme wa Daudi (David) ambaye ndiye muasisi wa Ufalme wa Israel uliojulikana kama United Monarch mnamo mwaka 1004- 960BC. Baada ya kifo cha Daudi, mwanaye Suleiman (Solomon) alishika hatamu ya uongozi kuanzia mwaka 961-922BC. Baada ya kifo cha mfalme Suleiman mwaka  922BC Makabila kumi ya upande wa Kaskazini yalikataa kuwa chini ya Utawala wa mfalme Rehoboam ambaye alikuwa ni mtoto wa Mfalme Suleiman, hivyo makabila haya yalifanya uasi na kuanzisha ufalme wao walioupa jina la Ufalme wa Israel-Samaria, mji mkuu wa Ufalme huu uliitwa Samaria, baadae walihamishia makao makuu kwenda mji wa Wacaanan wa Sichem ambao kwa sasa unajulikana kama Nablus. Ufalme huu ulisambaratika baada ya kuangukia mikononi mwa dola ya Assyria ( Assyrian Empire) mnamo mwaka 720BC.

Hali hii ilipelekea kuwepo kwa falme mbili za Kiebrania za upande wa Kaskazini na upande wa kusini ambayo hii ya upande wa kusini ilibaki kuwa chini ya Mfalme Rehoboam ilijulikana kama nchi ya Yuda (Judah), makao yake Makuu yalibaki katika mji wa Jerusalem na baadae yalihamishiwa katika mji wa Hebron. Ufalme huu ulisambaratika baada ya kushindwa vita na kuangukia mikononi mwa mfalme Nebuchadnezzar wa Babeli mnamo mwaka 587BC.

Mwaka 63BC nchi ya Yuda iliwekwa chini ya uangalizi wa dola ya Kirumi na mwaka wa 6CE iliunganishwa na kuwa jimbo la Warumi. Mnamo kwaka 135CE Wayahudi waliasi na kupelekea vita baina yao na Warumi ambapo walishindwa vibaya, walipoteza uhuru wao na mji wa Jerusalem uligeuzwa kuwa mji wa kipagani.Wayahudi walipigwa marufuku kuishi Jerusalem na Warumi waliibadili jina nchi ya Yuda na kuiita Syria Palestina.

Kusambaratika kwa falme hizi mbili za kiyahudi na kutawaliwa na madola makubwa kuanza Assyria empire, Babylonian empire, Persian Empire (Iran), Greek empire, Roman Empire, Rashidun Caliphate, Ummayad Caliphate, Ayyubid Dynasty, Mamluk Sultanate, Ottoman Empire na British Empire (United Kingdom) kulipelekea Wayahudi kutawanyika katika maeneo mbali mbali Duniani. Kutawanyika huku kuliwagawa Wayahudi kwa majina kutegemea na maeneo waliyotawanyikia. Makundi haya ya Wayahudi ni Ashkenazi (Ashkenazi Jews) kundi hili ni lile lililohamia katikati na Mashariki ya bara la Ulaya. Sephard (Sephardic Jews ) ni kundi lililohamia maeneo ya kusini ya bara la Ulaya na Kaskazini ya Afrika na Mizrahi (Mizrahi Jews) ambao walibaki mashariki ya kati, Asia ya Kusini na Asia ya kati.

JE WAYAHUDI WALIIKUTA ISRAEL IKIWA TUPU BILA WATU?
Ardhi ya Israel (Palestina) ilikuwa na wenyeji ambao ni makabila ya mwanzo kuja kuweka makazi yao katika nchi ya Palestina. Makabila haya yalihamia huko kutoka kusini na Kaskazini mwa Bara Arabu takriban mwaka 3000 BC. Makabila hayo ni  Wayebusi (Jebusites), Waamori (Amorites), Wahiti (Hittites) Wakanaani (Canaanites) na Waperizi(Perizzites). Makabila haya yalikaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo: Wakanaani waliweka makazi yao katika eneo la Gaza na Wayebusi walibuni mji wa Yebus, ambao kwa sasa unajulikana kama mji wa Jerusalem. Wayebusi walipokonywa mji huo na Wayahudi baada ya kutoka Utumwani nchini Misri mwaka 1003BC chini ya utawala wa mfalme Daudi ambaye aliufanya kuwa makao makuu ya ufalme wake.

