Saturday, April 6, 2019


BRIGEDIA JENERALI HASHIM MBITA NI ALAMA YA MAPAMBANO YA UKOMBOZI BARANI AFRIKA

Na Masudi Rugombana.

Brigedia Jenerali Hashim Mbita bado anaendelea kuheshimika kama shujaa wa harakati za ukombozi barani Afrika, anaheshimika sana Afrika nzima kutokana na uaminifu wake na kujitolea katika kuhakikisha mataifa ya Afrika yaliyokuwa bado chini ya utawala wa Kikoloni yanapata uhuru. Jina la Hashim Mbita ni lenye kuheshimika ndani na nje ya mipaka ya bara la Afrika kuanzia Msumbiji, Sao tome na Principe, Zimbabwe, Angola na Afrika Kusini. Maisha ya Hashim Mbita yanamgusa kila mtu anayeishi katika mataifa hayo ama awe anajua au hajui. Uaminifu na kujituma kwa Mtanzania huyu mzaliwa wa Mkoa wa Tabora katika harakati za ukombozi barani Afrika kuliifanya Tanzania kujivunia na hata kutembea kifua mbele kama moja wapo ya nchi zilizotoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara hili.

Brigedia Jenerali Mstaafu Hashim Mbita alikuwa katibu mtendaji wa kamati ya ukombozi ya Umoja wa nchi za Afrika kwa muda wa miaka ishirini na mbili kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 1994 pale harakati za ukombozi zilipokamilika baada ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, uchaguzi uliopelekea Waafrika weusi wakiongozwa na Nelson Rolihlahla Mandela kushika hatamu ya uongozi.

Brigedia Jenerali Hashim Mbita

Alitunukiwa medali ya Seretse Khama ( Sir Seretse Khama medal )na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), tuzo ya Mtoto wa Africa (Son of Africa award) kutoka Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2014 na tuzo ya Munhumutapa ambayo ni ya heshima ya juu ya Taifa la Zimbabwe anayoweza kupewa raia wa kigeni. Hashim Mbita alipewa tuzo hiyo kwenye mkutano wa SADC uliofanyika kwenye mji wa Victoria falls nchini Zimbabwe mwaka 2014 ikiwa ni kutambua mchango wake katika mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika. Kwa kupewa tuzo hiyo aliingia katika orodha ya watu sita pekee kuwahi kutunukiwa tuzo hiyo ambapo ukimtoa Hashimu Mbita wengine ni marais waasisi Mwalimu Julias Nyerere (Tanzania), Augustino Neto (Angola), Seretse Khama (Botswana), Samora Machel (Mozambique) na Kenneth Kaunda (Zambia). Maandishi katika tuzo ya munhumutapa aliyotunukiwa Hashim Mbita yanasomeka kama ifuatavyo:-

 "Kwa jukumu muhimu alilotekeleza katika ukombozi wa kikanda pamoja na ushirikiano wakati wa uongozi wake wa miaka 20 kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya ukombozi ya Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) - mtangulizi wa Umoja wa Afrika (AU).”

Kamati hiyo ya Ukombozi ya umoja wa Afrika iliendesha shughuli zake ikitokea jijini Dar es salaam kwa mwaliko wa rais wa kwanza na Baba wa Taifa la Tanzania hayati Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mwalimu , mshauri na kamanda wa Hashimu Mbita. Kamati hiyo ya ukombozi ilifanya kazi ya kuratibu misaada ya vifaa kwa ajili ya wanapigania uhuru kwa kipindi cha miaka thelasini kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1994 ambapo inaelezwa kuwa bila hiyo misaada baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika zingeendelea kuwa chini ya utawala wa Kikoloni.

