Wednesday, February 15, 2017

Rais Hassan Rouhani wa Iran azitembelea Kuwait na Oman

Kuwait City.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Amir wa Kuwait wamesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano wa nchi jirani na za Kiislamu hasa kwa kuzingatia hali ya hivi sasa Mashariki ya Kati.

Rsis Hassan Rouhani akizungumza na Emir wa Kuwait
Sheikh Sabah Al- Ahmad Al-Jaber Al-Sabah

Rais Hassan Rouhani wa Iran na Amir wa Kuwait Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah wamesisitiza hayo katika mkutano wao mjini Kuwait Jumatano usiku. Akiwa katika  ziara rasmi nchini Kuwait, Rais wa Iran amemfahamisha Amir wa nchi hiyo kuwa nchi mbili hizi zina nukta za pamoja za kiutamaduni, kihistoria na kidini na kwamba uhusiano wa karibu na wa kidugu wa nchi mbili umekuwepo kwa muda mrefu.
Rais Rouhani amesema kuna fursa nyingi za kuimarisha uhusiano wa Iran na Kuwait katika nyanja mbali mbali.


Aidha amesema hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati linakabiliwa na hatari kubwa ya ugaidi na kuongeza kuwa, tatizo hilo ambalo linawasibu wote linaweza kutatuliwa kwa ushirikiano wa nchi za eneo. Rais Rouhani amesisitiza haja ya nchi za eneo kujiepusha na mifarakano na kuongeza kuwa, 'sote tunapaswa kuishi kwa pamoja kwa msingi wa udugu wa Uislamu na tujiepushe na mifarakano.


Kwa upande wake, Amir wa Kuwait Sheikh Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah amesema amefurahishwa na safari ya Rais wa Iran nchini Kuwait pamoja na mitazamo yake ya kuleta umoja. Amir wa Kuwait amesema kwa kuzingatia hali ya sasa katika eneo, nchi yake ina azma ya kuimarisha uhusiano wa pande zote na Iran. Sheikh Al Sabah amesisitiza ulazima wa umoja na mashikamano wa nchi za eneo na Waislamu kwa ujumla kutokana na hali ya hivi sasa katika eneo na kuongeza kuwa: "Sisi sote ni Waislamu na kwa kuzingatia udugu wetu tunapaswa kuishi kwa pamoja katika mkondo wa ustawi, uthabiti na amani."


Rais wa Iran pia mapema Jumatano alitembelea Oman na kufanya mazungumzo na Sultan Qaboos wa nchi hiyo.
Baada ya safari yake hiyo ya siku moja nchini Kuwait na Oman, Rais Rouhani alirejea Tehran jana usiku.

No comments:

Post a Comment