Ibrahim ambaye uzao wake ndio unaounda jamii ya wana wa Israel alihamia Palestina wakati huo ikiitwa nchi ya Wacaanan mwaka 1900BC akitokea Kusini mwa Iraq katika eneo lilijulikana kama Uru ya Wakaldayo (Ur of Chaldeans). Ibrahim  aliishi kwa amani na jamii za eneo hilo ambapo alizaa watoto wawili Ismail na Issaack. Ismail na Mama yake walihama Canaan na kuweka makazi yao katika mji wa Makka wakati Issack alibaki Caanan na baba yake Mzee Ibrahim na makazi yao yalikuwa katika mji wa Hebron( Halil). Issack alimzaa Jacob (Yakubu) ambaye naye alifanikiwa kuzaa Watoto kumi na mbili.Kutokana na nchi ya Canaan kukumbwa na baa kali la njaa, Jacob ambaye baadae  alibadili jina na kuitwa Israel na watoto zake walihamia Misri.

Wakiwa Misri walizaliana kwa wingi na kuishi kama watumwa kwa muda wa miaka mia nne (400) hadi Mwaka 1190BC waliporudi katika nchi ya Caanan wakiongozwa na Viongozi wao walioitwa Mussa(Moses) na Joshua Nun (Yusha bin Nuun).  Mussa (Mosses) alifariki wakati wakiwa safarini hivyo Joshua ndiye aliyefanikiwa kuwafikisha katika nchi ya Caanan ambapo walifanikiwa kuteka maeneo kadhaa baada ya kuingia kwenye mapigano na wenyeji wao Wacaanan na makabila mengine. Hapo ndipo Joshua alifanikiwa kuanzisha na kuongoza dola ya Wana wa Israel.

Dola hii haikuweza kudumu muda mrefu kwani Ilisambaratika baada ya kufa Joshua (Yusha bin Nuun) hivyo Wana wa Israel waliangukia kwenye mateso ya Wafilisti ambao ni jamii ya Wacaanan waliokuwa wakielekea upande wa Kaskazini kutokea kwenye miji yao ya pwani ya kusini ambayo ni Gaza, Ekron, Gath, Ashdod, na Ashkelon. Wana wa Israel wakiongozwa na Sauli (ambaye kwa kiarabu anatajwa kwa jina la Twaaluti) walifanikiwa kuwashinda Wafilisti na kuanzisha tena Dola ya Wana wa Israel mnamo mwaka 1025BC.

 Sauli alifariki mwaka 1004BC na hivyo Daudi alishika uongozi na kuwa mfalme wa Dola ya Israel iliyojulikana kama United Monarch. Ni katika utawala wa mfalme Daudi (King David) ndipo dola ya Israel ilipoimarika na kujitanua katika maeneo mengi ikiwa ni pamoja na kuuteka mji wa Jerusalem kutoka mikononi mwa Wayebusi (Jebusites) mnamo mwaka 1003BC. Mfalme Daudi alifariki mwaka 960 na mtoto wake Suleiman ( King Solomon) alishika hatamu ya Uongozi hadi Mwaka 922BC alipofariki. Kufariki kwa Mfalme Suleiman kulipelekea kugawanyika kwa dola Israel (United Monarch) baada ya makabila kumi ya upande wa Kaskazini kukataa kuutambua utawala wa mfalme Rehoboamu ambaye alikuwa mtoto wa Mfalme Suleiman. Hali hii ilipelekea dola hii kuanguka na kutawaliwa na madola mengine makubwa.

