Saturday, December 22, 2018

MISRI ILISHINDA VITA YA YOM KIPPUR DHIDI YA ISRAEL NAYO ISRAEL ILISHINDA DHIDI YA SYRIA.

Na Masudi Rugombana.

Vita ya Yom Kippur (Yom Kippur war) kama inavyojulikana huko Israel au Operation Badri kama inavyojulikana huko nchini Misri au Ramadan War kama inavyojulikana katika Ulimwengu wa Kiarabu na ukipenda unaweza kuiita Vita baina ya Waarab na Waisrael ya mwaka 1973 (Arab-Israel war of 1973) ilipiganwa baina ya Misri na Syria kwa upande mmoja dhidi ya Israel.

Kulikuwa na mambo makuu mawili yaliyopelekea kuzuka kwa vita hii. Jambo la kwanza ni kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro uliotokana na matokeo ya vita ya siku sita. Mgogoro huo si mwingine bali ni kurejeshwa kwa ardhi iliyotekwa na Israel ambayo ni eneo la Sinai kwa upande wa Misri na Milima ya Golan kwa upande wa Syria. Juhudi za kuleta amani zilizofanywa na umoja wa mataifa kupitia azimio namba 242 na zile za Rais Anwar Sadat wa Misri hazikuzaa matunda.

Anwar Sadat

Mara baada ya kuingia Madarakani tarehe 15 October 1970, Rais Mohamed Anwar el-Sadat alikusudia kufikia makubaliano ya kudumu ya amani na Israel ambapo Misri ingeitambua rasmi Israel kama taifa huru iwapo Israel ingejiondoa katika eneo la Sinai. Hata hivyo Israel chini ya Waziri mkuu Bi Golda Meir ilikataa mazungumzo na Misri na pia ilikataa kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Sinai.

Sababu ya pili iliyopelekea kuzuka kwa vita ya Yom Kippur inafanana na ile ya kwanza, nayo ni kwamba Israel haikuwa na nia ya kufikia makubaliano ya amani na Waarab kwa kujiondoa kwenye ardhi ya Waarab iliyoiteka katika vita ya siku sita badala yake Israel iligeuza maeneo ya Waarabu iliyoyateka kuwa kama ukanda mkubwa uliokatazwa kufanyika harakati za kijeshi  (Huge buffer zone) kwa ajili ya kujihakikishia usalama wake. Jeuri hii ya Israel ilitokana na kuamini kuwa Jeshi lake (IDF) lilikuwa na nguvu kubwa ya kutoweza kushindwa na majeshi ya nchi za kiarabu.

Kwa kuzingatia kwamba hapakuwa na maendeleo yeyote kuelekea kupatikana kwa amani itakayorejesha eneo la Sinai kwa Misri, Rais Anwar Sadat aliamua kuingia vitani kwa malengo yenye mipaka maalum.
Anwar el-Sadat, mwanasiasa mwenye kipaji na mwanajeshi aliyerithi madaraka kutoka kwa rais wa muda mrefu Gamal Abdel Nasser aliamini kuwa hakuwa na chaguo lingine isipokuwa kuingia vitani dhidi ya Israel. Aliamini kuwa Israel chini ya Waziri mkuu shupavu Mwanamama Goda Meir kamwe isingeweza kuingia kwenye mazungumzo ya kutafuta suluhu bila kutishiwa kijeshi.

Sadat hakuwa amepanga kuiangamiza Israel kwa sababu aliamini kuwa hilo lisingewezekana kutokana na Uimara wa Jeshi la Israel, pia alitambua kuwa Marekani kamwe isingekubali kumuona Mshirika wake Israel akiangamia.

