Deng Xiaoping |
Saturday, August 22, 2020
DENG XIAOPING: MBUNIFU WA CHINA YA KISASA ALIYEIFUNGUA CHINA NA CHINA IKAFUNGUKA
TARECK EL AISSAMI: MSHIRIKA WA RAIS MADURO ANAYETAFUTWA SANA NA MAREKANI.
Na Masudi Rugombana.
Venezuela, taifa la Amerika ya kusini lenye hifadhi kubwa ya mafuta ghafi sasa limejikuta likikumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta na gesi. Vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani kwa lengo la kutaka kuiangusha Serikali ya Chama cha kijamaa ya Rais Nwicolas Maduro vimesababisha wawekezaji wa kigeni kuondoka na wananchi takriban milioni tatu wa taifa hilo kuikimbia nchi yao na kwenda kutafuta unafuu wa maisha ughaibuni.
Vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya taifa hilo lenye idadi ya watu milioni 28,644,603 vimeilenga zaidi sekta ya mafuta ambayo ndicho chanzo kikuu cha mapato cha Venezuela. Kwa miaka kadhaa uhaba wa mafuta na gesi umekuwa ukiathiri zaidi maeneo ya vijijini, lakini katika miezi ya hivi karibuni tatizo hilo limehamia mijini hasa kwenye miji yenye msongamano wa watu wengi ukiwemo mji mkuu Caracas. Uhaba wa mafuta unazidi kushika kasi wakati taifa hilo likikabiliana na ugonjwa wa Covid19.
Venezuela inavichukulia vikwazo vya Marekani kama ni vita rasmi ya kiuchumi na mapambano ya kuokoa uhai na ustawi wa Wananchi wake. Vita hii ya kiuchumi ni kongwe na ilianza toka enzi za utawala wa Hugo Chavez, ni vita iliyotangazwa rasmi mwaka 1998, kwa hakika ni muendelezo ule ule wa mpango wa Marekani katika kuhakikisha chembe chembe za kijamaa zinatokomezwa kabisa kwenye eneo lote la Amerika ya kusini.
Kama ilivyo kawaida kwenye uwanja wa vita huwa kuna wapiganaji shupavu, wazalendo wa kweli na watu wenye uchungu na taifa lao. Kamanda mkuu wa mapambano haya ya vita vya kiuchumi ni Raia Nicolas Maduro akisaidiwa na makamanda wengine shupavu wenye uzalendo wa hali juu.
Miongoni wa makamanda wanaofanya kazi kubwa zaidi kwenye vita hii ya kiuchumi na wenye kuaminika na pia wenye ushawishi mkubwa katika Serikali ya Rais Nicolas Maduro ni waziri wa viwanda na uzalishaji ambaye pia ni waziri wa mafuta Bwana Tareck Zaidan El Aissami Maddah.
Tarreck al Aissami |
Tareck El Aissam, gavana wa zamani wa jimbo la Aragua alizaliwa mwaka 1974 kwenye mji wa El Vigia, Merida, magharibi ya nchi ya Venezuela. Mama yake May Maddah ni muhamiaji kutoka Lebanon na Baba yake Zaidan El Aissami ni muhamiaji kutoka Syria. Kama ilivyo kawaida kwa maji kufuata mkondo basi ndivyo ilivyo kwa Tareck El Aissami, huyu anatoka kwenye familia yenye historia ya uongozi kwani baba yake mkubwa Shibli El Aissami alikuwa katibu mkuu msaidizi wa Chama cha Baath (Chama tawala cha Syria) na Makamu wa Rais wa Syria kati ya 28 December 1965 – 23 February 1966 wakati huo Syria ikiongozwa na Rais Amin el Hafez.
Tareck amesomea Sheria na Elimu ya jinai (law and criminology) katika Chuo kikuu cha Andes jijini Merida. Ni katika chuo hicho ndipo alipomezeshwa itikadi za kijamaa na mwalimu wake Adan Chavez ambaye ni kaka yake na Rais wa zamani wa Venezuela Marehemu Hugo Chavez. Baba yake Zaidan El Aisami maarufu kama Carlos Zaidan alikuwa rafiki wa Hugo Chavez na miongoni mwa watu waliokamatwa kwa kuhusika na Jaribio na mapinduzi dhidi ya serikali lilioongozwa na Hugo Chavez mnamo Mwezi February mwaka 1992.
