Na Masudi Rugombana
Mnamo tarehe 03 January 2020, jeshi la anga la Marekani (USAF) likitumia ndege yake hatari isiyokuwa na rubani (Unmanned Aerial Vehicle-UAV) aina ya MQ-9 Reaper, kwa amri ya Rais Donald Trump lilimuua Major General Qassem Suleiman, kamanda wa ngazi ya juu katika jeshi la Ulinzi wa mapinduzi ya Kiislam ( The Islamic Revolutionary Guard Corps- IRGC) aliyekuwa akiongoza tawi la kijeshi la Quds (Jerusalem) linalohusika na oparesheni maalumu katika vita visivyo vya kawaida (unconventional warfare) nje ya Iran na shughuli za upelelezi wa kijeshi (military intelligence operations) nje na ndani ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran.
|
Major General Qassem Suleiman |
Qassem Suleiman ambaye vyombo vya habari vya magharibi vimembatiza jina la " the shadow commander" kutokana na umahiri wake wa kuongoza, kupanga na kutekeleza mashambulizi dhidi ya maslahi ya Marekani na washirika zake katika eneo lote la mashariki ya kati kupitia vita vya kiwakala ( Proxy war), aliuawa nje kidogo ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Baghdad nchini Iraq alipokuwa kwenye ziara ya kikazi. Kamanda Suleiman aliingia Iraq akitokea nchini Syria akisafiri kwa kutumia ndege ya abiria aina ya Airbus A320 mali ya kampuni binafsi ya usafiri wa anga ya Cham Wings Airlines yenye makao yake makuu jijini Damascus nchini Syria.
Aliingia kwenye uwanja wa ndege wa Damascus akitumia gari yenye vioo vya giza( dark-tinted glass) akifuatana na askari wanne wa kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi (IRGC). Suleiman na askari wake wanne hawakuwa wamesajiliwa kwenye fomu ya usajili wa abiria ( passenger manifest form ) na gari aliyopanda Soleiman lilisimama moja kwa moja kwenye ngazi ya kupandia ndani ya ndege ( staircase ) ambapo Soleiman na wenzake walipanda ndege tayari kuelekea jijini Baghadad. Waliwasili Kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad saa sita na nusu usiku na kupokelewa na naibu kiongozi wa kundi la Wapiganaji la al-Hashd al-Shaabi (Popular Mobilazation Forces-PMF) Abu Mahdi al Muhandis akifuatana na viongozi wenzake wanne. Msafara wao uliokuwa na magari mawili ulishambuliwa kwa kombora lililorushwa kutoka kwenye ndege isiyokuwa na rubani mara tu baada ya kutoka nje ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad na hivyo kupelekea kifo cha Soleiman na wenzake kumi akiwemo mshirika wake Abu Mahdi al Muhandis.
Kamanda Soleiman alipanga kufanya mazungumzo na viongozi wa kisiasa ikiwa ni katika juhudi za kumuunga mkono Waziri mkuu wa Iraq bwana Adil Abdul-Mahdi al-Muntafiki anayekabiliwa na maandamano ya wananchi wanaotaka aondoke madarakani kufuatia hali ngumu ya maisha inayotokana na kuyumba kwa uchumi wa Iraq. Pia Waziri mkuu Mahdi alithibitisha kuwa alipanga kukutana na Kamanda Suleiman ili kujadili namna ya kumaliza msuguano wa muda mrefu baina ya Mataifa ya Iran na Saudi Arabia muda mfupi kabla hajauawa.
Marekani, taifa tajiri lenye nguvu kubwa kiuchumi na kijeshi kuliko taifa lolote Duniani imetetea uamuzi wa kumuua Major General Qassem Suleiman kwa kusema kwamba mauaji ya Soleimani yalikuwa ni jaribio la kuzuia mashambulizi dhidi ya balozi za Marekani, wanajeshi wake pamoja na wanadiplomasia katika eneo lote la Mashariki ya kati. Uamuzi wa Marekani kuwauwa Qassem Suleiman na Abu Mahdi Al Muhandis ni jambo la hatari linaloendelea kusababisha mtikisiko mkubwa katika mataifa ya Iran, Iraq na eneo zima la mashariki ya kati kiasi cha kukaribia kusababisha vita kamili baina ya Iran na Marekani na wakati huo huo tukishuhudia kuathirika kwa uhusiano wa kiulinzi na kidiplomasia baina ya Marekani na Iraq.