Hivyo kusudio lake ilikuwa ni kushusha kipigo cha kushtukiza ili kulitikisa jeshi la Israel ambalo lilikuwa limejengwa kisaikolojia kama jeshi lisiloshindwa kirahisi kufuatia ushindi mkubwa wa kihistoria lililopata katika vita ya siku sita dhidi ya Mataifa Manne ya kiarabu (The Six day war or 1967 Israel-Arab war).
Sadat aliwahi kunukuliwa akisema "Kama tukifanikiwa kuteka angalau hata inchi nne za ardhi ya Sinai basi hali itabadilika kuanzia Mashariki, Magharabi na Sehemu zote"

Sadat aliamini kuwa alipaswa kushambulia kwa nguvu na kwa haraka na kwamba kitisho cha mashambulizi kingelazimisha Marekani na Soviet Union kujiingiza katika vita kwa Marekani kuilinda Israel na Soviet  kuisaidia Syria ili kuimarisha ushawishi wao katika eneo la Mashariki ya kati.

Hali hii ingeulazimu umoja wa Mataifa kuingilia kati ili kusimamisha mapigano katika wakati ambao Misri ingekuwa tayari imesharudisha baadhi ya sehemu yake ya  ardhi iliyotekwa na Israel katika vita ya siku sita  hivyo kurahisisha uwezekano wa kufikia Makubaliano ya kudumu ya amani na Israel.

Misri ilianza kuimarisha majeshi yake mwishoni mwa mwaka 1972 kwa kununua zana za kisasa za kijeshi kutoka
Soviet Union kama vifaru aina ya  T-62 ndege za kivita (Jet fighters) aina ya Mig 23, Mig 21, Mig 17, Su 7 nk. Pia makombora ya kutungua ndege (Ant-Aircraft missiles), makombora ya kulipua vifaru (ant-tank missiles) na Makombora yenye kuongozwa na mitambo maalum (Guided Missiles)

Hata hivyo maandalizi yote ya Misri kuhusiana na kuvuka mfereji wa Suez yalivuja hivyo kumpa Rais Anwar Sadat sababu ya kuwafukuza wakufunzi wa kijeshi elfu ishirini kutoka Urusi (Soviet Union) mnamo tarehe 01 Julai mwaka 1972 ikiwa ni mojawapo katika mkakati wa kujenga taswira ya kuaminika na Marekani na hivyo kuitumia Marekani
kuishawishi Israel ikubali pendekezo la Misri la kufanya mazungumzo ili kufikia amani ya kudumu.

Katika jitihada za kufanikisha mpango huo,  Rais Anwar Sadat alianzisha Cheo kipya cha Mshauri wa Masuala ya Usalama na kumteua Mwanadiplomasia Mohammed Hafez Ismail ambaye alikuwa balozi wa Misri kwa nyakati tofauti katika nchi za Uingereza, Ufaransa na Italia kuwa mshauri wake wa Masuala ya Usalama. Lengo la uteuzi huo lilikuwa ni kufungua mlango wa majadiliano na Israel kwa lengo la kufikia makubaliano ya kudumu ya amani.

Mei 20 Mwaka 1973 Rais Sadat alimtuma mshauri wake wa masuala ya Usalama Mwanadiplomasia  Mohammed Hafez Ismail kwenda Marekani kufanya Mazungumzo na Mshauri wa Masuala ya usalama wa Marekani Dr. Henry Kissinger kwa lengo la kuishawishi Marekani ikubaliane na mpango wa amani wa Misri ambapo Misri ingeitambua haki ya Israel kama taifa huru kwa makubaliano kuwa Israel irejeshe ardhi ya Sinai kwa Misri.

Marekani ilikubaliana na pendekezo hilo na kuliwasilisha rasmi kwa Waziri mkuu wa Israel Golda Meir na Waziri wake wa Ulinzi Moshe Dayan. Israel ilikataa pendekezo la Misri na hivyo kuendelea kukalia eneo la Sinai.

Hatua ya Israel kukataa kufanya mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu ndiyo iliyopelekea Rais Anwar Sadat kuingia rasmi vitani.

Syria nayo ilikuwa katika maandalizi mazito ya vita kama ilivyokuwa kwa upande wa Israel kwa lengo la kukomboa ardhi yake ya Milima  ya Golan. Rais Hafez al Assad aliamini kuwa njia pekee ya kuweza kurudisha ardhi ya Milima ya Golan sio nyingine zaidi ya ushindi kwenye medani ya vita. Chini ya Marais Anwar Sadat na Hafez al Assad, Misri na Syria zilikubaliana kuunganisha majeshi yao chini ya kamandi moja.

