Saturday, March 3, 2018

KUSAMBARATIKA KWA YUGOSLAVIA NA MACHAFUKO KATIKA ENEO LA  KUSINI MASHARIKI YA ULAYA

Na Masudi Rugombana
Shirikisho la kijamaa la Jamhuri ya watu wa Yugoslavia ilikuwa ni nchi katika eneo la kusini mashariki ya bara la Ulaya. Taifa hilo liliundwa baada ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya Dunia tarehe 29 Novemba 1945. Taifa hili la kijamaa lilikuwa ni mojawapo katika mataifa yaliyoendelea zaidi kuliko mataifa mengine katika eneo la kusini mashariki ya bara la Ulaya ( eneo hili linajulikana kama Balkan).

Shirikisho hilo la kijamaa liliundwa na muungano wa Jamhuri sita ambazo ni Bosnia-Herzegovina, Croatia, Macedonia, Montenegro, Serbia, na Slovenia. Jamhuri hizi zilikuwa na mchanganyiko wa makundi ya makabila na dini mbali mbali. Kosovo na Vojvodina yalikuwa ni majimbo yenye utawala wa ndani (autonomous provinces) ndani ya Jamhuri ya Serbia.

Yugoslavia ya Zamani

Yugoslavia, ikiwa na maana ya nchi ya Waslav wa Kusini ilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 255,804 (sawa na maili za mraba 98,766). Ilipakana na mataifa ya Italy kwa upande wa magharibi, Austria na Hungary kwa upande wa kaskazini, Bulgaria na Romania kwa upande wa Mashariki, Albania na Ugiriki kwa upande wa Kusini. Mji mkuu wa taifa hilo la kijamaa ulikuwa Belgrade ambao kwa sasa ni mji mkuu wa Jamhuri ya Serbia. Kiongozi wa kwanza wa Shirikisho hilo la kijamaa alikuwa Josip Broz Tito.

Josip Broz Tito
Serikali ya kijamaa chini ya Josip Tito iliegemea zaidi upande wa Ulaya Mashariki (Eastern bloc) hadi mwaka 1948 ilipoamua kuwa nchi isiyofungamana na upande wowote baada ya kutokea sintofahamu kati ya Rais Josip Tito na mshirika wake Rais Joseph Stalin wa USSR (Union of Soviet Socialist Republics) baada ya Josip Tito kukataa kuifanya Yugoslavia kuwa nchi inayoendeshwa kwa ushawishi wa Urusi kiuchumi, kisiasa na kijeshi (Satelite state) kama zilivyokuwa nchi nyingine za umoja wa Soviet.

Ikumbukwe kuwa Rais Josip Tito alikuwa ni miongoni mwa viongozi waasisi wa umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (The Non-Aligned Movement (NAM), viongozi wengine ni Jawaharlal Nehru wa India, Sukarno wa Indonesia, Gamal Abdul Nasser wa Misri na Kwame Nkrumah wa Ghana.

KUFARIKI KWA JOSIP TITO NA KUANZISHWA KWA MTINDO WA UONGOZI WA URAIS WA PAMOJA.
Josip Tito alifariki tarehe 4 May 1980. Kufuatia kifo cha Josip Tito ambaye alikuwa ni rais wa maisha, Yugoslavia iliongozwa kwa mtindo wa Urais wa pamoja (collective presidency) kwa kuanzisha Ofisi ya Rais wa Urais wa Yugoslavia (The office of the President of the Presidency of Yugoslavia) ambapo nafasi ya Urais ilikuwa ni ya kupokezana kwa zamu kila mwaka baina ya Jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho la Yugoslavia. Kuanzia kwa Rais Lazar Koliševski aliyechukua madaraka baada ya kufariki Josip Tito tarehe 4 May 1980 hadi kwa Rais Branko Kostić tarehe 27 April 1992 ambapo ndio ulikuwa mwisho wa uhai wa Shirikisho la kijamaa la Yugoslavia.

KUIBUKA KWA HARAKATI ZA UTAIFA KWA MISINGI YA UKABILA NA UDINI
Kufuatia kifo cha Josip Tito, ambaye aliiunganisha Yugoslavia kwa mkono wa chuma, kuliibuka harakati kubwa za utaifa kwa misingi ya ukabila na udini zilizoleta migawanyiko baina ya raia katika jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho hilo.

Kuanguka kwa ujamaa katika eneo la Ulaya Mashariki, kuporomoka kwa uchumi na kushindwa kwa mazungumzo ya kulifanyia mageuzi shirikisho baina ya Jamhuri sita zilizokuwa zikiunda shirikisho hilo kulipelekea baadhi ya Jamhuri hizo kujitangazia uhuru na uhuru wao kutambuliwa na baadhi ya mataifa ya Ulaya. Hali hiyo ilipelekea kuanguka kwa Shirikisho la Yugoslavia kwa jamhuri hizo kutangaza kujitenga rasmi kulingana na mipaka ya shirikisho hivyo kupelekea kuibuka kwa vita iliyojulikana kama vita vya Yugoslavia ( Yugoslav Wars)

