Thursday, July 28, 2022

XINJIANG: KICHAKA CHA MATAIFA YA MAGHARIBI KATIKA HARAKATI ZA KUIDHOOFISHA CHINA.

 Na Masudi Rugombana   


Xinjiang ni mkoa mkubwa kuliko yote nchini China. Mkoa huu unaopatikana kaskazini magharibi ya China una jumla ya kilometa za mraba milioni moja, laki sita na elfu sitini na tano (1.665 million km²). Kwa ukubwa wa eneo mkoa huu umeizidi kidogo nchi ya Iran. Mkoa huu unajulikana rasmi kama XUAR yaani Mkoa unaojiendesha wa Wauighur wa Xinjiang ( Xinjiang Uighur Autonomous Region ) ni eneo lenye utajiri mkubwa wa maliasili ikiwemo Mafuta, gesi asilia, makaa ya mawe na dhahabu unapakana na nchi za Mongolia, Russia, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Afghanistan, India na Pakistan. 



Mbali na utajiri wa maliasili, mkoa huu wenye utajiri mkubwa wa kitamaduni wenye  idadi ya makabila yenye asili, lugha, imani za kidini, mila na tabia ya tofauti umekuwa na mawasiliano ya karibu ya kiuchumi na kiutamaduni na nchi jirani inazopakana nazo. Mkoa una jumla ya watu milioni 25, ambapo watu milioni 12 sawa na asilimia 44.96 ni wa jamii ya Uighur. Wauighur, ni jamii ya Kituruki yenye uhusiano wa kitamaduni na eneo la Mashariki na Asia ya Kati. Watu wa jamii ya Han huko Xinjiang ni asilimia 42.24 na asilimia 12.80 ni watu wa jamii za Kazakh, Kyrygz, Hui, Mongol , Tibet, Xibe, Tajik, Ozbek, Manchu, Daur, Tatar na Russians (Warusi).  Lugha rasmi  zinazozungumzwa mkoani Xinjiang ni Uighur na Mandarin. Waislam ni zaidi ya nusu ya wakazi wote wa Xinjiang.  Mji mkuu wa mkoa ni Ürümqi.


China imekuwa ikishutumiwa na mataifa ya Ulaya Magharibi  kuhusika na uhalifu dhidi ya ubinadamu ikiwemo kufanya   mauaji ya halaiki dhidi ya wakazi wa Uyghur sambamba na  makabila mengine yenye idadi kubwa ya watu wanaofuata imani ya dini ya Kiislam hasa katika mkoa wa kaskazini magharibi wa Xinjiang.Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanailaumu China kwa kuwazuilia zaidi ya Wauyghur milioni moja kinyume na matakwa yao katika makambi ya mateso ( Concentration Camp), hata hivyo serikali ya China inasema kuwa hayo sio makambi ya mateso bali  ni vituo vya mafunzo (Education training centers) vyenye lengo la kukomesha itikadi kali za kidini na kuwapa watu ujuzi mpya. 


Mapema katika karne ya 20, Marekani na nchi nyingine za Ulaya Magharibi zilianzisha juhudi za kuunga mkono harakati za kujitenga kwa mkoa wa Xinjiang ili kuunda Taifa litakalojulikana kama Turkestan Mashariki ( East Turkestan), juhudi hizo zilizokwenda sambamba na kufadhili matendo ya kigaidi huko Xinjiang kwa lengo la kuiyumbisha China na kudhibiti kasi yake ya Maendeleo.


Mnamo Mwezi August 2018 akizungumza katika taasisi ya Ron Paul (Ron Paul Institute) kanali mstaafu Lawrence Wilkerson, mkuu wa zamani wa wafanyakazi (Former Chief of staff) katika wizara ya mambo ya nje ya Marekani wakati huo ikiongozwa na General Mstaafu Collin Powell, alisema kwamba mojawapo ya sababu za Marekani kuwepo nchini Afghanistan ni kwa sababu kuna watu wa jamii ya Uighur huko Xinjiang wapatao milioni 20, kwa hivyo CIA ingetaka kuivuruga China kupitia harakati za WaUighur na kwamba hiyo ndiyo ingekuwa njia bora ya kufanya ili kuzusha machafuko baina ya jamii za WaUighur na Han na kwamba Marekani ingewasaidia WaUighur kuwatimua watu wa jamii ya Han na kuwaondoa katoka mkoa wa Xinjiang. 


Kwa miaka mingi, kumeibuka idadi ya taasisi zinazoipinga China ikiwa ni pamoja na kuanzishwa makundi yenye itikadi kali yanayopigania kuanzishwa kwa taifa la  Turkistan Mashariki kupitia kile kinahoitwa "uhuru" wa Xinjiang. Miongoni mwa harakati hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa bunge la Uighur na Serikali ya Turkistan Mashariki, vyote vikifanya kazi uhamishoni kwa kufadhiliwa na Marekani na Uturuki. Kwa mujibu wa vyanzo vya kiintelijensia vya China,  mwaka 2004,  Marekani ilitoa dola  milioni 8.76 kwa makundi ya watu wanaoishi nje ya Uighur wanaofanya kampeni dhidi ya China huko Xinjiang.