Ilipofika Octoba 03 mwaka 1973 maandalizi yote ya vita yalikuwa yamekamilika  na vita ilipangwa kuanza tarehe 6 October 1973 Mwezi wa Ramadhan ambapo tarehe kama hiyo nchini Israel ilikuwa ni sikukuu ya kidini kubwa kuliko zote ijulikanyo kama Yom Kippur. Siku ambayo shughuli zote za kiserikali husimama ikiwa ni pamoja na matangazo katika vituo vya radio na runinga. Pia wanajeshi wengi nchini Israel huwa wanakuwa mapumziko wakisherehekea sikukuu hii tukufu kwa imani ya Kiyahudi.

Misri ilipeleka wanajeshi laki moja iliyowagawa katika Makundi (divisions) tano sambamba na vifaru 1350 na mizinga 2000 ikiwa ni maandalizi ya shambulio la kuvuka mfereji wa Suez (Suez Canal).

Ilipofika October 6 majira ya saa nane kamili mchana Misri ilifanya shambulizi zito la kustukiza la anga likihusisha ndege za kivita 200 dhidi ya Vikosi vya Israel vilivyokuwa vimejiimarisha kwenye mstari wa kujihami wa Bar lev (Bar-Lev Defensive line). Mstari huu wa kujihami wa Bar-lev ni tuta kubwa la udongo lililokuwa na kimo cha futi 66 na umbali wa kilomita 150 (Maili 93) kutoka Kaskazini hadi kusini ya mfereji wa Suez.

Tuta hilo ilitengenezwa na Israel upande wa Mashariki wa Mfereji wa Suez wakati wa vita iliyojulikana kama Vita ya Msuguano ( The War of attrition) iliyopiganwa kati ya July 1, 1967 hadi August 7, 1970 baina ya Israel dhidi ya Syria, Jordan, Chama cha ukombozi wa Palestina (P.L.O) na Misri ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyotokana na ushindi mnono wa Israel katika vita ya siku sita. Israel ilitengeneza tuta hili kama ngao kwa ajili ya kujihami na mashambulizi kutoka majeshi ya Misri yaliyokuwa upande wa Magharibi ya mfereji wa Suez.

Askari 32,000 wa Misri walifanikiwa kuvuka mfereji wa Suez na kuwatimua askari wa Israel waliokuwa wakiimarisha ulinzi kwenye mstari wa kujihami wa Bar lev na hivyo kufanikiwa kuzishambulia ngome za majeshi ya Israel. Kwa mujibu wa Kamanda Saad Mohamed el-Shazly ambae alikuwa mnadhimu mkuu wa jeshi la Misri wakati wa vita ya Yom Kippur ni kwamba ndani ya masaa sita tokea kuanza kwa vita majeshi ya Misri yalikuwa tayari yameshasambaratisha ngome kumi na tano za kijeshi za Israel na hivyo kusonga mbele kilomita kadhaa ndani ya ardhi ya Sinai.

Wanajeshi wa Misri
Wakisimika bendera ya Taifa
lao Mara baada ya kuingia
Katika ardhi ya Sinai 
Baada ya siku tatu tokea kuanza kwa Mashambulizi ya Misri, Israel ilikuwa tayari imeshahamasisha askari wake tayari kwa vita ambapo ilipeleka vikosi zaidi kwa ajili ya kuongeza nguvu huko Sinai na hatimaye kufanikiwa kuyazuia majeshi ya Misri kusonga mbele zaidi.