NANI NI CHANZO CHA KUSAMBARATIKA KWA YUGOSLAVIA?
Ni Slobadan Milosevic, mwanasiasa wa Serbia mwenye msimamo mkali aliyeingia madarakani kupitia harakati kali za utaifa wa Serbia, baada ya kushika hatamu ya madaraka  ya rais wa urais wa Jamhuri ya kijamaa ya Serbia mnamo tarehe 8 May 1989 hadi tarehe 11 January 1991 na Urais wa Jamhuri ya Serbia kuanzia tarehe 11 January 1991– 23 July 1997.
Slobadan Milosevic
Kitendo chake cha kutaka kuwapa nguvu kubwa raia wachache wenye asili ya Serbia ambao ni Wakristo katika jimbo la Kosovo dhidi ya raia wenye asili ya Albania walio wengi ambao ni Waislamu kwa madai kuwa raia wenye asili ya Serbia ambao ni Wakristo walikuwa wanabaguliwa katika jimbo hilo. Pia hatua yake ya kupingana na jamhuri nyingine zilizokuwa zinaunda shirikisho la kijamaa la Yugoslavia katika mpango wa kulifanyia mageuzi shirikisho hilo kulipelekea kuibuka kwa chuki kali dhidi ya raia wenye asili ya Serbia waliokuwa wakiishi katika Jamhuri nyingine za shirikisho.

Akiungwa mkono na wanaharakati wa utaifa wa Serbia walio wachache kutoka Kosovo na Bosnia-Herzegovina pia kwa kupewa msaada na  washirika wake katika television ya Taifa ya Serbia, aliendelea kueneza chuki miongoni wa raia wenye asili ya Serbia walio wachache katika jamhuri za Croatia na Bosnia. Television ya Serbia ilikuwa ikionyesha matukio ya mauaji ya kutisha yaliyofanywa na mafashisti wa Croatia dhidi ya Waserb wakati wa vita kuu ya pili ya Dunia. Hofu ilitawala miongoni mwa jamii ya Waserb huko Croatia na Bosnia kwamba hatima kama hiyo iliyowakuta wenzao na wao inawasubiri.

Hali hii ilipelekea kuibuka kwa itikadi za kuweka msingi wa uanzishwaji wa Serbia kubwa "Greater Serbia" taifa ambalo halitakuwa Serbia tu, bali litakalojumuisha na maeneo ya Bosnia na Croatia yenye idadi kubwa ya wakazi wenye asili ya Serbia. Na ili kufanikisha mpango huo, mkakati uliokuwa umewekwa ilikuwa ni kuwaondoa raia wote wasiokuwa Waserb ( Ethnic Cleansing) katika Serbia na miji inayokaliwa na Waserb wengi katika jamhuri za Croatia na Bosnia.

Tarehe 26 March 1990 uongozi wa Serbia chini ya Rais Slobadan Milosevic ulikutana kujadili hali ya uhasama ulivyokuwa  ikiendelea ndani ya shirikisho la Yugoslavia na kufikia makubaliano rasmi kuwa vita katika Jamhuri za Croatia na Bosnia-Herzegovina ni suala lisiloepukika.
Tarehe 2 July 1990 bunge la Kosovo nalo lilitangaza kuwa Kosovo ni Jamhuri yenye hadhi kama zilivyo jamhuri nyingine sita zilizokuwa zikiunda shirikisho la Yugoslavia. Kufuatia tangazo hilo, Bunge la Serbia lilipiga kura kuweka marufuku kwa jimbo la Kosovo lenye Waislamu wengi ambao ni wakazi wenye asili ya Albania kuwa na Bunge lake.

KUJITENGA KWA JAMHURI ZA SLOVENIA NA CROATIA
Slovenia chini ya Milan Kučan na Croatia chini ya mwanasiasa Franjo Tudman zilijitangazia uhuru wao Juni 25 mwaka 1991 na kujiondoa rasmi kwenye shirikisho la kijamaa la Yugoslavia kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutoridhika na mgawanyo usio sawia wa madaraka kutokana na Waserbia kujitwalia madaraka makubwa zaidi katika Shirikisho. Hii ni kwa sababu muundo wa Urais wa Yugoslavia ulikuwa unawapa Waserbia kura nne za maamuzi kati ya nane. Kura nyingine nne zilikuwa ni za jamhuri za Bosnia-Herzegovina, Croatia, Macedonia na Slovenia.

Jeshi la Yugoslavia lililokuwa na Waserbia wengi lilijaribu kuzuia kujitenga kwa jamhuri ya Slovenia katika vita iliyodumu kwa muda wa siku kumi kuanzia tarehe 27 June 1991 hadi 7 July 1991,  ambapo vikosi vya Yugoslavia vilirudishwa nyuma na vikosi vya ulinzi wa mipaka vya Jamhuri ya Slovenia. Pande mbili zilisaini makubaliano ya kumaliza vita katika mazungumzo ya amani yaliyofanyika kwenye kisiwa cha Brion nchini Croatia. Makubaliano hayo  yaliyosimamiwa na Jumuiya ya Ulaya yanajulikana kama Brioni Agreement. Tarehe 15 January 1992 Jumuiya ya Ulaya ilitangaza kutambua uhuru wa Jamhuri za Croatia na Slovenia.

