Thursday, August 4, 2016

Kujua lugha ya Kiarabu sio kuujua Mwongozo wa Allah

Na Sadiq M. Sadiq. (Gazeti la Annur

Haya ni maelezo ya wazi kwa watu (wote na uongozi na mauidha kwa wamchao (Mwenyezi Mungu). Na kwa yakini tumeifanya Qur-an iwe ni nyepesi kufahamika lakini yuko anayekumbuka" (54:17).

"Kitabu kinachopambanuliwa aya zake ni kisomi (kikilichoteremka) kwa lugha ya Kiarabu kwa wanaojua kheri. Kitoacho habari njema na kionyacho lakini wengi katika wao wamekengeuka kwa hiyo hawasikii" (54:3-5).

Aya zilizotangulia hapo juu bila shaka zinajieleza wazi hazihitaji ufafanuzi wa kina. Mwenyezi Mungu (s.w) kateremsha Qur-an kama ni mwongozo.

"Tukasema shukeni humo nyote na kama ukikufikieni mwongozo utokao kwangu, basi watakaoufuata mwongozo wangu haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika" (2:38).

"Hivyo Qur-an ni mwongozo kwa wamchao Allah (s.w)" (2:2).

Allah (s.w) ameteremsha Qur-an kwa watu wote lugha zote hivyo watu wataifahamu Qur-an kama mwongozo wao kwa lugha wanayoielewa wao.
Na Qur-an haina maana ni kitabu tu bali ni uongozi kamili kwa wanaomcha Allah (s.w) utakuta humo maonyo. Mawaidha, rehema, n.k. Hivyo ujumbe uliomo ndani yake ndio hitajio la watu kama aya zote nilizozitaja hapo juu zinavyojieleza wazi. Sasa inachoshangaza kukuta mtu anadai kwamba huwezi ukaisoma Qur-an mpaka ujue kiarabu, kwa maana nyingine huwezi kuongozwa na Qur-an mpaka ujue kiarabu.

Pili, huyo huyo mtu anaedai mtu anasimama katika mimbari hali ana Uislamu wa Kimarekani kwa kuwa amevaa suruali aina ya jeans au suti na tai na pia anaongea kingereza mtu wa aina hiyo ana Uislamu wa Kimarekani.

Nianze na la kwanza. Ni kweli kwamba huwezi kufasiri Qur-an mpaka utimize masharti yake na moja ya sharti ni kujua lugha ya Kiarabu. Lakini kuwa mimi nisiefahamu Kiarabu siwezi kusoma Qur-an ama siwezi kuongozwa na Qru-an hii si kweli kwa sababu japo Qur-an imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu haiitaji lugha bali mwongozo. Hivyo mwongozo humwongoza mtu kwa kuelewa hiki ni nini na hiki ni nini.

Kiarabu ni lugha ya Mtume (s.a.w) ndio maana Allah akamteremshia kwa lugha hiyo na kama Mtume (s.a.w) angekuwa msukuma basi Qur-an ingeshuka kwa lugha ya kisukuma ili wale wanaoteremshiwa wapokee kwa lugha wanayoifahamu ndio maana Mtume (s.a.w) alituma baadhi ya maswahaba wake ili wajifunze lugha zingine kusudi kubwa lilikuwa ni mawasiliano pamoja na kuwafikishia ujumbe wa Allah (s.w) kwa lugha wanayoielewa wao.

Si lengo langu kupinga Waislamu wasijifunze Kiarabu la. Nia yangu wale wanaoifahamu Qur-an kwa maana wanaofahamu ujumbe uliomo ndani yake basi wawafikishie wengine kwa lugha wanayoielewa. Ajabu huyo anaedai huwezi kusoma Qur-an mpaka ujue Kiarabu anatumia aya za duniani kisha anatafsiri kwa lugha ya kiswahili halafu anawambia wengine hawataifahamu au wajue Kiarabu.

