Sunday, September 25, 2016

KIKWETE APIGIWA CHAPUO UWENYEKITI WA UMOJA WA AFRICA (AU)

MWANA DIPLOMASIA Mashuhuri barani Afrika, ambaye pia ni Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ana uwezekano mkubwa wa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU) endapo Tanzania itakubali kumuunga mkono kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mwanadiplomasia Mashuhuri Afrika na
Rais Mstaafu wa Tanzania Dr. Jakaya Kukwete


AU inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wa AU Januari mwakani, baada ya kushindikana kupatikana kwa mshindi miongoni mwa watu watatu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hapo awali. Waliochukua fomu na kujitokeza hapo awali ni Makamu wa Rais wa zamani wa Uganda, Dk. Specioza Kazibwe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Botwana, Pelonomi Venson-Moitoi na Agapito Mokuy kutoka Guinea ya Ikweta.

Hata hivyo, vyanzo vya kuaminika vinasema kuwa viongozi wa Afrika sasa wako tayari kumpa Kikwete nafasi hiyo endapo tu nchi yake itakubali kumuunga mkono katika mchakato huo. Katika uchaguzi wa kwanza uliofanyika Kigali, Tanzania pamoja na nchi nyingine za Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zilimuunga mkono Moitoi.



Kwa mujibu wa gazeti maarufu la Botswana, Sunday Standard, viongozi wa SADC sasa wamegawanyika baada ya kuonekana kwamba Kikwete ana nia ya kuwania nafasi hiyo; akionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kushika wadhifa huo kuliko washindani wake.
Likinukuu vyanzo mbalimbali vya kidiplomasia, gazeti hilo limedai kwamba zaidi ya ujio wa Kikwete, jambo jingine lililomharibia mtarajiwa huyo wa SADC ni habari zilizoibuka hivi karibuni kwamba mgombea huyo sasa anaungwa mkono na Marekani.

“Kuna baadhi ya nchi wanachama wa SADC kwa kupitia njia zao za kijasusi zimedaka taarifa za kiintelijensia jijini Gaborobe kwamba Moitoi ndiye kipenzi cha Wamarekani. Kuna nchi kama Zimbabwe na Lesotho hazitaki kusikia mtu anatumika na Marekani. Hiki ni kikwazo kwa Moitoi.
“Kuna shaka kuwa Venson-Moitoi atakuwa kibaraka wa Marekani barani Afrika kwani zipo taarifa kuwa nchi hiyo imemuahidi mgombea huyo kuwa itamsaidia kifedha kwenye kampeni yake ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa AU,” limeandika gazeti hilo.

Katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Julai mwaka huu jijini Kigali, Rwanda, nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wenye nchi 15 haukupiga kura kwa kile kilichoelezwa kuwa haukuona kama kuna mgombea makini miongoni mwa watatu hao wa kwanza.

Vyanzo vya kuaminika vinasema kuwa viongozi wa Afrika Magharibi wanamuunga mkono Kikwete; huku Rais wa Senegal, Macky Sall, akitajwa kuwa mmoja wa waungaji mkono wake wa wazi.

Viongozi wengine wa Afrika ambao tayari wanafahamika kwa kuunga mkono Uenyekiti wa Kikwete ni Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Mfalme Mswati wa Swaziland, Rais Ali Bongo wa Gabon, Mugabe, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Kwa sababu nchi za ECOWAS hazikupiga kura Kigali, ndiyo sababu akina Moitoi walishindwa kupata kura za kutosha kuweza kushinda nafasi hiyo.

Pamoja na uungwaji mkono huo wa Kikwete, hadi mwezi uliopita Tanzania ilikuwa ikimuunga mkono mgombea wa SADC, Venson-Moitoi na hakuna taarifa mpya zilitolewa na serikali kama imebadili msimamo wake.

Mpaka sasa Rais huyo mstaafu hajachukua fomu na taratibu za kuwania nafasi hiyo zinataka mtu achukue fomu kwanza.


Dr. Jakaya Kikwete akizungumza na Rais Barack Obama
na mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama
cha Democratic Bi Hillary Clinton Ikulu mjini Washington

Kikwete ni miongoni mwa wanadiplomasia mashuhuri katika duru za AU ambapo mwaka huu aliteuliwa kuwa Mwakilishi wake maalumu katika mgogoro unaoendelea hivi sasa nchini Libya.
Kwa vile sehemu kubwa ya shughuli za AU zinafadhiliwa na nchi wahisani, Mwenyekiti wa chombo hicho anatakiwa kuwa mtu ambaye ana uhusiano mzuri na wahisani na mwenye uwezo wa kuzungumza nao na wakamsikiliza; sifa ambazo inaelezwa kuwa Kikwete tayari anazo.

No comments:

Post a Comment