Kwa upande wa Croatia, vita iliendelea hadi November mwaka 1995 dhidi ya vikosi vya Yugoslavia na wanamgambo wa Kiserbia wakiongozwa na Milan Babic waliokuwa wanapigania jimbo linalokaliwa  na Waserbia wengi la Krajina kuwa Jamhuri yenye utawala wake wa ndani (autonomous republic) katika ardhi ya Croatia. Jimbo hilo lilikuwa na jumla wa Wakazi 469, 700 ambapo idadi ya wakazi wenye asili ya Serbia walikuwa 245,800 sawa na  52.3%, Wacroatia walikuwa 168,000 (35.8%) na jamii nyingine walikuwa 55,900 (11.9%). Croatia ikiungwa mkono na Marekani ilifanya mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waserb mnamo tarehe 4 August 1995 katika vita iliyopewa jina la Operation Storm. Waserbia 2,650 waliuwa kikatili na wengine zaidi ya laki mbili (200,000) walilazimishwa kuhama katika jimbo hilo na kukimbilia katika jimbo la Vojvojina nchini Serbia, tukio hilo linaelezwa kuwa ndio tukio baya zaidi la safisha ya kikabila (Ethnic Cleansing ) barani Ulaya tokea kumalizika vita kuu ya pili ya Dunia.

KUJITENGA KWA JAMHURI YA MACEDONIA
Jamhuri ya Macedonia iliitisha kura ya maoni chini ya uongozi wa rais Kiro Gligorov kuamua kujiondoa katika Shirikisho ya Kijamaa la Yugoslavia tarehe 8 Septemba 1991 ambapo asilimia 75 ya wananchi walijitokeza na kupiga kura ya ndio kwa asilimia 95. Tangazo la uhuru likidhinishwa rasmi na bunge mnamo tarehe 25 Septemba 1991. Tofauti na Jamhuri nyingine za shirikisho hilo, kujitenga kwa Macedonia kulitawaliwa na amani. Hata migogoro michache ya mpaka iliyokuwepo baina yake na shirikisho la Yugoslavia ilijadiliwa na kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo. Taifa la Macedonia lilitambuliwa rasmi na umoja wa mataifa tarehe 8 April, 1993.

KUJITENGA KWA JAMHURI YA BOSNIA-HERZEGOVINA
Wakati Croatia ikiwa vitani dhidi ya majeshi ya Yugoslavia na wapiganaji wa kiserbia, Jamhuri ya Bosnia-Herzegovina iliitisha kura ya maoni kuhusu kujiondoa kwenye Shirikisho tarehe 29 February na tarehe 01 March 1992 ambapo asilimia 64 ya wananchi walijitokeza  kupiga kura ambapo asilimia 97 ya wapiga kura wote walipiga kura ya kukubali kujitenga. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na wakazi wenye asili ya Bosnia na wale wa jimbo la Herzeg ambao asili yao ni Croatia  huku ikisusiwa na raia wenye asili ya Serbia ambao wanaishi kwa wingi katika jimbo la Srpska (Republica Srpska).

Mnamo tarehe 3 March 1992 Mwenyekiti wa Urais wa Bosnia Alija Izetbegović ambaye ni Muislamu alitangaza rasmi uhuru wa Bosnia-Herzegovina na bunge likaidhinisha tangazo la uhuru. Mnamo tarehe 6 April 1992 Marekani na Jumuia ya kiuchumi ya Ulaya zilitangaza rasmi kuutambua uhuru wa Bosnia-Herzegovina na tarehe 22 May 1992 Bosnia ilikubaliwa kuwa mwanachama wa umoja wa mataifa(UN).

VITA VYA KUPIGANIA UHURU WA BOSNIA- HERZEGOVINA
Tangazo hilo la uhuru lilipingwa na wananchi wenye asili ya Serbia ambao wengi wao ni Wakristo. Wakiongozwa na Radovan Karadzic na General Ratko Mladic mnamo tarehe 6 April, 1992 waliamua kutangaza uasi dhidi ya raia Waislamu wa Bosnia na Wale wenye asili ya Croatia, hivyo kupelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ilikuwa ni vita ndani ya vita. Majeshi ya Croatia ambayo kwa wakati huo yalikuwa vitani dhidi ya Yugoslavia na Waasi wa kiserbia nayo yaliingia vitani pia huko Bosnia kuwaunga mkono Wabosnia na Wakroatia waliokuwa wanapigana chini ya makamanda shupavu Alija Izetbegović, Haris Silajdžić, Jenerali Sefer Halilović, Luteni kanali Rasim Delić, Meja Jenerali Enver Hadžihasanovic na Mate Boban katika vita dhidi ya raia wenye asili ya Serbia. Majeshi ya Jamhuri ya Serbia chini ya Rais Slobadan Milosevic nayo yaliingia vitani kusaidi upande wa raia wenye asili ya Serbia ambao wengi wao ni Wakristo. Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) uliunga mkono upande wa Waislamu wa Wabosnia na Wacroatia ambao waliungana kupigana na adui yao mkuu ambaye ni Mserbia.

Vita iliingia katika hatua mbaya zaidi kati ya mwaka 1993-1994 baada ya Waislamu wa Bosnia na raia wenye asili ya Croatia kushindwa kuelewana na kujikuta wakiingia katika mapigano baina yao ambapo Majeshi ya Jamhuri ya Croatia yaliwasaidia Wacroatia wenzao wa Bosnia. Hivyo kulikuwa na vita tatu ndani ya Bosnia ambapo Waislamu wa Wabosnia walikuwa wanapigana na Waserb waliokuwa wakisaidiwa na majeshi ya Jamhuri ya Serbia na Yugoslavia. Wacroatia nao walikuwa wanapigana dhidi ya Waserbia na Waislamu wa Wabosnia walikuwa wanapigana dhidi ya Wacroatia katika jimbo lao la Herzeg-Bosnia.