Ni vizuri wewe unaeijua watungie watu vitabu kwa lugha wanazofahamu ili iwe rahisi kwao kuelewa ujumbe uliomo kuliko kuwakatisha tamaa kabisa kuwa mpaka wafahamu Kiarabu ndio wajue huku ni kuturudishia maendeleo yetu nyuma.
Wawepo wasomi, katika jamii wataozama katika elimu ili watufahamishe misingi ya Uislamu katika lugha tunayoielewa. Hamwezi wote kuwa watabibu, wanasayansi, wanasiasa, wachumi n.k., lakini wachache wakifahamu watakidhi mahitaji ya wengi. Hivyo si wote wataifahamu Qur-an katika lugha yake ya asili lakini ikifanywa juhudi ya kuitafsiri katika lugha mbalimbali kama ambavyo ilivyo hivi sasa watu watafahamu kulingana na lugha zao. Mswahili, mwingereza, mmasai, mnyamwezi n.k., wote hao wakifikishiwa ujumbe kwa lugha wanazozielewa itakuwa ni busara sana. Kwa kuwa Allah (s.w) anasema Qur-an ni nyepesi kufahamika yaani miongozo yake inakubaliana na akili ya mtu ni wajibu kuifikisha kwetu japo si kwa lugha ya Kiarabu. Maadamu Qur-an inatafsirika kwa lugha zote basi wanazuoni ndio wenye jukumu la kuifasiri katika lugha mbali ili iweze kuwafikia walengwa.

Pili, kwamba kuna Uislamu wa Kimarekani. Sasa yule anaedai kwamba mvaa jeans au suti kisha akasimama katika membari na huku akitoa mawaidha akichanganya na kingereza kwa mtazamo wa mtu huyo, huyo ni Muislamu wa Kimarekani. Kwa uoni wangu madai ya mtu wa aina hii si yenye upeo na bado hajafahamu kuwa Qur-an ni mwongozo. Na kama anafahamu Qur-an kuwa ni mwongozo basi fikra zake zinamtuma kuwa wanaoongozwa ni wavaa kanzu, vilemba, hajari akiwa na tasbihi (shanga) ndefu kama mtu huyo ndie ataeongozwa na Qur-an.
Fikra ya aina hii si ya msomi na kama ni msomi basi ni msomi wa lugha na sio Qur-an ndio maana madai yake yanalenga kujua lugha ndio ujue Qur-an. Mfano mimi nimesilimu kutoka ukristo na kuingia Uislamu itakuwaje basi mpaka nijue lugha ndio nijue mwongozo? Kwa maana hiyo wanaosoma mfano, Tafsiri ya Qur-an ya Abdallah Farsy hawajui Qur-an kwa kuwa lugha imewatupa mkono.

Vivyo hivyo anaevaa jeans atakapoelewa kwamba Qur-an ni mwongozo vipi asiongozwe kwa kuwa amevaa jeans? Watu wa namna ya huyu wanataka Uislamu wa Saudi Arabia wa kanzu, kitu ambacho sicho kinachoupeleka Uislamu mbele. Wapo wanafiki wao hurudisha nyuma maendeleo ya Uislamu, lakini nao utawakuta wamefuga ndevu wamevaa suruali fupi wamenyoa nywele lakini hayo yote ni mapambo ya mwili vitendo ni mnafiki huyu je? Tena na lugha anaijua vizuri sana.
Kwa kifupi Uislamu si kanzu wala kofia bali ni kuukubali moyoni na kuutia katika vitendo kwa lengo la kusimamisha serikali ya Allah (s.w).
Mashariki ya kati vazi lao ni kanzu utakuta mkristo myahudi na mwislamu wote wamevaa kanzu. Kwa hiyo ukidai mvaa jeans ni mwislamu wa kimarekani nasi tutaona mvaa kanzu mwislamu wa saudia au mashariki ya kati kutokana na uvao wake.
Ningeshauri watu wa namna hii wawafunze Waislamu wasiofahamu mwongozo wa Allah (s.w) jinsi ipasavyo Muislamu kutenda na sio kuwakatisha tamaa kwa mavazi, lugha n.k.
"Allah (s.w) anatazama nafsi zetu na matendo yetu, kama yanalingana na mwongozo wake.

No comments:

Post a Comment