Na Masudi Rugombana.
“Kwa hakika huyu ni mtu mwenye ubongo bora kuliko watu wote niliowahi kukutana nao katika nyanja ya siasa za kimataifa” Maneno haya aliyatamka Dag Hammarskjöld wakati huo akihudumu katika nafasi ya ukatibu mkuu wa umoja wa mataifa alipokuwa akimzungumzia Zhou Enlai, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Utawala wa Mao Zedong (Mao Tse Tung)
Zhou Enlai |
Zhou Enlai (tamka Chou En-lai) anatajwa kuwa miongoni mwa wanadiplomasia mashuhuri kabisa kuwahi kutokea nchini China na barani Asia. Alihudumu katika cheo cha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya watu wa china kuanzia Octoba 1949 hadi Januari 1976 na wakati huo huo akitumikia cheo cha Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China kati ya mwaka 1949 hadi mwaka 1958. Anaheshimika zaidi nchini mwake kuwa ndiye Muasisi wa diplomasia ya China na Mhamasishaji mkubwa wa amani Duniani. Yeye pamoja na Mao ndio waliosisi na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa sera huru ya mambo ya nchi za nje ya China. Ndiye mwanadiplomasia aliyefanya juhudi kubwa za kuondoa uhasama uliokuwepo baina ya Jamhuri ya watu wa China na Mataifa ya Ulaya Magharibi, uhasama uliotokana na vita ya Korea.
Mwaka 1971 Zhou Enlai alikutana kwa siri na Henry Kissinger, mshauri wa masuala ya usalama wa rais Richard Nixon wa Marekani alipokwenda China kwa ajili ya kuandaa mkutano kati ya marais Richard Nixon na Mao Tse Tung. Ni matokeo ya mkutano huo ndio yaliyoanzisha uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China ambapo Marekani iliruhusu meli zake kufanya biashara na China huku zikipeperusha bendera za nchi nyingine (under foreign flags) na kuruhusu China kuuza bidhaa zake nchini Marekani kwa mara ya kwanza tokea kumalizika wa vita vya Korea.
Juhudi za Mwanadiplomasia Zhou Enlai zilipelekea uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Marekani kuimarika zaidi baada ya kufanikisha ziara ya kihistoria ya rais Richard Nixon mnamo mwaka 1972. Na hatimaye Marekani kutangaza rasmi kuitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kuvunja uhusiano wa moja kwa moja wa kidiplomasia na Kisiwa cha Taiwan mwaka 1979. Pia umahiri wake katika masuala ya diplomasia ndio uliofanikisha kurejesha kiti cha Jamhuri ya Watu wa China katika umoja wa Mataifa mnamo October 25 mwaka 1971, awali ya hapo, Taiwan ndiyo ilikuwa ikitambuliwa rasmi kama Mwakilishi halali wa wananchi wa China katika umoja wa Mataifa.
USHIRIKIANO BAINA YA CHINA NA MATAIFA YA AFRIKA
Ni Zhou Enlai ndiye aliyeasisi Ushirikiano baina ya China na Afrika. Ni baada ya kuhudhuria mkutano wa Bandung ( Bandung Conference), mkutano wa Kwanza mkubwa baina ya Nchi za Afrika na bara la Asia ulifanyika huko nchini Indonesia mwaka 1955 uliohudhuriwa na mataifa 29, sita kutoka Afrika ambayo ni Ethiopia, Misri, Libya, Sudan, Liberia na Guinea. Mkutano huo ulikusudiwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi za Asia na Afrika, pia kupinga ukoloni na ukoloni mamboleo. Mkutano wa Bandung ulikuwa ni mojawapo katika hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote ( The Non-Aligned Movement ).
Ni katika mkutano huo ndipo Zhou Enlai alipofanya majadiliano ya kwanza na nchi za Kiafrika yaliyopelekea kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya China na nchi za kiafrika. Na mwaka ulifuata (Mwezi May, 1956) Misri ikawa taifa la kwanza barani Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China. Hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1960 nchi kumi za Afrika ikiwa ni pamoja na Morocco, Algeria na Sudan zilikuwa tayari zimeshaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China.
Uhusiano baina ya China na Afrika uliimarika zaidi baada ya Ziara ndefu ya siku 51 ya Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai kwenye mataifa kumi ya Afrika kati ya December 14, 1963 hadi February 04, 1964, akiweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu katika Serikali ya China kuzuru bara la Afrika akitembelea mataifa ya Misri, Somalia, Tunisia, Ethiopia, Algeria, Morocco, Ghana, Mali, Guinea na Sudan. Ziara hiyo inaelezwa kuwa ndio ziara ndefu kuliko zote kuwahi kufanywa na kiongozi wa China barani Afrika.
ZHOU ENLAI AITEMBELEA TANZANIA
Tanganyika ilikuwa ni miongoni mwa nchi alizopanga kutembelea, lakini ziara yake iliahirishwa kutokana na kuingiliana na tukio la kihistoria la mapinduzi ya Zanzibar. Hata hivyo Zhou Enlai alifanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania mnamo June 4, 1965 kwa Mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Julius Nyerere. Ziara ambayo ilifungua ushirikiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi baina ya China na Tanzania.
Zhou Enlai na Julius Nyerere |
"Kama watawaletea maneno matupu bila vitendo, China itawafanyia kwa vitendo, na kama Watajenga nusu, kisha wakaacha bila kumalizia, China itakuja kumalizia sehemu iliyobaki" hiyo ilikuwa ni ahadi nzito kwa Mataifa ya Afrika kutoka Jamhuri ya watu wa China iliyotolewa na Waziri Mkuu Zhou Enlai alipokuwa akizungumza na Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa ziara yake hapa Tanzania.