Hali hiyo ilipelekea Marekani kuanza juhudi za kuwapatanisha Waislamu wa Bosnia na Wananchi wenye asili ya Croatia ili wamalize tofauti zao na kuelekeza nguvu zote dhidi ya adui yao mkuu ambaye ni Serbia. Mazungumzo ya amani yalifanyika Washington Marekani na Pande mbili zifikia muafaka na kusaini makubaliano ya amani yaliyojulikana kama Makubaliano ya Washington mnamo tarehe 18 March 1994. Makubaliano hayo yalisainiwa na Waziri mkuu wa Bosnia Haris Silajdžić, Waziri wa Mambo ya nje wa Croatia Mate Granić na Rais wa Wacroatia wa Herzeg-Bosnia Krešimir Zubak.Baada ya kuondoa tofauti zao Wabosnia na Wacroatia waliunganisha nguvu katika vita dhidi ya adui yao mkuu Mserbia.

Umoja wa mataifa (UN) ulipeleka rasmi wanajeshi wa kulinda amani Mwezi February 1992 kwa lengo la kuhakikisha misaada kibinadamu inawafikia raia na pia kulinda usalama wa raia wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea kwa kuanzisha ukanda salama (safe zone) kwa ajili ya raia waliokuwa wanakimbia mapigano.

Vita ya Bosnia Ilikuwa ni vita iliyohusisha mauaji ya halaiki na safisha ya watu wa jamii na dini tofauti katika baadhi ya miji (Ethnic cleansing). Safisha hiyo ilishuhudia mauaji makubwa ya halaiki dhidi ya Waislamu katika Miji ya Zepa, Foča, Zvornik, Cerska, Snagovo, Banjaluka na Srebrenica inayopatika katika jimbo la Srpska lenye Waserbia wengi. Mauaji hayo yaliongozwa na kamanda wa vita Jenerali Ratko Mladic akisaidiwa na Makamanda Zdravko Tolimir na Radomir Miletic.

Katika mji wa Zepa uliokuwa na idadi ya watu 2441 ambapo Waislamu Wabosnia walikuwa 2330 sawa na asilimia 95 ya wakazi wote. Kamanda Zdravko Tolimir aliongoza mauaji ya  Waislamu 116  siku ya tarehe 25 July 1995 muda mfupi baada ya kuuteka mji huo kutoka mikononi wa askari wa kulinda amani wa umoja wa mataifa hatua iliyopelekea Waislamu wengine kulazimika kuuhama mji wa Zepa.

Katika mji wa Foca uliokuwa na idadi ya watu 48,741 ambapo Waislamu walikuwa zaidi ya nusu ya Wakazi wote sawa na asilimia 52, Waislamu 2704 waliuawa na vikosi vya Waserbia kati ya 7 April 1992 hadi January 1994. Waislamu zaidi ya  22,000 walilazimishwa kuondoka, misikiti yote 13 katika mji wa Foca ililipuliwa na kuteketezwa. Matukio hayo yalikwenda sambamba na vitendo vya ubakaji dhidi ya Wanawake na watoto wa kike wa Kiislamu. Mpaka mwisho wa vita vya Bosnia, ni Waislamu 10 tu ndio waliokuwa wamebaki katika mji wa Foca.

Katika mji wa Cerska uliokuwa na idadi ya Waislamu 1409 na kijiji cha jirani cha Velici, vikosi vya Waserb viliwauwa Waislamu 250 mwanzoni mwa mwezi March 1993 na kuwalazimisha wengine kuhamia katika mji wa Tuzla na Mashariki mwa mji wa Srebrenica.

MAUAJI YA HALAIKI DHIDI YA WAISLAMU KATIKA MJI WA SREBRENICA ( SREBRENICA GENOCIDE )
Wakati vita ya kupigania Uhuru wa Bosnia ikielekea ukingoni baada ya majeshi ya Jamhuri ya Croatia yaliyokuwa  yakishirikiana na majeshi ya ulinzi wa mipaka ya Bosnia kufanikiwa kuteka maeneo mengi ya Jamhuri ya Bosnia-Herzegovina na kuelekea kuwashinda wapiganaji wa Kiserbia waliokuwa wakisaidiwa na Majeshi ya Rais Slobadan Milosevic wa Serbia pamoja na vikosi vya shirikisho la kijamaa la Yugoslavia, wapiganaji wa Kiserbia katika jimbo lao la Srpska lenye waserbia wengi walifanya mauaji makubwa ya halaiki (Genocide) na safisha ya kidini na kikabila (Ethnic Cleansing) dhidi ya Waislamu wa Bosnia katika mji wa Srebrenica.

Mji huo ambao ulikuwa ni moja wapo kati ya maeneo yaliyotengwa na Umoja wa Mataifa kama kanda salama (Safe Zone) ulikuwa chini ya ulinzi wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa kutoka Uholanzi. Vikosi hivyo vilipoteza udhibiti wa mji huo baada ya kuzidiwa nguvu na Wapiganaji wa Kiserbia wa jimbo la Srpska (Republika Srpska) waliokuwa wakiongozwa Radovan Karadžić na Jenerali Ratko Mladic siku ya tarehe 1 Julai 1995.

Kamanda Jenerali Ratko Mladic na wasaidizi wake
wakiingia katika mji wa Srebrenica mara baada
ya Wapiganaji wake kuuteka mji huo kutoka
mikononi mwa walinda amani wa umoja wa mataifa.

