Thursday, August 11, 2016

MAAMBUKIZI SUGU YA NJIA YA MKOJO


Maambukizi Sugu ya Njia ya Mkojo (Chronic UTI) ni Nini?

Njia ya mkojo ni sehemu ya mfumo wa mkojo wenye ogani mbalimbali kama figo, urethra (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo.



Yapo maambukizi ambayo hayatibiki kwa urahisi au yanajirudia mara kwa mara licha ya kutibiwa. Maambukizi sugu ya njia ya mkojo (Chronic Urinary Tract Infections (UTIs)  ni miongoni.
Njia ya mkojo ni sehemu ya mfumo wa mkojo wenye ogani mbalimbali kama figo, urethra (mirija inayobeba mkojo kutoka kwenye figo kwenda kwenye kibofu cha mkojo).

Maambukizi kwenye njia ya mkojo yanaweza kutokea sehemu yoyote katika mfumo huu. Ikiwa maambukizi yataathiri kibofu cha mkojo peke yake ni rahisi kutibika lakini yakisambaa mpaka kwenye figo, mwathirika huumwa zaidi na pengine kulazwa hospitali.

Ingawa maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kumpata mtu yeyote kwa wakati wowote, sanasana wanawake. Utafiti wa National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK) inakadiria kuwa katika kila wanawake watano, mmoja ana maambukizi sugu ya njia ya mkojo yanayojirudia mara kwa mara.
Kinachoongeza hatari ya maambukizi sugu ya njia ya mkojo

Maumbile: Maambukizi sugu ya njia ya mkojo huwapata sana wanawake kutokana na maumbile yao.

Kwanza, urethra yao ipo karibu sana na puru (rectum) hivyo kurahisisha bakteria kutoka kwenye puru kuingia kwenye urethra hasa wakati wa kutawaza. Mara nyingi hutokea endapo mhusika atajisafisha kwa kurudisha mkono kutoka nyuma kwenda mbele. Watoto wadogo wa kike hupata maambukizi ya UTI kwa kuwa hawaijui kanuni hii.
Pili, urethra ya mwanamke ni fupi zaidi ikilinganishwa na ya mwanaume. Bakteria wana umbali mfupi wa kusafiri kufika kwenye kibofu cha mkojo ambako wanaweza kuzaliana na kuongezeka kiurahisi na kusababisha maambukizi.

Aina ya Maisha: Kuna aina ya maisha ambayo yanaweza kukufanya uwe kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi kwa urahisi. Kwa mfano kutumia diaphragm (mpira laini maalumu unaowekwa ukeni wenye kizibo cha kuzuia mbegu za mwanamme kupenya ili  kukutana na yai la mwanamke) inaweza kusukuma juu urethra na kufanya iwe vigumu kutoa mkojo wote baada ya kukojoa. Mkojo unaobaki kwenye kibofu huongeza uwezekano wa bakteria kuzaliana na kusababisha maambukizi.

Vilevile, matumizi ya vitu vyenye kemikali kuosha uke vinavyoua bakteria walinzi wa kwenye uke, kama sabuni, marashi au viua mbegu za kiume (spermicides). Pia, kunywa dawa za kuua bakteria mwilini huweza kuua walinzi kwenye uke. Hii inaweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi sugu ya njia ya mkojo.

Kukoma hedhi: Kukoma hedhi husababisha mabadiliko ya homoni ambayo mwisho husababisha kubadilika kwa hali ya bakteria walinzi ndani ya uke hivyo kufanya wafe kwa wingi na uke kukosa ulinzi na kufanya iwe rahisi kupata maambukizi ya njia ya mkojo mara kwa mara.

Aina za maambukizi ya UTI
Maambukizi ya njia ya mkojo husababishwa na bakteria ambao mara nyingi huingia kwenye mfumo wa mkojo kupitia urethra na kisha kuzaliana na kuongezeka zaidi kwenye kibofu cha mkojo. Ili kuelewa zaidi maambukizi haya  namna yanavyotokea ni vizuri kugawanya maambukizi katika kibofu cha mkojo na maambukizi katika urethra.

Maambukizi katika kibofu cha mkojo (Cystitis) mara nyingi husababishwa na bakteria waitwao Escherichia coli. E.coli ni bakteria wanaoishi kwenye utumbo wa watu na wanyama wenye afya nzuri. Bakteria hawa wakiwa mahala pao hawana madhara, isipokuwa wakipata upenyo wa kutoka huenda njia ya mkojo na kusababisha maambukizi.
Mara nyingi hutokea pale mabaki ya kinyesi yasiyoonekana yanapoingia kwenye njia ya mkojo.
Kushiriki ngono ya kinyume na maumbile kunaongeza hatari ya kupata maambukizi ya UTI.
Maambukizi katika urethra (Urethritis) yanaweza kusababishwa na E.coli au magonjwa na maambikizi ya zinaa au yanayofahamika Sexually Transimitted Infections (STI) kama pangusa, kisonono au klamidia. Hata hivyo, magonjwa na maambukizi haya ya zinaa mara chache husababisha maambukizi ya njia ya mkojo.