Kwa upande wa milima ya Golan askari elfu arobaoni wa Syria wakiongozwa na Luteni Jenerali Ali Aslan wakiwa na Vifaru 1300 vingi kati ya hivyo ni aina ya T-55s vya Kisoviet, mizinga 600, ndege za kivita 100 na Makombora 400 ya kutungulia ndege walivuka mstari wa kusitisha vita wa mwaka 1967 unaojulikana kama Purple ( Purple Cease fire line ) na kuyashambulia majeshi ya Israel yaliyokuwa na vifaru 170 tu na mizinga 60 hivyo  kuyarudisha nyuma hadi kwenye mpaka wa nchi hiyo na Israel wa kabla ya mwaka 1967.
Majeshi ya Syria hayakuishia hapo bali yaliendelea kufanya mashambulizi mazito ndani ya ardhi ya Israel.

Hali ilikuwa mbaya kwa upande wa Israel kwa sababu ndani ya siku nne tu ndege zake 49 za kivita ziliangushwa pamoja na vifaru 500 vilikuwa tayari vimeshaharibiwa. Hali ya hofu ilitawala ndani ya Serikali. Kwenye kikao chake na Waziri mkuu Golda Meir, waziri wa Ulinzi Moshe Dayan alijadili kuhusu uwezekano wa kutumia silaha za Nyuklia, kwani kwa wakati huo Israel ilikuwa na Mabomu 13 ya Nyuklia kwenye ghala lake la makombora mjini Jericho.
Waziri Mkuu Golda Meir hakukubaliana na pendekezo la kutumia silaha za nyuklia, badala yake aliomba msaada wa silaha kutoka Marekani.

Golda Meir
Rais Richard Nixon na Mshauri wake wa Masuala ya Usalama Dr. Henry Kissinger waliamini kuwa Israel kushindwa vita na nchi zinazotumia silaha za Kisoviet ungekuwa ni mkasa wenye athari mbaya sana kwa maslahi ya Marekani. Hivyo basi rais Richard Nixon aliidhinisha msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 2.2 kwenda Israel.

Jeshi la anga la Marekani lilizindua operation iliyopewa jina la Nickel Grass (Operation Nickel Grass) kati ya October 14  na November 14, 1973 kwa kusafirisha tani elfu 22 za silaha kuelekea Israel. Miongoni mwa silaha zilizosafirishwa ni  Vifaru aina ya M60,  Mizinga na Mabomu. Tani nyingine elfu 33 za silaha zilisafirishwa kwa njia ya bahari. Inaelezwa kuwa huo ilikuwa ni zaidi ya  msaada wa kijeshi, ulikuwa ni msaada wa kuokoa maisha.

Baada ya kuongezewa nguvu na Marekani, Majeshi ya Israel yakiongozwa na Makanda Rafael Eitan, Dan Laner, na  Moshe Peled yalijibu mashambulizi kwa ustadi wa hali ya juu na hivyo kufanikiwa kuyaondoa majeshi ya Syria kutoka milima ya Golan ndani ya siku tatu. Baada ya kuikamata  milima ya Golan, Israel ilifanya mashambulizi makali ndani ya Syria kwa muda wa siku nne mfululizo na ndani ya wiki moja vifaru vya Israel vilikuwa vikishambulia viunga vya mji mkuu wa Syria Damascus kutoka umbali wa takriban kilometa 30 tu. Ikumbukwe kuwa Mji mkuu wa Syria Damascus unapatikana Kilomita 71.93 sawa na Maili 44.70 tu kutoka eneo la Milima ya Golan.

Kwa upande wa Sinai Vikosi vya Israel ambayo vilipangwa katika divisions tatu vikisaidiwa na ndege za kivita aina ya A-4E Skyhawk na  F-4E Phantoms havikufanikiwa kuyarudisha majeshi ya Misri nyuma ila viliweza kuyazuia kusonga mbele kwa upande wa Kaskazini mashariki na katikati ya mfereji wa Suez.