Ni nani huyu Abu Mahdi al Muhandis aliyeuawa sambamba na Major General Qassem Suleiman?
Jina lake halisi ni Jamal Jaafar Muhammad Ali Al Ibrahim. Alizaliwa kwenye mji wa Basra kusini mwa Iraq tarehe 01 Julai mwaka 1954. Baba yake ni raia wa Iraq na mama yake ni raia wa Iran, mke wake pia ni raia wa Iran. Ni msomi katika fani ya uhandisi ( Engineering) aliyohitimu mnamo mwaka 1977, pia ana Shahada ya uzamivu (PhD) ya Sayansi ya siasa. Nchini Iran anajulikana sana kwa jina la Abu Mahdi al Muhandis.
Mara tu baada ya kuhitimu masomo ya uhandisi, alijiunga na Dawah party, chama cha kisiasa kilichokuwa kikipinga serikali ya rais Sadam Hussein, mwaka 1979 wakati utawala wa Sadam Hussein ulipowahukumu adhabu ya kifo wafuasi wengi wa chama cha Dawah, Abu Mahdi alikimbilia Iran ambapo baadae alipewa uraia na kupatiwa mafunzo ya kijeshi kutoka jeshi la Ulinzi wa mapinduzi ya Kiislam (IRGC).
Mara baada ya kuhitimu mafunzo alianza rasmi kufanya kazi na IRGC tawi la Kuwait ambapo mwaka 1983 Abu Mahdi al Muhandis alishiriki kikamilifu katika mashambulizi ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani na Ufaransa nchini Kuwait katika kile kilichoelezwa kuwa ni kuishikisha adabu Kuwait, Marekani na Ufaransa dhidi ya hatua zao za kuiunga mkono Iraq wakati wa vita baina ya Iraq na Iran ya mwaka 1980-1988. Abu Mahdi akishirikiana na raia wanne wa Lebanon alishiriki kuiteka ndege ya abiria ya Kuwait (Kuwait Airliner) iliyokuwa ikitokea Kuwait City kuelekea Karachi nchini Pakistan siku ya tarehe 3 December 1984 na kuilekeza Tehran nchini Iran. Lengo la utekaji wa hiyo ndege lilikuwa ni kuishinikiza serikali ya Kuwait kuwaachia wanaharakati 17 wa Kishia iliyokuwa ikiwashikilia.
Kuwait ilimuhukumu adhabu ya kifo Abu Mahdi al Muhandis bila ya kuwepo mahakamani kwani alikuwa tayari amesharejea nchini Iran kwa tumia hati ya kusafiria (passport) ya Pakistan. Baada ya kurejea Iran, aliteuliwa kuwa mshauri wa kijeshi wa Quds force, tawi la kijeshi la IRGC. Ni hapo ndipo alipofahamiana na Kamanda Qassem Suleiman. Abu Mahdi al Muhandis alirejea nchi Iraq mwaka 2003 kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Marekani uliohitimisha utawala wa miaka 24 wa Saddam Hussein al Tikrit ambapo aliteuliwa kuwa mshauri wa Masuala ya Usalama wa Waziri mkuu wa Iraq Ibrahim al Jaafari.
Ni mwaka huo (2003) ndipo alipoanzisha na kuongoza kundi la wapiganaji wa kishia la Kata'ib Hezbollah ambalo kwa sasa ni mojawapo katika matawi ya kijeshi ya Popular Mobilization Forces (PMF).
Mwaka 2006 Abu Mahdi al Muhandis alipobaini kuwa tayari ameshatambuliwa na maofisa usalama wa Marekani kuwa ndiye aliyekuwa mpangaji mkuu wa mashambulizi katika balozi za Marekani na ufaransa nchini Kuwait, haraka sana aliondoka nchini Iraq na kurejea tena nchini Iran. Alirejea tena nchini Iraq mwaka 2011 kufuatia kujiondoa kwa sehemu kubwa ya vikosi vya Marekani nchini humo.