Wakitumia kisingizio cha kuwahamisha Waislamu wa Bosnia kwenye makazi salama, Waserb waliwasafirisha wanawake, wazee na watoto pekee wanaokadiriwa kufikia elfu thelasini (30,000) na kuwahifadhi katika makambi huku wakidai kuwa wanaume watu wazima na wavulana watasafirishwa baadae. Baada ya kufanikiwa kuwatenganisha kwenye makambi tofauti, Jenerali Ratko Mladic aliongoza Mauaji ya halaiki yaliyofanyika kati ya Julai 11–22, 1995 ambapo Waislamu Wanaume watu wazima na wavulana wanaofikia 8,373 Waliuawa kikatili na kuzikwa katika makaburi makubwa huku wanawake, wazee na watoto 30,000 waliotenganishwa wakilazimishwa kuondoka katika mji wa Srebranica.

Maiti za Waislamu wa Bosnia zikiwa zimesambaa katika
barabara za mji wa Srebrenica

Mauaji hayo yalikwenda sambamba na vitendo vya utesaji na ubakaji dhidi ya wanawake na watoto wa Kiislamu pamoja na ubomoaji wa nyumba za Waislamu na misikiti. Inaelezwa kuwa mauaji ya Srebrenica ndio makubwa zaidi ya halaiki kuwahi kutokea barani Ulaya tokea kumalizika kwa vita kuu ya Pili ya Dunia.

Lawama kubwa zilielekezwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa mataifa kutoka Uholanzi vilivyokuwa vikiongozwa na Kanali Thomas Jakob Peter Karremans ambavyo vilipewa dhamana ya usalama wa mji Srebrenica kwa kushindwa kuzuia mji huo usiangukie mikononi mwa Waserb na pia kushindwa kuwalinda raia dhidi ya mauaji ya halaiki.
Na katika hali ya kushtua ni kitendo cha walinda amani hao kuamua kujiondoa kutoka kwenye mji huo siku ya Ijumaa tarehe 21 July 1995 na hivyo kuwaacha raia bila ulinzi  wowote. Kabla ya vikosi vya UN kutoka Uholanzi kuondoka Srebrenika, Kamanda wa vikosi hivyo Kanali Thomas Karremans huku akiwa na furaha alionekana akigongeana glasi ya mvinyo na kinara wa mauaji ya Waislamu wa Bosnia huko Srebrenica Jenerali Ratko Mladic.

Kiongozi wa vikosi wa kulinda amani vya umoja wa mataifa
Kanali Thomas Karremans (aliyejishika kiuno katikati)
pamoja na kinara wa Mauaji ya Waislamu wa Bosnia mjini
Srebrenica Jenerali Ratko Mladic wakinywa mvinyo.


MAPIGANO MAKALI JIJINI SARAJEVO  SAMBAMBA NA MASHAMBULIZI YA ANGA KUTOKA VIKOSI VYA NATO
Jiji la Sarajevo lililokuwa na idadi ya wakazi 526,000 ni miongoni mwa miji iliyokumbwa na mapigano makali zaidi baada ya kuzingirwa kwa muda wa miaka mitatu kuanzia tarehe 5 April 1992 hadi tarehe 29 February 1996 na wapiganaji wa Kiserbia wanakadiriwa kufikia 13,000 kutoka jimbo ya Srpska (Republica Srpska) wakisaidiwa na majeshi ya Yugoslavia. Wapiganaji hao chini ya makamanda Milutin Kukanjac, Ratko Mladić,  Stanislav Galić na Dragomir Milošević walikuwa wamekusanyika kwenye milima inayozunguka jiji hilo huku wakiwa na silaha nzito. Wapiganaji hao walikuwa  wakipigania kijitangazia Jamhuri yao itakayojumuisha na maeneo yanayokaliwa  kwa wingi na Waislamu wa Bosnia.

Askari zaidi ya 70,000 wa vikosi vya ulinzi vya Bosnia chini ya makamanda Alija Izetbegović, Mustafa Hajrulahović, Vahid Karavelić, Nedžad Ajnadžić, Mušan Topalović na  Mcroatia Vladimir Šaf waliozingirwa katika jiji la Sarajevo hawakuweza kuuvunja mzingiro wa Waserb kutokana na kuwa na silaha dhaifu.

Miongoni mwa matukio mabaya ya kukumbukwa ni mauaji ya Wakristo wa Serbia waliokuwa wanaishi katika maeneo yanayokaliwa na Waislamu wengi wa Bosnia jijini Sarajevo. Mauaji hayo yalifanywa chini ya Kamanda ambaye pia ni jambazi na msafirishaji bidhaa na wahamiaji haramu kwa njia ya magendo (smuggler) Musan Topalovic ambaye aliwakusanya katika shimo la Kazan karibu na mji wa Sarajevo na kuwaua kikatili kisha kuwazika katika kaburi moja kubwa.
Tukio lingine ni kuuawa kwa Naibu Waziri mkuu wa Bosnia  Hakija Turajlic tarehe 8 January 1993 ambaye Msafara wake uliokuwa ukitokea uwanja wa ndege wa Sarajevo huku ukilindwa na askari wa umoja wa mataifa ulisimamishwa na wapiganaji wa Kiserb ambapo baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa na Hakija, walitoa amri kwa vikosi vya umoja wa Mataifa kumkabidhi mikononi mwao. Mara tu mlango wa gari alimokuwa ulipofunguliwa, askari mmoja wa Kiserb alimuua kwa kumfyatulia risasi sita za kifuani.  