Baada ya kipindi kirefu cha wastani wa miaka 1360 ya kutawaliwa na Madola mbali mbali makubwa kama Assyrian empire, Babylonian empire, Persian Empire (Iran), Greek empire na Roman Empire kilichopelekea Wayahudi wengi kupelekwa utumwani na wengine kutawanyika sehemu mbalimbali huku wakiziacha jamii nyingine zikiendelea kubaki katika eneo hilo la Palestine (Israel) hatimaye Mji wa Jerusalem uliingia mikononi mwa dola ya Kiislam (Rashidun Caliphate) mwaka 638CE baada ya kuwashinda Warumi wakati dola hiyo ya Kiislamu ilipokuwa chini ya uongozi wa Caliph Omar Al Khatwab ambaye alifunga safari kwenda Jerusalem kuchukua funguo za mji kutoka kwa kasisi Sophronius wa dola ya Kirumi.

Makabidhiano hayo ya mji wa Jerusalem yalifanyika katika kanisa linajulikana kama the Holy Sepulchre (Church of the Holy Sepulchre ), katika makabidhiano hayo ya mji wa Jerusalem, kasisi Sophronius na Caliph Omar Khatwab walisaini mkataba uliojulikana kama OMAR TREAT, mkataba uliotoa hakikisho kwa Wakristo kuishi na kufanya ibada zao bila kubughudhiwa. Mkataba huo ulisomeka hivi:

"Haya ndiyo ya amani aliyowapa Umar kiongozi wa Waislamu watu wa Jerusalem. Amewapa amani kwa nafsi zao na makanisa yao na misalaba yao, na kuwa hayatakaliwa makanisa yao wala hayatavunjwa, wala hayatapunguzwa kitu katika majenzi yake wala katika nafasi yake, wala hawatalazimishwa kuacha dini yao wala kudhuriwa yeyote katika wao, na ni juu ya watu wa Jerusalem kutoa jizya (tribute) kama wanavyotoa watu wa Madain"

Ni mwaka huo huo ambapo miji mingi ya Palestina (Israel)iliingia katika Dola ya Kiislamu.
Ikumbukwe kuwa Caliph Omar ndiye alijenga msikiti mdogo kwa ajili ya kufanya ibada katika eneo ambalo Waislamu wanaamini ndipo ulipokuwa Msikiti wa Mbali (Al Aqsa) uliotajwa kwenye Kitabu kitukufu cha Quran, Sura ya Kumi na Saba (Surat Bani Israil). Kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya kiislam, ni eneo hili ambalo Mtume Muhammad aliwaongoza manabii katika ibada kabla hajapaa kwenda mbinguni katika kisa maarufu kinachojulikana kama MIRAJI. Baadae msikiti huo uliongezwa ukubwa hadi kufikia muonekano wake wa hivi sasa. Na kwa mujibu wa imani ya kiyahudi, katika eneo hilo ndipo Mfalme Suleiman (King Solomon) alipojenga hekalu la kwanza. Pia wanaamini kuwa ni katika eneo hilo ndipo patakapojengwa hekalu la tatu na la mwisho. Eneo hilo ni sehemu takatifu kuliko zote katika imani ya kiyahudi.

Msikiti wa Al Aqsa

Nchi ya Palestine pamoja na nchi za Sham zote zilibakia chini ya utawala wa dola ya Kiislamu (Rashidun Caliphate) kwa muda wa miaka 461. Ni katika kipindi hicho ndipo jamii za eneo hilo la Palestina zilipojifunza lugha ya kiarabu,  kubadili dini na kuingia katika Uislamu.

Dola ya Kiislamu ya Rashidun ilipokonywa eneo la Palestina (Israel) mwaka 1099CE na Wakristo kutoka Ulaya walipokuja kuzivamia ardhi hizo katika vita ya Msalaba iliyoshuhudia mauaji ya Waislamu elfu sabini (70,000) katika eneo la Msikiti wa Aqsa ( Temple Mount). Watu wa Msalaba (Crusaders) waliikalia ardhi ya Palestina wa muda wa miaka 88 kabla ya kutimuliwa na Majeshi ya Waislamu wa Ayyubid Dynasty chini ya Sultan wa Syria na Misri mwenye asili ya Kikurdi Swalaahud-Diyn Hasan al-Ayyuubiy ambaye aliweza kuirudisha Palestina mikononi mwa Dola ya Kiislamu mwaka 1187CE. Makao makuu ya dola hii ya kiislamu yalikuwa Cairo  nchini Misri kati ya mwaka 1174CE hadi Mwaka 1250CE, baadae makao makuu ya dola hii yalihamishiwa Allepo nchini Syria mnamo mwaka 1250-1260CE.