Mara baada ya kuteuliwa kuongoza kamati ya ukombozi, ambayo moja ya kazi zake ilikuwa ni kutafuta vikundi vya ukombozi katika mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakitawaliwa na wakoloni, Brigedia Jenerali Hashim Mbita alishiriki kuvijenga vikosi vya SWAPO(Namibia), MOLINACO (Comoro), PAIGC (Guinea Bissau na Cape Verde), Frelimo (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), ZANU-PF (Zimbabwe) na MPLA (Angola)n.k. Aliviandaa vikosi hivi kupambana na majeshi makubwa yenye silaha nzito za kisasa kwa wakati huo. Alichochea hamasa kubwa katika mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika kwa kutembelea maeneo yaliyokombolewa kaskazini ya Msumbiji yaliyokuwa chini ya chama cha Frelimo (Mozambique Liberation Front au kwa Kireno “Frente de Libertação de Moçambique”) akitaka kushuhudia kwa macho yake hali ilivyokuwa katika uwanja wa mapambano na kuangalia ni aina gani ya mahitaji yaliyokuwa yakihitajika.

Alibaini kuwa kikwazo kikubwa kilichowasumbua  wapiganaji wa Frelimo ni mashambulizi ya anga dhidi yao yaliyokuwa yakifanywa na ndege za kivita za wakoloni wa Kireno. Hivyo alifanya juhudi za kuwapatia wapiganaji silaha zilizowawezesha kukabiliana na mashambulizi hayo, hivyo kuviwezesha vikosi vya Frelimo kusonga mbele zaidi hatua iliyofanya maofisa wa kijeshi wa Ureno kutambua kuwa hali katika medani ya vita imeshabadilika na kwamba wasingeweza tena kushinda vita vya ukoloni barani Afrika.

Hali hii iliwalazimu Wareno kusalimu amri na kuanzisha majadiliano na chama cha Frelimo kwa ajili ya kuunda serikali ya mpito iliyochukua madaraka mwaka 1974 na hatimaye kupelekea uhuru kamili wa Msumbiji mwezi Juni, mwaka 1975. Mipango madhubuti ya Kamati ya ukombozi ya umoja wa nchi za Afrika chini ya Hashimu Mbita ilipelekea kupatikana kwa uhuru wa Sao Tome na Principe mwezi Julai mwaka 1975, Angola mwezi November mwaka 1975, Uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980, uhuru wa Namibia mwaka 1990 na hatimaye uchaguzi wa kidemocrasia huko Afrika ya kusini mnamo mwaka 1994.

Kwenye mkutano uliofanyika Arusha mwezi August mwaka 1994 kwa ajili ya kuhitimisha shughuli za kamati ya ukombozi, Brigedia jenerali Hashim Mbita alisoma hotuba iliyopewa jina “Jukumu limekamilika” kupitia hotuba hiyo Mpambanaji Hashim Mbita hakusita kuwaenzi mashujaa wenzake katika harakati za ukombozi barani Afrika waliopatwa na umauti kabla ya kushuhudia uhuru katika mataifa waliyokuwa wakiyapigania. Mashujaa hao ni Amilcal Cabral (Guinea Bissau), Herbert Chitepo, Jason Ziyaphapha Moyo, Josiah Tongogara (Zimbabwe), Eduardo Mondlane (Msumbiji), Steve Biko, David Sebeko aliyejulikana kama  "Malcolm X wa Afrika Kusini”, Solomon Mahlangu, Christ Hani, Duma Nokwe ambaye alikuwa katibu mkuu wa ANC kati ya mwaka 1958 hadi 1969, Johnny Makatini na Oliver Reginald Kaizana Tambo (Afrika Kusini), mwingine ni Kamanda Peter Nanyemba wa Namibia.

Hashim Mbita, ambaye baba yake alikuwa karani wa shirika la reli la Tanganyika, alizaliwa mwaka 1933 mkoani Tabora na kupata elimu yake kwenye shule ya watoto wenye vipaji ya Tabora boys. Alijiunga na chama cha TANU mwaka 1958 na kuhamia Dar es salaam mwaka mmoja kabla ya uhuru wa Tanganyika wakati huo vijana hasa wanaume wakiajiriwa kwenye mafunzo ya huduma katika utumishi wa kiraia ikiwa ni katika hatua za maandalizi ya uhuru wa Tanganyika mwezi December 1961.

