Saturday, December 10, 2016

MELI YENYE MAROLI 600 MALI YA DANGOTE CEMENT YATIA NANGA BANDARI YA MTWARA.

Mfanyabiashara tajiri zaidi barani Afrika, Alhaji Aliko Dangote leo December 10, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam. Dangote alimthibitishia rais Magufuli kuwa hana lengo la kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa badala yake anatafuta fursa nyingine za kuwekeza hapa nchini.


Katika kuthibitisha hilo, Mfanyabiashara huyo alisema leo meli yenye malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake itawasili nchini. Ameongeza kuwa lengo la kufanyabiashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi ambazo zinapatikana hapa nchini.

Mara tu baada ya kumaliza mazungumzo na Rais, Meli kubwa yenye baadhi ya magari hayo imetia nanga katika bandari ya Mtwara ambapo ndipo kiwanda cha Saruji cha Dangote kilipo. Pia imeelezwa kuwa wiki ijayo meli nyingine kutoka Korea Kusini yenye malori 451 inatarajiwa kuwasili katika bandari ya Mtwara.

Pichani ni  meli hiyo ikiwa bandarini Mtwara




DR. MAGUFULI NA ALHAJI DANGOTE WAFANYA MAZUNGUMZO IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Dar es salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Desemba 2016, amekutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Alhaji Aliko Dangote.

Rais John Magufuli na Mmiliki wa kiwanda cha
Dangote Cement, Alhaji Aliko Dangote wakifanya mazungumzo
Ikulu Jijini Dar es salaam leo December 10, 2016.


Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.

Rais Magufuli amesema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho serikali yake haikiruhusu.
Amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.


''Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili '' amesema Rais Magufuli.
Dokta Magufuli amesema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.

Kwa upande wake mmiliki wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote, Alhaji Aliko Dangote ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.


Katika kuthibitisha hilo, tayari Mfanyabiashara huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake. Ameongeza kuwa lengo la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.

Rais Magufuli na Alhaji Dangote wakiongea na
waandishi wa habari mara baada ya kufanya mazungumzo
Ikulu jijini Dar es salaam.
Alhaji Dangote amemuhakikishia Rais magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari bali ana mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.