Mwaka 1250CE dola ya Kiislamu ya Mamluk ilikamata hatamu ya kuiongoza Palestina na eneo lote la Sham (The Levent) kutoka mikononi mwa utawala wa Swalaahudin al Ayyuubin (Ayyubid Dynasty). Dola hii ya Mamluk ndiyo iliyopigana na kushinda vita dhidi ya wapiganaji shupavu wa jeshi la Mongol tarehe 6 Septemba 1260CE pale walipoivamia na kutaka kuikalia ardhi ya Sham. Ushindi huu wa dola ya Mamluk dhidi ya Wamongol ulikwenda sambamba na safisha safisha ya mabaki ya Wapiganai wa Msalaba (Crusaders) waliokuwa wamebakia katika maeneo ya ardhi ya Sham ( Syria, Jordan na Lebanon)

Baada ya dola ya Mamluk kuishiwa nguvu, hatimaye ardhi ya Palestina na eneo lote la ardhi ya Sham liliangukia Mikononi mwa dola ya Kiislam ya Ottoman (Ottoman empire) mwaka  1516CE. Dola ya Ottoman iliitawala Palestina kwa muda wa miaka 400 hadi ilipoikabidhi mikononi mwa Utawala wa Uingereza (United Kingdom empire) mwishoni mwa vita kuu ya kwanza ya Dunia mwaka 1918CE. (Rejea: kitabu cha The Palestinian Issue kilichoandikwa na Dr. Mohsen M. Saleh)

KUREJEA KWA WAYAHUDI KATIKA NCHI YA PALESTINA NA KUUNDWA KWA TAIFA LA ISRAEL.
Kutokana na manyanyaso, kuteswa na kubaguliwa kwa Wayahudi barani Ulaya, hali hii ilipelekea Wayahudi kuanza kufuatilia kwa ukaribu zaidi asili yao. Ni wakati huo katika karne ya 19 ndipo Wasomi wa kiyahudi walipoona umuhimu wa kuwa na taifa lao katika ardhi ya asili ya mababu zao. Mwandishi wa Kiyahudi mzaliwa wa Austria Theodor Herzl alikuwa mtu wa kwanza kupaza sauti kuhusiana suala la utaifa wa kiyahudi (Jewish nationalism) katika harakati za kimataifa mnamo mwaka 1896.

Herz ambaye alishuhudia unyanyasaji mkubwa wa Wayahudi alishawishika kuamini kuwa Wayahudi hawangeweza kuishi kwa usalama wakiwa nje ya taifa lao. Aliandika Insha (essays) na kuandaa mikutano iliyochochea uhamiaji mkubwa wa Wayahudi kutoka Ulaya kwenda katika ardhi ya Palestine (Israel). Kabla ya harakati za Herz, ni Wayahudi elfu ishirini tu (20,000) waliokuwa wakiishi katika ardhi ya Palestina. Lakini hadi Adolf Hitler anafanikiwa kukamata madaraka idadi ya Wayahudi iliongezeka mara nane.