Julius Nyerere hakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kufanya mazungumzo na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka China. Kwani wakati wa harakati za kupinga ukoloni barani Afrika, mwanaharaka kutoka visiwani Zanzibar na mfuasi kindakindaki wa sera za kijamaa Abdulrahaman Mohammed Babu wakati huo akiwa katibu wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party ndiye alikuwa Mwafrika wa kwanza kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati kutembelea Jamhuri ya watu wa China mwaka 1959 akiwa katika kampeni ya kushawishi taifa hilo la kijamaa kuunga mkono harakati za kupinga ukoloni barani Afrika. Ni wakati huo ndipo Abdulrahman Babu alipokutana na kufanya Mazungumzo na viongozi wa chama cha kijamaa cha China (Chinese Communist Party-CCP) akiwemo Waziri mkuu na Waziri wa Mambo ya nchi za nje Zhou Enlai.
Ni ukaribu huo wa Abdulrahman Babu na Wachina ndio uliopelekea watawala wa kikoloni wa Uingereza visiwani Zanzibar kumwita "The best known Sinophile in Tanzania” ikimaanisha mtu anayevutiwa sana na aina ya maisha na utamaduni wa Kichina.
Abdulrahaman Mohammed Babu akihudumu katika cheo cha Waziri wa biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa kiungo muhimu kati ya China na Tanzania na anaelezwa kuwa alichangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha mkataba wa mradi wa ujenzi wa reli ya TAZARA inayounganisha nchi za Tanzania na Zambia. Reli iliyotoa mchango mkubwa sana katika harakati za ukombozi kwa Mataifa ya Kusini mwa Afrika.
HUYU NDIYE ZHOU ENLAI
Alizaliwa tarehe 05 March 1898 katika Mji wa Huaian, Jimbo la Jiangsu Mashariki ya China katika familia ya watu wasomi yenye kipato cha hali ya juu. Bahati mbaya wazazi wake walifariki akiwa bado mtoto hivyo alichukuliwa na mjomba wake mwaka 1910 na kwenda kuishi katika mji wa Shenyang kaskazini ya China, Ilipata elimu yake ya msingi katika shule ya Dongguan Model Academy, Mwaka 1913 mjomba wake alihamishiwa katika mji wa Tianjin ambapo Zhou Enlai alihama pamoja na mjomba wake na kuendelea na masomo katika shule maarufu ya Nankai Middle School shule iliyokuwa ikifundisha kwa kufuata mitaala ya elimu ya Kimarekani.
Baada ya kumaliza masomo na kupata ufaulu mzuri katika shule ya Nankai, mwaka 1917 Zhou Enlai alikwenda Tokyo Japan kuendelea na elimu ya juu. Mwaka 1919 Zhou Enlai alirejea China na kushiriki katika Maandamano yaliyojulikana kama May Fourth Movement ( Maandamano makubwa yaliyoshirikisha vijana wasomi wakipinga hatua dhaifu zilizochukuliwa na serikali ya China dhidi ya mkataba wa Versailles (Treaty of Versailles) uliomaliza vita kuu ya kwanza ya Dunia na kupelekea peninsula ya Shadong ambayo ni ardhi ya China iliyokuwa ikikaliwa na Ujerumani kuangukia Mikononi mwa Japan. Zhou Enlai alikuwa ni miongoni mwa Waandamanaji waliokamatwa na kutupwa jela.
Baada ya kuachiwa huru mnamo mwaka 1920 Zhou alisafiri kuelekea Marseilles nchini Ufaransa kwa ajili ya kazi na masomo. Alijiunga na Chama Cha Kijamaa cha China (CCP) akiwa nchini Ufaransa mara tu baada ya kuanzishwa kwake mwaka 1921 ikiwa ni matokeo ya harakati za May Fourth Movement.
Baada ya kumaliza masomo nchini ufaransa, Mwaka 1924 Zhou Enlai alirejea nchini China na kuendeleza harakati za kisiasa katika chama cha CCP katika mji wa Guangzhou. Mwaka uliofuata (1925) alimuoa Deng Yingchao, mwanafunzi mwanaharakati ambaye baadaye alikuwa mwanachama maarufu wa chama cha CCP. Umaarufu wa Zhou katika chama cha CCP uliongezeka zaidi na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama sambamba na kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa idara ya jeshi katika kamati kuu ya chama cha CCP mwaka 1927.
Kutokana na kushika kasi kwa vita vya kiraia vya China kati ya Wafuasi wa Chama tawala cha Kuomintang chenye kufuata sera za kibepari na wafuasi wa chama cha kijamaa cha CCP, Zhou aliukimbia mji wa Guangzhou na kwenda katika mji wa Jiangxi kushirikiana na Mao Zedong ambaye alikuwa akiendeleza kambi za kijamaa katika maeneo ya vijijini tangu mwaka 1928. Baada ya wafuasi wa sera za kijamaa kushinda vita na kukiondoa madarakani chama Tawala cha Kuomintang mwaka 1949 , Chama cha CCP kilitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Uongozi wa Mao Tse Tung ambaye alimteua Zhou Enlai kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa mambo ya nje. Zhou Enlai aliaga Dunia mjini Beijing tarehe 8 January 1976 akiwa na umri wa miaka 77, alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kibofu cha mkojo akiacha mke na watoto wawili wa kupanga (Adopted Children)
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana
Napatikana kupitia simu namba
+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com
No comments:
Post a Comment