Dalili za Maambukizi sugu ya UTI
Kwa mtu anayehisi maumivu chini ya kitovu au kwenye kibofu cha mkojo au mara kwa mara, kukojoa mkojo uliochanganyika na damu  ni dalili za wazi za maambukizi haya.
Dalili zingine ni kutoa mkojo mzito, kuhisi kuchomwa au maumivu wakati wa haja ndogo na maumivu kwenye figo yaani chini ya mgongo au mbavu.


Ikiwa maambukizi yatasambaa hadi kwenye figo, yanaweza kusababisha kichefuchefu, kutapika, baridi, homa kali (zaidi ya nyuzi joto 38.3), uchovu na kuchanganyikiwa.
Mara nyingi, dalili hizi hutofautiana kati ya watoto na watu wazima. Umakini unahitajika kumbaini mtoto mwenye maambukizi haya.

Wakati gani wa kumuona daktari?
Mwanzoni, dalili za maambukizi ya njia ya mkojo zinaweza zisiwe zenye maumivu makali lakini baadaye yakawa makali kiasi cha kutovumilika na kuathiri shughuli za kila siku.
Ikiwa dalili zitakuwapo kwa zaidi ya siku tano, inashauriwa ni vyema ukamuona daktari. Pia, muone daktari haraka ikiwa mwili utachemka sana, ikiwa una mimba au kisukari.

Ikiwa una maambukizi sugu ya njia ya mkojo hii ina maana ulikuwa na maambukizi ambayo hayakutibiwa ipasavyo. Madaktari huwatuma wateja wao maabara kwa ajili ya vipimo zaidi kubaini ni maambukizi ya aina gani. Wataalamu wa maabara huangalia mkojo kupitia hadubini ili kuona bakteria wanaosababisha maambukizi.
Kuotesha mkojo (urine culture test) ni kipimo kingine kinachoweza kufanywa na wataalamu wa maabara ili kubaini aina mahususi ya bakteria aliyemshambulia mgonjwa husika na mara nyingi  hurahisisha uchaguzi wa dawa kwa  daktari anayetoa tiba. Kipimo hiki huchukua siku moja mpaka tatu kabla majibu kutoka.

Ikiwa daktari atahisi kuna uharibifu wa figo uliosababishwa na maambukizi hayo atapendekeza vipimo zaidi vya figo kama X-ray na Ultrasound. Kama una maambukizi yanayojirudia mara kwa mara daktari anaweza kufanya kipimo cha cystoscopy kinachohusisha mpira mrefu wenye lenzi mwishoni unaotumika kuangalia urethra na kibofu cha mkojo. Daktari anaweza kuangalia pia tofauti za kimaumbile alizonazo mwanamke zinazosababisha kujirudia kwa maambukizi.

Madhara ya muda mrefu ya UTI                                 
Maambukizi sugu ya njia ya mkojo yanaweza kusababisha madhara  kwenye figo. Ugonjwa wa figo husababisha kuharibika kwa figo yenyewe na  kwa watoto wadogo, kusambaa kwa bakteria kwenye damu (septicaemia). Kwa wajawazito  huongeza hatari ya kuzaa watoto njiti endapo hautakabiliwa kwa wakati.

Kujikinga na UTI 
Kojoa mara nyingi uwezavyo muda wowote unapojihisi kufanya hivyo.

Wakati wa kutawaza, safisha kwa kupeleka mkono nyuma.

Kunywa maji mengi kusafisha bakteria kwenye njia ya mkojo kila mara unapokojoa bila kusahau kuvaa chupi iliyotengenezwa kwa pamba.

Epuka kuvaa nguo za ndani zinazobana sana na kutumia diaphragm kama njia ya uzazi wa mpango.

Tumia mafuta ya kulainisha wakati wa tendo la ndoa ikiwa inawezekana ili kuondoa michubuko isiyo ya lazima yenye kufanya upenyo wa bakteria.

Kwa wanawake, epuka kuoga ndani ya mapovu mengi kwa kuwa kemikali zilizopo  kwenye sabuni huingia kwenye uke na kuua bakteria walinzi hivyo kufanya iwe rahisi kupata maambukizi.

Kwa wanaume, ikiwa haujatahiriwa osha vizuri uume wako mara kwa mara baada ya haja ndogo au tendo la ndoa

No comments:

Post a Comment