Kwa upande wa kusini ya mfereji wa Suez, kati ya October 16 hadi October 27 vikosi vya Israel vikiongozwa na makamanda Ariel Sharon, Danny Matt, Amnon Reshef, Haim Erez na Avraham Adon vilifanikiwa kuwazingira kila upande wanajeshi 35,000 wa Misri kutoka kikosi cha tatu chini ya Makamanda Abd Rab el-Nabi Hafez Na Ibrahim El-Orabi hivyo kuzuia shehena ya silaha na chakula iliyotakiwa kwenda kwa vikosi hivyo, lengo likiwa ni kuvilazimisha vikosi hivyo kusalimu amri jambo ambalo halikufanikiwa

Baada ya kufanikiwa kuwazingira askari hao wa Misri vikosi vya Israel vilifanikiwa kuvuka mfereji wa Suez kwa upande wa kusini bila upinzani mkubwa na kufanikiwa kuteka eneo la ardhi lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 1600 (1600 square Km) karibu na Miji ya Suez na Ismailia hivyo kuviwezesha kuwa umbali wa Kilomita 100 kuelekea mji mkuu Cairo katika operation iliyopewa jina la Abirey-Halev. Operation iliyosababisha vifo vya askari wengi na uhalibifu mkubwa wa dhana za kivita kwa pande zote mbili.

Hata hivyo vikosi vya Israel havikuweza kusonga mbele zaidi kuelekea Cairo kutokana na uhaba wa Silaha na uchache wa askari kuweza kukabiliana na mashambulizi   ya anga yaliyokuwa yakifanywa na Misri katika eneo hilo lililotekwa na Israel ikiwa ni pamoja na kuvunja daraja ili kuzuia vikosi vya Israel kuingia au kutoka kwa sababu askari wa Israel walikuwa wanategemea njia moja tu ya kuwawezesha kuingia na kutoka katika eneo hilo la mashariki ya Suez. Hali hii ilipelekea mkwamo wa kijeshi (Militarily stalemate) kwa kila upande kushindwa kusonga mbele.

Mkwamo huo ulisababisha hali ya Wasiwasi wa kushambuliana kijeshi  baina ya Marekani na Soviet baada ya kiongozi wa Soviet Leonid Brezhenev kutishia kuchukua hatua za kijeshi iwapo Israel ingeendelea na msimamo wake wa kuzuia mahitaji ya kibinadamu kuwafikia askari wa Misri iliyokuwa imewazingira katika eneo la kusini Mashariki ya mfereji wa Suez. Kitisho hiki kutoka Soviet kiliifanya Marekani nayo kuviweka vikosi vyake katika hali ya tahadhari.

Ni wakati huo ndipo rais Anwar Sadat alipotoa mwito wa kusitishwa kwa vita akisema kwamba aliingia vitani huku akijua uwezo halisi wa nchi yake na kwamba halikuwa kusudio lake kupigana vita na Marekani akilaumu msaada mkubwa wa kijeshi kutoka Marekani kwenda Israel.

Bahati nzuri wasiwasi ulitanzuliwa baada ya Israel kwa kushinikizwa na Marekani kukubali kuruhusu mahitaji ya kibinadamu kuwafikia askari hao.

Katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo, kati ya tarehe 21 October 1973 hadi tarehe 7 November 1973 rais Richard Nixon alimtuma Mshauri wake wa Masuala ya Usalama Dr. Henry Kissinger kwenda Moscow, Tel Aviv  na Cairo kujadiliana na kiongozi wa Soviet  Leonid Brezhenev, Waziri Mkuu Golda Meir na rais Anwar Sadat  namna ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita.

Hatimaye tarehe 11 November 1973 Israel na Misri zilisaini makubaliano ya kusitisha vita yaliyoandaliwa na Dr. Henry Kissinger na Rais Anwar Sadat yaliyopelekea vikosi vya Israel kuondoa mzingiro dhidi ya kikosi cha tatu cha jeshi la Misri na wakati huo huo Misri ilisitisha mashambulizi ya anga dhidi ya wanajeshi wa Israel waliokwama umbali wa km 100 kutoka Cairo hivyo kuwapa nafasi ya kuvuka mfereji wa Suez na kurejea Sinai.