Alipangiwa kazi kwenye kitengo cha habari cha wizara ya habari na muda mfupi baadaye aliteuliwa kuwa mwandishi wa habari wa Rais Julius Kambarage Nyerere akiandaa mikutano na waandishi wa habari hasa nyakati za ziara rasmi za viongozi wa Serikali kutoka nje ya Tanzania. Moja wapo ya mikutano yake na waandishi wa habari yenye kukumbukwa sana ni ule alioandaa wakati wa ziara ya Waziri mkuu wa China Zhou Enlai (tamka Chou En-lai) mwezi June mwaka 1965.

Hashimu Mbita alipanda cheo ndani ya chama na serikali hadi kuwa Katibu mtendaji Mkuu wa TANU kabla Rais Julius Nyerere kumpeleka katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi kuwa mkuu wa kitengo cha siasa (political commissar). Alipata mafunzo ya kijeshi hapa Tanzania na baadaye alipelekwa Uingereza kutoka Ikulu kwa lengo la kusaidia kulijenga Jeshi la Wananchi Tanzania liwe la kizalendo baada ya maasi ya mwaka 1964.

Baadaye rais Julius Kambarage Nyerere alimuandaa kwa jukumu muhimu zaidi kuliko yote, nalo ni kazi ya katibu mtendaji wa kamati ya ukombozi ya umoja wa nchi za Afrika. Kazi ambayo aliifanya kwa moyo na kujituma na hatimaye kumtambulisha kitaifa na kimataifa kama alama ya ukombozi (Liberation icon) ya Tanzania na Afrika.

Mwanadiplomasia Hashim Mbita ambaye aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe alifariki siku ya Jumapili, tarehe 26 April mwaka 2015 akipatiwa matibabu kwenye hospitali kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es salaam akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa kwenye makaburi ya Kisutu, jijini Dar es salaam. Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema roho ya marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita.

Makala hii nimeiandika kwa msaada mkubwa wa taarifa kutoka Southern African Research and Documentation Centre (SARDC). Shukrani za dhati ziende kwa rafiki yangu ndugu Hillary A. Silayo aliyeniomba kuandika makala hii.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com

Uwanja wa Diplomasia tunasema asante kwa makala hii.

UCHAGUZI MKUU NCHINI ISRAEL: NI VITA KATI YA NETANYAHU NA MKUU WA ZAMANI WA JESHI



Na  Masudi Rugombana

Uchaguzi mkuu wa bunge la 21 la Israel unatarajiwa kufanyika tarehe 9 April 2019. Sheria ya bunge la Israel (Knesset) inasema kuwa uchaguzi mkuu wa Israel unatakiwa ufanyike ndani ya mwezi wa Kiyahudi wa Heshvah (mwishoni wa Mwezi Septemba na mwanzoni mwa Mwezi Novemba) miaka minne baada ya kufanyika uchaguzi uliopita.

Hata hivyo, kwa kuwa mfumo wa serikali ya Israel ni wa kibunge (parliamentary system)  uchaguzi nchini humo unaweza kufanyika mapema ikiwa itatokea chama au Muungano wa vyama vinavyotawala kukosa idadi ya kutosha ya viti kuwezesha kuendelea kuongoza serikali. Miongoni mwa mambo yanayoweza kupelekea uchaguzi wa Mapema ni iwapo mojawapo kati ya vyama vinavyounda serikali kitaamua kujitoa hivyo kupelekea idadi ya viti vya chama au muungano wa vyama vinavyounda serikali ndani ya bunge lenye jumla ya viti 120 kushindwa kufikia idadi inayotakiwa ya viti 61 na kuendelea vya kuwawezesha kuunda serikali.