Ufadhili huo kutoka Marekani umesababisha kuenea haraka kwa fikra za itikadi kali za Kiislam huko Xinjiang na hivyo kupelekea Magaidi kutoka katika medani za vita nchini Afghanistan, Pakistan na Syria kumiminika kwa wingi mkoani Xinjiang. Baadhi ya makundi ya kigaidi yenye nguvu yaliendesha kampeni kali kushambulia raia wa China kupitia vuguvugu la Kiislamu la Turkestan Mashariki (East Turkestan Islamic Movement (ETIM) kati ya mwaka 1997 na 2014  yaliyogharimu maisha ya zaidi ya raia 1,000. Ikumbukwe kwamba kundi la Kiislam la ETIM lina uhusiano wa karibu na Mtandao wa Alqaeda unaoongozwa na Dr. Ayman al Zawahir. 


Katika kukabiliana na tishio la mashambulizi, serikali ya China imechukuwa hatua muhimu kuhakikisha utulivu na amani vinapatikana ili kuwezesha watu wa imani tofauti kuishi kwa pamoja katika mkoa wa Xinjiang. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kupambana kutokomeza makundi ya itikadi kali za kidini na kuweka sheria zinazolinda haki na uhuru wa kufanya ibada kwa watu wa imani zote. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha vyuo vya mafunzo ambapo makundi ya vijana wanaokamatwa kutokana na kuhusika na vurugu za kidini na kikabila hupelekwa kupewa ujuzi pamoja na kufundishwa uzalendo wa Kichina. 


Kufuatia hatua kali za kukabiliana na makundi ya itikadi kali za kidini zilizochukuliwa na serikali ya China, sasa ni miaka minne mfululizo hapajawahi kutokea shambulizi lolote la kigaidi huko Xinjiang. China inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha huduma za kijamii katika Uighur ikiwemo ukarabati wa misikiti. 


Xinjiang kuna misikiti elfu ishirini na nne, Mingi katika hiyo imejengwa miaka ya 1980 na 1990, na haikujengwa kwa Ubora unaotakiwa. Kutokana na ukuaji wa miji na vijiji kuna baadhi ya misikiti inawawia vigumu Waislamu kufanya Ibada kutokana na uchavu na kuna baadhi ya misikiti haifikiki kirahisi. Kwa hivyo Serikali ya China inafanya mambo matatu kwa ruhusa ya Waislamu wenyewe kupitia Serikali zao za mitaa. 


1. Kubomoa misikiti inayohatarisha Usalama na kujenga misikiti mipya, imara na ya kisasa.

2.Kukarabati Misikiti ya zamani 

3. Kuhamisha misikiti iliyojengwa mahala ambapo ni vigumu kufikika kwa kujenga sehemu ambayo ni kubwa zaidi na rahisi kufikika sambamba na upanuzi wa misikiti yenye maeneo madogo ya kufanyia ibada. 


Kinachofanywa na vyombo vya habari vya Ulaya Magharibi ni kupiga picha misikiti mibovu inapovunjwa kwa ajili ya ukarabati na kisha kuitangazia Dunia kuwa China inavunja misikiti huko Xinjiang. Lengo la propaganda hizo ni kuichafua China katika Ulimwengu wa Kiislamu. Propaganda ambazo zimeshindwa kuyashawishi Mataifa mengi ya Kiislam ikiwemo Umoja wa Ushirikiano wa nchi za Kiislamu (OIC) kuilaani China. 


Suala la Waislamu kuzuiwa kusali, kuzuiwa kutumia majina ya Kiarabu, kuzuiwa kufunga saumu ya Ramadhani na kulazimishwa kula nyama ya nguruwe ni mojawapo ya propaganda chafu zinazoenezwa na vyombo vya habari vya magharibi dhidi ya China. Ukweli ni kwamba Uhuru wa kuabudu mkoani Xinjiang ulikuwa mashakani kipindi ambacho makundi ya Itikadi kali za kidini yalipoimarisha harakati zao, ilikuwa ni vigumu kwa Waislamu kufanya ibada hadharani kutokana na tishio la kushambuliwa, pia viongozi wengi wa Kiislamu waliopingana na makundi ya itikadi kali walilengwa na kuuawa. 


