Friday, September 2, 2016

UJUE MMEA UNAOITWA BANGI

Bangi ni nini? Bangi ni mmea wenye rangi ya kijani, ambayo hutoa majani. Maua na mbegu zake hutumika kama kilevi. Bangi inastawi karibu maeneo yote hapa nchini na inatumika kwa wingi ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya. Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba mmea huo hulimwa na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Mara, Iringa, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Tabora, Tanga, Kagera na Mbeya.

Bangi hutumiwa zaidi na vijana na imepewa majina mengi kama vile msuba, ganja, jani, stiki, ndumu, kaya, msokoto na kadhalika.


Madhara ya bangi:
Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya inaelezea athari za bangi kupitia kijarida chenye ujumbe usemao, “Dawa za Kulevya Zisitawale Maisha Yetu.” Kijarida hicho kimezitaja athari nyingi zitokanazo na matumizi ya bangi.

Athari na madhara mbalimbali ya bangi ni pamoja na kuumwa koo, kupata kikohozi, macho kuwa mekundu na saratani ya mapafu. Pia madhara mengine yatokanayo na matumizi ya bangi ni kuathirika kwa mfumo wa uzazi, ikiwa ni pamoja na kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo na taahira ya akili pamoja na mabadiliko ya hedhi kwa wanawake.


Athari nyingine ni pamoja na kuchanganyikiwa, kufanya ukatili, ukorofi, uhalifu na kupungua kwa kinga ya mwili. Madhara mengine makubwa kwa watumiaji wa mmea huo ni kupoteza kumbukumbu, uoni hafifu hadi kutoona kabisa, ukosefu wa umakini wa kusikia na kufanya maamuzi, na kuhisi vitu visivyokuwepo sambamba na utegemezi na usugu. Athari ya bangi kwa wajawazito ambao ni watumiaji ni kuharibika kwa mimba, kuzaa mtoto njiti, kuzaa mtoto mwenye mtindio wa ubongo na matatizo ya ukuaji.



Pia watumiaji wa bangi huridhika na hali duni waliyo nayo, hivyo kukosa mwamko wa maendeleo huku hali ya kuchanganyikiwa ikimfanya ajihisi ni mwenye mafanikio makubwa! Hivyo mvutaji wa bangi hubakiza moshi mwingi kwenye mapafu kwa muda mrefu na moshi huo unapoingia kwenye mapafu hutengeneza kitu kama lami ambavyo huganda na kuathiri utendaji wa kazi wa mapafu. Kijarida hicho kinasema bangi ina kemikali ‘sumu’ inayosababisha saratani zaidi.
Bangi imeelezwa pia kwamba hufanya mishipa ya ubongo kusinyaa, hali inayosababisha kupungua kwa uwezo wa kufikiri na kukumbuka.

No comments:

Post a Comment