Mwaka 2014 alikuwa ni miongoni mwa waasisi wa kundi la Popular Mobilazation Forces lililoanzishwa mahususi kwa ajili ya kuyaunganisha makundi ya Wapiganaji wa kishia ili kukabiliana na kundi la kigaidi la Kiwahabi la Islamic State ambalo lilikuwa tayari likishikilia sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq. Baada ya kufanikiwa kulishinda kundi la kigaidi la Islamic state, PMF ilitambuliwa rasmi kama tawi la jeshi la Iraq linalowajibika moja kwa moja kwa Waziri mkuu na wapiganaji wake kulipwa mishahara sawa na wale wa jeshi kuu la Iraq.
Mpaka umauti unamkuta, alikuwa ni Naibu kiongozi mkuu wa kundi la PMF na pia katibu mkuu wa kundi la wapiganaji wa Kishia la Kata'ib Hezbollah. Hivyo basi katika lile shambulizi la ndege isiyokuwa na rubani Marekani ilifanikiwa kuwaua watu wawili iliyokuwa ikiwawinda sana na pia watu muhimu wenye ushawishi mkubwa sana nchini Iran na Iraq.
Athari za mauaji ya Qassem Suleiman na Abu Mahdi al Muhandis.
1. Kuibuka kwa kitisho cha vita kamili kati ya Marekani na Iran. Ni baada ya Iran kuapa kuwa ingelipiza kisasi na Marekani kupitia Rais Donald Trump kutishia kushambulia maeneo muhimu 52 ya kihistoria nchini Iran ikiwa tu Iran itathubutu kujibu Mashambulizi. Iran nayo ilijibu kwa kuionya Marekani kuwa kama itathubutu kushambulia maeneo yake ya kihistoria basi na yenyewe itashambulia maeneo muhimu 36 yenye maslahi ya Marekani katika Mashariki ya kati.
Pamoja na kitisho hicho cha Trump, Iran haikurudi nyuma badala yake siku ya tarehe 8 January 2020 saa saba usiku sawa na muda ule ule aliouwa Kamanda Qassem Suleiman, ilitekeleza mashambulizi mazito ya makombora ya kibalistic ya masafa ya kati na kupelekea uharibifu mkubwa kwenye kambi za jeshi la Iraq zinazotumiwa na vikosi vya Marekani za Ain al Assad mkoani Anbar na kambi moja ya kijeshi iliyopo Elbil mji mkuu wa Jimbo la Kurdistan katika operation iliyopewa jina la Shujaa Soleiman (Operation Martyr Soleimani)
Kambi zote mbili ni kubwa na muhimu sana kwa vikosi vya Marekani na zimeshawahi kutembelewa na viongozi wa Sasa wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump na Makamu wake Mike Pence. Iran ilidai kuuawa askari 80 wa Marekani na kujeruhi wengine 200 , huku Marekani na Iraq zikikanusha na kusisitiza kuwa hapakuwa na madhara yeyote kwa askari wake.
Siku kumi baada ya kushambuliwa hatimaye wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imethibitisha kuwa askari wake 11 wanapatiwa matibabu nchini Kuwait na Ujerumani kutokana na majeraha yaliyotokana na vishindo vya makombora ya Iran (Concussion). Ikimbukwe kuwa Iran iliijulisha serikali ya Iraq masaa kadhaa kabla ya kutekeleza mashambulizi hatua ambayo ilisaidia sana kupunguza idadi ya majeruhi. Labda walikusudia zaidi kuharibu miundombinu badala ya kupoteza maisha ya watu.
Kinyume na matarajio ya wengi, Marekani haikujibu mashambulizi ya Iran kama ilivyoahidi badala yake Rais Donald Trump aliahidi kuimarisha vikwazo. Uamuzi wa Marekani kutojibu mashambulizi umesaidia sana kuepusha vita. Inawezekana Marekani iliogopa kuingia vitani kwa sasa dhidi ya Iran kwa sababu zifuatazo
• Wananchi wa Iran walishakuwa kitu kimoja, wakiunganishwa na Mauaji ya Kamanda wao mpendwa Qassem Soleiman. Ushahidi ni namna walivyojitokea kwa mamilioni kuomboleza kifo chake huku wakitamka (chanting) maneno yenye kuhamasisha mshikamano na uzalendo kwa Taifa lao. Hivyo basi taifa zima la Iran lilikuwa na ari ya kuingia vitani, walishajipanga na kujengwa kisaikolojia kuikabili Marekani. Hapakuwa na mgawanyiko baina ya Wananchi na serikali yao.