Uchaguzi huu wa mapema unafanyika kufuatia kutokea hali ya kutokuelewana baina ya vyama vinavyounda serikali chini ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa chama cha mrengo wa kulia cha HaLikud (Uimarishaji). Mtikisiko ndani ya serikali hiyo inayoongozwa na Muungano wa vyama vyenye siasa kali za mrengo wa kulia ulisababishwa na kujiondoa serikalini kwa Waziri wa Ulinzi Avigdor Lieberman na chama chake cha Yisrael Beiteinu (Israel nyumbani kwetu) akipinga makubaliano ya kusimamisha mapigano baina ya Israel na kundi za Wanaharakati wa ukombozi wa Palestina la Hamas pamoja na kupinga muswaada wa sheria itakayowapa ruhusa ya kutojiunga na jeshi la Israel (IDF) wanafunzi wanaotumia muda wao wote katika masomo ya Torati.Muswada huo ulipelekwa bungeni na vyama vyenye kufuata siasa kali za dini ya Kiyahudi(ultra-Orthodox parties) ndani ya serikali ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Kufuatia Lieberman kujitoa serikalini, Waziri wa elimu Naftari Bennet alitishia kujitoa kwenye serikali yeye na chama chake cha HaBayit HaYehudi (Nyumba ya Wayahudi) ikiwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu hatamteua kuwa Waziri wa Ulinzi. Hata hivyo kwa shingo upande, Bennet ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kulia mwenye misimamo mikali dhidi ya Maslahi ya Wapalestina alikubali kwa shingo upande kuendelea na wadhifa wake wa waziri wa Elimu baada ya  Netanyahu kukataa shinikizo lake huku akiihamishia Wizara ya Ulinzi chini ya ofisi ya Waziri mkuu. Kutokana na kushindwa kufikia makubaliano katika masuala mbalimbali ndani ya Serikali, ilipelekea bunge kuvunjwa na hivyo nchi kuingia kwenye uchaguzi wa mapema.

Waziri mkuu Benjamin Netanyahu mwenye umri wa miaka 70 pamoja na chama chake cha Likud anakabiliana na upinzani Mkali kutoka kwa mkuu wa zamani wa Jeshi la Israel (IDF) Jenerali Benjamin (Benny) Gantz mwenye umri wa miaka 59 kutoka Chama cha mrengo wa kati cha Hosen L'Yisrael (Chama cha uvumilivu cha Israel). Chama cha bwana Gantz kinashirikiana na chama cha Yesh Atid ( Kuna mustakabali) kinachoongozwa na mwandishi wa habari wa zamani bwana Yair Lapid na kuunda Muungano unaojulikana kwa jina la kahol lavan (Bluu na Nyeupe). Ni muungano huo wa Mrengo wa kati unaotoa upinzani mkali na kumpeleka puta puta Waziri mkuu Netanyahu hivyo kutishia kuzima ndoto yake ya kutaka kuiongoza Israel kwa muhula wa nne mfululizo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa Waziri mkuu aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi katika katika historia ya taifa hilo pekee la Kiyahudi Duniani.

Benjamin Netanyahu
Jenerali Benjamin Gantz

Kampeni za uchaguzi zimegubikwa kwa kiasi kikubwa na mjadala kuhusu kashfa za rushwa zinazomkabili Waziri Mkuu Netanyahu ambazo zimepelekea hadi mwanasheria mkuu wa nchi hiyo Avichai Mandelblit kutangaza azma ya kumfungulia mashitaka kwa tuhuma kadhaa za rushwa na ufisadi ifikapo mwezi Julai mwaka huu hatua ambayo wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema huenda ikapelekea taifa hilo kuingia tena katika uchaguzi mwingine ikiwa Netanyahu atashinda uchaguzi wa sasa na kisha kutiwa hatiani katika mashtaka yatakayomkabili kwani itakuwa ni vigumu sana kwa chama chake cha Likud kupata washirika wa kuunda nao serikali.

Kwa mujibu wa katiba ya Israel, Waziri mkuu ni lazima ajiuzulu baada ya rufaa zote za kesi kushindwa, ikiwa Netanyahu atashinda kwenye uchaguzi wa April 9, 2019 inamaanisha kuwa atashitakiwa akiwa madarakani, hivyo katika mazingira hayo atakuwa na wakati mgumu kutafuta washirika wa kuungana naye katika kuunda serikali.