Pia harakati za Wayahudi kurudi katika ardhi ya Palestina zilichochewa zaidi na azimio la Balfour (Balfour Declaration) la mwaka 1917, mwishoni mwa vita kuu ya pili ya Dunia ambapo utawala wa Uingereza kupitia Waziri wake wa mambo ya nje Arthur James Balfour ulitangaza kuanzisha Taifa la Wayahudi kwenye ardhi ya Palestina kupitia barua yake aliyoiandika kwenda kwa Lord Rothschild aliyekuwa kiongozi wa Jumuiya ya Kiyahudi ya Uingereza (British Jewish Community)

Waarabu waliona kumiminika kwa Wayahudi kama ni harakati za ukoloni kutoka Ulaya. Pande hizo mbili za Wayahudi na Waarabu ziliingia katika mapigano makali yaliyoshindwa kudhibitiwa na Utawala wa Uingereza katika Palestina. Mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ulipiga kura kuigawa ardhi ya Palestina kuwa nchi mbili. Wayahudi ambao idadi yao ilikuwa 650,000   walikubaliana na uamuzi huo na kutangaza rasmi kuunda Taifa la Israel mnamo 14 May 1948 chini ya David Ben Gurion ambaye alikuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kizayuni Duniani (World Zionist Organization)

Wapalestina (Waarabu) ambao idadi yao ilikaribia 1,200,000 waliuchukulia uamuzi huo kama muendelezo wa mkakati wa muda mrefu  wa Wayahudi kuwaondoa katika ardhi zao waliukataa mpango huo. Huo ndio ukawa mwanzo wa Mgogoro wa ardhi unaoendelea sasa baina ya Wapalestina na Waisrael. Wanamgambo wa Wapalestina wakisadiwa na  mataifa ya kiarabu ya Misri, Jordan, Iraq na Syria walitangaza vita dhidi ya Israel mnamo tarehe 15 May, 1948.Vita vilimalizika tarehe 10 March 1949 kwa Israel kushinda na kunyakua ardhi zaidi kutoka mikononi mwa Wapalestina ambao wengi wao waliuawa na zaidi ya laki saba (700,000) kulazimishwa kuondoka katika ardhi zao hali iliyopelekea waishi katika makambi ya wakimbizi tatizo ambalo hadi sasa bado halijapata ufumbuzi.

Ardhi ya Palestina namna inavyokaliwa na
Waisrael kuanzia mwaka 1946 hadi mwaka 2000.

Hadi kufikia mwaka huu 2017 kuna idadi ya Wakimbizi milioni Saba wa Kipalestina sehemu mbali mbali Duniani ambao Israel imewanyima haki ya kurudi katika maeneo yao. Katika vita hiyo Israel iliongeza ukubwa wa ardhi kutoka asilimia 55 hadi 77. Wapalestina walibaki na asilimia 23 tu ya ardhi inayojumuisha eneo la Ukingo wa Magharibi (West bank) na Ukanda wa Gaza (Gaza Strip). Tukio hili linakumbukwa na Wapalestina kama Nakba ( Janga) au catastrophe kwa kiingereza na huko Israel siku ya Nakba husherehekewa kama kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Taifa la Israel.
Maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza yalitekwa na  Israel mwaka 1967 katika vita ya siku sita (Six day war) kati ya Israel na Mataifa ya Kiarabu ya Misri, Lebanon, Jordan na Syria. Israel iliruhusu Walowezi wa Kiyahudi kujenga makazi katika maeneo hayo ambapo makazi hayo yanachuliwa kuwa sio halali na sehemu kubwa ya Jumuiya ya Kimataifa.

Wapalestina waliendeleza harakati za kujikomboa kwa kuanzisha vyama vya ukombozi vya PLO (Palestine Liberation Organisation) kilichoanzishwa 28 May 1964 chini ya Yasser Arafat, sasa hivi PLO inaongozwa na Mahmoud Abbas (Abuu Mazen). Chama kingine ni HAMAS kilichoanzishwa mwaka 1987 chini ya Ahmed Yasin na Abdel Aziz al Rantiss, kwa sasa Chama hicho kinaongozwa na Ismail Haniya, waziri mkuu wa zamani wa Palestina . Chama cha Hamas kimejizatiti zaidi katika eneo la ukanda wa Gaza wakati chama cha PLO kikiwa na Ushawishi mkubwa katika eneo la ukingo wa Magharibi wa mto Jordan (West bank).

