Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Desemba 2016, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote.
Rais John Magufuli na Mmiliki wa kiwanda cha
Dangote Cement, Alhaji Aliko Dangote wakifanya mazungumzo
Ikulu Jijini Dar es salaam leo December 10, 2016.
|
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.
Rais Magufuli amesema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho serikali yake haikiruhusu.
Amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.
''Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili '' amesema Rais Magufuli.
Dokta Magufuli amesema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.
Kwa upande wake mmiliki wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.
Katika kuthibitisha hilo, tayari Mfanyabiashara huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake. Ameongeza kuwa lengo la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.
Rais Magufuli na Alhaji Dangote wakiongea na
waandishi wa habari mara baada ya kufanya mazungumzo
Ikulu jijini Dar es salaam.
|
No comments:
Post a Comment