Ukiondoa tuhuma za rushwa na ufisadi, Israel chini ya Netanyahu imeweza kuimarika kiuchumi, pia utawala wake umefanikiwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na mataifa kadhaa ikiwemo China, Urusi na baadhi ya mataifa ya Kiafrika. Kitisho cha Iran pia kimesaidia kuuleta karibu uongozi wa bwana Netanyahu na baadhi ya mataifa ya Kiarabu kama Saudi Arabia, Oman na Umoja wa nchi za falme za Kiarabu ambapo nchi hizo zimekuwa na mawasiliano ya siri ya kidiplomasia. Hii inadhihirika kufuatia ziara iliyofanywa na Waziri mkuu wa Israel huko Oman Oktoba 26, 2018.

Uamuzi wa Marekani kutangaza kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kuitambua ardhi ya Syria ya Milima ya Golan iliyotekwa na Israel katika vita ya siku sita mwaka 1967 kama ardhi halali ya Israel ni miongoni mwa mambo yanayaomfanya Netanyahu aendelee kuaminiwa na wapiga kura wengi wenye kupendelea siasa kali za mrengo wa kulia.

Netanyahu na kambi yake ya vyama vya mrengo wa kulia na itikadi kali za kidini wanamlaumu mpinzani wao Benny Gantz kuwa ni mtu anayepwaya katika cheo cha uwaziri mkuu  kutokana na tabia yake ya kutokujiamini linapokuja suala la usalama wa Israel. Wanasema Gantz ni mtu mwenye kusitasita kuchukua maamuzi linapokuja suala la kuyashambulia kijeshi makundi ya Hamas na Hizbullah. Wanapinga sera yake ya kuwatenga Wayahudi na Wapalestina katika eneo la Judea na Samaria ( Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan) wakilaumu kuwa kwa kufanya hivyo ni sawa na kuhalalisha kuundwa kwa taifa la Palestina katika ardhi ya ukingo wa Magharibi. Netanyahu alikwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa mpinzani wake mkuu Benny Gantz anapendwa na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kura za maoni zilizofanywa jana April 5 zinaonyesha pande mbili bado zinakabana koo, kwenye kura ya maoni iliyofanywa na gazeti la Yedioth Ahronoth  linalosomwa na idadi kubwa zaidi ya watu nchini humo inaonyesha chama cha bwana Gantz cha kahol lavan  kinaongoza kwa kupata viti 30 dhidi ya 26 vya chama cha Netanyahu cha HaLikud.

Lakini Netanyahu bado anapewa nafasi kubwa ya kusalia Madarakani kwani kura ya maoni ya kituo cha televisheni cha Israel cha Channel 13 zinaonyesha kambi ya Benjamin Netanyahu ya Muungano wa vyama vya mrengo wa kulia na itikadi kali za dini ya Kiyahudi itapata viti 66 kati ya viti 120 huku kambi ya Benjamin Gantz ya vyama vya mrengo wa kati na kushoto ikipata idadi ya viti 54. Matokeo hayo yanaweza kubadilika ndani ya siku chache zilizobaki kutegemea na upepo wa kampeni utakavyokuwa hasa ikizingatiwa kuwa bado kuna kundi la wapiga kura ambao hawajaamua wapigie kura upande  gani.

Changamoto kubwa kwa upande wa vyama vya mrengo wa kushoto kwa sasa ni kampeni  kubwa inayofanywa na makundi ya vijana wa Kiarabu yakihamasisha Waisrael Waarabu kususia uchaguzi huo. Hali hii inatishia vyama vya Waarabu vya Ra'am-Balad na Hadash-Ta'al kufikia kiwango kilichowekwa cha idadi ya kura (threshold) za kuwawezesha kupata Wabunge katika bunge la Israel (Knesset). Ikiwa kampeni hiyo itafanikiwa ni wazi kuwa itampa nafuu kubwa Waziri mkuu Netanyahu katika azma yake ya kuendelea kubaki Madarakani.

Yote kwa yote ni sanduku la kura ndilo litakaloamua muelekeo wa siasa za Israel siku hiyo ya April 9, 2019 inayosubiriwa kwa hamu nchini humo.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com