Kutokana na kuimarika kwa harakati za Mashambulizi ya Hamas kupitia tawi lao la kijeshi la Izzudin al Qassam brigades linaloongozwa na makamanda shupavu Mohammed Deif na  Marwan Issa dhidi ya Walowezi wa Kiyahudi huko Gaza, Israel ililazimika kujiondoa Gaza na kubomoa makazi yote ya Walowezi wa Kiyahudi. Hatua hiyo iliipa Hamas hatamu ya uongozi katika Ukanda wa Gaza.
Hata hivyo tangu Mwaka 2005 Israel kwa kushirikiana na Misri zimeendelea kuiwekea vikwazo Gaza kwa kuiwekea Mzingiro wenye lengo la kuzuia uingizaji wa silaha na harakati za wapiganaji wanaoingia na kutoka kwenye eneo hilo. Mzingiro huo umeleta madhara makubwa kwa wananchi wa Gaza kwa kulifanya eneo hilo kukosa mahitaji mengi muhimu ya kibinadamu kama mafuta, nishati ya umeme, na uagizaji wa  bidhaa za viwandani kutoka nje. 

Kujitoa kwa Israel kutoka ukanda wa Gaza (Unilateral Withdrawal) ilikuwa mwanzo wa taifa hilo la Kiyahudi kuanza harakati kubwa za ujenzi wa makazi ya Walowezi wa kiyahudi katika eneo la ukingo wa magharibi (West bank) ukiwemo mji wa Jerusalem Mashariki ambao Wapalestina wanatarajia kuwa ndio utakaokuwa Mji mkuu wa Taifa lao. Hadi mwaka huu 2017 idadi ya Walowezi wa Kiyahudi katika eneo hilo inafikia laki tano (500,000) ambapo Israel imeshasisitiza kuwa Jerusalem kamwe haitagawanyika na ndio mji wao mkuu wa milele.
Ukiondoa Marekani ambayo Mwezi Desemba 2017 kupitia Rais Donald Trump imetangaza rasmi kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuagiza Ofisi za ubalozi wa Marekani zihamishiwe Mjini Jerusalem kutoka jijini Tel Aviv, bado jumuiya ya Kimataifa imeendelea kutotambua msimamo huo wa Israel ambapo nchi nyingi zimefungua balozi zao Mjini Tel Aviv.

Eneo la West bank lina kumbukumbu Muhimu sana kwa dini za Kiyahudi, Kiislamu na Kikristo kutokana na kuwa na urithi wa maeneo matakatifu kwa dini hizo kama vile Misikiti ya Al Aqsa (The dome of the rock) na Haram al sharif (Temple mount) inayopatikana mjini Jerusalem, pia kuna Church of the Holy Sepulchre. Maeneo mengine ni Msikiti wa Ibrahim (Cave of the Patriarchs) mjini Hebron na Church of Nativity mjini Bethlehem ambako ndipo inasemekana alizaliwa Yesu Kristo.

JE WAISRAEL WATAENDELEA KUIKALIA ARDHI YA PALESTINA MILELE?
Ni swali linalosumbua sana Wanasiasa wa Israel kutokana na wingi wa makazi ya Walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina huko ukingo wa Magharibi. Vyama vya siasa  vya mrengo wa Kushoto, kati na kulia vimekuwa na mitazamo na sera tofauti kuhusiana na hatima ya makazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Palestina.

Misimamo ya vyama vya mrengo wa kulia:
Vyama vya Likud, Bayit Yehudi (Jewish Home), United Torah Judaism na SHAS vinapinga kuanzishwa kwa taifa la Palestina. Vyama hivi vinaunga mkono ujenzi wa makazi ya Walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina.
Msimamo wa vyama hivi ni kuwa na Taifa moja la Israel lenye wakazi wa jamii za Kiyahudi na Kiarabu ambao watakuwa na uhuru wa kuishi sehemu yeyote ndani ya Israel.

Kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 Waziri Mkuu Binyamin Netanyahu (Likud) akihutubia katika makazi ya walowezi wa kiyahudi ya Har Homa (Har Homa Settlements) aliahidi kujenga maelfu ya makazi ya walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi ya Palestina na kusisitiza kuwa hatoruhusu kuundwa kwa Taifa la Palestina katika utawala wake.

Naftari Bennett mtoto wa Wahamiaji wa kiyahudi kutoka Marekani na Mwanamama Ayelet Shaked (Waziri wa Sheria wa Israel) kutoka chama cha Bayit Yehudi ni wanasiasa wenye misimamo uliyofurutu mipaka wanaotaka Wapalestina wote wachukue uraia wa Israel na wale wasiotaka basi waishi Israel kwa vibali maalum kama raia wa kigeni au wakimbizi. Pia wanapinga haki ya kurejea nyumbani kwa wakimbizi wa Kipalestina waliokimbia wakati wa vita vya mwaka 1948 na 1967.

Chama kingine cha Mrengo wa kulia cha Yisrael Beiteinu (Israel nyumbani kwetu) kinachoongozwa na Avigdor Lieberman kinaunga mkono kuundwa kwa Taifa la Palestina. Chama hicho kupitia mpango wake unaojulikana kama Lieberman Plan (Populated Area Exchange Plan) kinataka Miji yote ya mipakani ya Israel yenye wakazi wengi Waarabu kama vile Umm el Fahm, Tayyibe, Ar'ar, Baqa al-Gharbiyye,Kafri Qara,Qalansawe, Kafr Qasim, Tira, Kafr Bara na Jaljulia ihamishiwe Palestina kwa kubadilishana na Makazi makubwa ya walowezi wa kiyahudi yaliyojengwa kwenye ardhi ya Palestina inayopakana na Israel kama vile Beital Illit, Ma'ale Adumin na Modi'in Illit. Kwa mujibu wa mpango huo Israel itajiondoa katika makazi mengine machache yaliyojengwa maeneo ya ndani zaidi kwenye ardhi ya Palestina.

Msimamo wa Vyama vya mrengo wa kati: Vyama vyote vya mrengo wa kati vinavyounda kundi la Zionist Union vya Hatnua, Labor, Green Movement, Yesh Atid na Kulanu vinaunga mkono Israel kujiondoa katika maeneo ya Palestina kupitia mpango wa kuanzishwa kwa mataifa mawili (Two state Solution). Isipokuwa msimamo wao kuhusu hatima ya mji wa Jerusalem hautofautiani na ule wa vyama vya mrengo wa kulia ambao unasisitiza kuwa Jerusalem isiyogawanyika ndio mji mkuu wa milele wa Israel. Pia vyama hivyo vinaunga mkono ujenzi wa ukuta (Separation wall ) utakaotenganisha eneo la Palestina la West bank na Israel.Mpango wa kujenga Ukuta ulianzishwa na Waziri mkuu wa zamani hayati Ariel Sharon lakini haukuweza kukamilishwa hadi sasa.

Msimamo wa vyama vya mrengo wa kushoto: Vyama vya mrengo wa kushoto  vinavyounda United Arab Joint List vya Hadash (The Democratic Front for Peace and Equality), Balad (National democratic assembly), Ta'al (Arab Movement for Renewal) na United Arab List vinapinga ujenzi wa Makazi la walowezi kwenye ardhi ya Palestina, pia vinataka kuundwa kwa taifa la Palestina ambalo mji wake mkuu utakuwa Jerusalem Mashariki. Pia msimamo wa chama cha Kiyahudi cha Meretz hautofautiani sana n msimamo wa vyama vinavyounda kundi la United Arab List.

Kutokana na tofauti hizo za kimitazamo baina ya vyama vya siasa vyenye nguvu kuhusu namna ya kutanzua mgogoro wa Palestina na suala la Makazi ya walowezi wa kiyahudi, uhakika wa Walowezi hao kuendelea kuikalia ardhi ya Palestina ni mdogo kwani Wakati wowote wanaweza kuondolewa kutegemea na sera za chama kilichopo Madarakani na makubaliano yatakayofikiwa baina ya Wapalestina na Waisrael.