• Marekani yenyewe haikuwa imejipanga kuingia vitani ghafla dhidi ya Iran. Hata washirika wake Uingereza na Ufaransa pia hawakuwa tayari kwa sababu ni suala lilioibuka ghafla kufuatia uamuzi wa Trump kuidhinisha mauaji ya Kamanda Soleiman.
• Marekani isingeweza kuingia vitani (Iliogopa) kwa sababu mazingira ya uwanja wa vita hayakuwa rafiki na mpaka sasa bado hayajawa Rafiki. Kwa sababu turufu ya Ushindi wa Marekani dhidi ya Iran inategemea uthabiti wa amani ya Iraq na Afghanistan nchi ambazo ndio hasa Marekani inazitegemea kama sehemu ya kuweka miguu wakati wa mapigano yake na Iran. Kwa kifupi ni kwamba Marekani haiwezi kuingia vitani hali ya kuwa nchini Iraq inashambuliwa na Wapiganaji wa Kishia na kule Afghanistan inashambuliwa na wapiganaji wa Taleban. Hapo itakuwa sio vita bali ni vurugu zitakazokuwa hazina mwisho.
• Shinikizo kutoka kwa washirika wake wa Mashariki ya kati (Kuwait, Oman, Bahrain, Qatar na Saudi Arabia). Ni wazi kuwa nchi hizo zingekuwa katika wakati mgumu zaidi, kwani mvua za makombora kutoka Iran zisingewaacha salama. Hii ni kwa sababu licha ya mataifa hayo kuitegemea Marekani kiulinzi lakini bado hayana mifumo imara ya kuzuia mvua za makombora ya kibalistic kutoka Iran. Hivyo basi nchi hizo zingepata maafa makubwa ya kupoteza watu na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu.
2. Iran kutangaza kutozingatia makubaliano yaliyopo kwenye mkataba wa nyuklia wa JCPOA.
Ni Uamuzi hatari zaidi uliochukuliwa na Iran baada ya kuchukizwa na mauaji ya Kamanda Soleiman.
Tayari Rais Hassan Rouhan ameshatangaza Kuwa nchi yake itarutubisha Uranium zaidi ya kiwango kilichokubaliwa kwenye mkataba wa JCPOA. Hii inamaanisha kuwa huenda Iran inakusudia kutengeneza mabomu ya nyuklia, hatua ambayo ni kitisho kikubwa kwa maadui zake wakuu katika eneo la Mashariki ya kati ambao ni Israel na Saudi Arabia. Hali hii inaweza kusababisha ushindani wa kumiliki silaha za nyuklia katika eneo la Mashariki ya kati jambo ambalo linaweza kusabisha hatari ya kusambaa hovyo kwa hizo silaha na hatimaye kuingia kwenye mikono isiyo salama.
3. Uwezekano wa kuibuka upya kwa makundi hatari ya kigaidi ya kisalafi na kiwahabi mfano wa Islamic state na vita vya Kiraia nchini Iraq.
Hii ni kutokana na uamuzi wa Iraq kutaka Marekani na mataifa ya kigeni kuondoa askari wake nchini humo baada ya kuchukizwa na uamuzi wa Marekani kuwaua makamada Qassem Suleiman na Abu Mahdi al Muhandis.
Ikumbukwe kuwa kundi la Islamic state liliibuka nchini Iraq mwaka 2014 na kusambaa hadi Syria kutokana na vurugu zilizosababishwa na tofauti za kimadhehenu baina ya Waislamu wa madhehebu ya Suni na shia mara baada ya Marekani kujiondoa Iraq mwaka 2011. Hofu nyingine inayoweza kusababishwa na kuondoka kwa vikosi vya Marekani huko Iraq ni kuibuka kwa vita vya kuwania udhibiti wa madaraka nchini Iraq baina ya Jeshi la Iraq linalopatiwa mafunzo na Marekani na Makundi ya wapiganaji wa Kishia yanayofadhiliwa na Iran.