Syria ilikataa kusaini makubaliano hayo ingawa pande hasimu yaani Israel na Syria zilikubali kusitisha mapigano. Mnamo tarehe 31 May 1974 nchi hizo zilifikia makubaliano ambapo Israel ilirudisha majeshi yake nyuma hadi kwenye mstari wa kusitisha vita wa mwaka 1967 (Purple cease fire line) huko kwenye milima ya Golan.

MATOKEO YA VITA KWA UPANDE WA SYRIA:
Malengo ya Syria kuikomboa Milima ya Golan yalishindwa na badala yake Israel ilifanikiwa kuendelea kuikalia milima hiyo huku ikihamishia uwanja wa vita ndani ya ardhi ya Syria hadi kufikia hatua ya kutishia kuuteka mji mkuu wa Syria Damascus.

MATOKEO YA VITA KWA UPANDE WA MISRI:
 1. Misri ilirejesha kipande kidogo cha sehemu ya ardhi iliyotekwa na Israel kwenye eneo la Sinai. Kipande hicho ni pwani ya Mashariki ya Mfereji wa Suez.

 2. Misri alifanikiwa katika mkakati wake wa kuileta Israel katika meza ya Mazungumzo ya amani ili kufikia makubaliano ya kudumu

 3. Mazungumzo ya amani ya Camp David (1978 Camp David Accords)
yaliyotokana na matokeo ya vita ya Yom Kippur yalipelekea kusainiwa kwa mkataba wa kudumu wa Amani baina ya Misri na Israel hivyo Israel kujiondoa moja kwa moja kwenye ardhi ya Sinai.

Mkataba wa amani wa Camp David  ulipelekea Israel na Misri kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Hivyo kuifanya Misri kuwa taifa la kwanza la Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Hatua iliyosababisha Rais Anwar Sadat kuchukiwa na Ulimwengu wa Kiarabu.

Rais Anwar Sadat, (Kushoto) na
   Waziri mkuu wa Israeli Menahem
Begin wakishikana mkono baada
ya  kusaini mkataba wa amani
mbele ya Rais Jimmy Carter
(katikati) kwenye Ikulu ya
Marekani (White house)
 March 26, 1979. 
Hii ndiyo sababu inayofanya Misri kila mwaka kufanya sherehe za kuadhimisha kumbukumbu ya Ushindi dhidi ya Israel katika vita ya Yom Kippur licha la kwamba katika vita hiyo idadi ya wanajeshi wake waliopoteza Maisha ilikuwa kubwa zaidi kuliko Israel sambamba na zana nyingi za kivita kuharibiwa vibaya, lakini malengo yote yaliyopelekea Misri kuingia vitani yalifanikiwa.

NINI KILITOKEA NCHINI ISRAEL BAADA YA MATOKEO MABAYA YA VITA YA YOM KIPPUR?
Waziri mkuu wa Israel Mwanamama Golda Meir alitangaza kujiuzulu mnamo April 10, 1974 na kukabidhi rasmi madaraka mnamo June 3, 1974 kwa Waziri mkuu mpya Yitzak Rabin kufuatia shutuma nzito alizotupiwa kutokana na kupuuza baadhi ya taarifa muhimu za kiintelijensia hivyo kupelekea matokeo mabaya ya vita ya Yom Kippur yaliyopelekea hasara kubwa ya mali na vifo vya askari wengi wa Israel kuwahi kutokea katika historia ya Israel tangu kuasisiwa kwa taifa hilo mwaka 1948.

Israel ilipata funzo kupitia Vita ya Yom Kippur kuwa licha ya ushindi iliyowahi kupata katika vita vilivyotangulia vya mwaka 1948, mgogoro wa Suez na vita ya siku sita isingeweza tena kuwa na uhakika wa kuzitawala kijeshi nchi za kiarabu. Hofu hii ndiyo iliyopelekea Israel kulainika na kulazimika kuingia kwenye mazungumzo kutafuta suluhu ya mgogoro wake na mataifa ya kiarabu.

Ukinakili makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.

© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

•Napatikana kwa mawasiliano yafuatayo:-
Simu namba  +255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com
            rugombanamasudi@live.com