Tukio baya kabisa kuliko yote ni shambulizi la mota katika soko la Markale jijini Sarajevo mnamo tarehe 5 Februari 1994 lililofanywa na wapiganaji wa Kiserb ambapo raia 68 waliuawa na wengine 200 kujeruhiwa. Waserb pia walifanya shambulio lingine kama hilo tarehe 28 August 1995 ambapo raia 43 waliuawa na wengine 75 kujeruhiwa. Ni tukio hili ndilo lililopelekea vikosi vya NATO kuingilia kati kwa kufanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya wapiganaji wa kiserbia baada ya kupata idhini kutoka baraza la usalama la umoja wa mataifa. Ni mashambuli hayo ndiyo yaliyowalazimisha Waserb kukubali kuingia kwenye mazungumzo ya amani kwa ajili ya kumaliza vita. Mazungumzo hayo yalifanyika huko Dayton, Marekani.
Jumla ya watu 14,000 waliuawa wakiwemo raia 5400 katika mapigano ya jijini Sarajevo pekee. Idadi yote ya vifo katika vita ya Bosnia inafikia watu 95,940 ikihusisha askari na raia.

MKATABA WA AMANI WA DAYTON (DAYTON-PARIS ACCORD)
Mazungumzo ya kutatua mgogoro wa vita ya Bosnia yalianza tarehe 1 had tarehe 21 November 1995. Mazungumzo hayo yalifanyika katika kambi ya ndege za kivita ya Wright-Patterson karibu na Dayton, huko Ohio nchini Marekani. Makubaliano ya amani yalifikiwa ambapo mkataba wa makubaliano hayo ulisainiwa rasmi jijini Paris nchini Ufaransa tarehe 14 December 1995 hivyo kumaliza rasmi vita nchini Bosnia. Utiaji saini wa mkataba huo ulishuhudiwa na Rais Jaques Chirac wa Ufaransa, Rais Bill Clinton wa Marekani, Waziri mkuu wa Uingereza John Major, Kansela Helmut Kohl wa Ujerumani na Waziri mkuu wa Urusi Victor Chernomyrdin.

Mkataba huo wa amani uliigawa Bosnia katika Jamhuri tatu zenye utawala wa ndani kila moja ikiwa na serikali yake, bunge na polisi. Jamhuri hizo ni ya Waislamu wa Bosnia, Wacroatia wa Bosnia katika jimbo la Herzeg na Waserb wa Bosnia katika jimbo la Sprska. Pia mkataba ulianzisha serikali kuu yenye mawaziri tisa, watatu kutoka kila jamhuri, inayoongozwa kwa mtindo wa kubadilishana madaraka kutoka Jamhuri moja kwenda nyingine.

Slobadan Milosevic (kushoto), Franjo Tudman (katikati) na
Elija Izetbegovich (kulia) wakisaini mkataba wa amani wa
Dayton kumaliza vita vya Bosnia
Washiriki katika Mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Mwanadiplomasia mashuhuri Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani bwana Warren Christopher  walikuwa rais Slobadan Milosevic wa Serbia akimwakilisha kiongozi wa Waserb wa Bosnia Radovan Karadzic, Rais Franjo Tudman wa Croatia, Rais wa Bosnia-Herzegovina Alija Izetbegovic  na waziri wa Mambo ya nje wa Bosnia-Herzegovina Mohamed Sacirbeg.

VITA YA KOSOVO NA MASHAMBULIZI YA NATO 1998-1999
Baada ya awamu ya pili ya uongozi wa Slobadan Milosevic nchini Serbia kumalizika kwa mujibu wa katiba, kiongozi huyo alichaguliwa kuwa rais wa Shirikisho la Yugoslavia mwaka 1997. Madaraka hayo mapya yalimpa nguvu kubwa zaidi katika Jeshi na vikosi vya Usalama ambapo alivielekeza vikosi hivyo kuanzisha mashambulizi dhidi ya wananchi wa jimbo Kosovo ambalo lilikuwa sehemu ya Jamhuri ya Serbia waliokuwa wanataka kujitenga na kuanzisha taifa lao. Hatua hiyo ilipelekea machafuko makubwa ambayo baadae yaligeuka na kuwa vita kamili kati ya Mwaka 1998-1999 baina ya Majeshi ya Yugoslavia na Jeshi la Ukombozi wa Kosovo ( Kosovo Liberation Army (KLA) likiongozwa na viongozi na makamanda shupavu kama Adem Jashari, Hashim Thaçi, Bilall Syla, Hamëz Jashari, Sylejman Selimi, Agim Çeku na Ramush Haradinaj ambaye kwa sasa ndiye Waziri mkuu wa Kosovo.

Majeshi ya Yugoslavia yakishirikiana na polisi pamoja na wanamgambo wa Kiserb yalifanya mauaji na vitendo vya kikatili dhidi ya Wakazi wa jimbo la Kosovo ambao zaidi ya asilimia 90 ni Waislamu wenye asili ya Albania. Miongoni mwa mauaji ya kutisha ni yale yaliyotokea katika kijiji cha Cuska karibu na mji wa Pec ambapo Waislamu wanaume 41 waliuawa na kila nyumba ilichomwa moto. Ili kuzuia safisha ya kikabila na kidini ( ethnic cleansing) dhidi ya Waislamu wa Kosovo, Umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) chini ya viongozi na makamanda Wesley Clark, Rupert Smith na Javier Solana ulifanya mashambulizi mazito ya anga yaliyopewa jina la Operation Allied Force dhidi ya majeshi ya Yugoslavia na wanajeshi wa Kiserb huko Kosovo. NATO iliweka sharti la kusitisha mashambulizi ikiwa tu rais Slobadan Milosevic atayaondoa majeshi yake na vikosi vya usalama vya Serbia huko Kosovo.