Mara baada ya Serikali ya China kukomesha harakati za makundi ya Kiislam yenye itikadi kali, katika kipindi cha miaka minne mfululizo Waislamu wamekuwa wakifanya ibada misikitini bila hofu sambamba na kushiriki ibada nyingine kama hija na funga ya Ramadhan. Kati ya mwaka 1996 hadi 2019, Jumuiya ya Kiislamu ya China  kwa kushirikiana na Serikali imeweza kugharamia hija kwa Waislamu elfu hamsini wa Xinjiang kwa safari za ndege za kukodi kwenda Makka, na pia kutoa huduma za tafsiri na matibabu. 


China ni Taifa linaloongozwa na serikali isiyofuata imani yeyote ya kidini (Secular State) ikiwa na Jumla ya watu Bilioni moja na milioni mia nne kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2020. Waislamu wanakadiriwa kufikia milioni 28 sawa na asilimia 1.73 wengi wao wakiwa ni kutoka jamii ya Hui wakifuatiwa na watu kutoka jamii ya Uighur. Hata hivyo kwa takwimu zisizo rasmi China inakadiriwa kuwa na idadi ya Waislamu milioni 150. Asilimia 74.5 ya Wachina ni Wapagani, Mabudha ni asilimia 18.3 na Wakristo ni asilimia 5.1.


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.


© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇


Email: masudirugombana@gmail.comSimu: 


0743 184 044

Monday, June 27, 2022

HATIMA YA UKRAINE IPO MIKONONI MWA URUSI.

Na Masudi Rugombana  

Tarehe 21 February 2022 Rais Vladmir Putin wa Urusi alitangaza kutambua uhuru wa eneo la Donbass, Jimbo la Mashariki ya Ukraine linaloundwa na mikoa miwili ya Luhansky na Donetsky, mikoa inayokaliwa na idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi. Mikoa hii ilijitangazia uhuru kutoka Ukraine mwaka 2014 kutokana na kura ya maoni iliyoongozwa na makundi ya wapiganaji kufuatia mgogoro wa kisiasa uliozusha maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Rais Viktor Yanukovych kiongozi aliyeegemea zaidi upande wa Urusi hatua ambayo Rais Vladmir Putin aliifananisha na mapinduzi ya kijeshi. Kuondolewa madarakani kwa Victor Yanukovych kulifuatiwa na maandamano makubwa ya makundi ya watu wanaounga mkono Urusi huko Mashariki na kusini mwa Ukraine ambapo mkoa wa Crimea wenye idadi kubwa ya Raia wenye asili ya Urusi uliitisha kura ya maoni iliyopelekea wakazi wake kuchagua kujiunga na Urusi hivyo kuipa uhalali Urusi kuitwaa Crimea na kuifanya eneo lake. 

Tangazo la Putin kutambua uhuru wa Donbass lilifuatiwa na uingiliaji kati kijeshi tarehe 24 February 2022  katika Operesheni inayokusudia kuvunja nguvu za kijeshi za Ukraine na kuondoa matendo ya kikatili yanayofanywa na wapiganaji wa jeshi la Ukraine wenye siasa kali za kizalendo zilizogubikwa na fikra za kinazi ( Operation demilitalize and denazify). Kiuhalisia, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine una malengo mapana zaidi ya hicho kinachoitwa ukombozi wa Donbass. Ni uvamizi unachagizwa na mambo mengi ya kiusalama na kimaslahi yanayohusu Urusi zaidi ya kusudio la kuikomboa Donbass.  

Baada ya umoja wa kisoviet kuanguka mwaka 1990, Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) ulijitanua kuelekea upande wa Mashariki na hatimaye kuyachukua mataifa ya eneo la Baltic, Jamhuri za Lithuania, Latvia na Estonia ambazo zilikuwa sehemu ya umoja wa Kisovieti (Soviet Union ) na kupeleka umoja huo wa kijeshi kujisogeza karibu na  Moscow kwa kupakana moja kwa moja Urusi. Mwaka 2008 NATO iliweka wazi mipango yake ya kutaka kuisajili Ukraine. Ikumbukwe kuwa  Rais Vladmir Putin aliwahi kusema kwamba kusambaratika kwa umoja wa Kisovieti lilikuwa ni janga kubwa katika karne ya ishirini lilipelekea Urusi kuporwa haki yake kama mojawapo ya Mataifa yenye nguvu kubwa Duniani. Putin ametumia miaka 22 madarakani kujenga upya jeshi la Urusi kwa lengo la kurejesha nguvu yake ya kiushawishi kwenye siasa, ulinzi pamoja na mahusiano ya kimataifa  (Geopolitical clout)

