Saturday, April 6, 2019

UCHAGUZI MKUU NCHINI ISRAEL: NI VITA KATI YA NETANYAHU NA MKUU WA ZAMANI WA JESHI



Na  Masudi Rugombana

Uchaguzi mkuu wa bunge la 21 la Israel unatarajiwa kufanyika tarehe 9 April 2019. Sheria ya bunge la Israel (Knesset) inasema kuwa uchaguzi mkuu wa Israel unatakiwa ufanyike ndani ya mwezi wa Kiyahudi wa Heshvah (mwishoni wa Mwezi Septemba na mwanzoni mwa Mwezi Novemba) miaka minne baada ya kufanyika uchaguzi uliopita.

Hata hivyo, kwa kuwa mfumo wa serikali ya Israel ni wa kibunge (parliamentary system)  uchaguzi nchini humo unaweza kufanyika mapema ikiwa itatokea chama au Muungano wa vyama vinavyotawala kukosa idadi ya kutosha ya viti kuwezesha kuendelea kuongoza serikali. Miongoni mwa mambo yanayoweza kupelekea uchaguzi wa Mapema ni iwapo mojawapo kati ya vyama vinavyounda serikali kitaamua kujitoa hivyo kupelekea idadi ya viti vya chama au muungano wa vyama vinavyounda serikali ndani ya bunge lenye jumla ya viti 120 kushindwa kufikia idadi inayotakiwa ya viti 61 na kuendelea vya kuwawezesha kuunda serikali.

Uchaguzi huu wa mapema unafanyika kufuatia kutokea hali ya kutokuelewana baina ya vyama vinavyounda serikali chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa chama cha mrengo wa kulia cha HaLikud (Uimarishaji). Mtikisiko ndani ya serikali hiyo inayoongozwa na Muungano wa vyama vyenye siasa kali za mrengo wa kulia ulisababishwa na kujiondoa serikalini kwa Waziri wa Ulinzi Avigdor Lieberman na chama chake cha Yisrael Beiteinu (Israel nyumbani kwetu) akipinga makubaliano ya kusimamisha mapigano baina ya Israel na kundi za Wanaharakati wa ukombozi wa Palestina la Hamas pamoja na kupinga muswaada wa sheria itakayowapa ruhusa ya kutojiunga na jeshi la Israel (IDF) wanafunzi wanaotumia muda wao wote katika masomo ya Torati.Muswada huo ulipelekwa bungeni na vyama vyenye kufuata siasa kali za dini ya Kiyahudi(ultra-Orthodox parties) ndani ya serikali ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Kufuatia Lieberman kujitoa serikalini, Waziri wa elimu Naftari Bennet alitishia kujitoa kwenye serikali yeye na chama chake cha HaBayit HaYehudi (Nyumba ya Wayahudi) ikiwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hatamteua kuwa Waziri wa Ulinzi. Hata hivyo kwa shingo upande, Bennet ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kulia mwenye misimamo mikali dhidi ya Maslahi ya Wapalestina alikubali kwa shingo upande kuendelea na wadhifa wake wa waziri wa Elimu baada ya  Netanyahu kukataa shinikizo lake huku akiihamishia Wizara ya Ulinzi chini ya ofisi ya Waziri mkuu. Kutokana na kushindwa kufikia makubaliano katika masuala mbalimbali ndani ya Serikali, ilipelekea bunge kuvunjwa na hivyo nchi kuingia kwenye uchaguzi wa mapema.

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu mwenye umri wa miaka 70 pamoja na chama chake cha Likud anakabiliana na upinzani Mkali kutoka kwa mkuu wa zamani wa Jeshi la Israel (IDF) Jenerali Benjamin (Benny) Gantz mwenye umri wa miaka 59 kutoka Chama cha mrengo wa kati cha Hosen L'Yisrael (Chama cha uvumilivu cha Israel). Chama cha bwana Gantz kinashirikiana na chama cha Yesh Atid ( Kuna mustakabali) kinachoongozwa na mwandishi wa habari wa zamani bwana Yair Lapid na kuunda Muungano unaojulikana kwa jina la kahol lavan (Bluu na Nyeupe). Ni muungano huo wa Mrengo wa kati unaotoa upinzani mkali na kumpeleka puta puta Waziri mkuu Netanyahu hivyo kutishia kuzima ndoto yake ya kutaka kuiongoza Israel kwa muhula wa nne mfululizo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa Waziri mkuu aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi katika katika historia ya taifa hilo pekee la Kiyahudi Duniani.