Mashambulizi ya NATO pia yalilenga miundombinu ya barabara na madaraja nchini Serbia na hivyo kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa Yugoslavia. Rais Milosevic alisalimu amri na kuondoa majeshi hivyo kuruhusu walinda amani wa NATO kuingia Kosovo baada kusaini makubaliano ya kumaliza vita na NATO yaliyofanyika katika mji wa Kumanovo nchini Macedonia.Makubaliano hayo yalipewa jina la Kumanovo Agreement.

Hatimaye tarehe 17 February 2008 Kosovo ilijitangazia uhuru baada ya azimio la kutangaza uhuru kupita kwa idadi ya kura 109 kati ya kura 120 za wajumbe wote wa bunge la Kosovo hivyo kujitenga rasmi na jamhuri ya Serbia na kuwa taifa huru ambalo kwa sasa linatambuliwa na mataifa machache ikiwemo Marekani, Canada, Uturuki na Jumuiya ya Ulaya (EU).

SHIRIKISHO LA YUGOSLAVIA BAADA YA JAMHURI NNE KUJITOA.
Baada ya Jamhuri hizo nne kufanikiwa kujitenga na kuwa nchi huru, shirikisho la Yugoslavia lilibaki kuwa muungano wa Jamhuri mbili za Serbia na Montenegro zikitumia jina la Shirikisho la Jamhuri ya Yugoslavia (Federal Republic of Yugoslavia) chini ya uongozi wa rais Slobadan Milosevic ambaye alitawala kama Rais wa Serbia hadi Mwaka 1997. Baada ya muhula wake wa pili kumalizika kama Rais wa Serbia, Milosevic alichaguliwa kuwa rais wa shirikisho la Yugoslavia kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2000 tarehe 7 October alipokabidhi madaraka kwa rais Vojslav Kostunica aliyeongoza hadi mwezi Februari mwaka 2003.

Kuanzia mwaka 2003 nchi hizo zilibadili jina na kujiita Muungano wa taifa la Serbia na Montenegro chini ya uongozi wa rais Svetozar Marovic aliyeongoza hadi tarehe 3 June Mwaka 2006 wakati jamhuri hizo zilipotengana baada ya Montenegro kuitisha kura ya maoni ya kuamua kujitenga na kuwa jamhuri huru ambapo wananchi walipiga kura ya kukubali kujitenga kwa asilimia hamsini na tano (55%). Hivyo kuanzia mwezi Juni  mwaka 2006 Serbia ikawa Jamhuri huru chini ya uongozi wa rais Boris Tadic na Montenegro nayo ikawa Jamhuri huru chini ya uongozi wa rais Filip Vujanovic.

Na huo ndio ulikuwa mwisho rasmi wa shirikisho la kijamaa la Yugoslavia ambalo kusambaratika kwake kuliambatana na  machafuko makubwa katika eneo zima la Balkan yaliyosabisha vifo vya watu 140,000 na wakimbizi milioni mbili na laki tatu.

KUANZISHWA KWA MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA UHALIFU WA KIVITA KATIKA ILIYOKUWA YUGOSLAVIA.
Wakati vita nchini Yugoslavia ilipokuwa inashika kasi hadi kufikia hatua mbaya ya uhalifu wa kutisha dhidi ya binadamu, ilionekana sio vyema mbele ya macho ya jamii ya kimataifa kwa watu waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kutekeleza mauaji, mateso na ubakaji kuachwa waendelee kufurahia maisha uraiani pasina kuchukuliwa hatua za kisheria.  Kwa muktadha huo Umoja wa Mataifa (UN) uliamua kuanzisha mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu wa kivita uliofanyika katika vita vya Yugoslavia kwa lengo la kuwashtaki na kuwafunga jela wale wote waliohusika na uhalifu wa kivita wa kiwango cha juu. Mahakama hiyo iliitwa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu katika Yugoslavia ya zamani. (International Criminal Tribunal for the former Yugoslavia (ICTY).

ICTY ilikuwa  ni mahakama ya kwanza ya uhalifu wa kivita kuundwa na umoja wa Mataifa ikiwa ni mahakama ya kwanza ya kimataifa ya uhalifu wa kivita tokea zilipoundwa mahakama za  Nuremberg na Tokyo ambazo zilianzishwa na mataifa yaliyoshinda vita kuu ya pili ya Dunia (Allied powers- Ufaransa, Muungano wa nchi za Soviet, Uingereza na Marekani) kwa ajili ya kuwashitaki na kuwahukumu wahalifu wakuu wa kivita kutoka mataifa yaliyoshindwa vita hivyo (Axis Powers-Italy, Ujerumani na Japan). Pia vita vya Yugoslavia ndiyo ilikuwa kichocheo kikubwa kilichopelekea kutengenezwa kwa mkataba wa Rome (Rome Statue ) ulioanzisha Mahakama ya kimataifa ya uhalifu mnamo mwaka 1998 ( International Criminal Court-ICC)