Baada ya kutunukiwa shahada ya sheria, El Aissami aliingia katika utumishi wa umma mwaka 2003 ambapo serikali ya Rais Hugo Chavez ilimteua kuwa mkuu wa kwanza wa Misheni iliyojulikana kwa jina la Identidad (mpango wa kusimamia kadi za utambulisho wa taifa). Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria na Mambo ya ndani. Ni katika wadhifa huo ndipo alipoanza kutazamwa na Marekani kwa jicho la pili, kwani ilimtuhumu kuwapatia vitambulisho vya uraia na hati za kusafiria za Venezuela maelfu ya wanaharakati wa makundi ya Hizbullah na Hamas hivyo kuwawezesha kuingia na kuishi Venezuela wakiendesha harakati zao dhidi ya Marekani na Israel. Ni hapo ndipo Marekani ilipoanza kumuwekea vikwazo.
Akiwa kama kiongozi mwandamizi wa serikali kwa miaka mingi, El-Aissami mwenye umri wa miaka 45, amehudumu kwenye nafasi mbalimbali. Amekuwa Waziri wa mambo ya ndani, Waziri wa viwanda na uzalishaji wa taifa, na Makamu wa Rais wa Venezuela, wadhifa uliompa jukumu la kusimamia idara ya ujasusi ya taifa hilo inayojulikana kama SEBIN. (The Bolivarian National Intelligence Service).
Sambamba na kuongoza wizara ya viwanda, mwezi April 2020 rais Nicolas Maduro alimteua kuwa Waziri wa Mafuta. Uzoefu pekee alionao katika sekta ya mafuta unatokana na nafasi aliyokuwa akiishikilia ya Mkurugenzi wa masuala ya nje wa shirika la taifa la mafuta na gesi asilia la Venezuela (PDVSA). Ni mshirika mkubwa wa Iran na Urusi na ndiye aliyeratibu zoezi zima la kusafirisha mamilioni ya tani za mafuta na gesi kutoka Iran kwenda Venezuela mwezi May 2020 hatua iliyosababisha msuguano na taharuki baina ya Marekani na Iran kutokana na kukiuka vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hizo mbili washirika. Anatajwa kuwa ni miongoni mwa watu wa karibu na Rais Nicolas Maduro wanaopewa nafasi ya kuiongoza Venezuela baada ya rais Nicolas Maduro kumaliza muda wake.
Mwaka 2017, ofisi ya idara ya Hazina ya Marekani yenye kuhusika na udhibiti wa rasilimali za kigeni (OFAC) ilisema kuwa El Aissami aliwezesha kufanikisha operesheni za usafirishaji wa wadawa ya kulevya na kuwapa ulinzi wasafirishaji wengine wa madawa ya kulevya wanaofanya shughuli zao nchini Venezuela. Kwa mujibu wa OFAC, El Aissami alipokea malipo kutoka kwa mfanyabiashara mkubwa wa madawa ya kulevya, raia wa Venezuela mwenye asili ya Syria bwana Walid Makled kwa ajili ya kusaidia kuratibu usafirishaji wa madawa ya kulevya kwenda Marekani.
Ripoti ya Marekani pia ilisema kwamba El Aissami anashirikiana kibiashara na Los Zetas, msambazaji maarufu wa dawa za kulevya (drug cartel) raia wa Mexico na Daniel Barrera Barrera raia wa Colombia anayejulikana kama kiongozi mkuu wa wauza madawa ya kulevya katika eneo la Mashariki ya Colombia. Pia Marekani inamtuhumu kwa kujihusisha na masuala ya kigaidi utakatishaji fedha na biashara ya magendo ya dhahabu.
Gazeti la The times of Israel la January 10, 2017 linamtaja bwana Aissami kama mpatanishi baina ya Iran na Argentina kwenye mpango wa kuwaficha watuhumiwa wa shambulizi la kigaidi dhidi ya kituo cha Wayahudi jijini Buenos Aires. Inaelezwa kuwa shambulizi dhidi ya kituo hicho kinachojulikana kama AIM liliua Wayahudi 85 na kujeruhi wengine mia tatu. Mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyetiwa hatiani kutokana na shambulio hilo.
Kwa tuhuma hizo, Tareck el Aissami anatajwa kwenye orodha ya watu kumi wenye kutafutwa zaidi na Marekani kwa sasa akielezwa kuwa ni mtu hatari kwa usalama wa Marekani. Marekani imemuwekea vikwazo vya kuingia nchi humo na kuzuia mali zake zote zilizopo Marekani, pia imetangaza dau la dola za kimarekani milioni 10 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 23 kama donge nono kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwake. Sambamba na Marekani, nchi za Canada na Jumuiya ya Ulaya pia zimemuwekea vikwazo vya kusafiri ikiwa ni pamoja na kuzuia mali zake.
Hata hivyo bwana Aissami anakanusha kuhusika na tuhuma hizo za Marekani akisema kuwa ni tuhuma zisizokuwa na msingi pia amekanusha kumiliki mali za aina yeyote nchini Marekani au taifa lolote nje ya Venezuela.
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana
Napatikana kupitia๐๐๐
Email: masudirugombana@gmail.com