Benjamin Netanyahu
Jenerali Benjamin Gantz

Kampeni za uchaguzi zimegubikwa kwa kiasi kikubwa na mjadala kuhusu kashfa za rushwa zinazomkabili Waziri Mkuu Netanyahu ambazo zimepelekea hadi mwanasheria mkuu wa nchi hiyo Avichai Mandelblit kutangaza azma ya kumfungulia mashitaka kwa tuhuma kadhaa za rushwa na ufisadi ifikapo mwezi Julai mwaka huu hatua ambayo wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema huenda ikapelekea taifa hilo kuingia tena katika uchaguzi mwingine ikiwa Netanyahu atashinda uchaguzi wa sasa na kisha kutiwa hatiani katika mashtaka yatakayomkabili kwani itakuwa ni vigumu sana kwa chama chake cha Likud kupata washirika wa kuunda nao serikali.

Kwa mujibu wa katiba ya Israel, Waziri mkuu ni lazima ajiuzulu baada ya rufaa zote za kesi kushindwa, ikiwa Netanyahu atashinda kwenye uchaguzi wa April 9, 2019 inamaanisha kuwa atashitakiwa akiwa madarakani, hivyo katika mazingira hayo atakuwa na wakati mgumu kutafuta washirika wa kuungana naye katika kuunda serikali.

Ukiondoa tuhuma za rushwa na ufisadi, Israel chini ya Netanyahu imeweza kuimarika kiuchumi, pia utawala wake umefanikiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa kadhaa ikiwemo China, Urusi na baadhi ya mataifa ya Kiafrika. Kitisho cha Iran pia kimesaidia kuuleta karibu uongozi wa bwana Netanyahu na baadhi ya mataifa ya Kiarabu kama Saudi Arabia, Oman na Umoja wa nchi za falme za Kiarabu ambapo nchi hizo zimekuwa na mawasiliano ya siri ya kidiplomasia. Hii inadhihirika kufuatia ziara iliyofanywa na Waziri mkuu wa Israel huko Oman Oktoba 26, 2018.

Uamuzi wa Marekani kutangaza kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuitambua ardhi ya Syria ya Milima ya Golan iliyotekwa na Israel katika vita ya siku sita mwaka 1967 kama ardhi halali ya Israel ni miongoni mwa mambo yanayaomfanya Netanyahu aendelee kuaminiwa na wapiga kura wengi wenye kupendelea siasa kali za mrengo wa kulia.

Netanyahu na kambi yake ya vyama vya mrengo wa kulia na itikadi kali za kidini wanamlaumu mpinzani wao Benny Gantz kuwa ni mtu anayepwaya katika cheo cha uwaziri mkuu  kutokana na tabia yake ya kutokujiamini linapokuja suala la usalama wa Israel. Wanasema Gantz ni mtu mwenye kusitasita kuchukua maamuzi linapokuja suala la kuyashambulia kijeshi makundi ya Hamas na Hizbullah. Wanapinga sera yake ya kuwatenga Wayahudi na Wapalestina katika eneo la Judea na Samaria ( Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan) wakilaumu kuwa kwa kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha kuundwa kwa taifa la Palestina katika ardhi ya ukingo wa Magharibi. Netanyahu alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa mpinzani wake mkuu Benny Gantz anapendwa na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kura za maoni zilizofanywa jana April 5 zinaonyesha pande mbili bado zinakabana koo, kwenye kura ya maoni iliyofanywa na gazeti la Yedioth Ahronoth  linalosomwa na idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo inaonyesha chama cha bwana Gantz cha kahol lavan  kinaongoza kwa kupata viti 30 dhidi ya 26 vya chama cha Netanyahu cha HaLikud.

Lakini Netanyahu bado anapewa nafasi kubwa ya kusalia Madarakani kwani kura ya maoni ya kituo cha televisheni cha Israel cha Channel 13 zinaonyesha kambi ya Benjamin Netanyahu ya Muungano wa vyama vya mrengo wa kulia na itikadi kali za dini ya Kiyahudi itapata viti 66 kati ya viti 120 huku kambi ya Benjamin Gantz ya vyama vya mrengo wa kati na kushoto ikipata idadi ya viti 54. Matokeo hayo yanaweza kubadilika ndani ya siku chache zilizobaki kutegemea na upepo wa kampeni utakavyokuwa hasa ikizingatiwa kuwa bado kuna kundi la wapiga kura ambao hawajaamua wapigie kura upande  gani.

Changamoto kubwa kwa upande wa vyama vya mrengo wa kushoto kwa sasa ni kampeni  kubwa inayofanywa na makundi ya vijana wa Kiarabu yakihamasisha Waisrael Waarabu kususia uchaguzi huo. Hali hii inatishia vyama vya Waarabu vya Ra'am-Balad na Hadash-Ta'al kufikia kiwango kilichowekwa cha idadi ya kura (threshold) za kuwawezesha kupata Wabunge katika bunge la Israel (Knesset). Ikiwa kampeni hiyo itafanikiwa ni wazi kuwa itampa nafuu kubwa Waziri mkuu Netanyahu katika azma yake ya kuendelea kubaki Madarakani.

Yote kwa yote ni sanduku la kura ndilo litakaloamua muelekeo wa siasa za Israel siku hiyo ya April 9, 2019 inayosubiriwa kwa hamu nchini humo.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

No comments:

Post a Comment