NINI SULUHISHO LA KUDUMU LA HUU MGOGORO
Kutokana na sababu za kihistoria, jamii zote mbili za Wayahudi (Waisrael) na Waarabu (Wapalestina) zina haki ya kuishi katika eneo hilo na kumiliki ardhi. Kila upande unapaswa kutambua na kuheshimu haki za upande mwingine. Mgogoro huu unaweza kutatuliwa kwa njia mbili tu ambazoni ni ama kuwa na Taifa moja lenye watu wa jamii mbili zenye kuishi pamoja (One state solution) au kuwa na mataifa mawili ya jamii mbili zinazopakana (Two state Solution) kama ilivyoamuliwa mwaka 1948 na Umoja wa Mataifa.

Wazo la kuwa na Taifa moja (One state solution):
Halikubaliki miongoni mwa Wapalestina ambao wana hofu kuwa hatua hiyo itawafanya wapoteze utambulisho wao na kufanywa watu wa daraja la pili nchini Israel. Kwa upande wa Israel wazo hili linakubalika zaidi na wanasiasa wa mrengo wa kulia nchini Israel ambao wanataka kuiona Israel ikiwa ni taifa moja. Wasichokitaka wanasiasa hao wa mrengo wa kulia ni haki ya Wakimbizi wa Kipalestina zaidi ya 7000,000 walioko nje ya Israel kuruhusiwa kurejea nchini humo.Hofu yao ni kwamba Waarabu watakuwa wengi (Majority) kuliko Wayahudi hivyo kupoteza hadhi ya Israel kuwa taifa Kiyahudi ( Jewish state )

Wazo la Kuwa na Mataifa Mawili (Two state solution)
Linakubalika kwa Wananchi na Wanasiasa wengi wa pande zote mbili. Kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa mpango huu ni hatma ya mji wa Jerusalem na Makazi (Settlements) ya Walowezi wa kiyahudi yaliyojengwa katika ardhi ambayo Palestina wanatarajia ndio iwe nchi yao. Ikiwa Palestina wataendelea na dai lao ya kutaka Jerusalem Mashariki kuwa mji mkuu, Israel inaweza kumaliza mgogoro kwa kuamua kuitwaa Jerusalem, kuondoa Makazi ya walowezi, kujenga mpaka wa ukuta utakaotenganisha Israel na eneo la Palestina la ukingo wa magharibi na kisha kuondoa wanajeshi wake kutoka ukingo wa Magharibi bila kushauriana na upande wowote (Unilateral Withdrawal). Kwa hatua hii Palestina itakuwa imepoteza dai lake la mji wa Jerusalem huku ikirejesha maeneo mengine yote yaliyokuwa yanakaliwa.

SULUHISHO LINALOKUBALIKA KIMATAIFA
 • Ni Israel kukaa meza moja na nchi za Palestina na Jordan ili kujadili na kufikia makubaliano juu ya hatma ya Wayahudi kufanya Ibada na kuzuru maeneo matakatifu yaliyopo Jerusalem Mashariki.
 • Kuondoa Makazi (Settlements) yote ya walowezi wa kiyahudi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi.
 • Kujiondoa kijeshi katika ardhi yote ya Palestina kwa kurudisha majeshi yake hadi kwenye mpaka wa Mwaka 1967 kabla ya vita ya siku sita. (1948 Armistice border)
 • Kuondoa mzingiro uliowekwa dhidi ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza.
Kwa kufanya hivyo Palestina itakuwa huru. Mgogoro wa haki ya Wakimbizi wa Kipalestina kurudi nchini mwao utakuwa umemalizika na nchi hizo mbili zitaweza kuishi pamoja ambapo Jerusalem Magharibi itakuwa mji mkuu wa Israel na Jerusalem Mashariki itabaki kuwa mji mkuu wa Palestina.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com