Sunday, October 15, 2017

Umoja wa falme za Kiarabu ulitaka kuivamia kijeshi Qatar kwa kutumia mamluki wa Marekani.

Doha.

Imebainika kuwa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulikula njama ya kuishambulia kijeshi Qatar, kwa kutumia maelfu ya mamluki waliopata mafunzo ya kijeshi kutoka kampuni moja ya Marekani.

Abdullah bin Hamad al-Attiyah, Naibu Waziri Mkuu wa zamani wa Qatar ameliambia gazeti la Uhispania la ABC kuwa, Umoja wa falme za Kiarabu (UAE) ilikodisha kampuni binafsi ya usalama ya Marekani iliyojulikana kama "Blackwater-linked" ambayo kwa sasa inafahamika kama Academi, kwa lengo la kuwapa mafunzo mamluki ambao wangetumwa katika operesheni ya kijeshi ya kuivamia Qatar.

Bin Hamad al-Attiyah amesema lengo la Umoja wa falme za Kiarabu kuwapa mamluki hao mafunzo ya kijeshi lilikuwa ni kuivamia kijeshi nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi na kumuondoa mamlakani kwa nguvu Amir wake Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani lakini ilishindwa kupata uungaji mkono wa Marekani.

Duru za habari zimeliambia gazeti la ABC kuwa, mamluki hao wa Umoja wa falme za kiarabu wamekuwa wakipokea mafunzo hayo ya kijeshi katika kambi ya Liwa Oasis mjini Abu Dhabi.

Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu (UAE), Bahrain na Misri tarehe 5 Juni mwaka huu zilitangaza kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar zikiituhumu Doha kuwa inaunga mkono ugaidi na kwamba haiendi sambamba na malengo ya nchi nyingine za Ghuba.

Baada ya kukata uhusiano huo wa kidiplomasia, nchi nne hizo za Kiarabu baadaye ziliiwekea Qatar vikwazo vya kiuchumi na kuipa masharti chungu nzima.

Qatar imekanusha madai ya kuunga mkono ugaidi na inasisitiza kuwa, ni nchi inayojitawala na kamwe haitafuata siasa za kiimla za Ufalme wa Saudia.

Trump ni mfanyabiashara, hajui chochote kuhusu siasa na diplomasia-Iran

Tehran.

Mshauri wa Kiongozi wa kidini wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Masuala ya Kimataifa amesema tabia zisizo na mantiki za Rais Donald Trump wa Marekani zinaashiria kuwa hajui siasa wala hana ufahamu kuhusu mambo ya historia.
Dr. Ali Akbar Velayati amesema matamshi ya kibabe ya Trump yanaonyesha wazi kuwa hana ujuzi wowote katika masuala ya siasa na diplomasia na ni mtu ambaye amekulia katika ulimwengu wa biashara.
Dr. Ali Akbar Velayati
Amesema vikosi vyote vya jeshi la Iran likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC ni milki ya Wairani wote, ambavyo si tu vimeimarisha mshikamano na usalama wa taifa la Iran, bali pia vimesimama kidete dhidi ya maadui wa Iran sambamba na kuyapigisha magoti magenge ya kigaidi na nchi zinazowaunga mkono magaidi hao.

Rais Donald Trump wa Marekani

Dr. Velayati amesisitiza kuwa makubaliano ya JCPOA yalipasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivi sasa yanatambuliwa kuwa ya kimataifa. Ameongeza kuwa, wanachama wengine wa kundi la 5+1 wanapasa kuilazimisha Marekani isikengeuke fremu iliyoainishwa na wakala wa shirika la nguvu za atomic (IAEA)na mazungumzo  ya JCPOA.
Siku ya IjumaaTrump alitoa matamshi yasiyo na msingi na kukariri tuhuma zisizo na maana za huko nyuma dhidi ya taifa la Iran; akidai kuwa Iran haijaonyesha moyo wa dhati katika kufungamana na makubaliano hayo ya nyuklia.
Aidha alikariri madai yake ya huko nyuma yasiyo ya kimantiki kwamba Tehran inaunga mkono ugaidi.

Source: Pars today.