Hivyo basi kuondoka kwa vikosi vya Marekani nchini Iraq kunaweza kusababisha janga kubwa la kibinadamu linaloweza kuleta athari mbaya hadi kwenye mataifa jirani na Iraq. Iraq inapaswa kutazama kwa makini zaidi uamuzi wa kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini humo.
4. Mauaji ya Qassem Soleiman yanapaswa kuwa funzo kwa Iran.
• Kuuawa kwa Major General Qassem Suleiman na kamanda Abu Mahdi al Muhandis ni ushindi kwa intelijensia ya Marekani na pigo kubwa kwa intelijensia ya Iran. Pengo la Qassem Suleiman ndani ya kikosi cha Quds na Pengo la Abu Mahdi al Muhandis ndani ya PMF sio rahisi kuzibika.
Pamoja na kwamba kundi la PMF lina maofisa wengi wa ngazi za juu waliopata mafunzo ya kijeshi nchini Iran, lakini Abu Mahdi al Muhandis ndiye aliyekuwa kinara na msimamizi mkuu wa maslahi na ushawishi wa Iran ndani ya Iraq, kwa kushirikiana na Qassem Soleiman walifanikisha kupeleka maelfu ya wapiganaji wa kishia nchini Syria hivyo kuchangia kwa asilimia kubwa ushindi wa Rais Bashar al Assad.
Kwa upande wa jeshi la Quds, Ingawa kamanda wake mpya Brigedier General Ismail Qaani amefanya kazi kwa muda mrefu kama msaidizi wa Soleiman lakini itamchukua muda kidogo kuweza kumudu kiukamilifu shughuli za kiutendaji zilizokuwa zikifanywa na mtangulizi wake.
• Iran haikuweka utaratibu mzuri katika tukio la maombolezo ya kifo cha Kamanda Suleiman hali ambayo ilisababisha vifo vya zaidi ya watu 40 kutokana na kukanyagana (Stampede) wakati wa maombolezo na mazishi ya shujaa wao.
• Iran ilipatwa na taharuki kutokana na mauaji ya kamanda wake wa ngazi ya juu, hata shambulizi la kulipiza kisasi dhidi ya Marekani halikupangiliwa vizuri na hivyo kupelekea mfumo wake wa Ulinzi wa anga kuangusha ndege ya abiria mali ya shirika la ndege la Ukraine International Airline na kuua abiria wote 176 wengi wao wakiwa ni raia wa Iran na raia wa Canada wenye asili ya Iran.
Ingawa Iran imeonyesha uwezo kwa kuwa na mfumo wa makombora wenye uwezo mkubwa wa kupiga kwa usahihi kwenye maeneo yaliyokusudiwa, lakini kwenye hali ya hatari inayohusisha uvurumishaji wa makombora dhidi ya taifa jingine tena taifa kubwa kama Marekani, ilipaswa kuchukua hatua za dharura kulinda usalama wa Raia ikiwa ni pamoja na kufunga anga (no-fly zone).
Kwa kifupi uamuzi wa jeshi kuitungua ndege ya Kiraia kwa kudhania kuwa ni ndege ya adui ulikuwa ni uamuzi sahihi kwani ni jukumu la jeshi kuhakikisha nchi inakuwa salama kwa kuzuia au kupambana na kitu chochote linachohisi kuwa kinaweza kuhatarisha usalama wa nchi. Katika medani ya vita madhara yasiyotarajiwa kwa raia wasiokuwa na hatia (collateral damage) huwa hayakosekani. Jambo la kutia moyo ni kwamba jeshi la Iran limeomba radhi na kuahidi kuimarisha mfumo wake wa ulinzi wa anga.
Vita baina ya Marekani na Iran vitasababisha janga kubwa la kibinadamu katika eneo la Mashariki ya kati na Dunia nzima ikiwa ni pamoja na kuzalisha makundi ya kigaidi, wimbi kubwa la wakimbizi na kuongezeka kwa bei za mafuta na gesi na hivyo kupelekea uchumi wa Dunia kutetereka. Juhudi za kidiplomasia zinahitajika ili kumaliza uhasama baina ya mahasimu hawa.
Ukinakili makala zangu kumbuka kufanya acknowledgement.
Napatikana kupitia email address: masudirugombana@gmail.com