Wednesday, October 5, 2016

MGOGORO CUF NI MATUNDA YA DHAMBI YA UBAGUZI-HAMAD RASHID

WAKATI viongozi wakuu wa CUF; Profesa Ibrahim Lipumba (Mwenyekiti) na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu) wakiendelea kuvutana, aliyewahi kuwa kigogo wa chama hicho, Hamad Rashid Mohamed (pichani) amesema mgogoro huo ni matunda ya dhambi ya ubaguzi.

Katika mahojiano maalumu na gazeti la jambo leo yaliyofanyika wiki hii, Hamad ambaye alikuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni katika Bunge la Tisa alisema wasipotubu, dhambi hiyo itawamaliza.
Akitumia uzoefu wake ndani ya CUF, Hamad ambaye alipofukuzwa kwenye chama hicho akaanzisha Chama cha Alliance for Demokratic Change (ADC), alitaja mambo kadhaa yanayokiharibu chama hicho kama inavyofafanuliwa kwenye kipengele kifuatacho cha maswali na majibu;

Swali: Unadhani nini kimejificha nyuma ya mgogoro wa CUF?

Jibu: CUF kimeondoka katika muundo wa kuwa taasisi na kimekuwa chama kinachoongozwa na mtu mmoja anayeshirikiana na watu wawili au watatu tu wanaomuunga mkono.
Sasa kama chama hakipo kwenye muundo wa taasisi, kitakuwa kinaendeshwa kwa matakwa ya mtu mmoja.
Lakini ikiwa watu wanaanzisha chama kinachoamini katika Muungano halafu ndani yake anatokea kiongozi anasema anataka Serikali ya Mkataba, hapa kuna tatizo.
Ugomvi CUF utaendelea kwa sababu kuna sultani anayetaka kusikilizwa kila anachotaka kifanyike bila kujali kina manufaa gani kwa chama.
Kwa mfano mimi nilishutumiwa kwamba nimetaka kugombea ukatibu mkuu ili nimpiku Maalim Seif. Nikaambiwa napelekwa kwenye kamati ya nidhamu ambayo haipo kikatiba na baadaye nikapelekwa katika Baraza Kuu la Uongozi na sikupewa hata nafasi ya kujieleza kwa sababu tu mtu fulani ana wasiwasi na nafasi yake.
Ukishachukua haya yote unakuta ugomvi ndani ya CUF utaendelea hadi watakapoondoa dhambi hii. Naamini itawaandama (dhambi) kwani wamedhulumu sana juhudi za watu, rasilimali na muda wa watu ili watu fulani wabaki kwenye madaraka na kutumia hata uongo ili wabaki katika nafasi zao.

Swali: Kuna sababu nyingine iliyofanya ufukuzwe CUF?

Jibu: Walinizushia nimepewa fedha na Pengo (Kardinali), Pinda (Waziri mkuu mstaafu) na Lowassa (aliyekuwa mgombea Urais kupitia Ukawa) ambaye ndiye wamemchukua na kufanya naye siasa kila mahala.

Swali: Unashauri Lipumba na Seif wafanye nini ili wamalize mgogoro huo?

Jibu: Kama hawataki kukaa na kuangalia Katiba ya Chama bila kumuangalia mtu usoni wataendelea kuteketea.

Swali: Kwa nini CCM hakuna migogoro mingi kama wapinzani?

Jibu: CCM wana madhambi yao, lakini wameweka utaratibu wa kuheshimu chama, lakini CUF inafukuza watu kwa sababu haiendeshwi kitaasisi.

Swali: Lakini kuna madai kuwa wewe unatumika na CCM?

Jibu: Sishangai kusikia hivyo, kwa kuwa hao hao wanaoniambia natumika na CCM walinishutumu natumika na Chadema nilipokuwa Kiongozi Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni. Nishazoea kushutumiwa ila tofauti yangu na wao ni kwamba mimi siwezi kutumia lugha ya matusi katika kuwajibu.

Swali: Kuna watu wanaamini kuwa ni tabia ya Seif anapomchoka mtu (mwenyekiti) anatengeneza zengwe. Wakitolea mfano kwa wenyeviti wastaafu kama kina Mapalala. Wewe una maoni gani?

Jibu: Ni kweli kwa mfano Mzee Mloo alikuja akasema anataka apumzike, lakini baadaye akaona aendelee na akapita kwa Katibu Mkuu (Seif) na alimkubalia, ila baadaye yakatengenezwa mazingira kuwa kauli yake aliyoitoa awali ndiyo iwe hiyo hiyo, hakuangalia kwamba ni mtu ambaye amejitolea katika chama.
Kuna watu walijitoa sana katika chama wakadhalilishwa na kufukuzwa, sasa hiki kinachotafuna CUF ni matunda ya dhambi ya ubaguzi na ubinafsi.

Swali: Unadhani nani kakosea kati ya Lipumba na Seif?

Jibu: Naona wote walikosea kwa namna walivyojiunga na Ukawa. Hawakuangalia madhara yanayoweza kukipata chama.
Walikosea kwa sababu uamuzi ule haukuwa na baraka za mkutano mkuu wa chama. Ilikuwa ni lazima mkutano wa CUF ukubali kwanza kwamba hawatasimamisha mgombea Urais kabla ya kujiunga na Ukawa, lakini wao wakajiamlia kirafiki rafiki.
Chadema walikuwa wajanja walienda katika mkutano wao mkuu kuomba baraka na wakawazidi ujanja wengine kwa kulazimisha kumpitisha Lowassa.

Swali: Unadhani ni kwanini Lipumba na Seif hawakushitukia njama hizo?

Jibu: Kwa sababu Chadema walisema hawatasimamisha mgombea Zanzibar, Maalim Seif aliwakubalia ili akagombee uraisi huko na aliona hilo lingefanikisha malengo yake.

Swali: Kuna maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Msajili dhidi ya mgogoro huo wa CUF.

Jibu: Msajili alikuwa sahihi kwa kuwa alizingatia katiba ya CUF inavyosema. Hakupendelea upande wowote. Ukiisoma katiba ya CUF hata wewe ambaye siyo mwanasheria utakuwa upande wa Msajili.


Swali: Kwa mgogoro uliopo nini inaweza kuwa hatima ya CUF?

Jibu: Naona CUF ikimfia Maalim Seif

Swali: Unaionaje CUF ndani ya Ukawa?

Jibu: CUF imemezwa na Ukawa. Haiwezi
kuendesha siasa ikiwa ndani ya umoja huo wa vyama vinne.

Swali: Unaweza kutofautishaje mgogoro wa sasa kati ya Seif na Lipumba na ule kati yako na Seif hata ukatimuliwa na kuamua kuunda chama kingine?

Jibu: Tofauti yake ni kwamba stori zetu zilivyotengenezwa tulitakiwa tupate tafsiri ya kisheria zaidi lakini mgogoro wa sasa unaendeshwa na siasa. Suala letu lilipata Baraka kwa wanachama wengi wa CUF waliamini tuna makosa hadi sasa ndio wanatufuata kutuomba radhi tofauti na sasa ambapo watu wengi wa Zanzibar na Bara wanamuunga mkono Lipumba.

Baada ya kushindwa kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Rais Zanzibar kupitia ADC, Hamad Rashid Mohamed akateuliwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein kuwa mmoja wa mawaziri katika Serikali yake.

No comments:

Post a Comment