Mahakama hii (ICTY) ilianzishwa tarehe 25 May, 1993 baada ya kupitishwa kwa azimio namba 827 la baraza la usalama la umoja wa mataifa na ilimaliza kazi iliyopangiwa tarehe 31 December 2017. Mahakama hiyo ilikuwa na mamlaka juu ya makundi manne ya uhalifu uliofanyanyika katika eneo la Yugoslavia ya zamani tangu mwaka 1991 ambayo ni uvunjifu wa hali ya juu wa mikataba ya Geneva ( grave breaches of the Geneva conventions), ukiukaji wa sheria au desturi za vita ( violations of the laws or customs of war), mauaji ya kimbari (genocide) na uhalifu dhidi ya ubinadamu (crimes against humanity ). Kiwango cha juu cha hukumu ambacho mahakama hiyo ilipewa uwezo wa kuhukumu  ilikuwa ni kifungo cha maisha.Mahakama hii iliweka makao yake huko Geneva nchini Switzeland.

Jumla ya watuhumiwa 161 wa uhalifu wa kivita walishtakiwa ikiwa ni pamoja na mawaziri wakuu, wakuu wa majeshi, mawaziri wa mambo ya ndani na viongozi wengine wengi wa ngazi ya juu na kati wa kisiasa, jeshi na polisi kutoka pande mbali mbali zilizopigana vita katika mgogoro wa Yugoslavia. Watuhumiwa 90 walikutwa na hatia na kuhukumiwa. Miongoni wa watuhiwa sita waliokutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela ni Makamanda Ratko Mladic, Zdravko Tolimir na Stanislav Galic wakati Radovan Karadzic alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela  na Dragomir Milosevic alihukumiwa kifungo cha miaka 33 wakiwa ni miongoni wa viongozi walifungwa miaka mingi jela. Rais Slobadan Milosevic alifariki mnamo tarehe 11 March 2006 akiwa kizuizini huko The Hague kabla ya mashtaka
yake kukamilika.

HALI YA UHUSIANO BAINA YA JAMHURI ZA ILIYOKUWA YUGOSLAVIA
Jamhuri hizo za zamani za iliyokuwa Yugoslavia zimejitahidi kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kwa manufaa ya raia wao. Serbia, Bosnia-Herzegovina, Macedonia, Montenegro na Slovenia zimekuwa na uhusiano mzuri zaidi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Serbia ndio mwekezaji wa pili mkubwa nchini Bosnia-Herzegovina.

Serikali ya za Croatia na Serbia zina uhusiano wa kidiplomasia licha ya hali ya uhasama na chuki ambazo bado hazijafutika katika fikra za wananchi wao zinazosababishwa na matukio yaliyotokea katika vita kuu ya pili ya Dunia na vita vya Yugoslavia. Pia mataifa hayo yana mgogoro wa mpaka ambao unaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo.

Hali ya uhusiano kati ya Serbia na Jamhuri ya Kosovo sio nzuri. Serbia bado inakataa kuitambua Kosovo kama nchi huru kutokana na kutokubaliana na hatua ya jimbo lake hilo la zamani kutangaza kujitenga na kuwa nchi huru. Licha ya Serbia kutoitambua Kosovo kama nchi huru, jamhuri nyingine za iliyokuwa Yugoslavia zilishatangaza rasmi kuutambua uhuru wa Kosovo hadi kufikia hatua ya kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia ikiwemo Montenegro ambayo ina mgogoro wa mpaka na jimbo la Kosovo ambao unaendelea kusuluhishwa kwa njia ya mazungumzo.

Viongozi wa mataifa haya wamekuwa wakiimarisha uhusiano kwa kutembeleana mara kwa mara licha ya ziara hizo kukabiliwa na upinzani wa mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya raia wa mataifa hayo ambao bado wana kumbukumbu za matukio ya kikatili yaliyofanywa na pande hasimu wakati wa vita vya Yugoslavia. Mara nyingi upinzani mkali zaidi hutokea pale kiongozi wa Serbia anapofanya ziara ya kiserikali katika nchi za Croatia, Slovenia au Bosnia na Herzegovina. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa ya vitendo vya kikatili dhidi ya ubinadamu vilivyotokea katika vita vya Yugoslavia vilifanywa na Wanajeshi wa Serbia waliokuwa wakipigana kuzuia Jamhuri hizo zisijitenge.

Walinzi wakimkinga Waziri mkuu wa Serbia Aleksandar
Vucic dhidi ya mashambulizi ya mawe yaliyokuwa
yakirushwa na waombolezaji katika kumbukumbu ya
mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu huko Srebrenica
nchini Bosnia Julai 11 mwaka 2015
Tukio la kukumbukwa zaidi ni la tarehe 11 Julai, 1995 ambapo Waziri mkuu wa Serbia bwana Aleksandar Vucic alipigwa mawe hadi kuvunjiwa miwani na Waombolezaji nchini Bosnia-Herzegovina waliokuwa wakimzomea kupinga uwepo wake katika kumbukumbu ya mauaji ya kikatili dhidi ya maelfu ya Waislamu wa mji wa Srebrenica. Aleksandar Vucic kwa sasa ndiye rais wa Serbia.

Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.
© Copy rights of this article reserved
®Written by Masudi Rugombana

Napatikana kupitia simu namba

+255743 184 044.
Email: masudirugombana@gmail.com