Putin alishaweka wazi kuwa kujitanua kwa NATO kuelekea Mashariki sambamba na mkakati wake wa kuisajili Ukraine kwamba ni kitisho kisichovumilika dhidi ya Urusi, akilaumu uwepo wa vikosi vya Marekani na makombora yao kibalistic  ya masafa Marefu nchini Ukraine, huku akisisitiza kuwa Ukraine ni sehemu muhimu ya Urusi kisiasa na kiutamaduni.Hivyo basi kutokana na tishio la NATO, Urusi iliamua kuongeza nguvu za kijeshi kuelekea upande wa Magharibi kwenye mpaka wake na Ukraine kwa lengo moja tu ambalo ni kufanya shambulizi (Pre-emptive strike) dhidi ya Ukraine kwa lengo la kujihami dhidi ya kitisho cha NATO. Katika jithada za kuepusha vita, NATO na Ukraine walitaka Urusi kuacha kujijenga kijeshi kwenye mpaka wake na Ukraine hivyo kufungua meza ya majadiliano baina ya pande mbili. Urusi ilitoa masharti makuu matatu ili ombi hilo la NATO liweze kutekelezwa. 

1. Ipewe hakikisho kwamba Ukraine haitajiunga na NATO.

2. NATO iondoe vikosi vyake katika nchi za Ulaya Mashariki.

3. Jeshi la Ukraine Kusitisha mapigano kwenye eneo la  Donbass kwa mujibu wa makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015  ambayo yaliweka masharti ya kuondolewa kwa silaha nzito kutoka kwenye uwanja wa vita, kuachiliwa kwa wafungwa wa pande zote mbili, na marekebisho ya katiba nchini Ukraine ikiwa ni pamoja na utoaji wa uhuru kwa mikoa ya Donetsk na Luhansk.

NATO na Ukraine waliyakataa madai yote ya Urusi, hivyo kupelekea Urusi kutokuwa na namna nyingine zaidi ya kulinda  usalama wake kwa kuivamia Ukraine katika kile kinachoitwa oparesheni maalum ya kijeshi ( Special military operation) ili kuzuia isijiunge na NATO. Ni uvamizi mkubwa wa kijeshi barani  Ulaya tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia. Lengo kubwa la Rais Vladmir Putin katika operesheni hii ni kurudisha Usawa baina ya Urusi na Marekani kwa kupunguza kitisho cha NATO. 

Urusi chini ya Putin ikisimama peke yake dhidi ya Ukraine inayoungwa mkono na NATO kifedha na kijeshi inapigana kwa tahadhari kubwa, akili nyingi na kwa mipango na mikakati ya kueleweka. Jeshi lake linasonga mbele taratibu lakini kwa uhakika, likipiga hatua tatu mbele na kurudi hatua moja nyuma pale uwanja wa mapambano unapokuwa mgumu. Urusi inashinda kwenye uwanja wa vita, inapambana kwenye uwanja wa Diplomasia na inashinda kwenye kampeni kali ya vikwazo dhidi ya uchumi wake na hivyo kumkatisha tamaa Rais Volodymyr Zelenskyy na washirika zake kutoka NATO na Umoja wa nchi za Ulaya ambazo kwa kiasi kikubwa uchumi wao umeathirika vibaya kutokana na vikwazo vyao wenyewe wanavyoweka dhidi ya Urusi. 

Kutekwa kwa miji muhimu kama Kherson na Mariupol lilikuwa pigo kubwa kwa Zelenskyy na NATO, lakini kudondoka kwa jiji la Severodonetsky, mji mkuu wa wakazi wa mkoa wa Luhansky wanaopinga kujitenga na Ukraine kunatuma ujumbe kwa Zelenskyy na mabwana zake wa Magharibi kuhusu uimara wa jeshi la Urusi na hatari ya Ukraine kugawanywa vipande viwili katika siku za usoni. 


Kuna kila dalili kuwa Ukombozi wa Donbass hautakuwa mwisho wa uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine, kwani lengo hasa la Putin ni kuhakikisha sehemu yote ya Mashariki na kusini mwa Ukraine inakuwa chini ya Urusi, hivyo basi kutekwa kwa mikoa mitano ya Kharkiv, Dnipropetrovsk, Zaporizhia, Mykolaiv na Odesa kuelekea Tranistria ni mojawapo ya malengo yajayo  ya operation maalum ya kijeshi ya Urusi inayoendelea nchini Ukraine. Hivyo basi kuna uwezekano mkubwa mapigano kuendelea kwa muda mrefu. 

Hatima ya Ukraine itaamuliwa na Urusi baada ya kuteka eneo la Mashariki na kusini mwa Ukraine, hapo ndipo itajulikana kama Ukraine itamegwa na kuanzishwa taifa jipya ama eneo hilo kuwa sehemu rasmi ya Urusi. Katika sakata hili la Ukraine ni dhahiri kuwa aliyeanzisha mapigano ndiye huyo huyo atakayeyamaliza mapigano naye siye mwingine isipokuwa ni Vladmir Putin. 


Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.

© Copy rights of this article reserved

®Written by Masudi Rugombana


Napatikana kupitia👇👇👇

Email: masudirugombana@gmail.com

Simu: 0743 184 044